How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 17 December 2024

Nafasi ya ndugu na jamaa katika ndoa

 

Kila mtu ana ndugu na jamaa ambao hawaepukiki kwa vile wahusika hawawapati kwa njia ya kuchagua au kupenda kama ilivyo katika ndoa. Hivyo, tokana na ukweli huu, kila wanandoa na hata ndugu na jamaa wanapaswa kujua nafasi na mipaka yao katika ndoa za ndugu zao. Kwa mfano, ndugu wote wa pande zote ni sawa kwa wanandoa. Wazazi kadhalika. Hivyo, wanandoa hata ndugu na jamaa, wanapaswa kujua namna wanvyoweza kuchangia kufanikisha au kutofanikisha ndoa za ndugu zao.
            Je ndugu na jamaa wana nafasi gani katika maisha ya ndoa za ndugu zao? Hapa hakuna jibu au majibu rahisi kwa swali hili. Maana kuna usemi kuwa ndugu wazuri ni wa mwenzio. Hivyo, unachopaswa kujiuliza ni kujiuliza. Je ingekuwa mimi, ningependa ndugu na jamaa zangu wafanye nini ili kuifanikisha ndoa yangu? Je nafasi, umuhimu hata ulazima wao ni upi? Je wanapaswa kuwekewa mipaka au kuwaachia uhuru wafanye watakavyo? Je wanajua thamani na uzito wa ndoa yetu? Je ndoa ikivunjika kutokana na sababu za ndugu, kwanza, nani waathirika wakuu, na pili, wao wataathirika vipi wakati watakuwa na ndoa zao?
            Japo mtu anaoa au kuolewa katika familia, ukoo, na jamii, bado ndoa ni mali ya wawili kabla ya wengine wote. Hivyo, katika mahusiano na ndugu na jamaa wa pande zote, ni muhimu kuzingatia uhalisia na ukweli huu. Hata katika nyumba iwe ya familia au ya ushirika, kuna mipaka. Mfano, siyo kila mwanakaya anaweza kuingia vyumba vyote. Pia, siyo kila mwanakaya ana umilki sawa wa nyumba. Nyumba ya familia ni mali ya baba na mama japo watoto na hata wageni wana haki ya kuishi humo tokana na utashi wa wenye nyumba.
            Tunatumia mfano wa nyuma na kaya kwa makusudi. Kuna baadhi ya jamii ambapo mtoto au ndugu yao akioa au kuolewa wao hufanya makazi yake kuwa makazi yao au sehemu ya kukimbilia adha na ugumu wa maisha. Hii si sawa. Ila kama wahusika watawakaribisha, si vibaya. Hata wakiwakaribisha, mjitahidi kutoingilia ndoa yao. Maana, ndoa ni agano la wawili tu. Japo watoto ni matunda ya agano hili, ila wao si sehemu ya agano. Hawakula kiapo wala kusaini vyeti vya ndoa, kwa wale waliosaini vyeti hivi. Matunda na maua ni sehemu ya mti ila ni kwa muda. Hata majani kadhalika na wakati mwingine matawi.
        Ndugu zenu wanapofunga ndoa, ni vizuri kuwapa muda wa kuishi peke yao na kusomana hata kufundishana, kupimana, kuzoeana na kujenga mazingira ya kuwakaribisha wengine katika familia yao changa. Mara nyingi tumekuwa tunasikia misemo ya ajabu kuwa mfa nawe si mzaliwe nawe bali mzaliwa nawe. Japo methali hii ina maana na mantiki, si katika kila jambo. Katika ndoa ni tofauti. Ndugu si mfa nawe na mwenzi si mla nawe bali mwenzi tena wa maisha. Usemi huu unaweza kutumiwa na watu wavivu na wajinga kuhalalisha uwepo wao katika familia ya ndugu zao hata kama hawatakiwi wala kuhitajika. Hapa ndipo usemi kama kichumvi cha mawifi husika tokana na kuwepo kwa kutokuelewana hata chuki baina ya wake na mawifi zao.  Tokana na mfumo dume, hakuna kichumvi cha mashemeji wa kiume. Je ina maana hakuna ugomvi baina ya wawili hawa hasa linapokuja suala la mali inapotokea mume akafariki au akiwa na mali jambo ambalo huvuta ndugu wa pande zote kutaka kutatulia matatizo yao?
            Tutatoa kisa kimoja. Ndugu wa mume aliwahi kumlalamikia kaka yake kuwa shemeji yake alikuwa akimzuia kuuza nyumba aliyojengewa na kaka yake mwingine. Kaka mkubwa alijibu kwa mkato, kama hakumzuia kukujengea nyumba, inakuwaje azuie isiuzwe? Japo kuna wake hata waume wabinafsi na wasiopenda ndugu wa upande wa pili, tunadhani, wahusika wa pande zote yaani wanandoa, ndugu, na jamaa, watumie busara kujua kuwa ndoa inapofungwa, inafungwa kwanza kabisa kwa mapenzi, makubaliano, mipango, maisha, na faida vya wanandoa. Tumalizie hapa.
Chanzo: Mwananchi Jpili, 11Desemba, 2024,

           

 

No comments: