MENGI yameishaandikwa kuhusiana na hotuba ya kipekee ya rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Mei 3 akiwatisha na kuwatukana wafanyakazi.
Rais alisema mengi. Cha mno na msingi mkuu wa hoja yake ilikuwa matusi na vitisho na kashfa. Huwezi kumwita mtu muongo na mnafiki ukaacha kumkashifu ikiachia mbali kumzushia. Ingawa rais yuko juu ya sheria, siyo dhidi ya makosa yasiyo ya jinai na baadhi ya makosa ya jinai.
Msingi mkuu wa hoja ya rais ilikuwa kwenye mfano wa mauaji ya Kilombero ambayo hakutaja yalifanyika lini.
Alikaririwa akisema kuwa yalitokea mauaji ya wafanyakazi wawili huko Kilombero wakati wa utawala wa awamu ya kwanza. Baada ya kutokea mauaji hayo, rais alisema kuwa mwalimu Julius Nyerere alijikuta akizongwa na viongozi wa wafanyakazi na wananchi.
Ndipo Nyerere aliposema kuwa vikosi vya kuzuia fujo (FFU) viliundwa na wananchi kwa ajili ya kuzuia fujo. Na katika kufanya hivyo lolote laweza kutokea hata mauaji!
Tuangalie hoja ya rais. Je waandamanaji ni wafanya fujo kisheria? Hapana. Kwani kuandamana ni kutekeleza haki ya kikatiba na si kufanya fujo au kuvunja sheria kama rais alivyosema.
Kwa kuwachukulia waandamanaji wanaotekeleza haki yao kikatiba kama wavunja sheria na wafanya fujo, rais amepotoka na kupotosha ukweli kwa makusudi mazima ili kufanikisha azma yake ya kuwatisha wafanyakazi wasigome.
Kimsingi alichokusudia rais ni kuwatisha wafanyakazi na kudhihirisha serikali yake ilivyokuwa imejiandaa kuwapiga na kuwaumiza kama wangeandamana. Je hapa kuna utawala bora na unaofuata sheria iwapo serikali chini ya amri ya rais inafinya na kukandamiza haki za kiraia?
Kitu kingine kinachojitokeza kwenye dhamira ya rais ni kuonyesha wazi wazi alivyo tayari kulitumia jeshi vibaya hasa kuzuia raia wasifaidi haki zao za kikatiba. Hii ni ishara ya uimla ambao haufai kwa taifa linalojiita la kidemokrasia. Ni kuishiwa kimkakati na kiutawala.
Kikosi cha kutuliza ghasia kimeundwa kwa mujibu wa sheria kuzuia fujo na siyo kukandamiza haki za kiraia kama maandamano na migomo. Maneno ya rais yanawapa kiburi askari wa FFU ukiachia mbali kubainisha kuwa wapo si kusimamia sheria bali kuilinda serikali hata inapovunja sheria. Yanalenga kuwapofua macho askari wajione ni bora hivyo kuwa tayari kupokea na kutekeleza amri kufanya uovu pale ambapo wanapaswa hata kukataa.
Kwa mujibu wa sheria ya sasa ya kupambana na jinai dhidi ya ubinadamu, ikitokea unyama ukafanyika kama ilivyotokea nchini Kenya baada ya uchaguzi, askari waliotii amri mbovu wanawajibika kama mtu binafsi na kutii amri haiwi kinga mbele ya mahakama ya jinai ya kimataifa (ICC).
Kikwete anaweza kutisha hata kuamru FFU watwange watu virungu na kuwatia ngeu hata kuwaua kama alivyokaririwa akisema, ajue. Mambo yamebadilika. Siku hizi marais kufikishwa mbele ya ICC huko The Hague si muujiza tena. Anaweza kutishia na watu wakapuuzia wakaadamana na akatimiza azma yake akaishia pabaya. Arejee ni kwanini kuna maridhiano ya haraka visiwani Zanzibar.
Kisa hiki cha matumizi ya maguvu na visingizio kinanikumbusha nchi ya Mizengwe kwenye kitabu cha SAA YA UKOMBOZI ambapo kikosi cha Pinga Pata Kipigo kinatumiwa na watawala wezi kujilinda dhidi ya wanakijiji wanaopinga kijiji chao kuuzwa kwa mwekezaji Gluton Sucker anayeshirikiana na watawala fisadi. Pamoja na kuogopewa kwake, PPK inajikuta si chochote si lolote mbele ya wanakijiji waliodhamiria kujiletea ukombozi.
Kimsingi hata polisi ni wafanyakazi tena wanaonyonywa na kufanya kazi kwenye mazingira hatari na magumu kuliko hata hao wanaokwenda “kuwatuliza”. Angalia nyumba wanazoishi na kiasi cha mshahara wanacholipwa. Angalia hali hii inapowasukumu kuishi kwa kutegemea rushwa kiasi cha idara yao kuwa kinara wa jinai hii. Hawa wakijitambua wanaweza kufanya kama polisi wa PPK katika kisa cha nchi ya Mizengwe.
Hapa lazima tutie nukta. Alichofanya rais ni gawanya na utawale au divide and rule mbinu chafu iliyotumiwa na wakoloni na maimla wengi duniani kutetesa na kunyonya umma. Tuliona kule DRC wakati ule Zaire. Imla Mobutu Seseseko alizoea kuwaachia askari wajifanyie watakavyo ili waendelee kujenga chuki na wananchi na kumlinda yeye wakijiona wao ni bora wakati siyo.
Hivyo, kabla ya kuendelea, tuweke msisitizo. Tunakosoa maana potofu iliyopokelewa kutokana na maneno ya rais. Tunafanya hivyo kama raia wenzake katika kutetea na kujadili masuala ya taifa letu. Laiti kosa hili lingetendwa na chombo cha habari,patilizi lisingeweza kumithilika.
Kama rais anawaona wafanyakazi kama wafanya fujo na wavunja sheria, basi hana haja ya kujadiliana nao. Kuondoa utata ni kwa rais kuitisha mkutano na kukanusha tafsiri mbovu ya matumizi na maksudi ya kikosi cha FFU na majina na sifa zisizofaa alivyowaita wafanyakazi yaani waongo, wanafiki, wafanyafujo na wavunja sheria.
Ingawa rais anaweza kujipa moyo kuwa ameshinda, ushindi huu ni kwa muda. Bila kugusa na kutatua kiini cha malalamiko ya wafanyakazi na watanzania wote,hata kama hawatagoma leo, watagoma kesho.
Na yote hii ni matokeo ya rais na utawala wake kushindwa kutimiza ahadi zake ukiachia mbali kutokidhi matarajio ya wananchi.
Hivyo ni vizuri kuacha jazba, matusi, visingizio na siasa na kuliangalia tatizo. Apambane na ufisadi ambao kimsingi ndiyo chanzo kikuu cha kushuka kwa mapato ya taifa. Hapa bila kufufua maadili ya uongozi yaliyorithiwa na madili ya viongozi, hata afanyeje hawezi kulikwepa jinamizi la migomo hata vurugu huko tuendako. Maana kilichofanywa na serikali ni kuwatisha ili wafanyakazi wakubali kufanya mazungumzo iwahadae.
Tufupishe makala kwa kumshauri rais aache kucheza na mgomo na kutegemea maguvu ambayo kimsingi ni matumizi mabaya ya vyombo vya dola ukiachia mbali kuwa ukandamizaji na uvunjaji wa katiba na haki za umma.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 12, 2010.
No comments:
Post a Comment