Kuna jamii zina mila na tabia chafu miongini mwetu. Leo, tutawaonya wanandoa na watarajiwa kuzidurusu na kuzitahadhari na kuziepuka hata kama zimezoeleka kwao, zina faida nazo au wanazikubali tokana na kuzikuta nao wakazipokea na kuzishiriki bila kufikiri au kuchelea madhara yake. Kila binadamu ana mila na tabia ziwe nzuri kama kuheshimiana na mbaya kama vile kuchukuana au kupandana kama wanyama baina ya ndugu hata kama zinafichwa au kutoongelewa. Kwani, huwaandaa wahusika kuumia katika kesho yao. Ujue. Jana yako inaweza kuvunja ndoa yako kama unashikilia na kushiriki uchafu tutakao jadili.
Mila za kuchukuana au kushiriki mapenzi baina au miongoni mwa ndugu zipo. Jamii na makabila yanayozidumisha yanajulikana japo maadili ya Kiafrika yako wazi. Yanakataza mapenzi baina ya maharimu. Kwake, ni laana na unyama japo kuna jamii zilizohalalisha mila na tabia hizi. Kwa Waafrika wengi haya ni miigizo na uchafu utokanao na mila na tabia za kigeni. Tunajua. Kuna jamii hata dini zinaruhusu mfano, watoto wa baba mdogo, mama mdogo, mjomba, hata shangazi kuoana. Kimsingi, washiriki wa mila na tabia hizi chafu kwanza, ni wale ambao dini na mila zao zimehalalisha haramu hii. Pili, ni wale walioigiza uchafu na mila hizi japo havijahalalishwa katika desturi na mila za jamii nyingine zilizowazunguka.
Inakuwaje, watu, kama wanyama, wanafanya unyama huu bila kuchelea madhara yake? Japo hatuna majibu sahihi au jibu moja, kimsingi, hii hutokana na kutojua madhara ya laana na uchafu huu kwa wasiohusika wanapotokea kuoa au kuolewa na watu wasio toka kwenye makundi haya. Pili, ni dhana dhaifu kuwa huenda wale wasiotoka kwenye jamii hizi hawajui uchafu huu. Tatu, ni ile hali ya kujiaminisha kuwa wanaweza kufanya uchafu wao na kuuficha.
Tutatoa visa vichache hapa. Kuna jamaa mmoja toka kwenye jamii ya mila zinazoruhusu ndugu kwa ndugu kuchukuana aliyeoa mtu toka jamii nyingine isiyokuwa na uchafu huu. Jamaa, alikuwa mtu aliyemtambulisha kwa mkewe mzinzi toka kabila lake kama dada yake japo hakuwa dada bali mshikaji wake. Mke wa huyu bwana alimwamini mumewe na kumkaribisha ‘dada’ yake au tuseme aliyedhania alikuwa wifi yake.
Tokana na kuamini kuwa uchafu na uhayawani wao visingefichuka, wahusika waliendelea na ufuska wao bila shaka yoyote. Siku na miaka vilipita bila mke kustuka. Siku moja, rafiki wa mke wa jamaa aliamua kupasua mbarika na kuweka kila kitu wazi kuwa ‘wifi’ hakuwa bali mshikaji wa mumewe. Yule mama, kwanza, hakuamini. Pili, aliweka mtego. Siku isiyo jina, aliwafuma kwenye nyumba ya wageni wagoni hawa kuwaweka wazi. Kumbe hata yule mama aliyekuwa akidhani alikuwa wifi yake alikuwa kaolewa na mume toka jamii nyingine isiyoshiriki uchafu huu. Kufupisha kisa, wawili hawa waliokuwa wakiziniwa waliamua kuwaacha wazinzi wao na kufunga ndoa na kuendelea na maisha wakiwaacha wagoni wao na aibu na majuto ya maisha.
Kisa cha pili, mama mwingine tena mzee kuliko mumewe na mwenye sura mbaya ambaye alikuwa akitembea na mtoto wa baba yake mkubwa na mwingine wa shangazi yake mbali na utitiri wa ndugu waliompitia ambapo wa kwanza inaaminiwa alikuwa baba yake mdogo tokana uvumi kuwa baba yake alipokwenda masomoni nje, baba yake alimpa mimba mkamwana wake na kuzaliwa ibilisi huyu aliyeitwa Jeromu. Huyu dada aliolewa na mume mzuri tu aliyempenda vilivyo. Baada ya ukweli kufichuka kuwa, pamoja na kwamba walikuwa ndugu wa damu aliokuwa amewatambulisha kwa mumewe kama kaka zake waliokuwa wakimchukua mkewe, ndoa ilivunjika hadi mama akafa akiwa nungaembe.
Je visa kama hivi vya uhayawani utendwao na binadamu ni vingi gani na vimeshakwaza au kuumiza wangapi? Wahenga wanaasa. Aliyesima aangalie asianguke. Wale ambao hawajafichuka wajue kuna siku watafichuka na kujuta. Kuna sababu gani ya kuumiza wenzako kwa kushikiri mila za kihayawani na kinyama? Kwa wahusika ambao hawajafichuka, wajue ni suala la muda. Siri zao na uchafu wao vitafichuka na wataumia pamoja na kuwaumiza wengine.
Chanzo: Mwananchi J'pili.
No comments:
Post a Comment