Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Friday 12 July 2024

Ndoa Zote Zina changamoto


Ndoa zote, sawa na taasisi yeyote ihusishayo binadamu zina chagamoto. Kinachotofautisha mafanikio na maanguko ya ndoa ni namna ya kuzikabili na kupambana na changamoto. Zinapotokea changamoto, jambo ambalo haliepukiki katika ndoa na maisha kwa ujumla, lazima wanandoa, kwanza wazikubali. Pili, wasisome na kuzielewa ili kuzitafutia majibu na ufumbuzi sahihi na kwa wakati. Tatu, wasione kama ni kitu kipya au cha ajabu. Hawa wote mnaona kama wamefanikiwa ima kitaaluma, vyeo, hata mali, bado ndoa zao zina changamoto sawa na binadamu wowote.
         Hivyo, changamoto katika ndoa ni jambo la kawaida na la lazima. Malkia wa Uingereza Elizabeth alisifika kwa ukubwa na hadhi ya mamlaka yake licha ya kuwa na changamoto katika ndoa yake. Changamoto ya kwanza ilitokana na mumewe Philip kupenda vimwana. Pili, changamoto nyingine ilitokana na kuvunjika kwa ndoa za watoto wake wote wa kike na kiume mbali na kashfa zilizowahusu. Cheo, mali au mamlaka ya mtu havifanyi awe na ndoa iliyofanikiwa. Hivyo, hata rais, profesa, milionea, wote wana changamoto katika ndoa zao. 
        Mfano, jarida maarufu la Marekani la the Washington Post (Desemba 25, 2017) https://www.washingtonpost.com/news/retropolis/wp/2017/12/16/fact-checking-the-crown-is-prince-phillip-a-total-jerk/ lilifichua kuwa Mwana wa mfalme. Philipo ambaye “hakuwa mwaminifu katika ndoa wa kiwango chake. Kwa miaka mingi, alikuwa akihusishwa na wanawake mbalimbali.” Je changamoto za ndoa ya Malkia zilijificha vipi?       
        Kwanza, malkia hakuwahi kulalamika au kutangaza mgogoro kwa kujua madhara yake kwake binafsi na cheo chake. Alitunza siri. Pili, waingereza wanasifika kwa unafiki na usiri wao. Hivyo, hawakutaka kumuaibisha kiongozi wao.
Mbali na Malkia wa Uingereza taifa linalojidai kufuata taratibu za kimila kwa kiwango cha juu, Ghengis Khan (1162–1227) anasifika kama mfalme aliyejenga himaya kubwa na yenye nguvu kuliko zote zilizowahi kutokea duniani. 
        Hata hivyo, alikuwa na udhaifu kingono. Mpaka anakufa, kuna taarifa kuwa alikuwa na watoto 44 aliowazaa na wanawake mbalimbali tena kwa kuwabaka. Kwa kuwazaa watoto wengi tena kwa njia hii, mke wake Khan aliyeitwa Hö’elün, unadhani alikuwa na changamoto kiasi gani hasa ikizingatiwa kuwa aliyekuwa akimkosea wakati wa uhai wake alikuwa na mamlaka kuliko mtu yeyote? Je ni wangapi wenye fedha, taaluma, na mamlaka wenye udhaifu huu? Ajabu, viumbe dhaifu na wadogo ukilinganisha nao kama vile njiwa, wanawazidi ufanisi katika hili. 
        Una habari kuna wanyama ambao wakioana ndo wamemaliza hadi watenganishwe na kifo wakiwa na mapenzi na uaminifu wao? Mjusi wapatikanao huko Australia waitwao shingleback au bobtail or Australia sleepy Lizards wanasifika kwa kuwa waaminifu kiasi cha kuishi na kufa bila kuchepuka. Basi, tuwapeni maua yao. Mbali na mijusi hao, kuna samaki waitwao diploozoom paradixum ambao nao wanaishi pamoja hadi kufa kwa sababu wawili wanapoamua kuwa kitu kimoja hubaki hivyo hadi kifo kiwatenganishe. Wengine ni tumbusi weusi waitwao kwa kimombo coragypas atratus. Hawa jamaa ni po asana. Katika kuzaa na kulea husaidiana kwa usawa tofauti na wanadamu na viumbe wengine waliolewa mfumo nyonyaji dume.
        Kwa ufupi, uzinzi na ukosefu wa uaminifu katika ufalme wa Uingereza, sawa na wengine waliofanikiwa kifedha, kimamlaka, na hata kitaaluma ni kitu cha kawaida. Unaweza kukuta tajiri mkubwa akiyumba katika ndoa huku maskini hata walemavu wakitanua na kuifaidi ndoa. Ndoa haina daktari, rais, profesa wala mwanasayansi. Ni taasisi ambayo imewakwaza wengi na kuwaenzi wachache. Helen Sirleaf na Mary Banda marais wa zamani wa Liberia na Malawi mtawalia, pamoja na urais, mafanikio na ukubwa wa nyadhifa zao waliachika. Pamoja na kuwa kiongozi mwenye nguvu sana duniani na anayeogopewa, Rais wa Urusi, Vladmir Putin alishindwa na ndoa kiasi cha kuishi kiseja bila kuta. 
        Kadhalika Rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi, aliishi bila mke kwa muda wote aliokuwa madarakani. Hapa hatujagusia watu maarufu na wenye ushawishi sana duniani waliooa na kuacha baada ya taasisi hii kuwapiga chenga tokana na sababu mbalimbali zilizo wazi na za siri. Ngugi wa Thiong’o (Kenya) na Wole Soyinka (Nigeria), pamoja na umahiri wao katika liwaya na uandishi walitaliki. waliachika. Wole Soyinka (Nigeria), watangazaji wa kimataifa kama vile Larry King (CNN), Dana Bash, Christiane Amanpour (CNN), matajiri kama vile Bill Gates, Elon Musk na wengine walivyoshindwa katika ndoa zao pamoja na kufanikiwa kifedha na kiuchumi. 
        Hili linatufundisha kuwa ndoa ni taasisi ya ubinadamu inayopaswa kuukubali na kuushughulikia ubinadamu na udhaifu wake. Hakuna wanandoa ambao ni malaika. Wapo hata walioogopa kuoa kama Plato, baba wa falsafa wa Kigiriki, Ludwig Beethoven, bingwa wa kupiga piano, Nicola Tesla mvumbiuzi wa kimarekani na William James Sadis aliyeaminika kuwa na kiwango kikubwa kiakili, pamoja na umahiri wao, waliishi na kufa wasera. Ndoa haina tajiri wala maskini, ukubwa wala udogo, uzuri au ubaya. Ndoa siku zote ni ndoa na lazima itakuwa na changamoto hata iwe imefanikiwa kiasi gani. Bill Gates, Elon Musk, Jeff Bizos, Reginald Mengi, pamoja na ukwasi wao, walishindwa hadi kutalakiana na wenzi wao.
          Tumalizie kusema kuwa kila ndoa ina changamoto yake iwe ya mkubwa au mdogo. Muhimu ni kupambana nazo kiakili na kwa usiri ili kulinda ndoa husika.
Chanzo: Mwananchi.

No comments: