How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 16 November 2024

“Wewe hukusoma” na Madhara Yake Katika Ndoa

Tokana na uzoefu wetu, tumesikia, kusoma au hata kushuhudia kisa kifuatacho ambacho ni chanzo kikubwa cha kudorora, kuvurugika, au hata kuvinjika kwa ndoa. Ni sumu kwa ndoa.  Tuanze na hadithi. Kuna jamaa mmoja ambaye aliishia darasa na la nne. Alibahatika kujihangaisha na kupata utajiri. Ulipofika wakati wa kuoa, alioa mwanamke aliyekuwa kamaliza fomu four tena failure. Huyu mama, kwa ujinga, alipojilinganisha na mumewe, alijiona msomi wakati hakuwa msomi bali mjinga mkubwa kuliko hata huyo mumewe ambaye aliweza kutengeneza utajiri bila ‘kusoma’ wakati yeye aliyesoma, aliufuata huo utajiri. Je wapo wangapi wa namna hii? Yaani form four inakutia kichaa hivyo? Ukipata PhD itakuwaje?

            Pamoja na kutolewa kwenye família maskini na umaskini unaonuka mbali na kukosa hata hizo sifa za chini kabisa kufaa kuolewa, huyu mama tunayemouna mpumbavu, alijiona msomi wa kupigiwa mfano wakati alikuwa mjinga asiyemithilika kama tutaangalia dhana ya usomi ni nini. Kwa ufupi, usomi siyo wingi wa shahada au miaka mingi darasani bali unyenyekevu na utayari kusaidia wengine. Ni kama mtu aliyebahatika kufumbuliwa macho anayeishi na vipofu au vyongo. Ni sawa na tembo anayeishi na wanyama wadogo wanaotegemea awasaidie maadui zao wanapowazengea. Usomi ni kujua udhaifu wako na kutambua ubora wa wengine hata kama unawazidi elimu. Huu ndiyo usomi tunaomaanisha hapa.

            Maisha na ndoa havina shahada zake bali unyenyekevu na kuwa tayari kunyenyekea na kuujua ubora na udhaifu wako na wa wengine. Hivyo, hata kama wewe umesoma kweli kuliko mwenzio, kisiwe kibali au nyenzo kumdhalilisha, kumdhulumu, na kumdhalilisha mwenzi wako hata wengine. Usomi si ubabe na majivuno bali unyenyekevu.

            Turejee kwenye kisa chetu. Mama huyu mjinga wa mwisho na failure, alijiona msomi si kwa sababu alikuwa amesoma bali kwa sababu hakuwa amesoma wala kuelimika. Usomi unapaswa kuchochea kumbukumbu na heshima kwa wengine. Tokana na ujinga hata upumbavu wa mama huyu, alikosa kumbukumbu mbali na wizi wa fadhila, uchumia tumbo, na ukatili vilivyotamalaki. Hata kama kweli mwenzio hakusoma, kwanini hukumwambia kabla ya kuoana? Kama usomi ilikuwa ni sifa uliyotaka mwenza wako awe nayo, kwanini hakusema mapema kabla ya kuingia makubaliano ya kufunga ndoa? Jibu ni rahisi. Alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo ila alifuata utajiri wa ‘mjinga’ huyu aliyetaka kumdhalilisha na kumnyanyasa,  kumwibia mbali na kumdhulumu.

            Iwe mwanamke au mwanaume, hupaswi kutumia usomi, utajiri, uzuri, ubora, na chochote kumdhalilisha, kumuumiza, na kumdhulumu mwenzako. Kabla ya kumuumiza, kumdhalilisha hata kumkatisha tamaa mwenzako, jiulize. “Kama unasema mumeo au mkeo hakusoma, je baba na mama, babu na bibi zako wamesoma?” Hata kama ungekuwa umesoma au wazazi wako wamesoma, bado huna haki wala haja ya kuutumia usomi wako dhidi ya mwenzio. Kabla ya kufanya hivyo, vaa viatu vyake. Jiulize “ingekuwa mimi, ningetaka nitenzwe vipi?” Kwa wanaotumia ujinga na upumbavu huu waambiwe. “Nyinyi si wajinga na wapumbavu tu bali mafisi ambao wako tayari kula hata watoto wao au fisi wenzao kwa sababu ya tamaa na upumbavu wao.”  Kama mlitaka kuoa au kuolewa na wasomi, au matajiri si mngechagua maprofesa au vyuo vikuu au mabenki. Mbona haya madai wahusika hawakuyatoa wakati wakiwabembeleza hao “wajinga’ wawaoe au kuolewa nao? Kimsingi, wote wanaokuja na visingizio kama hivi, si wajinga na wapumbavu tu bali matapeli na wavivu wa kutafuta wanaotumia ndoa kama sehemu ya kujipatia maisha tena kinyume cha maadili na utu. Tunasema hivi kwa sababu kabla ya kuingia makubaliano ya kuoana hasa kipindi cha uchumba, wahusika walikuwa na muda na sababu za kutosha kutoa mapendekezo, mapendeleo yao na ushauri kuhusiana na wanayetaka kuoa au kuolewa nao. Ni aibu kwa mtu mwenye akili kutumia upumbavu kama huu ili ima apate sababu ya kuvunja ndoa, kukomoa, kuumiza, au kumdhalilisha mwenzake.

            Tunashauri wenye tabia hizi mbaya waache. Pia, tunashauri wahanga wasimame na kuwauliza maswali magumu hawa ‘wasomi’ wao kama wazazi na ndugu zao hata nyumba zao wamesoma. Kwani, hata kama kweli wangekuwa wamesoma, usomi si majivuno wala manyanyaso bali msaada na unyenyekevu.

Chanzo: Mwananchi leo.


Monday, 11 November 2024

Usiolewe kwenda kufarakanisha ndugu

Kuna wanawake wapumbavu, wenye roho mbaya na wachoyo wanaokamia kuolewa huku wakipania kwenda eti ‘kuwakomesha’ ndugu wa mume! Mara nyingi, wanawake wa namna hii wanaokwenda kuolewa ili kufarakanisha wana familia ya waume zao ni mijitu isiyo na huruma wala maadili. Wanasumbuliwa na ujinga na uchoyo. Yupo mmoja alikamia kwenda kuwakomesha ndugu za mtarajiwa wake akidhani alikuwa anawapa fedha nyingi. Ajabu ya ajabu, huyu mama alimhusisha hata mama mkwe asijue hicho chema kakizaa, kukilea na kukisomesha tena akiwa single mother baada ya kufiwa na mumewe tena kwa kuuza vitumbua na kufanya kazi ndogondogo.

            Binti huyu kipofu kiakili, aliamua kupania jambo ambalo ima hakulijua vizuri wala kulifanyia utafiti. Pamoja, na kujiridhisha–––na waharibifu wengi wa namna hii hufanya hivyo–––mhusika hakufanya wala utafiti wala kuweka juhudi kulijua alilokuwa akipania kufanya. Kwanza, hakujua kuwa ukipanda ubaya, unavuna ubaya na isitoshe, maovu hayalipi ukiachia mbali ukweli kuwa tamaa mbele mauti nyuma. Alipofunga ndoa, alianza haraka kutekeleza malengo yake mabovu. Alianza kuwachukia ndugu za mumewe wazi wazi. Alianza kumdharau mama mkwe hata kumsingizia kuwa mchawa, kama wengi wafanyavyo wasijue wanaweza kuzaa watoto wa kiume wakalipwa na wakazawana wao au hata kabla.

            Pili, hakujua ukubwa wa tatizo alilotaka kulitengeneza hata aina ya adui aliyetaka kumtengeneza na kumteketeza. Hakujua kuwa kumbe mumewe alikuwa mdogo wa kwa kaka yake mwingine aliyekuwa akiishi kwenye nchi mojawapo ya Ulaya. Na katika mambo yaliyomvutia kuolewa na huyu jamaa ambaye hakumpenda vilivyo, ilikuwa ni kuambiwa mpango wake wa kuhamia Ulaya. Hata hivyo, mpango huu ulitegemea kaka mtu yaani shemeji yake ambaye alikuwa kipenzi cha familia na aliyekuwa na ushawishi mkubwa kufikia kuwa kama baba wa familia ambaye asingefanya uamuzi wowote bila kuhakikisha anapata na kuutumia ushauri wa mama yao. Hivyo, kuanza kupambana na mama mkwe, huyu mama alianza, bila kujua, kuvuruga ima mpango mzima wa kwenda Ulaya au kuendelea kuolewa. Kufupisha kisa, mama alikosa vyote kwani aliachika hata bila kwenda huko Ulaya alikokamia au kuwakomesha ndugu wa mumewe. Mume au mke haoti kwenye mti. Anatokana na ana watu waliomtegeneza na waliomzunguka. 

Hili liwe somo kwa wenye mawazo kama hayo. Kama wapo waliofanikiwa kuchonganisha na kukomesha familia walimoolewa, ni wachache. Nao pia, hawajui kama Mungu akiwapo uhai, wakazawana wao watawalipa vipi. Wahenga walituhusia kuwa malipo ni hapahapa duniani.

Kuna kisa kingine. Kupo mmoja aliyewahi kujuta kwanini hakuolewa na mume ambaye wazazi wake walikuwa wameisha kufa. Hii ilitokana naye kutoelewana na mama mkwe wake. Huyu mkazana mwana, alikuwa mjinga na mshirikina hakuna mfano.  Kuna siku alikwenda kuomba ushauri kwa mjomba wake ambaye alimkemea na kumuonya juu ya hisia na tabia hizo. Alimwambia ‘omba Mungu mama mkwe wako asifariki. Anaweza kufariki mambo yako yote yakaharibika.” Na kweli, tokana na kumtia presha za hapa na pale, mama mkwe hatimaye alikufa ghafla kiasi cha kuzua wasiwasi kuwa alikuwa ima amelishwa sumu au kuzidiwa na mawazo tokana na mkazamwana alivyokuwa akimtenza.

            Baada ya mazishi tu, mume wa yule mama alianza ufuska hadi kuzaa watoto kadhaa nje ya ndoa. Raha aliyokuwa akitegemea kuipata baada ya kufariki kwa mama mkwe ilitoweka na akaja kujutia kuwa kumbe kuwepo kwa mama mkwe kulikuwa na neema zake.

            Je ni wangapi wamefanya au wanajua au kuwajua waliofanya visa kama hivi viwili kati ya vingi katika ndoa kuhusiana na ndugu japo nao siyo malaika? Je vinawasaidia nini wao na wenzi wao na wale wanaotaka kuwaumiza tokana na ujinga na upumbavu wao? Ni wangapi wanaolewa na kupendelea ndugu zao huku wakiwatenga na kuwachukia ndugu za waume zao? Licha ya kuwa unyama na upumbavu, tabia kama hizi zinaonyesha roho mbaya, ujinga, uroho, uchoyo, ukale, ushamba, na mengine kama haya. Kwa wale wanaoolewa kwenda kula au kuchuma mali, walewe. Mara nyingi, huwa wanaishia kujuta. Kama wewe unawachukia ndugu wa mumeo  hivyo, kama una kaka, unajisikiaje mkewe anapoanza kuwachukia nyinyi na wazazi wenu? Mkuki kwa nguruwe.

Chanzo: Mwananchi Jpili.

Thursday, 7 November 2024

Kapumzike salama Jenerali David Musuguri


Mpendwa Jenerali David  Bugozi Waryoba Musuguri Nzangho aka Chakaza (RIP),
Kwanza, nakupigia saluti ya mwisho kama mgeshi aliyelala. Pili, niseme wazi. Najua hutapokea wala kujibu saluti yangu kama kiongozi na mkuu wa mafyatu. Nenda salama salimini ukijua kuwa mafyatu watakumiss sana. Ulikuwa fyatu wa kupigiwa mfano. 
    Siombolezi bali nasherehekea kuondoka kwako. Old soldiers never die, they simply fade away. Baada ya kushughulika kwa miaka 104 na ushei, kwani ulibakisha miezi miwili tu kupiga 105. Si haba. Sasa rasmi umelala milele. Nenda shujaa mwenye sifa zilizotuka ndani na nje ya kaya. Ulifanya mengi kwa kaya na Mungu akulipe huko uendako. Amina. 
   Najua hutanisikia. Lakini acha nikupe send off na maua vya kifyatu. 
Kwanza, ulikuwa fyatu mwenzangu uliyemfyatua na kumchakaza nduli Idi Amin na kuwakomboa waganda. Kila niendapo UG, huwa najisikia fahari niitwapo mkombozi. Wengine hunisonya kwa sababu tulimfyatua nduli tukafyatua M7 ambaye, kwa takriban miaka 40, amekuwa akitembeza undava yeye na familia na marafiki zake. Sorry bro. Siku hizi siruhusiwi kuongea siasa. Hivyo, naomba unisamehe nisikumegee ujiko mwingi tunaoupata tokana na kazi yako.
            Pili, kwa wasiokujua Jenerali na mkuu wa mageshi mstaafu, hasa vijana wa kileo, ni kwamba ulikuwa mwanajeshi tangu ujanani. Ulijiandikisha geshini mwaka 1942 ukiwa na umri wa miaka 20. Hii ni baada ya maza wako kunyotolewa roho kwa tuhuma za kijinga zisizokuwa na kichwa wala miguu za uchawi. Hivyo, ukiwa na vijana wenzako akina Mugendi Nyamatwema na Mkono wa Nzenzere, mliamua kujiandikisha geshini ili mkachichue na baadaye kuitumikia kaya.
Tatu, kwa mujibu wa historia yakeoambaye sisi tunaokujua tunaijua. 
Ulizaliwa Januari 4, 1920 huko Butiama alikozaliwa marehemu baba wa taifa. Hivyo, hamkuwa marafiki tu bali wa poti kama akina mura wapendavyo kuitana yaani wa kunyumba au wa nyumbani. Baada ya kujiandikisha, siyo kujiunga jeshini, ulipelekwa Madagascar na kupata mafunzo ya kigeshi kabla ya kwenda sehemu nyingine tena ukiwa chini ya KEA au King’s African Rifles (KAR) wakati wa mkoloni wa kiinglishi. 
Baadaye, ulipelekwa Nairoberry pale Kahawa Barracks ulipokutana na nduli na kumfundisha ugeshi. Kwa wasiojua, nduli aliposikia kuwa mmowapo wa makamanda waliokuwa wametumwa na kaya kumfyatua ulikuwa mwalimu wake, alichukua helkopta na kutoroka haraka ili asipate cha moto na kipigo cha mbwa kachoka toka kwa Jenerali Chakaza. Maana, alijua shughuli yako Jenerali ambaye kweli ulionyesha vitendo kwa kuikomboa UG ndani ya muda mfupi tofauti na wengi walivyotegemea.
        Katika uhai wako, nakumbuka ulipata masomo mbalimbali nchini China na Kanada na mbali na kuwakilisha Afrika Mashariki London Uingereza kwenye gwaride la Malkia mwaka 1957 mbali na kupigana vita nchini Burma, India, na Ujepu ambako ulijeruhiwa paja na kupona na kuendelea kudunda kigeshi.
            Jenerali, kama lilivyokuwa jina lako, ulichakaza lakini hukuchakaa. Kwani, ni wachache wanaoweza kupiga miaka mia na ushei halafu wakafyatuka wakiwa na hali nzuri kama ulivyokuwa. Mwenyezi Mungu amelipa ujasiri na wema wako kwa kaya yetu. 
    Naomba, ufikapo huko uendako, wasalimie rafiki na ndugu yako Bwana mdogo wako lakini bosi wako Julius Kambarage Nyerere, Eddie Soikoine, Rashid Kawawa, Ali Hassan Mwinyi, Hussein Shekilango, majenerali Abdallah Twalipo, Tumainiel Kiwelu, Ernest Mwita Kyaro, Mti Mkavu Silas Mayunga na wengine wengi bila kusahau wasoja wetu waliodedishwa kule Uganda wakipigania  ukombozi wa kaya yetu. Habari njema ni kwamba CDF wetu wa kwanza, Jenerali Mrisho Sam Hagai Sarakikya bado anadunda tana kama yanki na mgeshi asiye na mfano. Mungu amuongezee miaka kama wewe. Amina. Saluti yake kamanda.
            Kwa vijana wa sasa wasiokujua, natumia fursa hii kuwafyatuliwa ukweli juu ya kutukuka kwa urathi wako. Ulikuwa mkuu wa mageshi yetu ambaye aliteuliwa wiki moja baada ya kurejea toka kumfyatua nduli. Ukakamavu na weledi wako wa medani ya kivita ulisababisha kaya kumfyatua huyu mjivuni aliyekuwa na domo kubwa kiasi cha kuwanyanyasa na kuwatisha maadui zake lakini asifue dafu kwako. 
    Pia, ulikuwa kiongozi usiyejivuna wala kuwatumikisha wenzake zaidi ya kuwatumikia na kuwa tayari kujitoa kafala kwa ajili ya wengine. Umeacha turathi ya kuigwa na kupigiwa mfano kama msoja na mwanakaya fyatu ingawa siku hizi ni wachache wanaoweza kukuiga tokana na uongozi kugeuka uongo na usasi wa ngawira. Hayo tuache nisije nikafyatuliwa bure. Kimsingi, nidhamu yako iwe kijeshi au hata baada ya kustaafu havitasahaulika. Ulitumikia kaya kwa ari na mori vya hali ya juu.
        Nasikitika sitahudhuria mazishi yako kwa vile niko mbali kwenye misheni ya kuokoa kaya toka kwenye ufisi na ufisadi. Sitafaidi sauti za mizinga ikilipuliwa kuonyesha kuwa shujaa umeondoka kishujaa na kuagwa na mafyatu na mashujaa wenzako.
        Tokana na kutokuwa na muda wa kutosha, acha nikuage fyatu mwenzangu. RIP David Bugozi Musuguri shughuli umeimaliza na vita umeshinda.
Chanzo: Mwananchi jana.

Sunday, 3 November 2024

Ndoa, Mafanikio na Changamoto Zake

Ni watu wangapi wanatamani wangekuwa matajiri, kwa wale ambao si matajiri au ni matajiri lakini siyo matajiri wakubwa? Wangapi wanatamani kuoa au kuolewa na watu wenye mafanikio yawe kifedha, kielimu hata kimadaraka ambao ndiyo tunawaita matajiri? Bila shaka ni wengi. 
            Mafanikio au utajiri, una changamoto zake hasa kutokana na wahusika wanavyojiona au wanavyoonekana kwa wengine. Pia, mafanikio ni dhana ambayo inaweza kuwa na maana nyingi. Hivyo, hatutazama kwenye kuichambua au kuitafutia maana. Je mafanikio hata maanguko yanaondoa utu wa mtu au kumbadili kuwa kitu kingine? Je ni watu wangapi wanaotoka kwenye familia maskini wakaoa au kuolewa na watu matajiri au wanaotoka kwenye familia maskini wakaoa au kuolewa kwenye familia zilizofanikiwa? 
        Je mafanikio ni nini na tunayapimaji? Si rahisi kutoa majibu kwa maswali haya bila kujadili nini mtu binafsi anatafuta au kutaka.                                 Tunachoweza kufanya  hapa, ni kuangalia baadhi ya kesi zenye kutupa uzoefu ili katika kutafuta mwenza, mhusika ajue la kufanya au kutofanya.
 Je wakati wakitamani huu utajiri, waliwahi kujiuliza uhusiano wake na mafanikio katika mambo mengine muhimu katika maisha kama vile kupata watoto, ndoa bora, furaha, amani, ridhiko la moyo? Japo huu hauchukuliwi kama utajiri kwa vile ahusishi vitu anwai, vinaweza kuwa utajiri wa aina yake tena wenye thamani na umuhimu kuliko fedha au mali, madaraka, sifa na mambo mengine ya namna hii.
         Leo tutaongelea na kuunganisha mafanikio na ndoa. Tunatadurusu watu waliofanikiwa kuwa matajiri tena mabilionea duniani, au wenye madaraka makubwa duniani lakini wakashindwa katika taasisi ya ndoa.
                Kama utajiri wa fedha ungekuwa ndiyo ufanisi katika ndoa, matajiri wakubwa wa dunia kama vile Bill Gates, Elon Musk, na Jeff Bizos wasingetaliki baada ya kushindwa ndoa. Kama usomi ungekuwa ndiyo muhimili wa ndoa, wasomi wengi wasingeishi single pamoja na elimu na taaluma zao. Mapenzi hayana gwiji wa darasani bali wa darasa liitwalo dunia litoalo uzoefu kama tunaotumia mbali na kujielimisha. 
             Hakuna daktari wala profesa wa mapenzi. Hata marais pamoja na kulindwa na kushauriwa sana mbali na kuogopewa tokana na mamlaka yao, hawana mamlaka juu ya ndoa vinginevyo marais au mawaziri wakuu kama Boris Johnson (Uingereza), Justin Trudeau (Kanada), Silivio Berlusconi (Italia), Fredrik Reinfeldt (Sweden), Georgina Meloni (Italia) na marais kama vile Vladimir Putin (Urusi), Daniel arap Moi (Kenya) Fredrick Chiluba (Zambia),  Donald Trump (Marekani), Nicholaus Sarkozy (Ufaransa), Hellen Johnson (Liberia), na Mary Banda (Malawi) wasingeachika na kuishia kuishi wapweke.
            Hata hivyo, wapo watu waliofanikiwa katika yote japo, kwa watu maarufu ni wachache. Kwa uzoefu tu, tuawajua watu wachache wa namna hii kama vile bilionea Warren Buffett ambaye hata hivyo, pamoja na ubililonea wake, huishi maisha ya kawaida. Hatujui kama hii ndiyo sababu ya kuonekana amefanikiwa katika utajiri na ndoa. Pia, yupo Mark Zuckeberg na wengine wachache wakilinganishwa na walioshindwa katika taasisi hii. Hivyo, hatutajifanya majaji wa kuhukumu bali kutoa taaarifa kama chanzo na cheche vya wewe kufanya utafiti wako.
        Japo hatujui sababu za kutofanikiwa kwa ndoa za wahusika hapo juu, tunaweza kujenga dhana mbalimbali kama vile kuwa bize na mali, kuwa fahari tokana na nguvu ya fedha au madaraka kiasi cha kuamini kuwa mhusika anaweza kumpata yeyote amtakaye. 
                Tunajenga hoja hizi kutokana na hisia kuwa watu waliofanikiwa huvutia zaidi ya wasiofanikiwa. Hivyo, hii hali pekee yaweza kuwa chanzo cha kukwama katika ndoa. Hii hutokana na kuweza kuzidiwa ushawishi hata mikakati ya wale wanaotaka kuoa au kuolewa na matajiri. Wanaweza kujifanya kuwa yule ambaye siyo walivyo ili kupata fursa hii hasa wale wasaka ngawira, au kunyenyekea kwa muda ili waweze kupata wanachokitaka halafu wageuke na kurejea ule uhalisia wao. Pia, mafanikio yanaweza kuwa kichaka cha watu wengine kujiona ni bora kuliko wale ambao hawajafanikiwa kama wao. Hivyo, kuyatumia kuwanyanyasa hata kuwatumia kama vifaa vyao kiasi cha kuwaacha pale wanapowachoka au wanapogundua kuwa kumbe walitumika kama chanzo cha mapato kwa wenzao kiasi cha kustuka na kuachana nao. Pia, kupata wale ambao hawakuwategemea kinaweza kuwa chanzo cha kutofanikiwa kwa ndoa.
        Kwa machache tuliyodurusu hapo juu, unaweza kujitafutia mengine zaidi. Hivyo, tunaweza kuhitimisha kuwa mafanikio ya aina moja yanaweza kuwa maanguko ya aina nyingine. Si ajabu. Kuna usemi kuwa Mungu hakupi vyote. Mwingine unasema, kila neema ina mitihani yake na kila mitahani yaweza kuwa na neema zake.
Chanzo: Mwananchi leo.