How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday 30 September 2024

Mkeo Siyo Ngoma Upige




Mkeo ni mwenzi. Umtunze akutunze, umpende akupende, na ukimtesa utateseka. Hata hivyo, kuna imani potofu za baadhi ya makabila ambazo hatujui kama ni za kweli kuwa bila mume kumtandika mkewe inaonyesha hampendi vilivyo. Kadhalika, kwa baadhi ya makabila na karibu yote, dhana hii inashangaza na kufanya hata kuwa vigumu kuielewa achia mbali kuikubali. Gereza ni gereza hata liwekewe vyakula safi na kila anasa. Na kipigo ni kipigo na hakuna kipigo kizuri, kinachokubalika au kuzoeleka.
        Kabla hujaamua kumpiga au kumdhulumu mwenzako, jiulize. Je ningekuwa yeye ningependa nitendewe au nitenzwe vipi? Tunarudia. Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Sie waandishi siyo malaika. Pia, siyo mashetani. Tuna udhaifu wetu kama binadamu wengine. Ila tuna ubora ambao tunaweza kusema wengi hawana au unaoweza kuwafunza wengine vitu vya maana tokana na uzoefu wetu katika taasisi hii adhimu na ngumu. Pamoja na kukaa kwenye taasisi hii yenye kila aina ya changamoto na maadui, hatujawahi kupigana au kuitana majina mabaya hata siku moja. Tumewahi kununiana. Hili ni jambo la kawaida kwa binadamu. Hatujawahi kutukanana hata siku moja.
        Hatuandiki haya kinadharia, kujifurahisha, au kumfurahisha yeyote bali kufunza na kushare uzoefu wetu. Tumeyaishi na kujua kuwa yanawezekana. Kama yamewezekana kwetu, kwanini yasiwezekane kwa wengine? Amani, furaha, na ufanisi katika ndoa ni suala la uamuzi ila ni muhimu. Hata mafarakano, huzuni, na maanguko katika ndoa ni masuala ya kupima na kuamua.
Tutoe mfano wa mwanandoa anayemdhulumu au kumuumiza mwenzie. Je ni haki kwa mwanandoa huyu kutegemea kutendewa kinyume na atendavyo? Wahenga walisema kuwa dawa ya moto ni moto. Japo wanawake, mara nyingi, hawatumii fujo kama wanaume inapotokea ndoa ikawa na dhuluma na unyanyasaji, wana namna yao ya kulipiza kisasi hata kama wapo pia wanaosamehe, kuamua kuachana, au kuvumilia hata kuachika. Kumpiga mkeo, licha ya kumuumiza na kumdhalilisha, ni kumuonea na kumdhulumu. Ni dhuluma kama dhuluma nyingine.
        Kuna rafiki wa familia ambaye alikuwa na tabia ya kumtukana na kumpiga mkewe tena mbele ya watoto wake wachanga bila kujua kuwa angewaambukiza watoto uhovyo na ukatili huu.             Siku moja akiwa kazini, mtoto wake mmoja alimuomba mama yake ampe ice cream (hatuna Kiswahili chake). Mama alimpa ice cream. Hata hivyo, mtoto hakutosheka, pamoja na kupewa ice cream nyingi tu tena jioni jambo ambalo humsababishia kukosa usingizi na si jema kiafya.         Mtoto aliomba tena apewe ice cream. Safari hii, mama alimkatalia. Bila hili wala lile, yule mtoto mdogo alimrushia kibao mama yake huku akifoka kama afanyavyo baba yake. Kujua tatizo vilivyo, mama hakumrudishia kibao zaidi ya kumuonya asirudie. Mtoto naye hakukubali, badala ya kumpiga tena, alimwambia “kwanini nisikupige?”  Mama alimjibu mtoto “kwanini unipige kosa langu nini?” Mtoto alijibu “mbona baba huwa anakupiga na haelezi ni kwanini?”
        Mama alimdanganya mtoto kwa kumshauri asome kitabu na mtoto alisahau lakini bila kujutia. Je wewe baba unayempiga mkeo, ungekuwa wewe ungefanya nini? Ungemfanya nini yule mtoto? Si rahisi kujibu. Na kama ukijibu, majibu yatakuwa mengi na tofauti. Kwa ufupi ni kwamba, kama walivyosema wahenga, kazimbi si mchezo mwema.         Watoto wetu ni sisi wa jana na kesho. Hivyo, tunapofanya mambo, tusijiangalie au kuwaangalia tu wale tunaowaonea au kuwadhulumu. Dhuluma kwa mama ni dhuluma kwa mtoto. Hivyo, iwe ni mila au imani, kumpiga mkeo si jambo jema. Kuna jenga chuki ya chinichini na madhara yake yanaweza kuwa makubwa na ya muda mrefu kuliko unavyoweza kudhani. Mtoto wa nyoka ni nyoka.
        Hivyo, ni vizur ukajua kuwa kupigana ni udhalilishaji na ukatili. Je hakuna njia nyingine za kuonyeshana mapenzi au kutatua ugomvi?
Kisa kingine, kuna jamaa mmoja alizoea kumpiga mkewe mara kwa mara. Mama alichukia na kumwekea kisasi. Alipougua akawa hana uwezo wa kujisaidia, alihitaji mkewe amsaidie. Mkewe alimjibu “sitakusaidia ili upone uendelee kunipiga. Nawe, acha ugonjwa ukupige uonje uchungu wa kuumizwa.”
        Tumalazie. Mkeo siyo ngoma upige. Ni binadamu mwenye kuumia, anayehitaji heshima na mapenzi na si matezo na udhalilishaji. Je unapata faida gani kumuumiza mwenzio uliyeahidi kumpenda, kumlinda, na kumtunza ili naye akutenze hivyo?
Chanzo: Mwananchi jana.

Saturday 28 September 2024

How Berlin Conference Clung on Africa: What Africans Must Do

 



ISBN9789956554645
Pages478
Dimensions224x170 mm
Published2024
PublisherLangaa RPCIG, Cameroon
FormatPaperback

How Berlin Conference Clung on Africa

What Africans Must Do

by Nkwazi N. Mhango

The book How Berlin Conference Clung on Africa: What Africans Must Do aims to expose the root causes of Africa’s struggles, including colonialism, greed, and artificial national divisions. It examines the lasting impact of the Berlin Conference of 1884-85, where European powers divided Africa, leading to dependence and underdevelopment. The book also criticises the role of African leaders in perpetuating these divisions and hindering progress. It argues that the artificial borders created at the Berlin Conference have been detrimental to Africa, and calls for unity and a rejection of the colonial legacy to achieve true independence and prosperity.




Wednesday 25 September 2024

Kwanini Tumeamua Kuwa Wafungwa wa Hiari?


Mafyatu wenzangu naomba nianze na swali la kifyatu. Umewahi kujiuliza ni kwanini tumejigeuza au kugeuzwa wafungwa katika magereza ya kujitakia tena kwa kuyajenga wenyewe? Naona yule anatikisa kichwa. Nadanganya au huoni? Nenda uishiko. Kama kuna kibopa, angalia mjengo wake. Kila mjengo uitwao mjengo, umezungushiwa kuta. Je kuna tofauti gani na gereza? Je hili ndilo jibu? Je tatizo ni nini? Je tufanye nini? Je hatujiingiza hasara wakati njuluku ya kuondoa insecurity ni ndogo kuliko ya kujenga mikuta?

 Hata magereza yana nafuu kwa sababu unatumikia kifungo chako unaachiwa huru. Hili gereza la kujitakia ni la maisha. Kuwa huru ima ufe au upae mbinguni na mwili wako kama kile kitegemezi cha Josefu wa Nazareti kwenye zile ngano za zamani. Pia, unaweza kuwa huru kama utakuwa apechealolo aka kapuku.Japo ukapuku ni kitu kibaya, lau unakupa uhuru ambapo ukwasi unawafanya mafyatu wenye nao kuishi magerezani tena ya kujitakia na kujilipia. Hapa ndipo ulipo mzizi wa shule ya leo.

Acheni ufisadi kwani unazalisha wizi iwe ni wa kujitakia au kulazimika.

Tumegeuka jamii ya mijizi, mibaka, na vibaka. Mtu analala maskini. Anaamka tajiri. Hatuhoji wala kushuku ni miujiza gani amefanya! Hivi hawa mafyatu wanaokokotoa mafyatu badala ya kokoto mbona hawakokotoi hawa majambizi? Leo jambizi linatufyatua na njuluku zetu. Badala ya kulifyatulia mbali likafyatukia ima gerezani au kuzimu, eti tunaliabudia. Ebo! Enyi mafyatu wakumbaff, nani aliwaroga hadi mkafyatuka kinyume na kuabudia majizi na masanamu?

Mie Ntume Fyatu kwa mafyatu nasema, fyatueni majizi na majambazi wa njuluku zenu bila kujali cheo wala saizi. Inakuwaje mnaabudia mihalifu na kuwadharau madingi waadilifu waliotumikia jamii kwa uadilifu maisha yao yote wanaishi kimaskini wakati vibaka waliozaliwa jana wanaishi na kuogelea kwenye utajiri usio na maelezo wala kueleweka? Tell me. Naona yule anacheka akidhani sikijui kitasha wakati nilizaliwa utashani na kukulia umakondeni. You get it or it gets you? Usinicheke kwa kuongea broken ingilishi wakati wewe unaongea kiswanglish kama waishiwa wa njengoni. 

Mafyatu wa hovyo na wenye roho za wizi wanasema eti ujanja kupata. Ujanja si kupata ni umepata kihalali? Kama wewe umetumia kalamu kuiba, kwanini mafyatu wasitumie mapango kukuibia? Kama umetumia mtutu kuiba, nawe lazima tukunyake. Kama unateka wenzako na kuwapoteza, lazima tukunyake liwalo na liwe. Unapofyatua au kupiga njuluku za mafyatu, unatengeneza jamii isiyo salama na maskini. Wanene wanazidi kuiba ili kujenga mikuta na kuongeza walinzi wasijue kifo kinapenya hata kwenye moto.

         Hata ujizungushie mibomu ya nyuklia, kifo kikiamua kukutembelea kinakunyotoa roho tu. Je hizi kuta zinakupa uhakika wa kutofanyiwa kitu mbaya? Hebu jamanini tufikiri pamoja. Tumeishiwa akili hadi tunajisalimisha kwa jinai tena jumla na kirahisi hivi? Nani katuroga ingawa fyatu simo?

            Huwa nashangaa kuona mafyatu wakishangaa wafungwa wanapokuwa wamelindwa. Kwani, hao mandingi wenu hawalindwi kama wafungwa? Hawafungwi na ulaji wao tena mwingi wa haramu? Kama siyo wafungwa, kwanini wanalindwa? 

        Mbona mimi silindwi? Si kwamba mie sina njuluku za kuweka mabaunsa, sina kwa sababu siyo mhalifu wala siyo mshamba na wala usalama na uhai vyangu havitegemei ulinzi bali uadiilfu wangu. Hivyo, sihitaji makandokando wala makomando, kunilinda au kujieleza. You know what I mean. Nani anapenda kuishi kama msukule kulindwa wakati ulinzi wa kweli ni kugawana na kutendeana haki? 

        Hapa Ukanadani, majumba yetu hayazungushiwi kuta bali maua. Unaweza hata kulala mlango wazi na usiwe na hofu kwa vile kila fyatu hapa anakula na kushiba. Hili ndilo jibu la kuwa huru na salama. Pia, hili ndilo kubwa nililojifunza utashani. Lazima wanene wahakikishe wadogo wanapata milo yao yote mitano kwa siku. Nani anataka ulinzi wakati ulinzi wenyewe bandia? Anayelinda Mungu. Huoni hata papa na wachungaji mbali na wachunaji wanaojifanya kutenda miujiza wanalindwa na binadamu na bunduki kwa vile hawamuamini Mungu wanayemhubiri na kutumia kutengeza njuluku? Mie siyo bwege wa kupatikana nikidhani nimepata kama wao wanaolindwa kama wahalifu.

            Leo naandika kwa uchungu tokana na mafyatu wangu walio wengi wanavyosota. Pia, wote tunaangamia na kuangamizana tokana na kutoa majibu yasiyo sahihi katika matatizo yetu kama jamii ya mafyatu. Ukitaka jamii iliyo safi na salama, tenda haki. Hakikisha kila fyatu anafyatua milo yote mitano kwa siku uone. Badala ya kupoteza njuluku kwenye vikuta na walinzi, unakuwa na ulinzi wa uhakika. Huku hutuogopi ndata wala kutekwa. Nani atamteka nani wakati utekaji ni jambo la kijima na kinyama? Hata waanimo hawatekani. Huku waanimo wana haki sawa na mafyatu. Hivyo, usishangae jirani yako kuwa sungura tena aliyenona asiyeogopa kufyatuliwa na fyatu jangili kama huko.’

            Leo, nawataarifu kuwa nimeastaafu siasa. Hivyo, nitakuwa nafyatua mambo ya kijamii na siasa kwa mbali pale nitakapohisi kufyatuliwa. Wasalaaam.

Chanzo: Mwananchi leo.

Tuesday 24 September 2024

Mume Si Fedha, Elimu, wala Madaraka


 

Hivi karibuni kumezuka matapeli hata wadhalilishaji, tena wengine wasomi, wajiitao wataalamu wa ndoa na saikolojia ya mwanamke wanaipotosha jamii hata kuiibia kwa kisingizio cha kutoa ushauri juu ya ndoa. Watu hawa, kwa kujua na kudandia mfumo dume, wawe wanaume hata wanawake, waganganjaa, waganga wa kienyeji, na viongozi wengi wa dini wa kujipachika wamejigeuza wataalamu wa saikolojia ya ndoa na wanawake. Wanatoa ushauri ambao hauingii akilini vinginevyo mwenye kuuchukua na kuuamini ima awe na mjinga hata mpumbavu wa kutupwa, kuzidiwa, kutapatapa au kukata tamaa.
            Hivi karibuni tulitumiwa clip ya mshauri anayetambulishwa kama daktari wa saikolojia. Jamaa huyu anaongea bila aibu tena kwa mjumlisho (generalisation) na kujiamini. Anadai eti wanawake ima ni kama watoto au ni watoto kwenye masuala ya kutafuta fedha. Anadai kuwa kila mwanamke anaamini kuwa kila mwanaume ni gwiji wa kusaka pesa. Hivyo, wanaume wasilalamike wanapokuwa hawana fedha. Je hii ni kweli?
            Sisi kama wanandoa ambao tumedumu kwenye ndoa kwa miaka 27 tumestushwa na ushauri huu wa ajabu na hovyo. Kwa kutumia ujuzi na uzoefu wetu, tumeona huu ima ni kutojua, udhalilishaji wa akina mama au hata kuganga njaa.  
    Kwanza, haiwezekani wanawake wote, kama binadamu yeyote, wakawa na tabia sawa katika jambo moja, yaani uwezo wa mwanaume kutafuta fedha. Hata wanyama hawana tabia moja inayofanana kwa wote kwenye jambo moja. Hata mbuzi hawafanani kitabia. Mmoja anaweza kupenda kushambuliwa mashamba na kula mazao. Mwingine anaweza asipende kushambulia mashamba kwa vile alishaumizwa alipofanya hivyo nakadhalika.
         Kimsingi, uwezo wa mtu wa kutafuta au kutotafuta fedha unategemea mambo mengi kama vile mipango, motisha, uzoefu, malengo, makuzi, ndoto, aina ya jamii anamotoka, muda, mazingira, aina ya shughuli anayofanya kumuingizia fedha nakadhalika
        Pili, ni imani potofu kufikiri kuwa kila mwanamke, ima ni tegemezi au anaolewa kufuata fedha na si kutekeleza malengo na mipango yake kama binadamu. Hivyo, licha ya kuwa udhalilishaji na uongo, ni ujinga na upofu kudhani kila mwanamke anaingia kwenye ndoa kutafuta au kufuata fedha. Ingekuwa hivyo, wanaume maskini wasingeoa. Haimaanishi kuwa hakuna watafuta fedha katika ndoa hasa wanaosukumwa ima na tamaa binafsi au baadhi ya mila za kinyonyaji kama vile kutaka mume awe buzi la kumtunza mhusika na watu wake. Hii siyo kwa wote.
        Tatu, ni imani potofu na kutowajua wanawake kama binadamu wa kawaida wenye uwezo sawa na wanaume kudhani kuwa ni tegemezi kwa wanaume, hivyo, wanafikiri kuwa kila mwanaume ni mashine kutapika fedha yaani Automated Teller Machine (ATM) ambayo huwa haiishiwi au kukosa fedha. Hata ATM, wakati mwingine, huishiwa fedha na kungoja wahusika waongeze nyingine.
        Nne, kuna wanawake matajiri ima wa kutafuta au kurithi wanaojua kuitafuta, kuitunza na kuitumia kuliko wanaume ambavyo pia wapo wanaume wa namna hii. Unapodai eti wanawake wote wanaamini wanaume ni ATMs, unajikumbusha kuwa wapo matajiri, wasomi, wenye madaraka tena makubwa kuliko waume zao? Hawa nao si wanawake?
        Tano, ni wanaume wangapi waliooa wanawake matajiri kama vile Mtume Muhammad aliyemuoa Khadija mama aliyerithi utajiri mkubwa licha ya kuwa mfanyabiashara maarufu zame zile kule Makka. Je hili nalo watalisemeaje hawa watalaamu wetu wenye kutia shaka? Je waliioa tena wanajulikana toka kwenye familia maskini nao vipi?
        Pamoja na utaalamu, usomi na mengine kama hayo, wengi tunashauri kutokana na maisha yetu yaliyojengwa katika misingi fulani. Hivyo, usishangae mshauri unayemuamini au kumtegemea sana, akashauri kitu kisichokuingia akilini. Hivyo, tunasema asemacho kinaweza kuakisi ya maisha yake binafsi ambayo pia yanaweza kuhitaji ushauri japo yeye ni mshauri. 
        Binadamu hawezi kukimbia maisha na tabia zake. Kinyonga hata abadili rangi zake vipi bado ni kinyonga. Kama umesomea ushauri na maisha yako hayafanani na unachoshauri au unashauri utopolo, jua kuna tatizo. Faida za kitu chochote lazima zianze nawe. Huwezi kuhubiri maji ukanywa mvinyo. Kwa ufupi, katika ndoa, mume au mke si elimu, fedha, au madaraka bali ni mume au mke basi. Mengine, ni makandokando tu.
Chanzo: Mwananchi J'pili.

Tuesday 17 September 2024

FYATU MFYATUZI: Mrume kutoka kama manzi, unataka nini?


Juzi si nilifyatuka nikataka kufyatua nisijue fyatu mwenyewe nuksi! Si katika kujimwambafy, mtaani kwetu, nikakutana na njema amevaa hereni, suruali za kubana, na akijitembeza kinamna nikamshobokea lau nimfyatue. Fyatu nilidhani mwenzangu mdenge kumbe mrume aliyeanza kujiharibu hata kabla ya kuharibiwa. Ongea kidogo Bi Mkubwa asikusikie ukanifyatulisha au maadui zangu wakainyaka na kunirostisha kama yule katibua mkuu wa CcM aliyefyatuka na kukwareka asijue atafyatuliwa na kukitoa bila kuaga. Hivi dume zima kuvaa hivyo untakani jamani? Afa fyatu akikutokea un’anza kusema eti waogoopa poopobawa! Hapa unamaanisha nini kama siyo biashara tena biashara yenyewe chafu na haramu jamani? Je hawa mafyatu wanaoyafanya haya wanajua madhara yake kwao binafsi na jamii kwa ujumla au ni ulimbukeni wa kuigiza kila uchafu toka majuu ambako upopobawa umehalalishwa na kutetewa kama haki za mafyatu?  Kama mnataka kuishi kama watasha wakati nyinyi si watasha si muende kwao muone watakavyobagua. Si mlimsikia yule Bwana Mkubwa wa Rumi akifyatuka kuwa sasa makasisi waubariki upopobawa? Hayo tuyaache na kuwaachia wenyewe.

 Bila hili wala lile si nikadhani kaingia kwenye kumi nane zangu. Bila ajizi si nikatupa nyavu ili nimnase huyu msupu kumbe dude! Ile kupiga mbinja, si fyatu akafyatuka na kuchaji akitaka kunikungfuu eti namgeuza totoz. Lahaula! Kwanza, sikujua la kusema wala kufanya mbali na kupigwa butwaa nisiamini. Sasa kama wewe si totoz, mrume mzima unatilia vipuri kama totoz tukufanyeni kama siyo kufyatuka tukakufyatua? Basi, jamaa lilijifanya linayaweza ma kung-fu na magujulyoo! Kwa vile fyatu nina blackbelt, si nilimfyatukia kwa kupiga show kwa kusamasoti na kukrow hadi hadi akafyata. Utani tuache.

Huu ulimbukeni utamaliza baadhi ya mafyatu wetu. Sijui ni ufyatu, ujinga, au ukumbaff, sijui. Nisaidieni kabla sijapagawa na kujinyotoa au kumnyotoa fyatu roho. Unakuta fyatu jeusi kama lami eti linachora tattoo. Kwanza, mnajua maana yake? Ukiyaambia mafyatu yachanje kama akina njomba, yanasema hayo ni mambo ya kizamani na ya kishamba wakati mishamba ni yenyewe miana hizaya! Hii ni nini kama siyo kumtafuta paka mweusi kwenye kiza tena kinene? Kwani hizo tattoo na chale zina tofauti na upya gani kama siyo ukumbaff? Mikumbaff mingine ikiwa misupastaa siku moja kwa vile inafokafoka kwenye mic, inatoga masikio, inavaa milegezo, na kujichorachora mitattoo na kujiona iko Hollywood. Mtaliwa. Shauri yenu hata kama chama twawala chawala lakini si hivo mtavoliwa nawaonyeni fyatu nyie.

            Tokana na kukosa fyatu waliofyatuka kimaadili, siku hizi maadili yamegeuzwa madili. Zamani huteuliwi wala kupewa ulaji wa umma bila kufanana na umma. Mfano, zama zile, lazima kila anayeteuliwa iandikwe historia yake. Siku hizi? Hata msafara wa maza ni siri. Wateule wake ni siri. Wanaandikwa majina bila kueleza walivyozaliwa, kukua, kusoma, kuoa au kuolewa. Nani anataka aseme kila kitu wakati kuna hata wakwe wa maza waliopewa unene tokana na ukwe na siyo sifa? Nani anataka kutangaza majina ya wanaoandamana naye wakati kuna wengi wasiostahiki wanaofaidi ulaji wa dezo. Kaya hii inaliwa. We acha tu. Badala ya njemba kufyatukia kuliwa huu yanafyatukia na kushobokea ukumbaff wa maigizo ya kila uchafu.

            Turejee kwa huyu sijui nimwite sheitwan au aduw’Allah. Hata sijui. Baba zima eti linaweka kipindi puani halafu linataka lisipelekewe mashambulizi. Kama wewe unayaweza, dada zako watafanya nini mwana hizaya wee ibn muthnaxyz wal mujirm na mumu nyambaff kabisa? Sasa mnanilazimisha kufyatua kimanga kama Dip Weed na washikaji zake kule kukuu! Hivi nayo imefilia wapi au mafyatu wamefyatuliwa na kufishwa kinamna hadi wakaufyata ili waliwe uzuri? Mkiendekeza ukumbaff na ulimbukeni huu, mtapotezwa. Hivi jibaba linalojifanya manzi linaweza kufyatua vitegemezi vya nguvu kama vyetu? Mambo ya totoz waachie wao ufanye mambo ya warume hata kama ni kabuyange.

            Fyatu zima linajigeuza bwabwa. Hivi wazazi wako wangekuwa kama wewe ungekuwapo? Lazima niwafyatukie lau kieleweke. Sijui kwanini wanene wenye maulaji hawayafyatui mafyatu kama haya yanayosababisha laana Kayani na wana maslahi gani nayo? Wenzenu kwenye miji ya Gomla na Sodimu waliteketezwa, halafu mnatulete laana na ukumbaff wenu? Au mnafuata mafyatu ya kitasha yanayotaka kuwapunguza baada ya uzazi wa mpango kugoma kwa kuwaingiza kwenye gharika hili la kujitakia? Nyambaff kabisa. Mnaniuzi hadi natamani nifyatue hii mifyatu kwa kuinyotoa roho.

            Juzi nilisikia eti na manzi nao wanafanyiana mambo ya kabuyange! Kwani mawe ya kusagia yameisha hadi nao wafanye hayo mambo? Loh! Hicho kisagio mnacho au kujihadaa ili mfanane na watasha uchwara waliolaaniwa na kutaka laana zao zienee duniani ili wote tukose? Nenda kayafanye sauzi uone watakavyokuletea watu wa kukufanyia vitu ili ukome na kukomaa. Bahati yenu. Ningekuwa dingi wa kaya hii mbona ningewanyotolea roho mbali lau muwahi kuonana na ibilisi bosi wenu. Yaani warume wameisha hadi manzi wasyagane au mibaba igeuzane mitutu wakati manzi bwerere?

Hivi nimesemaje?

Chanzo: Mwananchi Jumatano iliyopita.

Monday 16 September 2024

Ndoa ni darasa jifunze na ufunze


Tuanze na kisa cha wanandoa wawili marafiki na wageni waliotutembelea hapa nyumbani. Walitoka Toronto kuja Manitoba. Hivyo, ilibidi walale lau tujadili hili na lile. Baba ni kutoka nchi jirani ya Tanzania. Mama ni mkanada mzaliwa wa Toronto. Ilipofika wakati wa kulala, tuliwakumbusha watoto wetu kwenda kupiga miswaki na kwenda vyumbani kwao. Baada ya hapo, na sie tuliwaaga wageni wetu kuwa tulikuwa tunawenda maliwatoni kupiga mswaki. Hawakuamini kama ambavyo nasi hatukuamini baada ya kueleza mshangao wao. Wale wanandoa walitushangaa kwanini tunapiga miswaki kabla ya kulala. Nasi, tuliwashangaa. Mama alisema kuwa akipiga mswaki wakati anakwenda kulala, asingeweza kupata usingizi mbali na kinyaa cha kufanya hivyo! Nesaa naye alimwambia kuwa akilala bila kupiga mswaki, asingepata usingizi. Hivyo, tulishangaana kama ambavyo hushangaana kwenye mbalimbali ambapo huishia kujisuta wakidhani wanawasuta wenzao.

Sasa unaweza kujiuliza. Kama una mazoea safi ya kupiga mswaki kila ulalapo , utajiuliza hata kushangaa inakuwaje walale bila kupiga miswaki. Ukiangalia kisa hiki, kinahusu jambo dogo lakini lenye umuhimu mkubwa na la binafsi lakini kinaweza kukufunza mengi. Je ni mangapi wanandoa hawayajui japo ni muhimu?

            Mnapofunga ndoa, kila mmoja anakuja na mambo yake, yawe mazuri au mabaya. Kila mmoja anakuja na mazoea yatokanayo na malezi, mazingira hata uchaguzi na utashi wake. Ni kapu mchanganyiko. Hivyo, mnapoanza kuishi kama wanandoa, jambo kubwa na la muhimu ni kuwa tayari kujifunza na kufundisha. Ndoa ni kama darasa au shule isiyokuwa na mwisho. Ili kuifanikisha, wanandoa, bila kujali viwango vya elimu au umri, lazima wawe tayari kuwa wanafunzi na walimu kwa wakati mmoja. Ukiangalia hili la kutopiga mswaki wakati wa kulala, pia laweza kuwapo la kulala bila hata kuoga. Binadamu ni viumbe wachafu. Unapalala mchafu, unategemea kweli mambo yaende vizuri? Umeshinda unakula, kujisaidia, kutoa jasho na mengine. Sasa inakuwaje unalala m chafu? Je kwa wale waliozoea kulala bila kupiga mswaki au kuoga hawajapata la kujifunza hapa? Je wale wenye utamaduni wa kuyafanya haya hawana la kuwafundisha wasioyafanya?

            Binadamu tuna mazoea na mila tofauti na saa nyingine kinzani kiasi cha kuchekana na kuishia kujicheka bila kujua. Mfano, kuna jamii huko bara Asia ambayo huamini kuwa kuramba vidole ni kuonyesha kuwa chakula kilicholiwa ni kitamu! Ukila na kumaliza bila kuramba vidole wanakushangaa kama unavyowashangaa kwa kuramba vidole. Pia, huko huko, wapo wanaokula kwa kupwakia na wengine wakiongea. Ukila kimya, bila shaka watakushangaa kama utakavyowashangaa. 

        Pia, kuna mazoea mabaya zaidi kwa wanandoa kula chakula cha usiku (wakubwa mnatuelewa) kwa kupigishana makelele bila kujali watoto hata kama wapo chumba cha pili hasa kwenye jamii za kibinafsi za Magharibi. Wakati kwa Waafrika hili ni mwiko, kwa wenzetu hutushangaa inawezekanaje kula chakula cha usiku cha baba na mama bila kupigishana makelele. Nasi huwashangaa inakuwaje wapige makelele kama nguruwe kiasi cha kuharibu watoto wao.

 Kwa watu hasa wa Pwani, haya ni makufuru. Je wanapooana watu toka kwenye hizi jamii tofauti, kweli hawana la kujifunza na kufundisha? Inakuwaje mtu ule kama mbwa, kuramba vidole, au kupwakia kama fisi? Unaweza kuhoji.

Turejee kwenye ndoa kama darasa hata shule. Je wewe au mwenzako alishawahi kukutana na mazoea, mila, au tabia ambazo ni tofauti hata kinzani na za mwenzako. Je huwa mnafanya nini mnapojikuta kwenye hali kama hii? Kama hamjawahi, mkijikuta kwenye hali kama hii, mtafanya nini? Hapa hakuna jibu moja. La muhimu, ni wote wawili kuwa tayari kujifunza na kufundishana bila kila mmoja kushikilia lake ndiyo sahihi. Mfano, katika kisa cha kutopiga mswaki, kupiga mswaki wakati wa kulala ni bora kuliko kutofanya hivyo. 

       Pia, katika kisa cha kupwakia kama wanyama na kuongea wakati wa kula, kukaa kimya ni bora kuliko kutofanya hivyo. Hata hivyo, tuonye. Mazoea ni magumu kuyaacha hasa yanapokuwa sehemu ya makuzi na malezi ya binadamu.

Tumalize kwa kushauri kuwa, katika kutatua matatizo kama hayo, wanandoa wanapaswa kuwa flexible (hatuna Kiswahili chake). Wawe tayari kujifunza na kufundisha na si mara moja bali miaka yao yote.

Chanzo: Mwananchi jana.

Thursday 12 September 2024

Tumekuwa Mateka wa Watekaji


Hapo zamani kaya ikiwa kaya, tulizoea kusikia utekaji na uuaji wa watu kisiasa kwa majirani zetu. Majirani zetu wa kaskazini mashariki walisifika kwa mchezo huu mchafu uliofyatua vigogo wengi wa kisiasa wakiwamo mwaziri kabla ya wale wa Kaskazini magharibi kuchukua ukanda. Ni pale nduli alipompoka madaraka Oboto ambaye naye alimpoka madaraka kabaka tena kwa kumtumia nduli huyuhuyu.
        Sasa inavyoonekana ni zamu yetu. Zamani tukiitana ndugu. Kila fyatu alikuwa ndugu wa mafyatu wote zama za mzee Nchonga (RIP SANA Nguli). Baadaye alikuja mzee Ruxa (RIP SANA Mwamba) kabla ya kuja kwa mzee Ben Nkapa (RIP SANA BRO). Baada yah apo alikuja BoysIIMen, na baadaye Jiwe (RIP). Katika awamu zote tano, mambo ya mafyatu kutekwa na kufyatuliwa na mafyatu wasiojulikana yalianza zama za jiwe. Hapa ndipo ulipomzizi wa kadhia hii ya ajabu na aibu kwa kaya iliyosifika kwa udugu, upendo, usawa, na mshikamano tena vya kupigiwa mfano. 
        Pamoja na mazuri yake kivitu, jiwe hakufanikiwa kiutu pamoja na kujiita mtetezi wa mafyatu wanyonge. Ni bahati mbaya, pamoja na ukali wake, Jiwe aliondoka bila hata kumnyaka mmoja wa wale waliojulikana kama wasiojulikana ingawa walikuwa wakijulikana. Kama wanaharakati huru ambao hawakuwa huru bali udhuru walijulikana, iweje wauaji wasiojulikana wasijulikane kwa lisrikal lenye kila aina ya wataalamu wa uchunguzi na udukuzi.
        Sina haja ya kumlaumu marehemu. Cha mno, historia huwa haina huruma wala upendeleo. Huripoti kitu kama kilivyofanyika au kutokea. Kwa muktadha huu, sasa najikita kwenye jinai, uchafu, na unyama wa kutekana na kutoana roho kwa mambo ya kidunia kana kwamba kuna atayeishi milele. 
            Ni kama tumekubali kutekwa na kugeuka mateka wa watekaji wetu. Je hawa ni nani, wanatoka wapi, kwanini wanaua mafyatu hovyo, wanatumwa, wanajituma, na nani anawalea hawa maafriti nduli wakubwa? Je vyombo vyetu vya uhasama, sorry, usalama, navyo viko wapi? Ndata wetu ambao mara nyingi wemejionyesha kushabikia na kutumiwa na chata fulani nao wako wapi? Je tunaanza kuwa na utawala wa kimafia bila kujua? Je tutaendelea kukubali kuwa mateka wa wahuni wachache hata kama wanaowatuma wanaweza kuwa na maulaji? Maana haieleweki mafyatu wanyotolewe roho mchana kweupe na hakuna anayeshikwa. 
            Je lisrikal liko wapi? Je nalo linahusika? Kwanini wanaotekwa na kunyatuliwa roho ni wa chata kimoja kati ya utitiri wa vyata vya upingaji? Je huu ni mchezo mchafu wa siasa? Je mafyatu wa kaya hii wakimbilie wapi? Je kasi ya lisrikal walilochagua na kulipa kodi kila siku ni nini? Je tuanze kulichunguza? Kwani, likijichunguza, hakuna atakayepatikana wala kujulikana. Kwa taarifa zilizopo ni kwamba kaya ishapoteza takriban mafyatu 80. Je wafe wangapi ndo wahusika wastuke na kutenda haki hata kusitisha kadhia hii?  Maswali ni mengi kuliko majibu.
            Yeyote anayewatuma, sababu zozote zinazowasukuma, yeyote anayewalea anapaswa kujua kitu kimoja. Wanaweza kumgeuka naye akajikuta kwenye wahanga sawa na wahanga wengine. Kabla ya kupinduliwa, Obote hakudhani kuwa uhuni lingekuwa tatizo lake wala jambo ambalo lingemfyatua na kumtemesha ulaji. Hivyo, nasi, tunapaswa kuwa makini kama mafyatu wenye akili timamu na tunduizi wanaoisoma historia na kujifunza namna ya kutatua baadhi ya matatizo kama hili la utekaji wa kaya na mafyatu wake. 
Haiwezekani mafyatu wafyatuliwe kila uchao halafu tunaambwa mambo poa. Hivi hawa wahanga wa utekaji huu siku watakapokengeuka hali itakuwaje? Mafyatu si wanyama, wadudu wala mataahira. Ni viumbe wanaobadilika na wasiotabirika. Hata hawa waliobadirikiana na kugeuziana kibao ni mafyatu kama hawa wanaofyatuliwa na hawa wahuni.
         Kwa vile huwa nasikia kuwa rahis wetu ni msikivu, si vibaya kumpa ushauri wa bure kuwa hali hii isipokomeshwa, uwezekano wa kuwachochea mafyatu ambao wanajiona kama wahanga wasio na mtetezi wala pa kwenda, kuamua kufyatuka na kuwatafuta hao wanaowateka ili nao wawateke waonje ladha ya dawa yao. Nadhani wanachosahau hawa watekaji, watesaji, na wauaji ni kwamba wao ni mafyatu tena wenye familia, ndugu, jamaa ambao wanaweza kujikuta katika ulipizaji visasi mbali na kutaka kukomesha hii jinai na dhuluma.
Kwanini tunaweza kupata ndata wa kuzuia maandamano au kukamata ng’ombe kwenye mbuga za wanyama lakini hawapo wakukamata watekaji au nao wametekwa bila kujijua? Uadui hata ugomvi wa kisiasa humalizwa kisiasa na si kihuni na kikatili hivi. Hii ni aibu kwa kaya yote. Je tumeishiwa kiasi hiki hadi tunatekwa na watekaji kiasi cha kugeuka mateka wa wawatekaji!?
Tumalizie. Chonde chonde msiharibu sifa nzuri ya kaya yetu. Maulaji yana mwisho. Na isitoshe, hakuna anatayeyafaidi wala kuishi milele. Kuna haja ya kujirudi na kuachana na uhuni wakati huu ambapo mnaweza kuwapa sababu ya baadhi ya wahuni na maadui wasiotakia kaya yetu mema kuanzisha machafuko na vita uchwara kama kule Somaliya. Tunfahamiana hapa? Hivi ni asubuhi au usiku? 
Chanzo: Mwananchi jana.

Friday 6 September 2024

Tumechatwa Hadi Tumechakatika Haswa


Juzi, mtukufu doktari rahis alipofyatua na kuchakata, viherehere, vibwengo, na visebengo waso adabu wenye wivu waliawashwa midomo wakafyatua yasopaswa. Alipowaweka kando njemba wawili waliozoea kupayuka bila midomo kuwasiliana na bongo, wapo waliompongeza na kulaumu kwa kutumbua majipu, kujivua magamba, na kutua mizigo. Hakika, mafyatu si binadamu kama wajumbe! 
        Alipochakatua na kuchakata kwarejesha wakongwe wabee, vibabu tena chakatwa badala ya gen Z. walianza, mara “anatuletea Gen Zees makapi.” Jamani, mnataka afanye nini mfurahi au kuridhika? Akiteua wakweze, mnasema ufamilia na ufalme. Akinyamaza kama chura, mnasema mwoga!
            Ukizungukwa na jalala, kila kikufaacho ni uchafu tokana na kuwa nyenzo pekee jalalani. Jikumbusheni profedheha mwenye jina kama kabundi kadogo aliyechemolewa jalalani na aliyemfinyanga kisiasa. Ukitumia nyundo, kila tatizo ni msumari. Ukizoea kunyonga, yanini kuchinja?
            Mnafyatuka eti kazi sasa ni kuchakata na kuchakatua hata maiti. Kazi ya urahisi ni nini? Akisafiri, mnazoza. Afanye nini wakati urahisi ni uungu mtu unaompa madaraka yaso mipaka kufanya atakalo akasifiwa hata akikosea? Akirejesha vibabu, yawahusuni? Mwataka ateue wajukuu zake au wapingaji kama Looter kule kwa jirani? Kwani, hamuoni?
        Nawashangaa.  Mshindwe na waregee. Kitu gani siyo recycled? Mmesahau, uchakachuaji, sorry, uchaguzi uliopita uliochakata hawa mnaowaita recycled materials? Ebo! Nani, mara hii, kasahau mchakato wa bao la mkono? Je huku siyo kuchakata tena kisiasa ambako nyie huita uchakachuaji? Ni uchakataji kuanzia chini hadi juu, juu hadi chini na kila kitu kimechakatwa. Sera hazitoki majuu? Shopping na wachukuaji siyo majuu?
        Kwanini tumegeuka kaya ya uchakataji aka recycled kaya? Mosi, ni ukosefu wa nyenzo aka materials zifaazo. Jiulize. Kisiasa, maadili yamegeuka madili na siasa sasa ni sanaa na usanii bila kusahau misifa na usifiaji hadi njemba nzima zinampigia magoti mja utadhani Mungu.                         Tumeishiwa sera nini? Sifa zinageuka sera na sera zinageuka maudhi, uongozi umegeuka uongo, ukale umegeuzwa usasa na usasa ukale. Tunazalisha pamba. Tunavaa mitumba. Tunasomesha na kuzalisha mitumba. 
        Hizi ni zama za kujihudumia badala ya kuhudumu, na kutumikisha badala ya kutumikia. Haki na stahiki vimegeuzwa hisani, ukweli umegeuka uongo, ubangaizaji umegeuka kazi, haramu imehalalishwa na halali imeharamishwa. Akina Yero wamegeuzwa wakimbizi Kayani mwao. Kwani, hamuyaoni jamani? Mnasema ujanja kupata? Mwataka nifyatuke vipi mnielewe muache kulalama mfanye kweli?
        Pia, kijamii, ni kuchakata kwenda mbele. Jitu jeusi ja mkaa linatoja tojo (tattoos) nyeusi likiigiza watasha. Mingine mibwabwa na misagaji. Kama haitoshi, siku hizi, imbaba mizima inavaa hereni, vipuri, miregezo, kuonyesha ‘undaweya’ chafu bila aibu, kusuka na kutoboa masikio mbali na miziki recycled na wanamuziki walochakatwa kiubunifu waharibuo maadili nasi tukishuhudia kana kwamba haituhusu? Mwachakatuliwa na kuchakatwa bila chekeche. Mwacheza chakacha!
            Kiuchumi, zamani ulikuwapo uchumi si uchumiatumbo. Tulikuwa na wachumi si wachumaji, wawekezaji wamegeuka wachukuaji, watawaliwa wamegeuka watu waliwao, wafadhiliwa wamegeuka wafadhili. Wezi wanalinda fedha na mbwa kulinda nyama. Mnalalamika nini wakipiga njuluku na kutajirika mkageuzwa makapuku na walalamikaji wasiochukua hatua? Mnadhani kuna wafadhili watakuja kuwakomboa? Thubutu yenu!                             
Jikomboeni. Uchumi mmeugenisha. Mmegeuzwa manamba kwa kisingizio cha kutengeza vibarua muitavyo ajira. Kwanini kutegemea ajira? Kuweni wabunifu mjiajiri na kuwaajiri hao wageni wanaowaajiri? Imefikia mahali Afrika inakodisha ardhi kwa wageni kuzalisha chakula kwa ajili ya watu wao kukwepa kukinunua kwa bei mbaya wakati inaagiza hata nyanya na mayai visa toka ughaibuni halafu inasema iko huru. Uhuru au udhuru?                                     Wanene  watanuaji wanatanua sirkal na mikanda wakati nyie mkiambwa mfunge mikanda. Mtakula lini au mwangoja muingie peponi ambako hamna uhakika mbali na kuingia bila midomo wala matumbo? Mla kala leo kesho kalani.
        Siku hizi, uchatakataji umevamia hata anga za kiroho na kugeuza uroho kuwa dili na dini. Zamani, tulikuwa na mashehe kwelikweli siyo mashehena waliosheheni uroho hadi wanauza mali za wakfu au kugeuka wapiga ramli na waganganjaa wa kienyeji. Msiseme nazusha. Kumbuka mwendazake alivyoshupalia kurejesha baadhi ya mali za baadhi ya wale ambao siwataji. Wamejaa wachungaji waliogeuka wachunaji kondoo waliopaswa kuwachunga. 
            Wanawatoza njuluku eti kuwapa huduma wakati ni hujuma tupu. Kwani hawapo? Hamkusikia zile kashfa za ngono? Hamuoni kuibuka utitiri wa manabii na mitume uchwara?             
    Zamani, dini ilikuwa huduma si hujuma. Siku hizi, imechakatwa nasi tukiangalia tu na kugeuzwa biashara ya mabilioni. Utapeli na mauzauza vinaiitwa miujiza wakati ni wizi itumiayo mijizi iliyojificha nyuma ya imani sawa na ile imani ya amani katikati ya vurugu, utekaji, ujambazi, upigaji njuluku za umma n.k. Kwani, hayapo? Nasi tumevamiwa.Tuna makanjanja wanaosaka bahasha badala ya habari wajaze mitumbo yao isiyotosheka.
            Nimalize. Muacheni bibie achape kazi, kutanua hasa usawa huu anapokwenda kusaka kura ya kula ili kuendelea kukamua. Mwenye wivu ajinyonge. Msitupigie kelele vinginevyo tutawasweka lupango kama akina Tunda Lishe aka lion na wenzake. Juzi, nilisikia akichangisha njuluku kutengeza gari lake. Kwani halikuwa na bima? Nimesemaje?
Chanzo: Mwananchi Jumatano juzi.


Sunday 1 September 2024

Hakuna Daktari, Mchungaji/Mganga wa Ndoa

Ndoa nyingi zimevunjika kutokana na wanandoa kutojiamini na badala yake wakaamini miujiza au ushirikina. Hakuna muujiza kwenye ndoa zaidi ya wanandoa wenyewe. Hakuna ushirikina unaoweza kuimarisha ndoa. Wahenga walisema; hakuna dawa ya mapenzi. Kama ipo si nyingine ni uaminifu, upendo, utayari, usiri, uwajibikaji, matendo, na maneno mema baina ya wahusika. 
        Tumeweka ushirikina na ushauri pamoja kutokana na uzoefu wetu. Tunajua. Kuna wanandoa walioishiwa hadi kuamini kuwa maombi, tunguli, n.k. vinaweza kuokoa ndoa ambazo wameziua tokana na ujinga na upumbavu wao. Tangu tumeoana, hakuna kitu tulichojiepusha nacho kama kuweka mambo yetu ya ndani siyo nje tu ya nyumba yetu bali nje ya chumba chetu cha kulala ambayo ndiyo makao makuu ya ndoa yetu. 
        Haiingii mtu yeyote humo isipokuwa watoto wetu wachanga tu. Siri za humo hazitoki hata kwa viboko. Hivyo, unapoanza kuingiza mashoga kwenye chumba chako cha kulala na baadaye kwenye kitanda chako ujue unamtafuta na kumtengeneza mchawi au wachawi wa ndoa yako. Tusisitize mambo makuu yafuatayo:

            Mosi, ndoa yako ni siri yako binafsi asiyopaswa kujua mtu yeyote. Ndoa siyo gazeti wala kitabu ambacho unaweza kusoma na wenzako. Ndoa yako ni siri kuliko hata nguo zako za ndani, maana huwa unazinunua au wengine kuzianika zikaonekana. Ndo ani kama moyo wako. Anayeweza kuuona ni daktari wako pekee na Mungu aliyeuumba.

Pili, chumba chenu cha kulala ni sehemu ya siri asiyopaswa kuijua wala kuingia mtu yeyote isipokuwa wawili nyinyi. Hivyo, wale wanaowaruhusu mashoga au wasichana wao wa kazi kuingia kwenye chumba chao cha kulala ni makosa makubwa.

Tatu, matatizo yako ya ndoa yanapaswa kutatuliwa na wawili. Kwanini iwezekane kuyatengeneza mshindwe kuyatatua? Ushauri wa mashoga na marafiki hausadii. Hawajui thamani ya ndoa yako. Na lolote baya likitokea, wao hawatakuwapo. Kitanda usicholala hujui kunguni wake. Hapa lazima usiri uwepo na si usiri tu bali hata hofu na kutomwamini mtu yeyote. Hata inapotokea ukapata ushauri, lazima uupime kwa kuangalia thamani ya ndoa yako na si mawazo ya aliyekupa ushauri. Kupewa ushauri ni jambo moja na kulifanyia kazi ni jambo jingine.

Hakuna anayefungwa na ushauri wa mtu yeyote. Kupanga–––tujue–––ni kuchagua. Unapopanga au kuchagua, fanya hivyo vizuri ukijua wazi. Ndoa yako ni sawa na kaburi. Tunatoa mfano huu siyo kwa sababu ya kukutisha. Tunataka upate ujumbe kama ulivyokusudiwa. Hebu piga picha mtu anapokufa. Kuna mtu anaweza kumsaidia kukaa kwenye kaburi lake? Msaada pekee hapa ni kumchimbia kaburi na kumuingiza wakimuacha mhusika aingie na kuishi kwenye kaburi lake. Unaweza kuugua au kuhisi njaa na kupata msaada lakini si kwenye kaburi. Samahani kwa kutoa mfano wenye majonzi ingawa ndiyo hali halisi.

Kitu kingine wanachopaswa kufahamu wanandoa ni mategemeo au matarajio yao. Wengi wanapofunga ndoa huangalia upande mmoja yaani wa kufaidi. Wanasahau kuwa­­­–––kama ilivyo katika nyanja nyingine za maisha–––kila kitu lazima kiwe na majaribu na mitihani mbalimbali yenye changamoto juu ya kujifunza namna ya kutatua matatizo. Hivyo, unapoingia kwenye ndoa, lazima uangalie pande zote. Ndiyo maana baadhi ya dini na mila hufundisha kuwa ndoa ni kifungo ambamo mhusika asitegemee vinono tu hata machungu. Hata hivyo, ikitokea mitihani, dawa si kuachana wala kukimbiana. Kwani unaweza kumkimbia mjuzi ukajikuta uso kwa uso na mamba. Hii maana yake ni nini? 

    Ni kwamba mwanandoa mzuri unaweza kudhani ni wa mwenzako kwa sababu kitanda usicholalia hujui kunguni wake. Kila binadamu ana matatizo awe hata rais au msomi wa kiwango cha juu. Huu ndiyo ubinadamu tunaopaswa kuukubali na kuufanyia kazi si katika ndoa tu bali katika maisha yetu yote. Maisha ni safari ndefu yenye kona, mabonde, mito, milima, vikwazo na hata lift.

Ni bora kuhitimisha tukisema wazi. Pig aua. Jua. Hakuna Daktari, mchungaji, mganga, fundi wa ndoa wala mwalimu bali wanandoa wenyewe kuwa tayari kuilinda ndoa yao, kujifunza, kufundisha, kujielimisha, na kuelimishana. Tumeyaona. Tumeyapitia.

Chanzo: Mwananchi leo.