The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Tuesday, 30 June 2026

Tusiwacheke na kuwahukumu watalaka



Kawaida, wawili wafungapo ndoa hutegemea kuishi pamoja hadi kifo kiwatenganishe. Haya ndiyo maneno wasemayo katika viapo vya ndoa kwa wakristo. Kwa imani nyingine, hatujui. Hata kama hawatamki au kutamkiana haya maneno, tunaamini wote wanaofunga ndoa hutegemea kuishi pamoja maisha yao yote. Hapa, swali ni je, ni kwanini ndoa huvunjika japo si zote? Hili swali, japo ni fupi na dogo ni gumu na halija jibu moja.
            Tujuacho ni kwamba kudumu au kuvunjika kwa ndoa ni matokeo ya mambo mengi hata majaliwa, hasa wawili wanafungapo ndoa bila kujua wanachofanya japo wanaweza kujihisi wanajua wasijue hawajui. Pia, yapo mambo mengine mengi ambayo ni matokeo ya matendo au tabia za wahusika. Hivyo, kudumu au kutodumu kwa ndoa ni mkusanyiko wa mambo mengi makubwa na madogo.
            Tokana na uzoefu, kitu tunachoweza kusema ni kwamba wanaojenga ndoa ndiyo hao waidumishao au kuibomoa. Mfano, wawili wanapofunga ndoa, hufikia uamuzi huu wao peke yao tena bila shuruti. Hivyo, kila matokeo ya ndoa huwategemea wao. Hata hivyo, pamoja na kuamua wenyewe peke yao, wapo baadhi ya ndoa ambao huigeuza ndoa kama klabu au ushirika. Hii maana yake ni nini? Bahati mbaya, wahusika huwaruhusu wasiohusika kujihusisha na ndoa yao. Kimsingi, wawili husahau kuwa ndoa ikidumu au kuvunjika, wanufaika au waathirika ni wao na si hao waliowahusisha.
            Katika suluhisha migogoro mingi ya ndoa au kushuhudia zikivunjika, tumejifunza mambo makuu manne.
Mosi, wote huumia hata kuumizana tokana na pigo au hasara wanayopata tofauti na walivyotegemea wala kupanga. Asikudanganye mtu kuwa anaweza kuacha au kuachika akasherehekea japo, siku hizi, kumezuka uongo wa walioachika au kuacha kujifanya wanasherehekea. Ndiyo, wanaweza kutuonyesha kuwa wanasherehekea usoni. Ila nyoyoni wanaumia. Hili, halina mjadala. Jiulize. Walipofunga ndoa walihuzunika au kufurahi? Jibu liko wazi. Sasa inakuwaje waathirika hawa washerehekee hasara na pigo kubwa kama hili?
            Pili, wote uhisi hasara na hata mapungufu. Kwanini wengine waweze sisi tushindwe? Binadamu, kiasili, anapenda mafanikio na kuchukia maanguko. Hivyo, ndoa inapodumu, wanandoa huona fahari na furaha. Ikivunjika, hata wajikaze vipi, maumivu tena makubwa yapo. Kwanza, kuna wasi wasi wa namna jamii inavyowaangalia. Pili, kuna malengo na matarajio yaliyouawa. Na tatu, kuna aibu ya kushindwa tofauti na ridhiko la kufanikiwa. Mara nyingi, wengi walioacha au kuachwa hasa wenye watoto, hushindwa kuwashauri watoto wao juu ya ndoa kwa vile wao walishindwa.
            Tatu, ipo jamii inayowazunguka. Hapa, ndipo kichwa cha makala hii kinapoingia na kugusa pabaya. Wengi hasa wasiojua uhalisia wa ndoa wanaweza kuwacheka na kuwaona wanandoa ambao ndoa yao imesambaratika na kuvunjika kama watu walioshindwa. Hapa ndipo tatizo la kuwacheka wahusika au kuchekwa linapoanza. Kama tulivosema, wanaovunja ndoa ni wanandoa wengine wakisaidiwa na wasio wanandoa kwa namna mbalimbali. Je, kuna haja ya kuwacheka au kuwaonea huruma?
            Nani anajua kesho yake au nani ni mkamilifu kiasi cha kuwacheka wengine badala ya kuwaonea huruma na kuwasaidia? Kabla ya kuwacheka, vaeni viatu vya wahusika. Jiulize swali moja kuu japo dogo lakini lenye mafunzo makubwa na mengi “je, ingekuwa mimi, ningetaka wenzangu wanifanyie nini au kunichukuliaje?” Tuwe na huruma na utu. Badala ya kuwacheka wanandoa, tushukuru Mungu kuwa hatupitii wanayopitia. Tujifunze kitu toka kwao badala ya kuwabaghaza, kuwacheka, na kuwasimanga. Kwani, hujafa hujaumbika na kutenda makosa ni asili ya binadamu.
            Wanandoa ambao ndoa yao imevunjika ni kama wagonjwa. Hakuna haja ya kuwalaumu wala kuwasimanga bali kuwaonea huruma au kuwasaidia. Hakuna anayependa ndoa yake ivunjike japo wahusika wanavunja ndoa yao tokana na ujinga juu ya mambo fulani fulani yawe ya kimalezi, kitabia, kimahusiano, kiuchumi, kitaaluma, ubinafsi, uchoyo, upumbavu, hata kutojali mambo fulani fulani kwa wakati fulani.
            Tumalizie kwa kusisitiza kuwa kuwacheka wanandoa walioachana si kuwatendea haki. Maana, kitanda usicholalia hujui kunguni wake. Ni rahisi kuhukumu, kulaumu, hata kutweza. Je, ushawahi kujiuliza? Ningekuwa mimi, ningependa nichukuliweje hasa kipindi hiki kigumu na pigo kubwa katika maisha?
Kwani, si wote wanaoacha au kuachika huoa au kuolewa tena. Tuwaoneeni huruma watu hawa.
Chanzo: Mwananchi Jpili juzi.

           

Wednesday, 24 June 2026

Fyatu afaidi IEFUDI kwa raha zake!

Juzi, nikiwa napata kalaji si nikajifunza kitu. Kwanza, nilikasirika nusu niue fyatu. Nilichanganyikiwa hadi nikachanganyikana! Nikiwa ndo nimerudi kupata, si akaja afisa wa mamlaka ya kuibiana. Kumbe kuna jirani yangu mnoko alinichoma. Si niliuza vikuku vitatu tena kwa bei ya kutupa. Loh! Jamaa kanijia nyumbani eti kutaka nimuonyeshe IEFUDI . Nilimuuliza IEFUDI  ni mnyama gani. Hakujibu zaidi ya kunitisha kuwa lisrikali litakamata kuku wangu waliobaki hadi nionyeshe IEFUDI . Bila ajizi, nilimuomba naye anipe hiyo IEFUDI yake kama siyo ukosefu wa ubunifu, ujambazi na wizi vya kichovu.
            Kwa uzwazwa wake alinijibu kuwa mie nilikuwa nani kumtakisha  IEFUDI  wakati yeye ndiye hiyo IEFUDI . Nilizidi kumchanganya. Niliuliza hilo lisrkali lake mbona halituonyeshi IEFUDI  linapopata misaada na kukopa likaihomola na kuondomola. Niizidi kumzonga anieleze nielewe kama wapigaji wa njuluku ndefu inayofichuliwa kila mwaka na KAG (Kagua, Aibisha, na Kuufyata), nao, wana hiyo IEFUDI . Jamaa zwazwa kweli. Si lilianza kupayuka utadhani kaya ya Fyatuland ni mali ya baba au mama yake. Baada ya kuona rongorongo zimezidi, nililipiga mkwara kwa kupiga simu ya mshirika wangu wa bedroom nikijidai ni mwanasharia wangu ili alishitaki na waliolituma.
            Huu ujambazi na wizi wa mchana umeniudhi sana. Mbona pale kwa Gabacho wanauza bidhaa zilizoisha muda wa matumizi. Je, hawa wa IEFUDI hawaoni haya au wanatuchukulia ufala na uzwazwa? Nani hajui kuwa Fyatuland ishauzwa zamani gani au wanataka kutuuza baada ya kutuchuuza? Mbona misongamano imezidi hadi makaburini? Je, kazi ya lisrikal ni nini au ni kutupiga Mafyatu wachovu? Kweli, wamejua kututenda na kututenza. Kuanzia leo, nataka kujua mwenye kaya kati ya wanakaya na walakaya ili kijulikane. Kama mbaya mbaya. Fyatu anaanzisha genge. Kila jizi, tena bila aibu wala adabu linakuja kudai sijui tozo la nini, sijui IEFUDI sijui utopolo na upuuzi gani. Je, namna hii twaweza kuendelea au kuendelea katika kutoendelea?
            Ngoja nizoze kiprofesoo. Hivi, tumeishiwa hivi kiasi cha kuhangaishwa na mafyatu wadogo na vitu vidogo wakati uchumi tunao tunaukalia na wachukuaji wanakuja na kujizolea? Je, Fyatuland siyo shamba la bibi tena bibi mwenye kipofu na taahira? Basi, tubadili jina iitwe Shambalabibiland kijulikane. Ajabu ya maajabu, hii mijizi inayokuja kutunyima raha haijui hata hiyo njuluku inatafutwaje. Kazi, kuja kutughasi na kutuibia. Nasi Mafyatu tuna dhambi. Kwanini tunakubali wizi huu wa nchana? Hii njuluku wanayozoa na kupiga wanaifanyia nini? Kazi yao ni nini au wanatugeuza kuku na mbuzi? Kwanini tujirahisi na kukubali kunyonywa hivi na chawa, kunguni, funza, luba, na wadudu wengine ambao siku hizi wamenenepeana wakati twakondeana? Hivi, nani alituroga  hadi tukajihisi wageni kwetu?
            Hapa, naongelea IEFUDI . Bado madude mengine ya kimchoromchoro yaliyotamalaki. Ajabu, haya machawa na ma IEFUDI yanayotunyonya na kutuuma yanajiita matumishi ya umma! Ni matumishi ya umma au ya kuuma Mafyatu? Kama unaona mimi kufuga vijikuku vitatu na kuuza nawe ukanijia na hizo IEFUDI  zako, jaribu ufuge uone cha moto. Huwa siachi kuudhika na kushangaa. Hii soma kimya kimya. Juzi, si kuna changu kaniuzia dhambi zake. Baada ya kumaliza kanchezo si alitaka nimpe ujira wake. Sikupinga wala kubisha. Nilimtaka anipe IEFUDI  yake ili nimlipe na kunipatia risiti. We! Hilo zegere, usipime. Dada wa watu alinifyatukia na kunitukana mitusi ya nguoni kama hakuwa na akili nzuri. Baada ya kumalizana aliponitishia angekwenda kudai kwa bi Mkubwa wangu, nilimlipa na kutoka nduki kama kibaka aliyekwapua cheni pale Migomigo.
Tuache utani. Kama ni hivyo, ili kutenda haki, na wala rushwa wakipokea mlungura lazima nao wawe na IEFUDI s na kutoa risiti. Badala ya kudai haki eti tunafundishwa kudai risiti wakati wanaosimamia hizo risiti nao haawatoi risiti. Uko wapi usawa na haki hapa au navyo vinaendelea kuwa machukizo mbele ya majizi wanene?
            Pamoja na kuichukia IEFUDI, siku hizi naanza kuipenda badala ya kuiponda. Kwani, nakata kanywaji bila kulipa. Nikiletewa vyupa,  navipiga kwa raha zangu. Baada ya hapo, akija muuzaji, namtakisha IEFUDI ili anipe risiti. Hivyo, hivyo, nimepiga kalaji dezo hadi wauza wakagutuka. Siku hizi, nikiingia tu na kuagiza, wanataka nilipe kwanza. Huwa nawatakisha IEFUDI. Maskini wengi hawajui hata hiyo IEFUDI ni nini! Hata niendapo kwenye vyoo za kulipia, huwa nadai wanipe IEFUDI . Huu ndiyo uzuri wa IEFUDI kwa wajanja kama mimi.
Hayo tuyaache. Kama ni lazima kuwa na IEFUDI s, basi, na wanene watoe risiti wanapokwapua njuluku za Mafyatu waliogoma kufyatuka wakawafyatua wanaowafyatua kila uchao. Bila kufyatuka na kufyatua, Mafyatu watafyatuliwa hadi waone kaburi. Hivi, hawa wanaotuuzia ulabu, nao wanazo IEFUDI? Haya si mmbo ya nchezo wala uchonganishi na uchocheaji bali jiani iliyohalalishwa na kuwa nyenzo ya wachache kutupiga na kutuumiza. Kesho, mtatwambia tutoe hata risiti za marehemu wetu waliozikwa miaka mingi iliyopita.
            Sina ugomvi na kukusanya njuluku na mapato. Je, Mafyatu wananufaika vipi na hayo mapato wakati kila mwaka KAG anaibua kashfa ya upigaji wa njuluku ndefu na majizi hayakamatwi wala kushitakiwa? Hapa, hatujaliwa tukijiona kweli? Tunahitaji sana kufanya mapinduzi ya kifikra. Hivi, naota au naweweseka!!! Kkkkkk!
Chanzo: Mwananchi leo Jtano.

Friday, 19 June 2026

Onyo Mafyatu wanaohoji ulaji na uhalali wangu


Kuna mafyatu katika kaya yangu ya Fyatuland waliofyatuka kwelikweli hadi wanataka kunifyatua kabla sijawafyatua. Siku hizi,  mafyatu wangu wana kamchezo ka kunifyatua bila aibu wala sababu. Si juzi, kajitokeza mmoja aliyetaka kunifyatua na kunivua nguo tena haradhani akiongelea mambo ya kale. Hakujua kuwa ya kale yananuka hata kama yaliwahi kunuka baada ya mafyatu kukinukisha. 
            Kwa vile nilikuwa na inshu nyingi kwenda zangu ughaibuni kutanua na kujinadi, nilimlia pini. Si kwamba nilimgwaya. Never. Muache. Ngoja nipoe. Lazima nnitamfyatua ashike adabu na adabu imshike akome na kukomaa. Senzi kabisaka. Akizidisha kiherehere na kiranga chake, namfyatua kwa kumtumia wasiojulikana wamshughulikie kwa vile anajulikana. Hapa lazima nimpopoea kabla ya kunipopoa. Akishupaza shingo, namslowslow polepole na anapotea milele. Anacheza nami! Inaonekana hanijui vizuri.Anadhani upole wangu ni woga asijue mie ni katili hakuna mfano.
Wakati akizoza, nilimuuliza tena kwa upole ‘manapata wapi jeuri kuhoji wasiohojiwa au kutaka kuwafyatua wasiofyatuliwa ila kuwafyatua nyinyi mafyatu ambao kumbe mkifyatua ni hatari eeh? Nadhani hawa wanatumwa na mabeberu waje kunibeberu wasijue mie siyo mbuzi jike bali  beberu lenyewe tena la kunuka na kukinukisha. Akawaulize wale wahuni waliojifyatua wakataka kunifyatua nikawafyatua wakasahaulika. Hawa mahuluku taabu wana taabu, we acha tu.
    Ngoja niwape inshu nzima. Tulikuwa na uchaguzi wa ndani siku zilizopita ambapo nilishinda baada ya wanoko fulani kutaka kuniengua nikaishia kuwaengua na kujisimika na kushinda kwa kishindo na vishindo na kuwaacha solemba. Baada ya kuona walitaka eti kugombea nami, nikaitisha kikao cha chata changu cha Chata cha Mafyatu (CcM) wakanipitsha bila kutaka pale walipotaka nitoke nje eti wanichinje nikagoma nao wakagwaya na kuniptisha bila kupingwa. 
    Tokana na kuwafyatua mafyatu waliotaka kunifyatua, si kuna mafyatu waliojitokeza kunipaka matope. Si walihoji kuwa nilishiriki uchaguzi sijui uchakachuaji sijui uchafuzi, wala sijui. Kwanza, walitaka eti yapelekwe majina kadhaa kwenye kamati kuu inikamate! Kuona hivyo, nilichenji gea angani na kufyatua taratibu zote za chata letu. Badala ya kufuata katiba, niliamua kuifyatua na kuwafyaulia mbali hadi nikashinda ulaji kihalali na kwa kishindo japo mafyatu adui wanadia kuwa nilishinda kwa fujo, ukatili, na mambo mengine ambayo sitaki kuyarudia. Unawezaje kushinda kwa asilimia 1000 kama kweli kuna kamchezo ulifanya? Mie napendwa na kukubalika bwana. Hata kama ndege na wadudu wangeruhusiwa kupiga kura, wangenichagua mimi chaguo na kipenzi cha Mungu Dk. Dk. Dk. Daktari, Profesa, Shehe, Askofu, Field Marshall, Jenerali, Al haj, Mtakatifu Fyatu Mfyatuzi Esq n.k.n.k.
    Ilibidi nijiapishe mwenyewe tena kwenye chumba chetu cha kulala na bi Mkubwa. Waweza kuamini? Wengi walizoza na kusema eti haya yalikuwa maajabu na matokeo ya uchakachuaji. Kwani, niliwazuia wasichakachue? Walitaka niapishwe kwenye uwanja wa mpira wanipopoea kwa mimawe nami niwaslowslow kama siyo kuwapoteza. Mie ni mtu wa Mungu na mcha Mungu hakuna duniani isipokuwa mimi. Kawaulize wale mashehena wanaonijua. Si waliwaasa kuwa baada ya kuumbwa mwana wa Maria na Ntume, hakuna kiumbe bora mwingine aliyeumbwa isipokuwa Fyatu Mfyatuzi mjukuu wa Mfyatuko? Walidhani hawa wanaweza kuongopa?
    Baada ya kuwazidi kete mafyatu uchwara nilisikia wakilalamika. Mara chata kililazimisha mgombea wake wa urahis hata kwa kuvunja na kuvuruga kanuni zake chenyewe. Eti chata letu lilipoteza njuluku na muda kutupigia makelele kwa kisingizio cha kampeni za uongo na vitisho. Wamezoza na kuzua mengi. Mara eti chata letu linadai linadumisha amani kwa kuivunja tena kwa miaka mingi tena kwa kuongoza kwa fujo. Ebo! Bila fujo waweza kuongoza au kuongozwa? Wanadai ninawaminisha kuwa nitatenda haki wakati ni bingwa wa kudhulumu, kuteka, kupoteza, na kuua. Wanadai najiridhisha kutaka kuwaridhisha kuwa nilivyofanya ni sawa.  
        Nalaumiwa kwa kusifiwa na kujisifu hata ninapostahili kulaumiwa na kulaaniwa! Ebo! Hamjaambwa raha jipe mwenyewe? Nisipojisifu, nani atanisifu? Nilizuliwa eti nawanyanyasa wapingaji wangu. Ebo! Mlitaka niwaache waninyanyase hata kupoka ulaji wangu wa dezo!  Nani yuko tayari kufua nguzo zake za ndani hadharani tena mbele ya maadui zake huyo? Japo mafyatu wanasema niko uchi nikijidanganya nimevaa, nasema sibadiliki.
Hakuna umbea na urongo vimeniudhi kama kudai niligombea na kivuli changu. Walitaka nigombee na nani wakati wao ndiyo vivuli vyangu? Si wapo waliosusa sie tukajitwalia na kujilia wakabaki kulalama na kulaani wakidhani kelele za chura zinamzuia nguruwe kunywa na kunya kwenye kisima. Lo! Imkula kwao.
Kwa vile naipenda sana Fyatuland kiasi cha kuwa tayari kuua, sorry, kuuawa kwa ajili yake, sitasikia kelele za vyura. Naendela kukandamiza na kutanua na kutesa wakati mafyatu wanajifyatua na kulalamika wakati mie nazidi kuziba masikio.
Kwa hiyo, natoa onyo la mwisho. Komeni kuniandama. Nendeni mkaandamane mkione cha moto. Kula na kutesa ni kwa zamu. Ngojeeni zamu yenu. Tumeelewana? Lo! kumbe nililewa chakari hadi nikalala mtaroni!
Chanzo: Mwananchi Jtano juzi.

Wednesday, 10 June 2026

Fyatu aanzisha vita ya ‘lapdogs’ na Tarampu


Baada ya mtanange wa ghuba ya Ua Jeni kukaza, si Tarampu akajifyatua ufahamu na kuanzisha vita ya lapdogs na Fyatuland! Japo Tarampu ni fyatu uchwara, si aliwafyatua lapdogs wangu eti wasiende majuu kujienjoi! Nilipata habari hii mbaya nikiwa pipani nikielekea majuu kwa Put in. Nsharejea wanoko msianze kutafuta mambo yangu na kunifyatua. Sikujua kuwa Tarampu anafyatuka vibaya. Si aliamua kuwafyatua lapdogs eti kwa vile walirarua wanakondoo! Alisema wasikanyage Umarekanini! Nilishangaa sana. Kwani, wanakondoo wangu wanamhusu nini yarabi? Kutaka sifa na kukimbia kipigo cha maajemi si Tarampu akajifyatua na kuwafyatua bila kujali kuwa wanafanya kazi zangu! Ukijifyatua na kunichokoza au kutaka kunifyatua, nawaamuru wakufyatue haraka sana.
Kwa vile mie ni Fyatu zaidi ya Tarampu, nilimuonya. Kama ataendelea na ufyatu wake uchwara, nitazuia wake kuingia Fyatuland. Akiendelea nampiga marufuku hata yeye kuingia Fyatuland. Mambo ya Fyatuland yanamhusu nini au anadhani mie ni kama Maduro aje animaduro? Athubutu aone kilichofanya ngamia kuwa na nundu. Shauri yake.
Nimegundua kuwa Tarampu ni mwoga wa kaiwada na bingwa wa mikwara uchwara. Huenda anatingisha kibiriti kwa kutumia vita ya lapdogs ili anifyatue au anaogopa kunifyatua. Vinginevyo anataka kunitia kashkash ili apata namna ya kuifyatua Fyatuland kama alivyoifanyia Venezuela. Maana, haiinigi akilini ang’ang’anie kufyatua lapdogs ilhali mwenyewe nipo. Najiuliza bila majibu. Inakuwaje?
Huwezi kung’atwa na chawa ukawalaumu zaidi ya yule aliyewafuga au kuacha kuwateketeza. Mnaninyaka hapa? Imenishangaza sana. Eti dogii kuwararua wanakondoo anaadhibiwa bila kujali nani alimwamuru awararue! Kwani kazi ya dogii ni nini kama siyo kuwafyatua wengine kwa amri ya mwenye kumfuga? Nadhani amewaonea wivu lapdogs wangu niliowalisha wakanenepeana wakati wake wanakondeana. Kama siyo hivyo, basi uzee unamuijia vibaya. Haiingii akilini. Unamuadhibuje mbwa na siyo mwenye mbwa? Kweli, hii ni haki? Wahenga waliasa kuwa ukimuona dogii, jua kuna mwenyewe. Na dogii hafanyi kitu bila amri ya mwenye kumfuga. Inakuwaje unamwadhibu mbwa na kumuacha amfugaye? Kwanini kumfyatua mjumbe wakati aliyetuma humfyatui?
Sasa natangaza vita. Natangaza vita ya wanene na siyo  guard dogs wao. Kama ataendelea kubwekabweka, nitamfanyia kitu ambacho hajawahi kufanyiwa Fyatu yoyote. Huwezi kuwaandama lapdogs wangu nami nikakuacha. Hapa, Tarampu ajue. Tutafyatuana hadi kieleweke.
Inaonekana wadukuzi wake ni wavivu wa kufikiri na kudukua. Kama hajui ni kwanini wanakondoo walifyatuliwa na attack dogs wangu si aniulize nimpe inshu nzima badala ya kutishiana kufyatuana na asifyatuke na kufyatua. Kwanini Tarampu hataki kukubali kuwa wanakondoo walivyatuliwa kwa sababu walitaka kujigeuza mbwa mwitu halafu wanifyatue?
            Kwanza, namjuza Tarampu na wengine wanaojifyatua ufahamu. Wajue na wakome na kukomaa. Lapdogs wangu si washari. Ukiona wamewafyatua wanakondoo, ujue kuna kitu wanakondoo walitaka kufyanya. Maana, haiingii akilini kuwaacha wanakondoo waliozoea kuishi kwa amani kujigeuza mbwa mwitu. Ili iweje kama siyo kunifyatua mie mwenye kuwatunza?
            Pili, namuonya Tarampu na wenzake wanaodhani wanaweza kunifyatua. Najua. Wameanza na lapdogs wangu ili baadaye nifuate. Sitakubali. Tarampu, who are  you? Kama wana kondoo wangekuwa wake, lau angekuwa na hoja. Mambo ya Fyatu amuachia Fyatu mwenyewe. Hayamhusu hata kidogo.       
            Tatu, hakuna kondoo walioraruriwa toka Fyatuland. Waliofyatuliwa ni wa kaya ya jirani waliofyatuka na kutaka kuwafundisha umbwa mwitu kondoo wangu waaminifu na wasio na hatia wala washari.
            Nne, namuonya kwa mara ya mwisho Tarampu. Asitake kutuletea ubeberu na kujitia ufahari asijue nasi tunauweza huo ubeberu wake. Tarampu ajue. Mie simshobokei wala kumnyenyekea eti kwa vile ana njuluku. Si alikata misaada kwa Fyatuland baada ya kukataa ubeberu uchwara wake. Kuna Fyatu amekufa kwa kukatiwa hiyo misaada yake?
            Tano, Tarampu ajue hanitishi. Na kama ni ufyatu mie ndo mfalme wa Mafyatu akiwamo yeye. Lazima tuheshimiane. Aniheshimu. Aheshimu dog wangu. Akiendelea kujifyatuafyatua, nitamuwekea vikwazo vya kiuchumi. Angejua kuwa kupeleka lapdogs wangu kwenye kaya yake kulikuwa kunamuingizia njuluku kibao, asingejifyatua na kutaka eti kuwafyatua dog wangu wapendwa.
            Sita, kama Tarampu ataendelea na ubeberu wake, nitaanza kufanya mipango ya kutengeneza bomu la nyukilia ili kiumane. Anadhani siwezi? Akamuulize Kiduku ambaye amekuwa akimtoa jasho. Hapa, sijagusia kwenda kwa swahiba yangu Xii Jin Pingu ampige pingu. Nlishaonya. Fyatuland inawenyewe na wenyewe ni sisi. Hatutishwi wala kuyumbishwa. Tunatesa kwa raha zetu. Hata kama nitaamuru attack dogs wawafyatue wanakondoo tena, yeye inamhusu nini. Si akafyatue wake waligeuka mbwa mwitu zamani kiasi cha kufyatuana wao kwa wao kwa vile dog wake hawana uwezo wa kuwafyatua.
            Mwisho, ni vizuri Tarampu akajuzwa na kujua. Sisi huku tuna haki za kila kitu kuanzia dog hata chawa. Tunaheshimu haki za viumbe wote kwa sharti kuwa wasijifyatue kutaka kutufyatua. Hapa, tutawafyatua kama tulivyoamuru dog wawafyatue wanakondoo.
            Du! Kwani, nimesemaje? Naongelea lapdog au madogii? Kumbe naota nikipata kichapo cha dirisha la Horumuziiii Uajemiii!
Chanzo: Mwananchi J'tano leo.

Wednesday, 3 June 2026

Fyatu Fwala na siasa za maji taka

Japo Fyatu Fala–––binafsi simjui –––ambaye wengi humuita mnene wa kiroho bila kumalizia, sawa na wengine wa aina yake, kuwa ni wa kujipa au kujipachika, amenifikirisha hata kunifyatua. Kwanza, nampongeza kwa ufyatu wake. Najaribu kumdurusu kwa sifa zake za utata alizoonyesha hivi karibuni. Huwa siandiki juu ya Mafyatu. Ila, leo, nimewiwa. Naufyatua mwiko niliojiwekea baada ya kusoma habari kuwa Fyatu tajwa amerejea Chandimu akitokea Chawalaji. Japo ni haki yake kuruka vyata, kwani katiba inaruhusu––– alinistua na kunitanza hadi nikafyatuka. Je, Fyatutajwa anakumbuka aliyosema aliposepa na sasa kujifyatua na kujirejesha baada ya kufyatuliwa na aliotoka kuwafyatua? Je, anajua kuwa na Mafyatu wana akili na kumbukumbu? Je, huu ni utoto au usanii kisiasa au? Nashindwa kujua. Hakuna kilichonigomba na kunifyatua kama sababu kinzani alizotoa na za kushangaza.
Sina ugomvi na wanasiasa wala watu wanaojitafutia riziki––––ila kwa kuwafanya wengine hamnazo–––hasa kwa kutumia kile ambacho marehemu Sam Sixx, microphone wa zamani wa njengo–––alichoita siasa za maji taka.
            Wote tunayajua maji taka. Ni machafu. Yananuka. Pia, yanakera kiasi cha kutushughulisha kuyaondoa katika makazi yetu. Kama maji ni hivyo, siasa za maji taka, hali inakuwaje? Tunaweza kuzomea waitwao machawa lakini tukawashabikia maji taka ya kisiasa wanaohamahama kwa kutoa sababu zisizoingia kichwani.
              Tujikumbushe. Fyatu tajwa alisepa miaka miwili iliyopoita. Kati ya mengi aliyosema ni kwamba Fyatuland hakukuwa na chata kama cha maulaji akikionya kutoshirikiana na wapingaji. Ajabu ya maajabu, ndani ya miaka miwili, ndoa imemshinda akaamua–––ila hata chembe ya aibu–––kuramba matapishi yake! Je, huy Fyatu anakumbuka aliyosema hapo juu na alichomaanisha au kulikuwa na namna?
                Wapo wanaodai Fyatu tajwa alitumwa kufanya ‘kazi maalumu’–––ipi ambayo sasa ‘ameikamilisha’ na kurejea nyumbani! Ajabu. Hii ni kumpa mhusika sifa asizostahili. Kwa wanaojua namna baadhi ya wasanii walivyo nyemelezi hata matapeli, hakubaliani na hili. Kwani, linawanyima kuaminika hata kuheshimika sawa na mwingine kama yule aliyewahi kusema kuwa kazi yake ya uchunaji na utapeli ni bora kuliko urahis. Ajabu, alipopitishwa kwa rafu kugombea unene jimbo fulani, alisahau sijui alichosema na kupwakia matapishi yake huku akiimba kila sifa hata zisizokuwepo.
             Kumjua Fyatu tajwa na wengine wa aina yake, turejee maneno yake hapo juu ukiyalinganisha na aliyosema ndoa ilipomshinda. Alinukuliwa akisema  kuwa ameamua kuachana na chamaulaji kutokana na unyotoaji uliofanyika juzi! Lahaula! Je, kuanzia wakati huo–––kama kweli analiyachukia na kuyapinga–––alikuwa wapi? Alingoja nini au alikuwa akivuta kamba lau apate mradi? Je, ameamua kutumia unyotoaji tajwa kupata ujiko kama mwenzake ambaye–––alipopigwa chini–––kuushupalia? Je, kufyatuka na kusepa vinaleta suluhisho?  Je, mauaji unyotoaji roho chanzo chake hakiwezi kuwa siasa za maji taka zilizojitenga na ukweli na kukumbatia uongo na uzushi? Ni jemedari gani hukimbia mapigano akidhani analeta suluhisho au ushindi? Natamani chata cha maulaji  wafyatuke  na kufichua walivyompokea, kumjua, kumchukulia, na kumtenza hadi ndoa ikamshinda akarejea alikokandia vibaya.
            Hapa, kuna maswali muhimu. Je, Fyatu tajwa na wengine kama yeye wanafuata sera au vyeo na ulaji? Je, kwanini ameamua kuramba matapishi yake na kujigeuza maji taka baada ya
            Kwa mtu wa kada ya Fyatu tajwa ya uchungaji kama siyo ‘uchunaji’, wengi walitegemea awe mkweli, mwenye maadili na si wa kusema hili leo na kesho, anajipiga mtama. Angeona lau hata aibu kuwa ni vibaya kwa Fyatu mzima tena ‘ wa God’ kuonekana kigeugeu, kizabazabina, na mtata kiasi cha kufanya siasa kuwa maji taka ambayo yakishachafuka, huwezi kuyarejesha kwenye usafi na usalama. Je, Fyatu tajwa, wenzake, waliompokea, na wamaomshabikia wanayajua haya au la? Je, anaweza kuaminika na kuheshimika tena ilhali akisema hili na kesho akasema kinyume chake kiasi cha kufanya wanaomsikiliza wasijue kati ya ukweli, uongo, na uzushi ni upi mbali na uchumia tumbo na usasi wa ngawira?
            Japo si kosa kwa Chandimu kumpokea na kumrejesha kundini Fyatu tajwa, je, hii haionyeshi kuwa baadhi ya vyata ni kama maabara ambayo kazi yake ni kufanyiwa majaribio? Je wanajua maana ya kuwa hivyo? Japo, Fyatu huyu si wa kwanza wala mwisho kufanya siasa hizi zinaoanza kuzoeleka, kuna haja ya wapiga kura na wananchi kwa ujumla kuweka nukta na kukumbuka matendo na matamshi ya wote wanaotuaminisha kuwa wanatufaa wakati hawafai wala kujifaa.
            Mwisho, kwa alichofyatua Fyatu, nashindwa kumuelewa wala kumpongeza zaidi ya kumpa pole. Maana, ana ndimi mbili. Isitoshe, kama ni upotezaji na unyotoaji roho, kwani, vilianza awamu jana? Je, ni unyotoaji roho gani ni muhimu kuliko mwingine tena chini ya chata lile lile? Je, Fyatu alikwenda kuwafyatua wenzake wakaishia kumfyatua? Maswali ni mengi kuliko majibu. Niwezacho kusema ni kutahadhari siasa za maji taka na wanasiasa maji taka.
Chanzo: Mwananchi, leo Jtano.