How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 15 January 2025

Uhuru na usiri ni siri za mafanikio ya ndoa


Ndoa inapaswa kuwa huru na isiyotegemea au kuingiliwa na watu wengine katika uendeshaji wenu. Mliapishwa wawili tu na si mia mbili. Hivyo, jukumu na wajibu wa kutunza kiapo chenu ni lenu. Si la watoto wenu, marafiki, wazazi, mashoga, na wengine hata muwapende, kuwathamini, na kuwaamini vipi. Ndoa ni kama sehemu zenu za siri au siri asiyopaswa  kujua yeyote isipokuwa wanandoa. Hivyo, mna jukumu la kuilinda, kuitunza, na kuiimarisha au kuiachia ibomoke tokana na kushindwa kutimiza wajibu wenu. Hakuna apaswaye kuziona au kuzihudumia siri na sehemu zenu za siri isipokuwa wanandoa wenyewe. Nani mpambavu huanika chupi zake hadharani?
        Binadamu tumeumbwa na kujipenda na kujipendelea kuliko wengine hata kama kufanya hivyo kunaweza kuwaudhi au kuwaumiza wengine. Hivyo, unapaswa kujua kuwa mafanikio yako ni yako siyo ya kuwasimulia wenzako. Kitanda usicholalia, hupaswi kujua kunguni wake. Kama ilivyo kwenye siri ya mtungi, muachie kata pekee ajue siri za mtungi. Unawambia wenzio habari na siri za mwenzi wako ili iweje? Unategemea nini? Je wakikuumiza utamlaumu mwenzio au mwenyewe? Japo mfano wa hapo juu mwenzi wa mmbea aliyewapa siri za mwenzi wake ana makosa, na mumewe pia ana makosa. Ukilinganisha makosa ya wawili, utagundua kuwa mama ana makosa makubwa kuliko mumewe ingawa wote wana makosa.
        Japo kuna kipindi mambo huzidi kiasi cha waliotanzwa kutafuta msaada. Katika ndoa, linapotokea tatizo, ni muhimu likashughulikiwa na wahusika peke yao tena kwa usiri. Ndiyo mana tunasema siri za ndani ziishie chumbani. Zisivushwe hata kuchungulia sebuleni. Kama ikizidi sana, basi wahusishe wazazi wenuwa pande zote. Wao, wana uzoefu na uchungu na ndoa na mafanikio yenu kama wazazi. Na hata mkiwahusisha, mpime  michango na ushauri wao. Maana, wao hawajui thamani na umuhimu wa ndoa yenu kama nyinyi wenyewe. Ajuaye thamani ya mkonga ni tembo aliyeubeba. Na ndoa ni mkonga wenu. Wengine wanaweza kuukata wakauuza mkauawa au kuumia.
        Wakati mkikumbana na mitihani katika ndoa na kutaka msaada au ushauri, mnapaswa kujua kuwa hao mnaowafuata nao wana changamoto, kasoro, na matatizo yao. Kama ikizidi sana, turudie na kusisitiza wahusisheni wazazi wa pande mbili japo nalo hili linataka utafiti na umakini vya hali ya juu. Hata hivyo, kuna angalizo. Kuna baadhi yetu wamezaliwa kwenye ndoa za mitala au zilizoharibika.             Hivyo, unapowahusisha wazazi, pia uzingatie ithibati, ubora, au udhaifu wa ndoa yao mbali na uwezo wao wa kujadili matatizo na kuyatafutia suluhu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa ndoa yako ni yako na si yao kama ambavyo ndoa yao si yako bali yao. Mnapozoea kuwapelekea watu matatizo yenu, mnayazidisha na kuyafanya yawe magumu zaidi kuliko mkiyashughulikia wenyewe. Hii ni kutokana na namna mnavyoyaeleza kwao na namna wanavyoyaelewa au hata kutoyaelewa. 
Mlipoamua kufunga ndoa mlikuwa peke yenu na wengine walikuwa mashahidi tu. Mjue baada ya kukubaliana na kufunga ndoa, mlitoa taarifa kwao kama sehemu ya hitajio la kijamii na kisheria. Kwenye changamoto, matatizo, na migogoro ya ndoa, msiwahusishe hata wapambe au mashahidi wenu. Wanaweza wasiwe na utashi, uzoefu, hata nia njema nanyi.
        Mwisho, jikumbusheni. Ni ndoa ngapi zimevunjwa na mashahidi wake? Hakimu wa kwanza wa kushgulikia changamoto na matatizo ya ndoa ni wanandoa wenyewe na mahakama yao ni chumba cha kulala.
         Hivyo, ndoa inapaswa kuwa taasisi huru ambapo uhuru huu ulindwa kwa wivu na tahadhari kubwa. Tunaposema uhuru, tunamaanisha uhuru wa kutoingiliwa na yeyote. Hakuna apaswaye kuwa na uwezo wa kuamua lolote kwenye ndoa isipokuwa wanandoa wenyewe. Tutoe mfano. Mwanandoa mmoja mzembe na hatari kwa ndoa yake alizoea kuwapa marafiki zake siri za mwenzi wake. Moja ya siri alizotoa ilikuwa ni ukubwa wa maumbile yake na namna alivyojua shughuli. Katika hao marafiki, walikuwamo wakware waliokuwa wakimmezea mate mwenzi wake. Hivyo, kutotunza na kulinda siri za ndoa yake kuligeuka angamizi la ndoa yenyewe hasa wahusika walipokula njama kumuandamana mhusika na wakampata kirahisi.
Chanzo: Mwananchi, J'pili.


No comments: