How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday 28 November 2012

Kushitakiwa Simone Gbagbo ni somo kwa wake za marais

KITENDO cha mahakama ya kimataifa ya makosa ya Jinai (ICC) kuamua kumfungulia mashtaka mke wa rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, Simone, ni cha kimapinduzi kwa bara la Afrika.
Hivi karibuni ICC ilitoa hati za kutaka kukamatwa na kufikisha kwenye mahakama hiyo Simone akikabiliwa na makosa ya ubakaji, mauaji na uharifu dhidi ya ubinadamu yaliyotendeka wakati wa mwisho wa utawala wa mumewe mapema mwaka juzi kuja mwaka jana.
Gbagbo aliangushwa baada ya majeshi ya Umoja wa Mataifa na Ufaransa kuingilia kwenye mzozo nchini mle mnamo Aprili 2011.
Jumuia ya kimataifa iliamua kuingilia kwenye mgogoro wa Ivory Coast baada ya Gbagbo kuandaa uchaguzi na baadaye kudharau matokeo ya yaliyompa ushindi mpinzani wake Allasane Ouattra rais wa sasa.
Kitendo cha Gbagbo kugoma kuachia madaraka kilimfanya mpinzani wake aungane na waasi waliokuwa upande wa Kaskazini.
Kitendo hiki kiliigawa Ivory Coast kati ya Kaskazini kwenye waislamu wengi na watu wenye asili ya Burkinabe na Kusini kwenye wakristo wengi na waliojiona kama wenye haki ya kutawala kwa sababu ya asili yao ya hapo hapo Ivory Coast.
Mvutano baina ya Gbagbo na Ouattra ulidumu kwa miezi mitano. Hata hivyo, matokeo ya hali hii hayakuwa mazuri. Kwani watu wapatao 3,000 walipoteza maisha huku mamia wakikimbia nchi yao. Pia mvutano huu uliivuruga Ivory Coast kiuchumi, kisiasa na kijamii. Bado nchi inauguza madonda baada ya kuondolewa kwa Gbagbo aliyetolewa kwenye handaki akiwa hoi bin taabani kutokana na kuishiwa matumizi.
Baada ya Gbagbo kutolewa shimoni, alipelekwa sehemu mojawapo ya Ivory Coast na baadaye akasafirishwa kwenda The Hague ambako alikuwa ameishafunguliwa mashtaka. Tangu wakati huo Gbagbo amekuwa akishikiliwa mjini The Hague akingojea kusikilizwa na kuamriwa kwa kesi yake.
Baada ya kupelekwa Gbagbo The Hague wengi walidhani ulikuwa mwisho wa sakata. Hawakujua kuwa kumbe na washirika wake hasa mkewe na waziri wake mkuu wa zamani wangefikishwa mahakamani kujibu mashitaka sambamba na Gbagbo.
Simone anasemekana kuwa nguzo na sababu ya Gbagbo kung’ang’ania madaraka. Pia kama mke wa rais na msomi mwenye shahada ya juu ya PhD kwenye historia kama mumewe, Simone anasemekana kuwa na nguvu sana nchini humo kiasi cha kuogopewa kuliko hata Gbagbo mwenyewe.
Na huu umekuwa mchezo mchafu ulioanza kuota mizizi katika tawala nyingi fisadi na za hovyo za kiafrika ambapo wake wa marais hujigeuza marais kwa vile wanalala kitanda kimoja na rais. Miaka michache iliyopita tulishuhudia mke wa rais wa Kenya, Lucy Kibaki akiwachapa makofi waandishi wa habari baada ya kuvamia ofisi zao na kuwazuia kurusha habari zilizokuwa zikionyesha ufisadi wake kwenye sakata la wizi wa mahindi ya umma.
Nchini Zimbabwe mke wa rais Robert Mugabe, Grace Marufu anatuhumiwa kuibia benki kuu ya nchi hiyo mamilioni ya dola akiyatapanya kwenye vipodozi na mavazi ya fasheni ya bei mbaya hadi kuitwa Grace Gucchi. wakati mke wa rais akifanya upuuzi wote huu, wazimbabwe walio wengi wanakufa kutokana na ukata na kuvurugika kwa uchumi wa nchi hiyo vilivyosababishwa na ung’ang’anizi wa rais wa nchi hiyo.
Pia hivi karibuni tulisikia kuwa nchini Uganda rais Yoweri Museveni anamuandaa mkewe kumrithi. Hakika hali ni mbaya kwenye nchi nyingi za kiafrika. Wake wa marais hata watoto wao ima huingia moja kwa moja kwenye siasa au kuanzisha NGO na kuzitumia kuibia umma ukiachia mbali kupata upendeleo kwenye taasisi za kifedha na hata wengine kushiriki biashara haramu kama vile madawa ya kulevya.
Hivyo, kilichotokea kwa mke wa Gbagbo kinapaswa kuwa somo tosha kwa wake wa marais wanaotumia madaraka ya waume zao vibaya. Inashangaza kuona kuwa kizazi cha sasa cha watawala kimekuwa na upofu kiasi cha kutoogopa kinachoweza kutokea hapo baadaye.
Siyo siri wala uchochezi: Afrika kwa sasa ina akina Imelda Marcos wengi. Imelda alisifika sana nchini Ufilipino kwa kutumia madaraka ya mumewe kuiba na kufuja pesa ya umma huku umma ukiangamia hadi siku serikali ya mumewe ilipoondolewa kwa maandamano ya umma mwaka 1986. Inashangaza ni kwanini hawajifunzi hata kutokana na matukio ya karibu kama vile kukamatwa kwa rais wa Misri Hosni Mubarak sambamba na watoto wake pekee wawili wa kiume. Bado hawajifunzi kutokana na yaliyomkuta Gaddafi na watoto wake ambapo baadhi waliuawa na aliyetarajiwa kumrithi anashikiliwa korokoroni huku akikabiliwa na mashtaka mbele ya ICC.
Kitendo cha ICC kumfungulia mke wa rais wa zamani wa Ivory Coast chaweza kuwa mwanzo wa mwisho wa wake za wakubwa wanaotumia madaraka ya waume zao vibaya. Ni vizuri nchi za Kiafrika kuanza kubadili katiba zake na kuweka vipengele vya kuwawajibisha wezi wa madaraka kama hawa sambamba na waume zao na hata familia zao.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 28, 2012.

No comments: