The Chant of Savant

Wednesday 2 November 2011

Makinda amedhalilishwa au kuambiwa ukweli?




Vyombo mbali mbali vya habari hivi kariubni viliripoti kile vilichokiita kudhalilishwa kwa spika wa Bunge Anne Makinda kunakodaiwa kufanywa na mtangulizi wake Samuel Sitta waziri wa ushikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa safu hii si mara ya kwanza wala ya mwisho kuandika kuhusiana na mnyukano huu baina ya maspika wawili aliyepo na aliyepita.

Maneno yaliyochukuliwa na vyombo vya habari kuwa yalilenga kumdhalilisha au yalimdhalilisha Makinda yalisemwa na Sitta aliyenukuliwa akisema, "Mwanzoni hakukuwa na suala la viti maalumu katika suala hili (la kuwania uteuzi wa kugombea uspika)...walidhani wataweza kutumia fedha kwa wabunge ndiyo maana tukagombea wengi, lakini wakaona haiwezekani kabisa, nikiingia nitashinda kwa kura, siku moja kabla ya uteuzi ndiyo wakaweka sharti hilo la mgombea awe mwanamke, hilo likanishinda..."

Tuangalie maneno ya Sitta. Je pesa haikutumika? Je ubaguzi, tena wa kijinsia, haukutumika tofauti na katiba isemayo ubaguzi ni mwiko? Je Makinda hakuchaguliwa kwa shinikizo la watu fulani waliotumia jinsia kama sababu tu? Kwanini Makinda siku zote alipokuwa akitakiwa kukanusha kuwa ni chaguo la mafisadi alikuwa akikaa kimya?

Ingawa safu hii haina tabia ya kumtetea mtu kutokana na kwamba hailipwi kwa kazi ya utetezi kama wasemaji wa wakubwa, kwa hili Sitta hajakosea. Amepiga kwenye kidonda na huenda bubu atasema kujibu mapigo na ukweli kujulikana. Maana, kwa wanaokumbuka mzengwe uliotembea kuhakikisha Sitta hakalii kiti cha spika bado wanakumbuka jinsi Makinda alivyochomolewa huko alikochomolewa na kusimikwa hapo alipo. Hili halina kudhalilishana wala kusingiziana. Je hawa wanaoona Makinda kadhalilishwa au hakupatikana kwa mizengwe wanawaona watanzania kama dagaa ambao hawana hata kumbukumbu?

Hata ukiwalinganisha Makinda na Sitta kielimu na uzoefu, Makinda hana uwezo wala sifa ya kumzidi Sitta kama tukiondoa makengeza. Kazi ya spika mara nyingi ni kazi ya kisheria yaani kutunga sheria. Ukiangalia mabunge yote ya nchi za Afrika Mashariki, ni Tanzania tu ambayo ina spika asiye na taaluma ya sheria. Hata ukiangalia kiwango cha elimu cha wawili hawa, utagundua kuwa Makinda hana elimu kumzidi Sitta hasa kwa kuzingatia uzito wa kazi ya spika. Je kwanini Makinda alifaa kuliko Sitta? Jibu ni rahisi kuwa kwa vile hana elimu wala uzoefu wa kutosha, ni rahisi kutumiwa na watu wachache kupitishia mambo yao bungeni. Makinda si hatari kwa mafisadi kama alivyokuwa Sitta.

Tangu Makinda aingie madarakani, ameishanusuru wakubwa zake. Mfano mzuri ni pale alipoamua kumfukuza mbunge wa Arusha Godbless Lema kwa kudai waziri mkuu Mizengo Pinda alilidanganya bunge na taifa aliposema watanzania waliouawa na jeshi la polisi kwenye maadamano ya CHADEMA ya Arusha ni watatu wakati ni wawili. Spika alipandwa na hasira kana kwamba aliyekuwa kaambiwa kadanganya si binadamu bali Mungu. Mfano huu mdogo waweza kukuonyesha tunachomaanisha tunaposema kuwa Makinda ni rahisi kutumiwa kutokana na upeo mdogo wa masuala ya kisheria na bunge.

Ukiachia kiwango cha elimu na uzoefu, hata ukiangalia nani anajulikana kwa watanzania kati ya Makinda na Sitta utaona tofauti. Kwa mfano, mwandishi wa makala hii anajua kuwa Sitta ni mume wa Magreth Simwanza Sitta. Ukimuuliza mwandishi mume wa Makinda, hawezi kukupa jibu. Japo suala la familia ni suala binafsi lina umuhimu katika uongozi wa umma. Familia zetu ni kielelezo cha sifa na uwezo wetu kwa taifa. Hivyo, kuna haja ya kujua maisha ya Makinda ya kifamilia na ikiwezekana kwa spika ajaye sawa na rais lazima familia yake ijulikane. Tunasema hivi kutokana na hivi karibuni nchi ya jirani ya Kenya jaji mkuu wa sasa Dk Willy Mutunga aliponea chupuchupu baada ya habari kutoka kuwa alikuwa kwenye taratibu za kuachana na mke wake. Ingawa alifanikiwa kuvuka kikwazo hiki, bado ithibati ya kifamilia ilionekana kuwa kitu muhimu katika uongozi. Hapa najua kuna wanaoweza kuja na utetezi kuwa watu kama Askofu Makarios wa Cicilia hakuwa na mke wala imla wa zamani wa Malawi Hastings Kamuzu Banda. Ukweli ni kwamba walikuwa na udhaifu mkubwa sana hasa Banda aliyefikia mahali pa kutaka kufilisi taifa kwa kutumia kimada wake Cecilia Kadzamira.

Turejee kwenye mada ya leo ya udhalilishaji. Makinda, kama hakupatikana kutokana na mizengwe baada ya mtangulizi wake kuonekana habebi mafisadi hasa kashfa ya Richmond, ni sifa gani ya muda aliyo nayo angalau moja acha nyingi? Tumalizie kwa kumshauri Makinda akubali ukweli kuwa uspika wake ulipatikana kwa njia haramu ya ubaguzi wa kijinsia ili kumkomoa Sitta kwa kuwashughulikia wezi wa Richmond ambao bado wana ndoto za kuwa rais wa Tanzania. Bila Makinda ama kutoa maelezo yanayoingia akili au hata kujiuzulu kutokana na kuendelea kuonekana tunda la mafisadi, ataendelea kukumbushwa ukweli huu. Historia ndivyo ilivyo.
Chanzo: Dira Novemba 3, 2011.

No comments: