The Curse of Salvation

The Curse of Salvation

Wednesday, 26 August 2026

Fyatu kugeuza Kijiji chake mji mkuu wa Fyatuland!


Baada ya kuonyesha umahiri usio wa kawaida kwa mafyatu wasiofyatuka na kumfyatua, Fyatu napanga kufyatua kitu ambacho kitamfyatua kila Fyatu diniani. Kwa wasiojua dili, wajue. Fyatu Mfyatuzi anapendwa sana na Mafyatu wote wa Fyatuland kiasi cha kuabudiwa, kusifiwa, kupendwa, na kuenziwa. Hivyo, kwa kuzingatia uzito huu, lazima nifyatue kitu. Napanga kufyatua amri ya kuanza kujenga kijiji nilichozaliwa cha Kifyatukizi kuwa mji mkuu wa Fyatuland ambao pia napanga kuiita Fyatu Mfyatuziland kwa hesima na ukumbusho wangu.
            Kuanzia sasa napanga kufyatua amri nyingine ambayo itahalalisha jina langu kupewa kila kitu kizuri na kikubwa. Barabara zote katika mji yote ya Fyatuland na madaraja makubwa na mashuhuri, vituo vya mabasi na vya treni vyote vikubwa lazima vipewe jina langu. Chuo kikuu pekee cha Fyatuland kiitwacho the University of Wisdom, Integrity, and Intellect (UoWiii) nacho nakifyatua na kukipa jina langu. Kuanzia sasa kitaichwa Dk. Profesa, Gwiji, Nguli Fyatu Mfyatuzi University (DPGNFMU).
            Baada ya kumalizana na chuo kikuu ambacho siku hizi kimegeuka choo kikuu, nafyatua mahospitali, mashule, na taasisi nyingine ambazo nazo zitapewa jina langu ili ziweze kuheshimika na kupendwa na kuabudiwa kama mimi. Pia, uwanja wa ndege wa Fyatuland utapewa jina langu ili kuongeza wasafiri wanaoutumia kwa heshima yangu.
            Baada ya kumaliza kuvipa jina langu vitajwavyo hapo juu, vitakavyobaki vitabeba jina la Bi Mkubwa wangu, Mama yangu, Dingi wangu, Shangazi zangu na hata vitegemezi vyangu.
            Kama haitoshi, nitafyatua na mbuga za waanimo ambazo zote zitapewa jina langu ili kukuza utalii. Bandari zote, maziwa makubwa, milima na mito mirefu na mikubwa, navyo vitabeba jina langu. Hii yote inalenga kukuza mapato ya kaya kwa kutangaza na kuuza jina langu tukufu. Naamini kuwa, kama ninavyozimikiwa, na vivutio hivi vitapendwa na kuvutia mafyatu wengi toka majuu kuja kushuhudia na kufyatua maajabu yangu.
            Najua yapo mafyatu mazuzu na mabishi yatakayopayuka na kufyatuka kuwa nageuza Fyatuland kuwa mali binafsi. Kwani, ni mali ya nani zaidi ya mimi? Mimi ni mwanzo na mwisho, chini na juu, kushoto na kulia na kila kitu cha Fyatuland. Mafyatu wanapaswa wafundishwe kujua ukweli kuwa Fyatuland iliumbwa kwa ajili yangu ambaye niliwapenda nikwaambia kuwa ni yao wakati ni yangu, familia, mashosti, na vitegemezi vyangu.
            Kwa ufyatu na ufyatuzi huu, usishangae siku moja ukikutana na mji au shule zenye majina ya ukoo wa Fyatu Mfyatuzi. Sambamba na kupandisha daraja kijiji chetu kitukufu cha Kifyatukizi, Hospitali kuu ya Fyatuland itaitwa Bi Fyatuwake Fyatu Mfyatuzi (BFFM).
            Lazima mafyatu wote, hasa wale wakumbaff na wabishi wanaopenda kuniponda badala ya kunipenda wajue kuwa mimi ndiyo katiba na sheria vya Fyatuland. Mimi ni zaidi ya mfalme kutokana na ubora wangu kama kiumbe aliye bora kuliko wote aliyeko hai baada ya kuondoka wale waliodai kuwa walitumwa na Sir God na kuwafyatua mafyatu wengi kwa kuwaahidi vinono ilhali wanaishi maisha machungu.
            Kwa vile Fyatu mie ni tofauti na hao juu, nafyatua utukufu wa kifyatu kwa kutangaza rasmi kuwa kijiji changu cha Kifytumfyatu kilichonifya kitaitwa sehemu takatifu kama zile za wale jamaa zangu hapo juu. Kwa hivyo, tokana na utakatifu ninaofyatua kwa kukipandisha kijiji changu kuwa jiji na mji mkuu wa Fyatuland, lazima kijengwe na kupanuliwa na kuwa jiji lenye kila aina ya maraha ili kuwafanya Mafyatu wayafyatue badala ya kungoja kuyapata watakapokuwa wamefyatuliwa na kuzikwa. Kwa Fyatu, pepo ni hapa hapa. Hii pia, italeta ubunifu na uwajibikaji wa kuwapa raha Mafyatu waliokubali mie niwe kiongozi wao.
            Pia, kutokana na ufanisi, utamu, na uzuri wa jina langu, kutakuwa na shahada vyuoni zitakazopewa jina langu. Mfano, shahada zote za uongozi, usimamizi wa fedha, sheria, sayansi ya jamii na nyingine zitafyatuliwa na kupewa jina langu. Hii inalenga kuwamotisha vijana kusoma sana kama mimi na kutenda miujiza ya kuwafyatua, sorry, kuwaokoa Mafyatu na Fyatuland kwa kujiletea, sorry, kuwaletea maendeleo yatokayo na uwezo wangu wa kufyatua miujiza.
            Wakati nikipanga kufanya mageuzi haya makubwa, kuna Fyatu mmoja mshauri wangu alishauri kuwa machinjio, magereza, na mochwari vikubwa vikubwa navyo vipewe jina langu. Kwa vile alitaka kuniuzi uzwazwa, huyu Fyatu nilimfyatua kwa kumuonyesha mlango. Hata hivyo, alinipa ujanja. Kwa vile mimi ni mwana demokrasia namba wani Fyatuland, hivyo, hapo juu vitapewa majina ya wapingaji ili nisifyatue kila kitu. Si inapendeza!!
            Kufunga kazi, vitegemezi vyote vitakavyozaliwa kuanzia sasa vitabeba jina langu na Bi Mkubwa kwa heshima na ukumbusho wetu.
            Naona yule anatikisha na kusonya. Ushindwe na uregee. Ukitaka kufyatua kama mimi fyatuka unifyatue uone nitakavyokufyatua. Hivi niko wapi na nafanya nini?
Chanzo: Mwananchi J'tano,leo.

Monday, 24 August 2026

Tusisingize ndoa kuzuia mabinti kujielimisha

Tuanze na usemi maarufu kuwa elimu ni ufunguo na elimu ni nyenzo inayoweza kuleta mageuzi ya kweli na kubadilisha jamii pakubwa kama alivyowahi kuasa nguli Nelson Lolihlahla Mandela. Kwetu binafsi, Nkwazi hakutaka kusomea shahada ya Uzamivu (PhD) lakini Nesaa alimghasi hadi akaamua kuisomea na kuipata. Kwa muktadha huu, juzi, kilitokea kituko kati ya vingi vinavyofanyika na kutoripotiwa au wahusika kushughulikiwa kisheria chini ya kisingizio cha mila na tamaduni.
        Kwenye kisa tajwa hapo juu, wazazi wajinga, wapumbavu, na wenye tamaa walitaka kumkatiri binti yao eti wakitaka wamuozeshe wapate utajiri. Ukiuliza ni utajiri gani huu na kiasi gani unaoruhusu na kuwezesha ukatili na unyama huu licha ya ukosefu wa ubunifu na uvivu, unashangaa na kuumia. Wazazi hawa laanifu wasioona mbele wala nyuma, walitaka kumuozesha binti kwa shilingi milioni nne na ushei! Yaani tumefikia pabaya hivi kiasi cha kumlinganisha binadamu na fedha zinayokuja na kupotea ilhali akabakia katika majuto na mateso visivyo na sababu zaidi ya ulafi, uroho, upofu, na tamaa?
        Kwanza, unapomuuza bintiyo kwa tamaa na upofu huu, unampa fursa aliyemnunua kwa kisingizo cha kumuoa kumtenza kama mali na kifaa alichonunua tena kwa bei mbaya. Unataka mamilioni ya fedha, unauza nini? Ni wangapi hujiuliza swali hili na mengine mengi au kuvaa viatu vya wahanga hawa wasio na hatia isipokuwa kuzaliwa na wazazi mafisi na wapumbavu wenye uroho usiomithilika? Je, hii siyo jinai inayopaswa kuadhibiwa vikali ili kutoa onyo kwa wengine wanaoshindwa kutafuta na kujikwamua toka kwenye umaskini kiasi cha kuishiwa na kutegemea mabinti zao kuwa chanzo cha utajiri uchwara?
            Pili, japo kuoa na kuolewa ni jambo la heri, hata hivyo, lifanyike kwa hiari na makubaliano kwa nia ya kuanzisha familia na si kuuzana. Baba unataka na kudai mamilioni ya fedha! Kwani bintiyo ni ng’ombe au shamba uuze na kujinasua kwenye umaskini?
            Tatu, wazazi mnapowauza mabinti zenu, licha ya kuwakatili na kuwadhalilisha, mnatoa mfano gani? Hizi siyo zama za ujima za kuuzana na kudhalilishana. Kumuuza mwanao kuna tofauti gani na utumwa uliopigwa marufuku duniani tokana na udhalilishaji, unyama, na ukatili wake? Binti wanaouzwa, wana tofauti gani na mbuzi au ng’ombe?
            Nnne, kwa mujibu wa gazeti la The Daily Monitor (Agosti 2, 2026) la Uganda, hali imekuwa mbaya nchini humo hadi rais Yoweri Museveni amelazimika kuingilia. Baada ya kupata taarifa kuwa kuna wazazi wanawauza mabinti zao kwa kisingizio cha kuozesha, Museveni alinukuliwa akisema “Wanyankole...ng’ombe 16...kwanini utake kutajirika kupitia watoto?”
            Tano, kwa vile hili ni janga linalokua si Uganda tu bali katika nchi nyingi hasa baada ya maisha kuwa magumu, tunatoa angalizo kama wandoa na wazazi. Msifanye watoto wenu kuwa chanzo au mtaji wa kupata utajiri hadi mnawauza na wengine, kuwakatisha masomo na kuharibu maisha yao ya baadaye kama kisa kingine kilichotokea hivi karibuni kule Shinyanga ambapo wazazi walitaka kumkatisha binti masomo kwa thamani ya shilingi milioni nne na ushee.
        Sita, hivi, mbali na ujinga hata upumbavu, tamaa na ukatili wa kijinsia, hawa wanaotenda jinai hii kweli wanajua thamani ya binadamu? Utashangaa kukuta hawa wanaotaka mamilioni, hawajawahi hata kumaliza kulipa mahali za wake zao.
        Saba, kabla ya kufikia uamuzi wa kumuuza mwanao, jikumbushe. Hivi, wanaawake waliofanya makubwa duniani kama vile Ellen Johnson, rais mwanamke pekee wa Liberia, Nandi-Ndaitwah (Namibia), Magreth Tatcher Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, na wengine kama hao wangelazimishwa kuozeshwa na kukatishwa masomo yao, wangeweza kufanya makuu waliyofanya?
        Nane, binti yako siyo chimbo la dhahabu wala nyenzo ya wewe kupata utajiri wa haraka. Ana haki na thamani sawa na binadamu yeyote. Mpe muda na uhuru wa kuamua ni lini ataolewa. Kwani, kuna usemi kuwa ukimuelimisha mwanamke, unaelimisha jamii nzima kwa ujumla. Tuna wanawake wafanyabiashara na wasomi maarufu nchini. Tujiulize. Kama wangeuzwa kama huyu binti wa Shinyanga, wangekuwa wapi?
        Tuhitimishe wa kuzishauri mamlaka zetu kuhakikisha jinai na kadhia hii inakomeshwa mara moja ili kuwanusuru mabinti waliopata bahati mbaya kuzalilwa na wazazi katili na mafisi. Pamoja na  ulazima na umuhimu wake, ndoa isitumike kama kisingizio cha kkuwakatili watoto wetu. Kesho ije kwanza na mengine yafuatie. Tuwape  haki ya kuchagua ima kuolewa au kujielimisha na si kuuzwa utumwani kwa kisingizio cha ndoa.
Chanzo: Mwananchi J'pili, jana.

Wednesday, 19 August 2026

Naunda tume tatu kwa mpigo kuchunguza tume

 
Juzi, Mafyatu walinikera sana. Si walidai eti nawachukia ndiyo maana maisha yao yamefyatuka kichwa chini miguu juu kwa shida na tabu. Utafiti niliofanya kwenye kanywaji umenipa matokeo yenye kutekenya akili. Nimegundua kuwa mafyatu wengi hawana raha. Hata wakipata kanywaji hawapati raha bali karaha. Kutokana na kadhia hii, napanga kuunda tume tatu kwa mpigo. Hii ni kusaidia mambo kadhaa. Kwanza, kuwafyatua mafyatu waamini nataka kusuluhisha matatizo yao. Pili, ni kutaka kuhakikisha wao wanajiona kama visababishi vya matatizo, mateso, shida, na taabu na siyo mimi rahis wao.
            Ili kufyatua kisawasawa wasifyatuke wakanifyatua, lazima niwafyatue kabla hawajanifyatua au hata kufyatuka wakajaribu. Tume ninazopanga kuunda zitakuwa ile ya kuchunguza kero, ya pili itakuwa ya kuchunguza tume ya kuchunguza kero, na ya mwisho itakuwa ile ya kuchunguza tume ya tume ya kuchunguza tume ya kunguza tuem ya kuchunguza tume ya kuchunguza tume ya kuchunguza kero. Naona yule anatikisa kichwa akidhani huu ni mkenge. Maana, haijawahi kutokea Fyatuland tume kuchungu tume na tume nyingine kuchunguza tume nyingine. Nikiona mkenge mafyatu hawaukwai huu mkeng, naunda ya nne, yaani, tume ya kuchunguza tume za kuchunguza tume za kuchunguza kero na kuchunguza zile za kuchunguza kero ad infinitum.
            Kwa vile Mafyatu hawaniamini kwa vile siwaamini, nitaarika marafiki zangu toka ughaibuni kuja kuchunguza kadhia zao zisizo na mwisho. Hapa, lazima washikaji wangu hawa wapinge njuluku ndefu ya mafyatu kudadeki! Maana njuluku ya mafyatu haiumi japo wao wanaumwa na kutofyatuka. Mifyatu inajifyatua kujiteka na kujitekesha halafu inalaumu ndata wangu. Mingine inajitoa roho nalaumiwa mimi. Kama wewe unapiga kanywaji hadi kanakufyatua akili nawe unajifyatua uhai kwanini unilaumu? Vitegemezi vipewa njuluku na maadui za Fyatuland wa kigeni vinaingia mtaani eti kunifyatua! Nikivifyatua, mnanilaani! Mlitaka vinivyatue siyo? Hafyatuliwi rahis hapa hasa mwenyewe anapokuwa Fyatu Mfyatuzi bingwa wa kufyatuka na kufyatua. Yeyote atakayejifyatua kunifyatua namfyatua kabla ya kunifyatua kama nilivyofyatua vile vitegemezi fyatu vya mafyatu uchwara.
            Hakuna kitu hunishangaza kama kufyatua mafyatu wasiofyatuka wakakufyatua wakaanza kulalamika na kulaumulaumu bila kufyatuka badala ya kujilaum kwa kutofyatuka wakati nguvu na uwezo wa kukufyatua wanavyosema hawafyatuki na kuvitumia. Hivyo, utawasikia wakilalamika kuwa hakuna njuluku na maisha ni magumu. Maisha magumu vipi wakati kuna njuluku ya kumwaga na kufyatuliwa na mafyatu wachache wanene wakati mafyatu waathirika wakigoma kufyatuka na kufyatua bali kuishia kulaani na kulalamika. Fyatukeni mfyatue muone kama hakuna njuluku tena zinazopigwa kila uchao na wachache wakati nyingi mkifyatuliwa na shida za kujitakia. Hil, nalo nitaulindia tume kulichunguza kujua ni kwanini mafyatu hawafyatuki hata wanapofyatuliwa.
            Utasikia fyatu limejifyatua au kumfyatua mwenzake roho halafu nalaumiwa mimi! Ebo! Kwani, nani alikuzuia kufyatuka na kufyatua wanaokufyatua badala ya kujiua au kuua wenzio? Wengi wa wanaojifyatua na kujitoa roho ni wakumbaff walioshindwa kuelewa inshu kutokana na kukosa ubunifu wa kujua kuwa jibu si kuwafyatua wenzao bali wale wanaowafyatua na kujifanya wanawapenda wakati wanawaponda. Nimesika vilio vingi kuwa maisha ni magumu! Magumu vipi wakati bila kufyatuka na kuwafyatua wanaowafyatua yatazidi kuwa magumu? Maisha ni rahisi na ya raha kwa mafyatu wanaofyatuka na kuwafyatua wanaowafyatua. Unalalamikaje maisha ni magumu wakati mvua zinavyesha, mito inatiririka, ardhi ipo ya kumwaga mbali na amani ya imani? Nenda kalime uone. Japo hii ni fomula, ukilima bila kujua anakula au kununa mazao yako, utanilaumu. Najua wengi wanafanya kazi tena kwa nguvu. Kinachokosekana na ufyatu wa kutojifyatua na kudai haki katika kila kitu kinachofanyika. Wakulima wanalima tena kwa sana lakini ajabu wanaotajirika ni madalali wanaowafyatua. Fyatueni madali muone kama hamtatajirika hata kuliko wao.
            Mafyatu yanachapa mzigo kama hayana akili nzuri lakini yanazidi kuwa makapuku. Guess what. Hata mfanye kazi vipi bila kufyatuka na kudai hata kuipoka haki, mtafyatuliwa muishie kulalamika hata kujiua na kuuana. Ni simpo. Fyatukeni muwafyatue wanaowafyatua muone maisha yatakavyo kuwa mukide kkkk. Na hili, nitaliundia tume ya kulichunguza na nyingine ya kuichunguza hii tume ya kulichunguza ilmradi inichunguze nikaifyatua kuzuia kufyatuliwa na wale ninaowafyatua tokana ufyatu wao wa kutofyatuka na kunifyatua hadi nawafyatua.
            Nadhani wengi wameishachukia kwanini siendi kwenye mada ya kuunda tume za kuchunguzana. Nafanya hivyo makusudi. Yote ni kwa sababu unapowafyatua mafyatu lazima uwazungushe na kuwachosha ili wachoke na kusahau. Kabla ya kuunda tume hizi tatu, mbali na nyingine nitakazounda kama zengwe halifatanikwa, nshaunda tume nyingine za kutaka kuwafyatua mafyatu wasinifyatue au kuamini kuwa niliwafyatua japo niliwafyatua. Hivyo, kuzungusha ndo mujarabu wa kuwapumbaza na kuwafyatua mkenge wasifyatuke. Nataka wafyatuane na kulaumiana badala ya kunifyatua au kunilaumu. Si inapendeza?
       Kwa vile bado nina masuala ya kwenda kundia tume za kuchunguza na kuchunguzana bila kunichunguza mimi, lazima niishie hapa kwanza niende kuunda tume za tume za tume za tume za kuchuuuzana, sorry, kuchunguzana. Tume lazima ichunguze tume na tume ziichunguze.
Kumbe hakujacha!!
Chanzo: Mwananchi J'tano Leo.
Dk. Nkwazi Mhango ni mwana kolumu wa Mwananchi na safu hii hutoka kila Jumatano.

Kabla ya kupanga mahari durusu sifa za waolewaji

Kuna mtindo mchafu umezuka wa kutafuta kupata utajiri wa haraka kwa njia ya mahari. Kwa lugha rahisi, huu ni uuzaji wa mabinti zetu tokana na ukosefu wa ubunifu na kufikiri. Japo mahari ni sehemu na hitajio la jamii nyingi kama shukrani kwa wazazi kuzaa, kulea na kutunza mabinti zetu tunaoozesha.

  Katika kudurusu dhana ya mahari, leo tutajikita kwenye mantiki na matatizo yatokanayo na dhana nzima. Tuanze kwa swali. Kweli binadamu anaweza kutathiminiwa na kupata thamani yake? Hatujui kama wale walafi wapendao kutoza mahali kubwa kama hujiuliza swali hili kabla ya kuweka kiwango kikubwa cha mahari ambacho siku hizi kimepanda utadhani kuna kinachouzwa na kununuliwa. Mfano, unakuta binti hajafundwa wala kulelewa vizuri halafu wazazi wanataka mamilioni ya fedha kama mahari! Wengine wanatoza makumi ya ng’ombe kama mahari ili kujitajirisha haraka.
            Tukizingatia kuharibika kwa dunia ya sasa na umomonyokaji wa maadili, unakuta binti lina tabia chafu, huni, na mengine mengi japo si wote lakini wazazi wanataka mamilioni ya fedha kama mahari. Kama tutakuwa wakweli, kuna wengine, kama mahari ni dili walipaswa kutolewa mahari ya fisi au nyoka na si ng’ombe tokana na ubovu na uoza wao. Kwanini wanaotaka kutajirika kwa mgongo wa mahari hawajui kuwa wanafanya maisha ya watoto wao na wa wenzao (waoaji) kuwa magumu!
            Baada ya wahusika kuweka ndani fedha au ng’ombe, binti akiteswa watamlaumu nani zaidi ya ujinga na tamaa zao? Watoto wetu siyo bidhaa tuwauze kwa tamaa, ulafi, na uvivu vyetu. Kinachoshangaza, ukiwauliza hawa wapenda mali kwa kuuza wenzao, wao walitoa mahari kiasi gani, utashangaa.
        Tukitafakari tabia za mabinti wetu hasa wale wenye tabia mbaya, wapo ambao mahari yao ilipaswa iwe fisi au nyoka tokana na walivyo hatari wachunaji wa mabuzi wanaotaka kujitajirisha  wao familia zao maskini kupitia ndoa bila huruma. Kwani, hawapo mabinti na wazazi wanatakao kutumia ndoa kama chimbo la fedha na utajiri?
        Kabla ya kutaka kuwatumia wenzako kujipatia utajiri wa haraka na haramu, jiulize. Ungekuwe wewe ndiyo muaoji, ungependa utenzwe hivyo ua ni yale ya mkuki kwa nguruwe? Kwa wazazi wanaopenda na kuwathamini mabinti zao na maisha yao ya baadaye, viwango vikubwa vya mahari ni jambo lisiloingia akilini hasa ikizingatiwa kuwa hao wanaowauzia hawa mabinti wanaweza kuwatesa kwa kisingizio cha kuwatolea mahali kubwa.
        Isitoshe, ukubwa wa mahari unachangia sana vijana wengi kutooa au kuolewa hadi wengine wanazalishana na kuanza maisha ya ndoa si kwa kutotaka kufuata taratibu bali kulazimika. Ndoa kama taasisi muhimu inalenga kuwakutanisha wawili wapendanao kujijenga na kuishi pamoja na si kukomoana na kunyonywa hata kuuzwa utumwani eti kisa mali na tamaa ya mali.
Ni aibu kubadilisha mwanao na fedha au wanyama. Wazazi tufikie mahali tukubali majaliwa yetu yatokanayo na juhudi, majaliwa, na mipango vyetu.  Pia, tukubali na kuelewa kuwa mabinti zetu, sawa na wanetu ni binadamu kama sisi wanaopaswa kuheshimiwa, kulindwa, na kuthaminiwa.
        Kabla ya kumaliza, tutoe funzo kuwa wote wanaotaka kutajirika kupitia mabinti zao wajifunze kwa Waislam ambao huruhusu binti kujipangia kiasi cha mahari ambayo, pia, si ya wazazi bali yake. Japo hili ni suala la kidini, lina funzo kubwa. Unapomruhusu bintiyo kupanga mahari yake, hawezi kumuumiza au kumchuna anayempenda na kuamua kuanza naye maisha. Isitishe, binti akiachiwa haki na uhuru wa kuchagua mahari, ataangalia mahitaji yake na mwenzake na mahari yake apewayo yaweza kuwa mtaji na nyenzo katika maisha ya ndoa anayoenda kuanza.
        Japo ni vigumu kwa binadamu kubadilika kirahisi na haraka, kuna haja ya kubadilika ili kuepusha mateso wakumbanavyo mabinti na unyonyaji wa wale wanaowao. Pia, tuchukue funzo na somo toka kwa mababu na nyanya zetu ambao mahari zao zilikuwa nafuu na vitu vilivyokuwa vinapatikana na kila mtu alikuwa na uwezo navyo. Mfano, wapo waliotolewa mahari ya jembe, mbuzi, mmoja na vitu vingine visivyomuumiza wala kumnyonya yeyote hadi watu kulazimika kukopa hata kuiba ili wapate mahari.
Chanzo: mwananchi J'pili iliyopita.

Wednesday, 12 August 2026

Wafyatuaji wafyatukapo wakifyatua nawe fyatuka wasikufyatue


Juzi, nilipiga kanywaji hadi kakanifyatua nikafyatuka nusu Bi Mkubwa anifyatue. Si mmeona wenyewe aina mpya ya ufyatuaji wa kulinda ufyatuaji kwa kufyatuana kinamna? Mafyatu wagomapo kufyatuka na kuwafyatua wawafyatuao, jua watafyatuliwa ile mbaya. Hii ni kutoa fursa ya wafyatuaji kufyatuka na kufyatuana ili wajenge mazingira safi ya kuendelea kuwafyatua mafyatu waliogoma kufyatuka na kufyatua.
            Katika kigwena kilichojiri hivi karibuni kule nonihino, nilishangaa kuona wezi wakifukuza wenzao ilhali lao moja. Sikujua kuwa fisi wanaweza kufyatuka na kufyatuana hadi mafyatu au tuseme kondoo wakajisahau na kuacha kuwafyatua wasiwamalize. Sijui tunaelewana?
 Ukiwa sehemu ya wafyatuaji wawafyatuao mafyatu ukajifyatua, unafyatuliwa kabla ya kuwafyatua mafyatu mnaoshirikiana kuwafyatua mafyatu wasiofyatuka. Ukipiga kelele, unafyatuliwa. Ukipingapinga hovyo, unafyatuliwa. Ukilaani, unafyatuliwa. Ukikataa kufyatuka na kusifia, unafyatuliwa. Hata wakati mwingine ukisifu kifyatufyatu bila busara unafyatuliwa. Ni kama ile hadithi ya njomba. Nyani akikruka, nchale. Akilala, nchale. Ni nchale kwenda mbele. Ni kufyatuka na kufyatuana mtindo mmoja.
            Yote katika yote, ufyatu upo wa aina nyingi. Upo ule wa kufyatuka na kupinga ufyatukaji na ule wa kufyatuka na kulinda ufyatuaji. Hata hivyo, ufyatu huu, uwe wa nia nzuri au mbaya, una gharama zake. Kama kenge akiingia kwenye kundi la mamaba, ajue. Atafyatuliwa akafyatukie mbali. Huwezi kuwa ndani na nje kwa wakati mmoja. Wala huwezi kupenda na kupenda sawia. Nani aweza kutegemea kupata kivuli kinene toka kwenye mti mwembamba? Hata ajifyatueje, fisi hawezi kuwa kondoo wala kondoo kuwa fisi. Ndoa ya samaki na ndege haiwezekani kwani waishi mazingira na maisha tofauti.
            Kadhalika, ndoa ya wafyatuaji na wafyatuliwao haipo na kama ipo lazima wafyatuliwaji wajue watafyatuliwa hadi wakome wasipofyatuka. Nani kakufyatua ukafyatulika kuwa maji na moto vinaweza kukaa kiti kimoja? Wafyatuliwaji na wawafyatuao wanaweza kukaa kaya moja iwapo wafyatuliwaji watagoma kufyatuka  hadi wakaruhusu wawafyatuao waendelee kuwafyatua kama ilivyo.
            Kwa vile wale waliofyatuka bila kufyatua wakaishia kufyatuliwa, tutegemee nini zaidi ya kufyatuliwa zaidi kwa sababu hamtaki kufyatuka na kuwafyatua watufyatuao na hata kufyatuana kwa vile tumegoma kufyatuka na kuwafyatua. Raha ya ufyatu si kufyatuka tu bali hata kugoma kufyatuka ukafyatuliwa. Linakuijia fyatu chafu likikuhimiza uwe msafi! Jingine linafyatua njuluku za mafyatu halafu linajifyatua na kutoa ahadi za kufyatua wezi! Hamuoni mifyatu inayowafyatua mafyatu na kula kwa mikono na miguu tena bila kunawa halafu linajifyatua na kuwafyatua mafyatu kuwa linawajali? Mengine yanawafyatua mafyatu na kujihudumia yakidai yanawahudimia mafyatu ilhali yanawafyatua!  Dunia hii japo gunia, imefyatuka na kugeuka ya ufyatuanaji.
            Hakuna kilichonifyatua, kunisononesha, na kunitisha kama kuona Mafyatu waliopaswa kuwa sauti ya wasio na sauti kuiingizwa kwenye ufyatuaji wa wale wasio na sauti. Yamejipa sauti ya kuwafyatua wasio na sauti. Hamshangai kuona fyatu lililobukua kuishia kujifyatua na kusema na kusifia hata uchafu? Hamjaona mafyatu masomi yakisifia maamuma ilmradi yapate fursa aya kuwafyatua mafyatu wengine wasiofyatuka na kufyatua?
Kama mafyatu wapaswao kuwatetea wasio na sauti yanajifyatua na kufyatukia ulaji uchwara uwaminyao na kuwanyima sauti wasio na sauti, sijui nani atawasemea hawa Mafyatu wasio na sauti waliofyatuliwa na Mafyatu wenzao waliopaswa kuwafyatua wafyatuzi? Ukiona jambazi na ndata wamefunga ndoa, jua umefyatuliwa. Ukiona wenye macho wanafyatuliwa na vipofu, jua wenye macho yatatobolewa ili msione huu ufyatuaji wa kunuka ambapo tumbo hufyatua kichwa na kichwa kikaacha kufyatuka na kulifyatua tumbo.
Nilishangaa kuona na kusikia mafyatu wawafyatuao mafyatu wakanona kama nune wakiwasihi mafyatu wafunge mikanda kwa vile mambo yamekuwa magumu. Kama kweli mambo ni magumu hivyo, hawa mafyatu wenye matumbo na makalio makubwa wanafyatua nani na nini zaidi ya mafyatu wawafyatuao kwa kuwahimiza wafunge mikanda. Kama kufunga mikanda ni dili na heri, kwanini hawa watufyatuao kwa kutuhimiza tufunge mikanda wasianze ili kuongoza kwa mfano? Ni uongozi gani anbapo kiongozi hukaa nyuma badala ya mbele? Msitugeuze meli na ngarawa ambapo nahodha huongoza kwa kukaa nyuma. Sisi si simaki kufyatuiwa tukijiona kwa kuwekewa chambo tena chambo chenyewe ahadi na maneno matamu. Jamani, maneno hata yawe matamu na mazuri kiasi gani, hayaliwi. Mengine yanatujia na maono. Hatutaki maono. Tunataka vitendo tena vinavyoingia akilini na si vya kujifyatua na kufyatua akili.
            Wakati wafyatuaji wa mafyatu wakifyatuana ilipaswa kuwa fursa kwa mafyatu kuwafyatua wakifyatuana juu ya kuwafyatua wao kwa vile hawafyatuki. Ni fursa ya fyatuaneni tuwafyatue badala ya kufyata kama mnavyolenga kutuaminisha ili muendelee kutufyatua kwa kujifanya mnafyatuana wakati lengo ni kutufyatua sisi tusiofyatuka na kuwafyatua tukabakia kufyatuana na kufyatuliwa. Kama wewe ni kondoo, ukiona fisi wanafyatuana, fyatuka haraka kabla hawajakufyatua. Ukiona adui wako anafanya makosa, usijifyatue na kumkosoa. Utampa fursa ya kukufyatua ufyatukie mbali.
            Nitamatike kwa kufyatuka kuwa ukiona wafyatuaji wakifyatuka na kufyatuana, nawe fyatuka wasikufyatue kabla hawajakufyatua ukafyatukia mbali.
Loo! Sasa naanza kufyatuka!
Chanzo: Mwananchi J'tano leo.

Sunday, 9 August 2026

Ukiona hivi, jua uchumi wa Fyatuland ‘umekua’kkkk!


Mtanange baina ya wanene na wanaojishaua kuonyesha mabulungutu ya njuluku mitandaoni una somo kubwa. Unafikirisha, kutekenya akili japo ni aibu na kiini cha ujambazi uliohalalishwa kwa mlango wa nyuma. Nani anapaswa kumaripia nani wakati wanene nao wanafanya hili? Tokana na kadhia hii ya kutaka misifa uchwara, ulimbukeni, na uzwazwa, Fyatu Mfyatuzi napanga kuanza kile kiitwacho kwa Kisambaa lifestyle audit. Hivyo, yeyote atayeonekana akijishebedua na kurusharusha njuluku hovyo kwenye matukio kama harusi, ubarikio, ufunguzi wa nyumba na mengine lazima anieleze amepataje hiyo njuluku ilhali Mafyatu walio wengi wanalia ukapuku.
            Kwanza, nitaanza na wanene wenzangu wanaohonga Mafyatu mchana kweupe wakichangia miradi iwe ni ya mahekalu ya kitapeli yaitwayo ya Sir God na mengine. Lugha za munene mkuu xyz anamwaga njuluku nataka ife haraka sana. Hizo njuluku kazipata wapi na vipi kama siyo kwa kupiga? Kwanini kila anayeukwaa unene anaanza kuwa na ‘huruma’ hadi kumwaga njuluku zetu kama vile ni zake? Mbona akina mzee Nchonga, pamoja na kukaa kwenye maulaji na kufanya makubwa, walikufa makapuku? Tunamdanganya nani ili iweje na kwanini?
 Tuanze na sisi wanene ili kuonyesha uongozi na uwajibikaji na si uongo na usanii. Lazima tuongoze tokea mbele na si nyuma. Je, njuluku tunayotumia na kufuja tunaipata kihalali au ni jinai inayoanza kuhalalishwa? Haiwezekani mafisi, mafisadi, na majizi yatukoge na mabulungutu ya noti ilhali wengi wanakufa kwa mabulungutu ya hasira na ukapuku. Lazima watueleze na tuelewe ‘miujiza’ wanayotenda hadi kuwa wakwasi hivi.
            Naona yule anatikisa kichwa na kusonya kwa ufyosi. Ukome. Tueleze tuelewe ulivyochuma hiyo njuluku mnayofanya ikose thamani kwa manavyoigawa. Nataka kuchukua hatua hizi madhubuti si kwa sababu ya husda wala wivu. Nachelea kuingizwa cha kike na wauza mihadarati, watakatishaji njuluku, majambazi, mafisi, na mafisadi wanaotuumiza na kujidai kutusaidia kwa kumwaga njuluku kwenye matukio ya kishakunaku na kilimbukeni.
            Hivi kweli inawezekanaje wakati huu ambapo mchizani Tarampu amesababisha kupanda bei ya wese na kuathiri kila kitu kupata njuluku ya kumwaga kama njugu? Kweli, mmejua kututenda! Kama nyinyi ni wakwasi na wakarimu hivi, kwanini hizo njuluku msizipeleke kunakostahiki? Hamuoni mahospitali na mashule yetu yalivyo kwenye hali mbaya?
            Tuache uzwazwa, roho mbaya na uroho. Utakuta jitu ambalo ni toto la kapuku lilololalia ngozi ya kondoo likijilimbikizia na kufuja mali za Mafyatu bila huruma halafu linajionyesha kwenye matukio uchwara kuwa lina njuluku na upendo! Mingine utaiona imejiwekea misafara mirefu ya ndinga na ving’ora ili kuepa misongamano liliyoisababisha kutokana na upofu, uroho, na ulimbukeni mbali na ufisadi na ukosefu wa uadilifu na ubunifu. Kwani, hatuwaoni? Mifyatu mifisi na mifisadi inaleta miradi ya kipigaji na kufanya maisha yawe magumu. Miundombinu yetu ni mibovu. Misongamano inazidi kutusonga hadi tunakuwa na msongo wa hasira na mawazo halafu inakuja mijizi na mijambazi kutokoga kwa njuluku zetu! Mkome kabla ya Mafyatu hawajakomaa, kufyatuka na kuwakomesha kwa kuwafyatua ili muache kuwafyatua kizwazwa.
            Licha ya kutaka kuanzisha lifestyle audit, nataka Mafyatu wafyatuke na kuuliza kama hawa wanaomwaga njuluku wanalipa kodi vilivyo. Pia, lazima Mafyatu wafyatuke na kujua kodi walipazo zinatumikaje. Je, zinaleta matokeo tegemewa na stahiki? Je, wahusika wanaweza kutuonyesha vyanzo vya ukwasi huu mchafu na wenye utata?
            Kwa vile mie ni profesa wa uchumi, nataka kuhakikisha Fyatuland haigeuzwi kaya ya ubishororo na ulimbukeni. Haiwezekani kaya kapuku inayoishi kwa kubomubomu na kukopa kopa ikawa na mabilionea wa kuibuka ghafla bin vu bila Fyatu mkuu kufyatuka na kuwafyatua. Natitachukua hatua zitakazowafyatua mafyatu kufyatuka na kufyatua wawafyatuao ili haki ifanyike na kweli ijulikane. Fyatuland haiwezi kuwa kaya ya kambale ambapo kila mmoja ana sharubu. Nitazikata hizi sharubu uchwara na zenye kutia shaka.
            Juzi, wakati fisadi mmoja mnene akipaki alionunua kwa kupiga njuluku za Mafyatu ndege alimnyea wakati akishuka. Kumbe na hayawani wanachukia ufujaji wanaofanyiwa Mafyatu wasiofyatuka hadi wanajirhusu kufyatuliwa tena kifala! Mtaani kwake, kila arejeapo, kunguru humzomea sana. Kumbe hata ndege wamefyutaka hadi kuchukia machukizo na makufuru wanayoshuhudia baadhi ya Mafyatu wakifanya kwa kutapanya njuluku!
            Kama haitoshi, kuna Fyatu alijifyatua na kuniita jizi na jambazi nambari moja kwa sababu alisema kuwa nina mamlaka ya kukomesha ujambazi huu wa wazi lakini sifanyi hivyo kutokana kuwa mshirika mkuu. Alihoji nashindwa wapi wakati taknolojia imerahisisha kwa kukamata ushahidi unaoweza kutumika dhidi ya wahalifu hawa wanaojifanya wanazo. Alinipa hadi clips zilizojaa mtandaoni zikiwaonyesha hawa majambazi wakimwaga njuluku. Aliongeza kuwa kuna majambazi yanashinda baa bila kujulikana yafanyapo kazi wala kazi yafanyayo lakini, kwenye sherehe, yanamwaga njuluku kama hayana akili nzuri.
            Nimalizie nikionya. Wote mliojijaza mitandaoni, naja. Akina Masunga kule Ngw’amapalala na Zanzui jiandae. Loh! Kumbe naweweseka usingizini!
Chanzo: Mwananchi Jtano iliyopita.

Kukosana katika ndoa yaweza kuwa fursa

Katika maisha yetu ya ndoa tuligundua kuwa hakuna kitu kinaua ndoa kama ukimya hasa wawili mnapokosana na kukaa kimya au kuepukana bila kuwa tayari kulikabili tatizo. Badala ya kuambiana makosa na ukweli, wengi, hununiana kiasi cha kila mmoja kukaa kimya na kuumia kivyake. Hii, licha ya kusababisha kukua kwa tatizo, husababisha hata magonjwa ya akili hata mwili.
Kuna kisa cha Ajak na Anyuak tulichiosimuliwa. Kisa hiki kinahusisha wanandoa wawili waliokosana na kukwepa kutatua matatizo yao kiasi cha mmoja kuishia kujuta na mwingine akiteketea huku kila mmoja akitamani angesema badala ya kujikalia kimya.
          Kama binadamu na wanandoa wowote, wawili hawa walikosana sehemu katika maisha yao ya ndoa. 
Kwanza, baada ya kuoana, waligundua kuwa wana tabia tofauti kinzani. Mmoja alikuwa muwazi na msemaji ilhali mwingine alikuwa mkimya na mwenye kuficha hisia zake. Hali hizi, licha ya kusababisha msuguano kitabia, ilisababisha kila mmoja kuanza kujifungia kwenye miili yao na kuteseka kimya bila kukabiliana na matatizo waliyosababishiana.
        Pili, baada ya wawili kukosana, walianza kununiana na kutowasiliana wakiamini tatizo lingejiishia. Lakini tatizo halikuisha bali kuzidi kuwa kubwa. Baada ya hapo, walianza kuepukana au tuseme kukwepana. Mwishowe, walitengana ndani ya nyumba yao na kuanza kuishi nyumba moja lakini vyumba tofauti. Katika ndoa, hii ni hatua na adhabu ya mwisho kwa wawili waliozoea kuwa kitu kimoja. Kutengana kimwili pia husababisha kutengana kiakili kiasi cha kila mmoja kumuona mwenzie kama mgeni na hata adui. Hivi kuna haja kufikia hatua hii hatarishi? Tutajibu baadae.
          Tatu, baada ya tatizo kuzidi kukua na mateso ya kisaikolojia kuongezeka, wawili waliamua kuachana wasijue kuwa halikuwa jibu wala suluhu. Wakiwa kwenye mgogoro wao, aliingia mtu wa tatu ambaye hawakujua kuwa alikuwa sehemu ya mgogoro. Punde, mtoto wao mkubwa aligundua tatizo lakini, naye kama wazazi wake, akaamua kukaa kimya asijaribu kuwakabili wazazi wake na kuuliza kunani. Hali hii ilimtafuna sana na kumsononesha sana hadi akajikuta amechanganyikiwa tokana na alivyowapenda wazazi wake.             Kufupisha hadithi ndefu, mtoto huyu alijinyonga nje ya nyumba yao baada ya kushindwa kukubali kuwa wazazi wake walikuwa wameachana na kila mmoja kuchukua njia yake.
Picha ya matukio hayo hapo juu inatuleta kwenye nini kifanyike.
        Kwanza, mkikosana msinuniane kwa muda mrefu. Kwani, si wa kwanza wala mwisho kukosana. Binadamu wote hukosana, hukabiliana, kukaa chini pamoja, au kuomba msaada na kutatua matatizo yao na maisha huendelea.
        Pili, kama kununiana kunawapa fursa na namna ya kutatua tatizo, nuniane kwa muda mfupi ili hasira zipoe halafu haraka sana muanze majadiliano ya kutatua tatizo.Wagombanao ndiyo wapatanao.
        Tatu, kabla ya kuchukua hatua za kununiana, ni vizuri mkajua kuwa ukimya au kukwepa tatizo ni gonjwa baya sana na madhara yake ni makubwa mno.
        Nne, mjue na kukikiri. Ndoa yenu si ya malaika wala mataahira wasiojitambua bali binadamu wenye akili na tabia tofauti. Hivyo, lazima mtakosana tu mtake msitake. Cha mno ni kukubali kuwa kukosana ni sehemu muhimu ya ubinadamu inayowawezesha kusababisha matatizo na kuyatatua tokana na aina ya matatizo na welewa wa wahusika.
        Tano, mjue kuwa kukosana ni fursa ya kubainisha tofauti na udhaifu wenu ambavyo huzaa ubora pale mnapoyakabili na kutayatua matatizo kwa njia zinazostahiki badala ya kukwepana au kununiana au kukaa kimya, kukomoana, au kususiana. Katika maisha, migongano na tofauti ni mambo yasiyoepukika. Hata njiwa, pamoja na kusifika kwa upendo, hukosana na kuyamaliza.
        Sita, mkikosana na kununiana msitegeane au kuviziana juu ya nani achukue hatua kwanza kuanza kutatua mgogoro kama wahusika hapo juu. Kwani, kunyamaziana au kuviziana ni ushahidi kuwa nyinyi ni wajinga ambao wanashindwa kujitambua, kutambuana, na kutambua matatizo yenu ili muyatatue.
        Saba, ni vizuri kujichunguza na kuchunguzana na kupeana mirejesho ili kujua aina na ukubwa wa (ma)tatizo ili muweze kuyatatua pamoja kwa haki na na ridhiko. Hapa, lazima muwe wakweli katika kueleza mnavyoliona au kulijua tatizo ili iwe rahisi kupata ufumbuzi baada ya kujua ubora, udhaifu, welewa, hata kutoelewa tatizo.
        Mwisho, msikimbiane mkidhani mnatatua tatizo wakati mnaliongeza ukubwa wala msifikirie kuumbana upya bali kujikubali kama mlivyo.  Fanyeni kukosana kwenu kuwa fursa ya kujuana na kusaidiana katika maisha ya ndoa.
Chanzo: Mwananchi Jpili iliyopita.