The Chant of Savant

Thursday 5 August 2010

Kuna nini bungeni hadi kukacha URC, U-DC?

HII si mara yangu ya kwanza kuandika haya niandikayo dhidi ya kadhia ya ufujaji wa fedha za walipa kodi maskini wa Tanzania.

Nimekuwa nikijitahidi kulidurusu na kulirejea kila nipatapo fursa. Hakuna kitu kinanikera kutokana na kupoteza pesa nyingi za umma ukiachia mbali kutumika kama mihuri kupitishia hoja mfu kama wabunge wa Viti Maalumu sambamba na wa kuteuliwa na rais.

Nijuavyo, mbunge ni mwakilishi wa umma katika chombo cha kutunga sheria. Na hawawakilishi hawa watu bali wamchague. Japo tumekuwa na sheria za kizamani za kikoloni zinazoruhusu gavana au rais ateue watu awatakao kumwakilisha bungeni na kupitisha hoja zake ilhali anawakilishwa tayari na waziri mkuu, tufikie mahali tukate minyonyoro hii ya ukoloni ambao unazidi kutufanya tuwe maskini na omba omba.

Bajeti yetu hutegemea wafadhili kwa zaidi ya asilimia 40. Bado tegemezi sisi hawa hawa tuna jeuri ya kupanua ukubwa wa serikali kwa kuongeza nafasi za uwakilishi wa makundi kupitia viti vya dezo au maarufu kama msukule ukiachia mbali kuongeza idadi ya wilaya majimbo na mikoa. Nani katuroga Yarabi!

Hivi karibuni kulitokea kituko ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma Betty Machangu, aliripotiwa kutiwa mbaroni na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kutoa rushwa ili achaguliwe kuwa mbunge wa viti maalum. Kunani bungeni kiasi cha watu kutelekeza hata ukuu wa wilaya ambao, kimsingi, hauna tofauti na ubunge kihadhi hadi wakimbilie huko?

Je, huyu mkuu wa wilaya pesa ya kuhonga kaipata wapi kama siyo rushwa? Ananunua nini ili afanye biashara gani? Je, anafaa kuendelea kuwa ofisini wakati kaishaonyesha wazi hafai na ana tamaa ukiachia mbali kuwa mtoa rushwa? Je, kuna tatizo wapi katika kuwachuja na kuwateua watendaji wa serikali siku hizi?

Maana huyu si wa kwanza wala mwisho kupatikana na kashfa kiasi cha kuthibitisha kuwa waliomteua hawakufanya home work yao vizuri kwa upande wa maadili na sifa ya kushika wadhifa husika.

Huyu licha ya kujidhalilisha amemdhalilisha na kumwonyesha rais kama kiongozi asiye makini katika uteuzi wa wasaidizi wake. Kituko zaidi, ni pale mtoa rushwa anaposhiriki kutunga sheria.

Hivi kweli huyu hatatunga sheria zinazolinda biashara yake kama ilivyowahi kutokea wabunge wetu kuidhinisha sheria ya kuridhia rushwa waliyoiita takrima? Je, namna hii tutamkomboa mwananchi?

Ubunge wa kina mama hapo zamani ulitumika kama uwanja wa wake za wakubwa na jamaa zao kuwabana na kuuhujumu umma. Sasa haitoshi, umegeuka wa watoa rushwa! Licha ya kuwadhalilisha akina mama na makundi, ni hongo ya jumla ya jamii.

Ni tunda la mfumo mchafu wa chama kimoja ambapo watawala waliwetengea akina mama na makundi ili kuwaingiza kwenye ulaji na kuwatumia, kuwanyamazisha, kuyahujumu na kuyachunguza makundi husika.

Unapingana na dhana nzima ya usawa na utawala bora ambapo jamii ilipaswa kuwawezesha wahusika kugombea nafasi za uwakilishi sawa na wengine. Tuwawezeshe akina mama badala ya kuwadhalilisha na viti vya upendeleo.

Kwanza, katiba yetu inapinga upendeleo, kujuana na mambo mengine kama haya. Bahati mbaya kansa hii imeukumba hata upinzani kiasi cha kuwa na nafasi hizi za udhalilishaji kwenye sera na uendeshaji wake!

Kama ubunge wa kuteuliwa kweli unalenga kuwakomboa walengwa basi wabunge husika wangetoka kwenye kada ya chini ambayo ina wana jamii wengi wanaodaiwa kuwakilishwa. Lakini si hivyo.

Pia ubunge huu ni mzigo kwa mlipa kodi ikichukuliwa kuwa mbunge atokanaye na makundi haya hulipwa marupurupu na mshahara mkubwa kwa kutofanya lolote sawa na wabunge wa kuchaguliwa zaidi ya kuwakilisha tumbo lake. Haya ni matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma.

Je, tufanye nini ili kuondoa huu motisha wa watu kukimbilia ubunge hata kama wanaofanya hivyo hawana sifa zaidi ya kuwa karibu na wakubwa na kutoa rushwa tena kwa mabilioni? Jibu ni rahisi kuwa siasa ni ajira kwa wababaishaji wengi japo si wote.

Si hilo tu. Ni katika siasa ambapo mwajiriwa yuko juu ya mwajiri, tofauti na ajira nyingine hadi kujipangia mshahara hata kwa kupingana na mwajiri kama ilivyotokea hivi karibuni nchi jirani ya Kenya, ambako wabunge walijipandisha mishahara na kutaka wasilipe hata kodi. Ni katika siasa ambapo rushwa uongo, kujuana na ubabaishaji kila aina humpatia mtu ajira.

Hapa Tanzania, kadhalika, wabunge wetu licha ya kutotimiza kile walichoahidi wakachaguliwa, ni watu wa kupokea pesa nyingi bila kufanya lolote la maana kwa mwananchi. Hivyo huu ni motisha mkubwa sana kwa watu wengi kukimbilia kwenye siasa. Maana ni ulaji wa dezo.

Kwa vile wananchi ambao hawawezi kuishi bila wawakilishi ingawa nayo ni dhana tu inayoanza kupitwa na wakati kutokana na wawakilishi kujiwakilisha, basi tukubaliane-tuwe na wabunge wa kuchaguliwa na wananchi kuwakilisha majimbo si jinsia, umri na upuuzi mwingine.

Kwani hao wanaowakilishwa na wabunge wa viti maalumu ni wana jamii ambao wanawakilishwa na wabunge wa majimbo. Kila jimbo la uchaguzi lina wanawake, wafanyakazi, watoto, wazazi, vijana na kadhalika. Isitoshe kuna wizara ya akina mama na watoto michezo, vijana na wengine.

Leo tuna wawakilishi wa kina mama, wazazi, vijana, wazee na upuuzi mwingine. Kesho tutakuwa na wawakilishi hata wa mashoga, tusipoangalia. Bado wakati tukitanua wigo wa utawala, tunatanua pia na ukubwa wa bakuli la kuombaomba!

Kuliwahi kutokea malalamiko mkoani Mbeya kuwa akina mama waliokuwa wakitaka kugombea ubunge wa viti maalumu walikuwa wakitakiwa rushwa ya ngono kiasi cha ubunge huu kuitwa wa chupi.

Ingawa hili lilizimwa kinamna, bado kuna ukweli. Huyu anayetoa rushwa kweli anadhamiria kumwakilisha mwananchi? Atamwakilishaje iwapo ameishamnunua tena kwa bei mbaya?

Kama tuna dhamira ya kweli ya kuwakomboa wanawake basi tuwape nafasi moja nyeti ya upendeleo (urais) ili wajikomboe vilivyo na kuondoka na nafasi hizi za rushwa na aibu.

Chonde chonde tuondolee aibu ya vitu maalumu. Tuwekee uwanja wa kupambana kwa usawa katika ubunge wa kuwawakilisha wananchi.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 4, 2010.

No comments: