The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 26 August 2026

Fyatu kugeuza Kijiji chake mji mkuu wa Fyatuland!


Baada ya kuonyesha umahiri usio wa kawaida kwa mafyatu wasiofyatuka na kumfyatua, Fyatu napanga kufyatua kitu ambacho kitamfyatua kila Fyatu diniani. Kwa wasiojua dili, wajue. Fyatu Mfyatuzi anapendwa sana na Mafyatu wote wa Fyatuland kiasi cha kuabudiwa, kusifiwa, kupendwa, na kuenziwa. Hivyo, kwa kuzingatia uzito huu, lazima nifyatue kitu. Napanga kufyatua amri ya kuanza kujenga kijiji nilichozaliwa cha Kifyatukizi kuwa mji mkuu wa Fyatuland ambao pia napanga kuiita Fyatu Mfyatuziland kwa hesima na ukumbusho wangu.
            Kuanzia sasa napanga kufyatua amri nyingine ambayo itahalalisha jina langu kupewa kila kitu kizuri na kikubwa. Barabara zote katika mji yote ya Fyatuland na madaraja makubwa na mashuhuri, vituo vya mabasi na vya treni vyote vikubwa lazima vipewe jina langu. Chuo kikuu pekee cha Fyatuland kiitwacho the University of Wisdom, Integrity, and Intellect (UoWiii) nacho nakifyatua na kukipa jina langu. Kuanzia sasa kitaichwa Dk. Profesa, Gwiji, Nguli Fyatu Mfyatuzi University (DPGNFMU).
            Baada ya kumalizana na chuo kikuu ambacho siku hizi kimegeuka choo kikuu, nafyatua mahospitali, mashule, na taasisi nyingine ambazo nazo zitapewa jina langu ili ziweze kuheshimika na kupendwa na kuabudiwa kama mimi. Pia, uwanja wa ndege wa Fyatuland utapewa jina langu ili kuongeza wasafiri wanaoutumia kwa heshima yangu.
            Baada ya kumaliza kuvipa jina langu vitajwavyo hapo juu, vitakavyobaki vitabeba jina la Bi Mkubwa wangu, Mama yangu, Dingi wangu, Shangazi zangu na hata vitegemezi vyangu.
            Kama haitoshi, nitafyatua na mbuga za waanimo ambazo zote zitapewa jina langu ili kukuza utalii. Bandari zote, maziwa makubwa, milima na mito mirefu na mikubwa, navyo vitabeba jina langu. Hii yote inalenga kukuza mapato ya kaya kwa kutangaza na kuuza jina langu tukufu. Naamini kuwa, kama ninavyozimikiwa, na vivutio hivi vitapendwa na kuvutia mafyatu wengi toka majuu kuja kushuhudia na kufyatua maajabu yangu.
            Najua yapo mafyatu mazuzu na mabishi yatakayopayuka na kufyatuka kuwa nageuza Fyatuland kuwa mali binafsi. Kwani, ni mali ya nani zaidi ya mimi? Mimi ni mwanzo na mwisho, chini na juu, kushoto na kulia na kila kitu cha Fyatuland. Mafyatu wanapaswa wafundishwe kujua ukweli kuwa Fyatuland iliumbwa kwa ajili yangu ambaye niliwapenda nikwaambia kuwa ni yao wakati ni yangu, familia, mashosti, na vitegemezi vyangu.
            Kwa ufyatu na ufyatuzi huu, usishangae siku moja ukikutana na mji au shule zenye majina ya ukoo wa Fyatu Mfyatuzi. Sambamba na kupandisha daraja kijiji chetu kitukufu cha Kifyatukizi, Hospitali kuu ya Fyatuland itaitwa Bi Fyatuwake Fyatu Mfyatuzi (BFFM).
            Lazima mafyatu wote, hasa wale wakumbaff na wabishi wanaopenda kuniponda badala ya kunipenda wajue kuwa mimi ndiyo katiba na sheria vya Fyatuland. Mimi ni zaidi ya mfalme kutokana na ubora wangu kama kiumbe aliye bora kuliko wote aliyeko hai baada ya kuondoka wale waliodai kuwa walitumwa na Sir God na kuwafyatua mafyatu wengi kwa kuwaahidi vinono ilhali wanaishi maisha machungu.
            Kwa vile Fyatu mie ni tofauti na hao juu, nafyatua utukufu wa kifyatu kwa kutangaza rasmi kuwa kijiji changu cha Kifytumfyatu kilichonifya kitaitwa sehemu takatifu kama zile za wale jamaa zangu hapo juu. Kwa hivyo, tokana na utakatifu ninaofyatua kwa kukipandisha kijiji changu kuwa jiji na mji mkuu wa Fyatuland, lazima kijengwe na kupanuliwa na kuwa jiji lenye kila aina ya maraha ili kuwafanya Mafyatu wayafyatue badala ya kungoja kuyapata watakapokuwa wamefyatuliwa na kuzikwa. Kwa Fyatu, pepo ni hapa hapa. Hii pia, italeta ubunifu na uwajibikaji wa kuwapa raha Mafyatu waliokubali mie niwe kiongozi wao.
            Pia, kutokana na ufanisi, utamu, na uzuri wa jina langu, kutakuwa na shahada vyuoni zitakazopewa jina langu. Mfano, shahada zote za uongozi, usimamizi wa fedha, sheria, sayansi ya jamii na nyingine zitafyatuliwa na kupewa jina langu. Hii inalenga kuwamotisha vijana kusoma sana kama mimi na kutenda miujiza ya kuwafyatua, sorry, kuwaokoa Mafyatu na Fyatuland kwa kujiletea, sorry, kuwaletea maendeleo yatokayo na uwezo wangu wa kufyatua miujiza.
            Wakati nikipanga kufanya mageuzi haya makubwa, kuna Fyatu mmoja mshauri wangu alishauri kuwa machinjio, magereza, na mochwari vikubwa vikubwa navyo vipewe jina langu. Kwa vile alitaka kuniuzi uzwazwa, huyu Fyatu nilimfyatua kwa kumuonyesha mlango. Hata hivyo, alinipa ujanja. Kwa vile mimi ni mwana demokrasia namba wani Fyatuland, hivyo, hapo juu vitapewa majina ya wapingaji ili nisifyatue kila kitu. Si inapendeza!!
            Kufunga kazi, vitegemezi vyote vitakavyozaliwa kuanzia sasa vitabeba jina langu na Bi Mkubwa kwa heshima na ukumbusho wetu.
            Naona yule anatikisha na kusonya. Ushindwe na uregee. Ukitaka kufyatua kama mimi fyatuka unifyatue uone nitakavyokufyatua. Hivi niko wapi na nafanya nini?
Chanzo: Mwananchi J'tano,leo.

No comments: