The Chant of Savant

Thursday 10 November 2011

Mpayukaji aanzisha CCM



NAJUA fika kichwa cha habari kitakong’ota wengi hasa wapenzi wa chama twawala. Pia kichwa cha habari kitaaacha hoi kwa mstuko huku viroho vikitweta kudhani nina mpango mchafu wa kukigaddafi kiama tawala.

Sina mpango huu wakati huu na si kwa njia hiyo ingawa kinafaa kufanyiwa hivyo. Kwa taarifa ya walevi ni kwamba nimeanzisha Chama Cha Mahangaiko au Mparaganyiko yaani CCM.

Hii ni baada ya kuona migongano kwenye Chama Chetu cha Magambagamba kuwa na misukosuko na kutaka kunyotoana roho, kuchafuana hata kutumiana.

Juzi hamkuwasikia akina Mjega wakitaka kina Sammy Sixx watimuliwe kwenye kiama wakati wasijue ni wadau wakubwa waliouza kaya kwenye kashfa ya Richmonduli ili wapewe uwaziri wa ulaji baada ya kunyimwa umicrophone.

Turejee kwenye CCM ya Mpayukaji inayochukua nafasi ya TLP yaani Timua Linda Personality yako. Baada ya kusifika kwa kuwafukuza wenzangu Kiarawaarawa, nimeamua kuanzisha zana nyingine ya kuusaka ulaji. Najua wengi wanaguna kusikia kuwa kuna CCM nyingine. Onyo: hii CCM yangu si ya mafisadi wala wasanii wala haina uhusiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). NLangu ni chata la ukombozi wa walevi na wadaganyika toka kizani na kwenye mporomoko wa njuluku na upuuzi mwingine.

Nimekuja na mikakati ya karne ya 21 ambapo badala ya kwenda kwenye majukwaa ya siasa nitatumia misikiti na makanisa kaya nzima kujitangaza na kujenga msingi wa kushinda uchaguzi utakapofika. Kwa vile nimeishachota pesa nyingi ya kahawa na kashata, nitahakikisha wale watu wa “Mungu” waliojazwa roho mtakakitu badala ya roho mtakatifu nawapa misaada kwenye miradi yao ya ulaji ili wanipigie debe na kunisafisha tokana na uchafu niliopakwa na kashfa ya wizi wa pesa ya kahawa na kashata.

Hivyo msishangae kuona siku hizi naingia kwenye nyumba za ibada kama sina akili nzuri. Nani mwenye jeuri ya kuikataa pesa iwapo ana njaa tena aliyoificha nyuma ya joho na jina zuri la mtumishi wa God?

Watu wa God nanyi nawaambia kuwa mchungaji lazima anywe maziwa ya hao awachungao hata kula nyama ya kondoo. Hivyo, msijivunge kuwatumia kondoo wenu kutengeneza ulaji binafsi. Wale ambao wanaendelea kujivunga nawashauri wajiunge nami ili niwatajirishe kwa vijisenti vya kahawa. Pia nasisitiza kuwa kondoo mnaowachunga ni mali yenu binafsi mkimwakilisha “Mungu”.

Msiwaogope wale wanaowaita wapakwa mafuta wa shetani na mbwa mwitu wawararuao kondoo. Kama wanasiasa wanawararua wapiga kura wao kwanini iwe kosa kwenu kuwararua kondoo? Hamuoni akina Katortoise, Gamanyua, Mwakasengesenge, Rwakatarehe na wengine wanavyowararua kondoo na kuwa mabilionea?

Kwa vile mie ni mjanja na si fala wa kutumia masaburi, nimeamua kuanza kampeni mapema. Hivyo kila siku za ibada msishangae kuniona nimezungukwa na mbwamwitu sorry wachungaji wa kondoo wa Bwana. Akina Masikasika na Mokiii wa mwanipata vile.

Najua kuchanganya siasa na dini inakatazwa katika kaya hii. Lakini kwa sisi ambao hatukukutana barabarani na mkuu na kufanya naye urafiki, hili si tatizo. Lazima kulindana. Si mnajua tena. Waarabu wa Pemba. Hivyo msichonge midomo kuanza kuzoza eti jamaa anatumia sehemu za ibada kufanya siasa tena chafu inayoendeshwa na pesa za ufisadi wa kahawa na kashata. Mtajisumbua bure. Mie na jamaa ni damu damu na tumesomea usanii kaya nzima hakuna wa kutufikia.

Juzi nilisikia maadui zangu wakiongozwa na Msomi mkatatamaa aka Sam Six Mwakiwembe kuwa ninatumia fedha za kifisadi kwenye majumba ya Mungu. Ujinga mtupu. Nani si fisadi katika kaya hii? Hata hao wanaoibiwa pesa yao yaani walala kiza si kwamba wanauchukia ufisadi.

Wanatamani ni lini wapate nafasi waufanye. Je, namna hii ufisadi utakwisha? Acha sasa tuupeleke kwenye nyumba za ibada ili ugeuke dini na mungu awe njuluku baada ya yule aliye juu. Mimi sikatai ni fisadi. Je wao si mafisadi?

Kama si mafisadi wanangoja nini kwenye kijiwe iwapo kijiwe kizima kinanuka ufisadi na ufisidunia? Kumbaff nyote mafi ya mbuzi.

Kwa kupeleka njuluku kwenye
mahekalu ya Bwana nasaidia madafu yetu yanayoporomoka kama mgonjwa wa kuharisha kuimarika. Kwa taarifa yenu, kumwaga vijisenti kwangu kunalenga kuimarisha lishiringi lenu linaroporomoka kama ndege iliyozimika injini huku wapuuzi fulani wakizidi kuwaaminisha kuwa haya ni matokeo ya kuvurugika uchumi dunia nzima.

Si kweli, kinachoporomosha madafu yenu ni mipango mibovu, sanaa, ufisadi na matumizi na matanuzi ya wakubwa. Huwezi ukawa na mkuu mzururaji, (Vasco da Gama) njuluku yenu na uchumi vikawa na nguvu. Huwezi kuwa na mafisadi na vidokozi kila kona huku watu wakikwepa kodi wakisaidiwa na waajiriwa wa lisirikali kaya ikasongoa mbele.

Huwezi ukawa na kaya inayowazawadia wezi malipo na marupurupu baada ya kuibia nchi isishuke thamani.

Aloo! Ngoja niwahi chachi nikasuke mipango na wale maaskofu na nikotoka pale nikafanye mikakati na wenyeviti wa mikoa wa CCM yangu. Mpo hapo waliwa?

Naona gari la msajili wa vyama. Acha nimuwahi anisajilie chama chap chap mradi hakitishii maslahi yake binafsi.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 9, 2011.

No comments: