How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 7 January 2009

Nini kitafuatia baada ya mawe?

WAHENGA walisema: Kila ufukapo moshi kuna moto, na mwanzo wa ngoma ni lele.

Hivi karibuni nchi yetu - ijiitayo kisiwa cha amani-imeshuhudia majigambo haya yakitiwa mitihani. Watanzania waliosifika kwa upole na upenzi wa amani walianza kuchoka. Wale waliozoea kutaniwa na majirani zao kuwa ni kondoo, walianza kuamka kwa kasi na namna ya ajabu.

Siku za hivi karibuni, tumeshuhudia matukio yanayoonyesha wazi kuwa Tanzania si kisiwa cha amani, bali kisiwa chenye imani ya amani.

Vilianza vitendo vya kuchoma moto nyumba za waliodhaniwa kuwa ni mafisadi huko Tabora. Baadaye kulifuatiwa na kuzomewa kwa mawaziri waliokwenda mikoani ‘kuelimisha’ umma juu ya bajeti.

Mambo yalienda yakiongezeka. Mara ghafla msafara wa Rais Jakaya Kikwete ukajikuta kwenye mashambulizi makali ya mawe kwenye Kijiji cha Kanga-Chunya Mbeya.

Funga mwaka ilitokea tarehe mosi Januari, 2009, ambapo msafara wa Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wassira, ulishambuliwa kwa mawe wakati ukitoka kwenye mkesha wa mwaka mpya huko Bunda. Bunda tuliyoizoea, mara iligeuka ‘Bonda.’

Je, nini kitafuatia baada ya umma kuonyesha wazi unavyoichukia serikali na ufisadi? Je, bado tuna ithibati ya kutamba kuwa tu kisiwa cha amani? Je, kweli tulikuwa kisiwa cha amani kimatendo au kinadharia.

Je, nchi yetu kweli ina amani iwapo kikundi kidogo cha wezi kinaweza kuuteka na kuutesa umma kikitajirishwa kwa jasho lao huku umma ukitopea kwenye umaskini?

Ni bora tukaambizana hasa watawala kuwa mambo yamebadilika. Tubadilike kabla hatujabadilishwa kwa nguvu na namna ambayo hatutaipenda, ukiachia mbali kutuacha msambweni.

Tuambizane tena na tena, haya yote tunayoshuhudia yakimong’onyoa ‘amani’ yamesababishwa na uongozi mbovu uliotanguliza tamaa na ubinafsi wa hali ya juu yamesababishwa na upofu na upogo wa walioshika usukani.

Haiingii akilini nchi inapata pesa ya kununua mashangingi ya wabunge lakini nchi hiyo hiyo ikakosa pesa ya kuwasomesha vijana wake, ukiachia mbali kuwa na hospitali, shule na barabara visivyolingana na kipato cha taifa.

Taifa limetekwa na wanasiasa na mafisadi. Wanalipokezana kama mpira au kijiti. Wanalielekeza kwenye maangamizi bila kuchelea lolote. Watu wanajifanyia madudu utadhani ni mwisho wa dunia. Ufisadi umepanda chati, hakuna anayekemea wala kuchukua hatua ukiachia mbali kesi za bora liende.

Kwa taifa makini, kashfa kama Richmond iliyomfukuzisha kazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mawaziri wengine, ingekuwa angalau imefikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Je, kinachongojewa ni nini kama si aina nyingine ya ufisadi wa kimfumo?

Kumekuwa na kansa ya IPTL. Serikali ya Awamu ya Tatu imelikalia hadi ikamaliza muda wake, sasa Awamu ya Nne imo madarakani, nayo ikilisogeza chini ya busati. Je, nani atalishughulikia balaa hili na lini?

Taifa lipo msambweni, kuna mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Vyombo vya habari vya ndani na nje vimeishahanikiza na kuchoka.

Je, serikali imefanya nini cha kuridhisha kuhakikisha usalama wa viumbe hawa? Je, hapa kuna amani iwapo baadhi ya Watanzania wanauawa kama wanyama huku serikali ikiwaridhisha na kuwaaminisha kuna amani?

Amani gani ambayo Watanzania hawa hawaioni ambapo uhai wao umegeuzwa bidhaa dukani?

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema: Afrika haiwezi kuwa huru iwapo kutabakia nchi hata iwe moja chini ya mikatale ya ukoloni. Kadhalika Tanzania haiwezi kuwa na amani iwapo kuna Mtanzania mmoja anauawa kama swala porini.

Kuna tatizo sugu la Zanzibar, mtafaruku wa Zanzibar sasa umekuwa ugonjwa sugu na kurithishana.

Mtafaruku ulianzia awamu zillizopita. Awamu ya Nne kabla ya kuingia madarakani iliahidi ingeumaliza. Waulize. Wamefikia wapi na kama hawajafika popote wana mipango gani inayoingia kichwani? Hakuna! Je, hapa bado kuna amani?

Leo hii Tanzania ni nchi pekee iliyoridhia ulanguzi wa mafuta na nishati, ajabu kisiwa hiki cha amani hakina muda wa kutenda haki sawa kwa wananchi wake. Wafanyabiashara wenye uchu na tamaa sasa wanafanya watakavyo kana kwamba hakuna serikali! Je, kunani? Je, kuna amani hapa? Kuna mshikamano hapa au mshikwamano?

Hali za maisha za Watanzania zinazidi kuwa ngumu. Gharama za maisha zimepanda sana. Je, haya ndiyo maisha bora tuliyoahidiwa na Rais Kikwete? Hii ndiyo safari ya Kanani tuliyoahidiwa tena kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya? Tutaanza lini safari ya maisha bora iwapo rais ameishakaa madarakani kwa zaidi ya nusu ya muda wa utawala wake?

Tumuulize rais bila kumuogopa, katika ahadi mia na kidogo alizotoa ametekeleza ngapi? Hakuna? Je, analipwa kwa kazi gani?

Ziko wapi nyumba zetu zilizonyakuliwa na utawala mbovu wa Benjamin Mkapa?

Tuulize bila kumung’unya maneno wala kuogopa kwani nyumba hizi ni mali yetu. Wako wapi kina EPA, hasa kampuni la Kagoda, Deep Green Finance, Meremeta na majambazi wengine? Serikali inangoja nini iwapo rais alituaminisha kuwa serikali yake si ya ubia na mtu?

Yako wapi maazimio ya kupunguza ukubwa wa serikali? Iko wapi mikakati na matendo ya kupunguza matumizi ya magari ya bei mbaya maarufu kama mashangingi? Ni hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alifanya mizengwe na kutuhadaa kuwa serikali ina nia na mipango ya kupunguza magari ya bei mbaya.

Kabla ya mate kukauka inagundulika kuwa kumbe serikali ile ile imeishaagiza utitiri mwingine wa magari hayo hayo! Je, hii biashara ya kuchuuza roho na rasilimali zetu bado inaacha mantiki ya kisiwa cha amani au kisiwa cha hayawani?

Umefika wakati ambapo kila muathirika aamke na kutetea uhai wake. Tuachane na kuishi kwa matumaini kuwa mambo yatanyoka na waliotuhadaa watatutendea haki.

Wameishachoka na kuishiwa, wameshiba mahajumati yatokanayo na jasho letu. Hamkusikia ya wahenga kuwa njaa ni mwana malegeza na shibe ni mwana malevya? Hamkuambiwa kuwa mwenye shibe hamjui mwenye njaa? Sasa nini kifanyike? Aliyeko juu usimngoje chini, mpandie na kumporomosha kwani huna cha kukosa ulikwisha kuporomoshwa naye.

Hapa ndipo umma unapopaswa kuacha masihara na mafisadi hata kama wako madarakani. Tutaendelea na kuganga njaa na kujikomba hadi lini? Tutaendelea kuwa mashahidi wa maangamizi yetu na vizazi vijavyo hadi lini? Mbona imetosha?

Tumechoka kudhulumiwa na kudanganywa. Tutangaze uhuru upya ili kujenga kisiwa cha amani ya kweli ambapo haki lazima itawale. Maana bila haki hakuna amani na bila amani hakuna haki.

Kwanini tumeridhika na kubinafsishwa kwa mafisadi na washirika wao wanaoitwa wawekezaji, wengi wao wakiwa ni kina IPTL, Kagoda, Richmond, ANBEN, Tanpower na wezi wengine?

Ni kisiwa gani cha amani ambapo watu wanapigwa risasi kwa kukatiza kwenye ardhi ya mgodi wa mwekezaji kama ilivyowahi kutokea huko Musoma?

Ni kisiwa gani cha amani ambapo wachimbaji wadogo wadogo wa Mererani wanawindwa kama swala? Ni kisiwa gani cha amani ambapo wastaafu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki wanakesha wakiomba mitaani kama hawakuifanyia kazi nchi yao?

Hakika tuseme kwa sauti moja na kuu. Hakuna kisiwa cha amani, na kama kipo ni kwa ajili ya wanasiasa na mafisadi wanaokula kushiba na kusaza huku umma ukiangamia kwa njaa, ujinga, maradhi na umaskini.

Hawa ndio maadui tulioazimia kuwatokomeza tulipopata uhuru. Bila maadui hawa kutokomezwa hakuna uhuru wala kisiwa cha amani. Kama kipo ni aina nyingine ya mahepe-usanii.

Je, umma utaendelea kugeuzwa mabunga na kundi dogo la wezi? Hakika umma huu utakuwa wa ovyo kuliko hata kundi la inzi. Je, baada ya mawe nini kitafuata? Hata zama za mawe zilifuatiwa na zama za moto.

Chanzo: Tanzania Daima Januari 7, 2009.

No comments: