The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Sunday, 19 April 2026

Waopanga au kutamani kuoa au kuolewa majuu wajue


Hivi karibuni, kumetokea visa vya kusikitisha tena vya kinyama. Jamaa waliohama Afrika wakitegemea kuukata ukaishia kuwakata. Wanaume hawa walipata mama wa kizungu toka nchini Marekani. Kwa matarajio na mapenzi makubwa, waliamua kuoa mama wa kizungu. Walihamia Marekani kwenye nchi inaayoitwa nchi yenye fursa ambako, ukiwa na dhamira na mipango madhubuti, unaukata.
Leo, tutaongelea visa vinne kama mfano ili kuonyesha changamoto wanazopata baadhi ya wale walioingia Marekani kwa kutumia njia ya ndoa. Kisa cha kwanza kinamhusisha mwanaume aitwaye Njamba (si jina lake halisi). Njamba alifanikiwa kumuoa mama mjane wa kimarekani aitwaye Mercy (si jinale halisi). Waliishi kwa furaha na amani kwa muda. Punde, mambo yakaanza kuharibika tokana na mke kutokubali kuishi maisha ya Kiafrika ambapo baba huwa na nguvu zisizopingika. Kwa Marekani, ni kinyume. Sheria za huku zinampa mama madaraka makubwa kuliko hata ya baba wa Kiafrika. Hivyo, mama anaweza kuamua kwenda likizo nchi yoyote peke yake na baba asiwe na uwezo wa kumzuia.
Piga picha. Hali inakuwaje kwa baba wa Kiafrika aliyezoea kummilki na kumpangia mkewe? Hii ndiyo hali iliyomkuta Njamba. Taratibu, alianza kujihoji kama ameoa au ameolewa. Katika kupambana na hali hii, Njamba aliamua kuonyesha uanaume wake. Alianza kutoa matishio kwanza. Baadaye, alianza kumtandika mkewe. Kwanza, mama hakuamini kama Mswahili angejiamini na kufanya haya. Wakati haya yakiendelea, wawili hawa walikuwa ndiyo wanamaliza kulipia deni la nyumba waliyoinunua kwa mkopo kama ilivyo kawaida huko Marekani.
Tokana na kuwa na deni la nyumba na kujua sheria na taratibu za Marekani vinavyompendelea mwanaume, mama alivumilia mateso kwa muda akisubiri wamalizie deni la nyumba naye afanye vitu vyake. Siku ya kwenda benki na kuagana nayo kwa kumaliza kulipia nyumba yao, mama aliruddi nyumbani na kuaza kujiamini na kujibu mapigo. Njamba hakuamini macho wala masikio yake kwa aliyoona na kusikia.
Kwa kujiamini kabisa, mama alimwambia kuwa alikuwa amechoka na mateso na hivyo, alitaka waachane. Kwanza, Njamba alidhani mkewe alikuwa akimtishia nyau asijue atafanya kweli. Mwezi ulipita halali ikiwa tete. Kumbe mama alishaenda kwa mwanasheria wake na kufungua kesi ya talaka bila hata mumewe kujua. 
        Siku ya siku, mama alirejea nyumbani na kumuamuru Njamba ahame toka nyumbani kwake. Njamba alishangaa, kuchukia, na kuhoji iweje wakati nyumba ni ya wawili? Mama alimjibu kuwa hayo hayajui wala hayamhusu. Isitoshe, alimwambia kuwa shauri la kuvunja ndoa lilikuwa tayari limeishafunguliwa mahakamani na Njamba angejulishwa wakati wowote. 
            Njamba aliapa kwa miungu yake yote kuwa asingehama kwenye nyumba yake. Naye, kadhalika alimtaka mkewe ahame kabla hajamfanyia kitu mbaya. Mama naye aliona kama alikuwa akitishia tu. Hivyo, aliinua simu na kupiga namba ambayo wengi huku wanaigopa kama ukoma yaani 911. Aliwajulisha polisi kuja haraka na kumhamisha mumewe toka nyumbani kwake kwa sababu alikuwa amemtishia angemfanyia kitu kibaya mbali na kumnyanyasa kindoa.
        Kwanza, Njamba hakuamini masikio yake. Hivyo, alimuamuru mkewe kukata simu. Mama hakukubali. Aliendelea kupiga makelele kwenye simu akiomba polisi waje haraka. Bila hili wala lile, Njamba aliingia chumba cha kulala na kuchukua bunduki na kumpiga risasi saba na kumuua hapo hapo Mercy.
        Baada ya hapo, alijigeuzia bunduki na kujimaliza. Hivyo, ndivyo ndoa ya majuu ya kuukata ilivyoishia kumkata Njamba baada ya kupitia mengi kiasi cha kukata tamaa na kuamua kuua na kujiua.
Kwa wale wanaopanga kuoa au kuolewa majuu bila kufanya utafiti na kujua tofauti za kimila na kijamii wajifunze kitu kuwa si kila king’aracho ni dhahabu.
Kuna kitu kinaitwa ndoto ya Marekani au American dream. Kitu hiki, kimewaponza wengi. Kuna njia nyingi za kufanikisha ndoto hii kubwa na ya kupigiwa mfano kwa wasiojua kilichoko nyuma ya pazia. Pamoja na kuwa sisi waandishi hatuishi Marekani, tunaishi jirani kwenye bara la Amerika. Kwa kiasi fulani, tunajua ukweli na undoto wa ndoto hii ambayo imegeuka jinamizi kwa wengi walioingia bila kufanya utafititi wa kutosha.
Chanzo: Mwananchi Jpili leo.


No comments: