Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Monday 29 July 2024

Ndoa inahitaji maandalizi kisaikolojia

Kama ilivyo kwenye uanachama wa chama au taasisi yoyote, anayefanya hivyo lazima, kwanza ajielimishe aweze kujiunga na chama au taasisi inyomfaa kutokana na uchaguzi, malengo, na matarajio yake. Kufanya hivyo, mhusika anapaswa kumjua anayetaka au kutarajia kumuoa au kuolewa naye. Tofatuti, mwanachama wa vyama vingine au makundi tofauti na ndoa, anaweza kuondoka wakati wowote na kujiunga na vingine. Kwenye ndoa ni tofauti. 
        Wengi huingia wakitarajia maisha yenye furaha na mafainiko hadi kifo kiwatenganisha. Hata hivyo, ambao hushindwa na kuachana jambo ambalo mwanzoni mwa kuingia mahusiano haya huwa si moja ya malengo wala matarajio ya wahusika. Hili linaweza kuepukika kama wahusika watafanya utafiti wa kutosha na kujielimisha kuhusu wenzi japo na majaliwa yana nafasi yake. 
Lazima wahusika wajue ubora na udhaifu wao, welewa hata ujinga wao kama binadamu kwenye safari hii yenye milima na mabonde na misukosuko lukuki. Kuyajua haya hutoa fursa kwa wahusika kujiandaa kisaikolojia na kulhali kuishi pamoja wakifundishana na kuelimishana somo la maisha.             Nani anaajiriwa bila kutakiwa kuonyesha taaluma, akili, uzoefu, na uwezo wa kufanya kazi anayomba? Tusikubali kuingia au kuingizwa kwenye ndoa bila maandalizi na utayari. Wahusika wasikilize roho zao na sauti zao za ndani bila kulazimishwa au kushawishiwa na yeyote kwani ni wao watakayoyaishi maisha wanayoingia.                         Tunasema hivi kutokana na kuzuka mtindo kwa baadhi ya wazazi kuwalamisha watoto wao waolewe au kuoa watu fulani kwa kuangalia vitu kama vile mali na wadhifa wa familia watokazo wasijue vinaweza kuwa chanzo cha maanguko kama wahusika hawakuchagua wenyewe. Hili ni muhimu kwa sababu ndiyo wao watakaofurahia au kuumia mambo yakienda yalivyopangwa au ndiyo siyo. 
        Kama tulivyosema hapo juu, tofauti na chama au taasisi nyingine ambako mhusika anaweza kuhama na kujiunga bila kuumia au kusababisha matatizo kwake binafsi na wengine, ndoa ni tofauti kabisa. Ikishindikana au kutofanikiwa, huleta hisia hafifu kuwa ndoa ni kifungo au ndoana.
         Mfano wa pili, huwezi kununua gari na kuanza kuliendesha kabla ya kujifunza namna ya kufanya hivyo. Hii hutokana na hatari ima ya kuiparamia gari na kusababisha ajali hata kifo au kununua bovu ukaambua hasara. 
            Kwa Waafrika walio wengi, kabla ya kuoa au kolewa au kuoana kama wasemavyo siku hizi, kulikuwa na kipindi maalumu cha kujifunza taasisi hii, nini vinahitajika, havihitajiki, mbinu na miiko ya kuifanikisha na kuifaidi. Pia, kulikuwa na kipindi cha mhusika na wanafamilia yake kumchunguza mtarajiwa ili kujiridhisha kama anakidhi matarajio na viwango vyao. Kwenye jamii nyingi, walichunguza vitu hatarishi vya kifamilia kama magonjwa ya kuambukiza, tabia mbaya kama uchawi, ulafi, kujinyonga, na vingine kama hivyo kulingana na kabila au jamii wanamotoka wahusika. Kwa Waswahili, kulikuwa na jando kwa wanaume na unyago kwa wanawake. 
        Tunaposema Waswahili, hapa tumaanisha Watanzania ambao lugha yao ya taifa na kitambulisho ni Kiswahili au Waafrika kwa ujumla kwa vile tunafanana kisura na kimila ukiachia mbali kuwa Kiswahili ndiyo lugha kubwa pekee ya Kiafrika inayoongelewa zaidi Afrika na ulimwenguni. Hivyo, dhana ya Waswahili inaweza kumaanisha Watanzania hata Waafrika kwa ujumla kulingana na anayeitumia na anavyokubaliana nayo.
        Kitu kingine muhimu ni kujua historia, tabia, sura, umri, na utayari wa anayetaka kufunga ndoa. Kisheria, kuna umri unaoruhusiwa kufanya maamuzi. Hivyo, wahusika wasifichane umri wala tabia zao. Vitu hivi unaweza kuvificha kwa muda. Baadaye vitafichuka hasa ikizingatiwa kuwa unaingia kwenye uhusiano wa kudumu. Kuna kisa cha mwanandoa mmoja aliyemdanganya mwenzie umri wake. Walifunga ndoa na wakaishi kwa furaha tele japo kitambo. Tatizo katika kuficha umri, mhusika hakuwaambia au hakuwa na uwezo wa kuwaambia wote wanaomfahamu. Siku moja wanandoa hawa wakiwa hawana hili wala lile, mwanandoa aliyemficha mwenzie umri alipatikana. Mara nyingi, umri huwa tatizo kwa wanawake kuliko wanaume. 
        Mume wa mhusika akiwa kazini, aliajiriwa mwanamke mmoja akiwa mfanyakazi mwenzao mpya. Katika kutamjitambulisha kwa wafanyakazi wenzake, alisema kuwa anatokea sehemu fulani ambacho kilikuwa ni Kijiji cha mke wa mwanandoa huyu. Baada ya kumaliza utambulisho wa kiofisi, mwanandoa huyu alimwendea yule mfanyakazi mpya. Walisabahiana kwa uchangamfu na akamuuliza moja kwa moja, “unamjua fulani?” Yule mfanyakazi mpya alijibu, “fulani, alimtaja jina. Namfahamu tumesoma wote. Na isitoshe tumetofautiana siku mbili kuzaliwa.” 
              Mwanandoa alimuuliza, “una maana ulizaliwa tarehe” alitaja tarehe. Yule mfanyakazi mpya aliyeonekana dhahiri kuwa mkubwa ikilingaishwa na mkewe alijibu. “Ndiyo, wote tulizaliwa mwaka” aliutaja. Yule jamaa alitabasamu ingawa aligundua kuwa mkewe alikuwa mkubwa miaka sita zaidi ya umri aliokuwa amemwambia. Alianza kujiuliza “je amenificha mangapi na kwanini?”
            Kukatiza kisa kirefu, mwanandoa alimkabili mwenzie na kumuuliza. “Hivi una cheti cha kuzaliwa?” Mwenzake aliuliza, “unataka cheti cha kuzaliwa cha nini?”
Tumalizie. Ndoa inahitaji maandalizi kisaikoloji, kiakili, na kulhali.
Chanzo: Mwananchi jana.

No comments: