The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 29 April 2026

Fyatu kufyatua mafyatu wanaofyatukafyatuka kumkosoa

Juzi, si nilifyatua uteuaji na utenguaji. Katika kufanya hivyo, si nikampa ulaji swahiba yangu mgoshi Machungi aka blackbox yangu. Acha mafyatu wazoze! Kwani, nimemkosea nani na wapi? Kasomeni katiba ya Mafyatu vizuri. Hata nikimteua kuku wangu, sivunji sharia kwa mujibu wa katiba yetu viraka. Huu ndo utamu wa kuwa na katiba huru itoayo uhuru kweli wa kufyatua na kupiga juluku. Hata ukiteua kitegemezi chako, shoga yako, nini, nimesemaje?Hata nikimteua Bi Mkubwa wangu poa tu.
Unene wa Fyatuland unanipa uhuru wa kufanya nitakavyo. Na nikifyatua hivyo sivunji sharia yoyote. Huu ndo uhuru na uzuri wa katiba huru. Inakuweka huru wa kufyatua na kula kwa uhuru. Huu ndo uhuru wa fyatuland tulioapa kuulinda hata kwa kuwanyotoa roho wanaotupinga. Huu ni uhuru wetu. Siyo wao. Kwa kuwaonea huruma, nawashauri wakatafute ulaji na unene wao, vinginevyo walie. Waache kutupotezea muda. Tena wajue. Itaendelea kula kwao wakati sie twajilia kwa raha zetu. Twala nyama tena minofu na kidari kwa raha zetu. Wao wameza mate kwa machungu yao. Hata mifupa hatuwapi. Halo halo! Mwenye wivu si ajinyonge tu.
Sasa tuje kwenye inshu. Baada ya katiba ya Fyatuland kunipa uhuru wa ki-god, naweza kufyatua yeyote na hakuna fyatu wa kuniuliza. Wapo mafyatu mazwazwa niliosikia wakihoji udhu wa mgoshi Machungi. Wanadai ni fisadi na mhujumu wa Uchumi. Ebo! Kwani, siku hizi kuna mwenye udhu? Yuko wapi? Nionyeshe nimuone. Mshaabwa. Kaya ina wenyewe na wenyewe ni sisi. Sasa mnaohoji nini tunapohomola na kuhondomola? Hakuna haja ya kubagazana. Eti wapo wanaodai mgoshi hana maadili? Lol! Mbona Fyatuland ilizika mambo ya maadili zamani gani! Mambo ya maadili ni ya kizamani. Tuache uzamani. Tuanze usasa. Fyatuland siyo kaya ya maadili bali ya madili. Ni kaya ya kupiga dili kama huna akili nzuri. Sijui kwanini nao hawatafuti madili ya kupiga na badala yake wanapiga kelele tu! Inashangaza na kusikitisha. Kapigeni madili na kuacha uvivu wa kufikiri.
Leo, natoa onyo. Hawa wapigao makelele wakiendelea, nitamteua Bi Mkubwa wangu au kitegemezi chetu kuwa makamu wangu tuone. Kwani, mie ni wa kwanza kumteua shwahiba yake? Nendeni pale jirani kwa M7 muone. Mbona Bi Mkubwa wake na kitegemezi chao wanatesa katika ulaji wa bwana kuba? Mbona kule Ikweta ya nonihino kitegemezi cha Obiangu ni vyangu ni makamu wake na hakuna anayeleta ngebe uchwara za maadili? Mbona hata Tarampu kawajaza vivyele na wakwe zake kwenye lisrikal lake tena kwenye kaya inayojidai kupigania haki na usawa? Kama Tarampu kafyatua, mie ni nani nisifyatue? Kama Tarampu anatawala kwa kutumia familia na maswahiba zake, kosa langu kumteua mgoshi Machungi nini?
Nilisikia fyatu mmoja zwazwa akisema eti huu ni ufamilia! Ebo! Bila familia anadhani naweza kupata muda wa kuwatumikia mafyatu waliogoma kufyatua hadi tukawa tunawafyatua tunavyotaka? Kwangu, familia ni kila kitu. Maswahiba ndiyo nguzo ya utawala wangu. Mjue msiojua. Na bado. Nitazidi kuwapa ulaji jamaa na maswahiba zangu mtake msitake. Huu ni wakati na zamu yetu kutesa. Si huwa mafyatu wanasema kuwa kutesa kwa zamu? Imefika zamu yetu, mnaanza ngebe. Jamani, ngojeni zamu yenu kama ipo.
Wengi wasiojua wala kuonja raha ya unene wanadai kuendelea kuteua jamaa zangu kutaongeza deni la Fyatuland! Ebo! Deni la kaya linanihusu nini wakati atakayelipa si mimi wala jamaa zangu? Kwani, mie ni wa kwanza kukopa na kutumia nitakavyo? Mali ya umma huwa haiumi. Kazi yetu ni kuiuma wenye kuumia na muumie tu. Pia, mjue, makelele ya chura hayazuii ng’ombe kunywa maji. Kazi ya maji ni kunywewa tu.
Kwa vile mie huwa sisikilizi makelele, nitazidi kuteua. Watakaozidisha ngebe wajue. Wasiojulikana bado wapo. Na hili ni onyo la mwisho. Kitakachofuata, tusilaumiane. Ukifyatukafyatuka, nakufungulia mbali na kesi ya uhaini au uhujumu uchumi ili ukose dhamana na kuozea lupango kama yule mtoto mtundu aliyekosa lishe akachezea lijisu aliyejifanya kukinukisha tukamnukisha. Usicheze nasi. Chini ya utawala wangu, hakuna fyatu atayefyatuka nimuache. Kawaulize Gen Ziro waliokuja na uziroziro wao tukawafyatua hadi wakakoma. Wako wapi siku hizi? Si wameufyata. Wafyatuke tena tuwafyatue. Fyatuland si kaya ya kuchezea tena na viumbe vichanga visivyojua maana ya ulaji na unene. Ndiyo maana vinaitwa Gen Ziro. Navyo vilivyo vizwazwa vilikubali kuitwa hivyo. Mimi ni Gen Fyatu. Lazima vijue. Vinginevyo tutaendelea kuvifyatua. Na tukifanya hivyo, tusilaumiwe vilaumiwe vyenyewe kwa bangi zao na kuhongwa viharibu amani yetu Fyatuland.
Nimalizie. Kumteua mgoshi Machungi ni mwanzo tu. Nitateua wengine wengi hata wawe hawana huo udhu wenu. Kwani, nawateua wakaswali hadi wahitaji udhu? Hamjui nawateua kula na siyo vinginevyo? Du! Hivi naota au sijameza dawa zangu?
Chanzo: Mwananchi Jtano, leo.

No comments: