Kazi na wajibu wa serikali yoyote halali duniani ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Serikali isiyoweza hili si serikali chochote bali kikundi cha watu kisichofaa kinachojipachika jina la serikali. Kinaweza kikawa na sura ya serikali kwa maana ya kuwa na mihimili mitatu ya dola, bila kutimiza wajibu wa kuhakikisha usalama wa mali na raia wa nchi inayoongozwa hata kutawaliwa na hiki kinachoitwa serikali, si chochote na haifai kujiona wala kuitwa serikali.
Ukiiangalia serikali ya awamu ya nne tangu iingie madarakani, unagundua: haijatimiza matarajio ya wapiga kura. Na ukiangalia wakati unavyoyoyoma ndiyo basi tena. Kile watoto wa mjini hukiita changa la macho kimeishajiri. Rais Jakaya Kikwete akiwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliwaahidi watanzania mambo mengi.
Na hii ilifanya wamwamini na kumpa kura zilizomwezesha kuwashinda wapinzani wake. Lakini ukiangalia utendaji wake, kwanza hakuna ahadi hata moja aliyokwisha kuitekeleza wala dalili za kufanya hivyo hakuna ukiachia mbali kukumbwa na kashfa lukuki zilizoliingizia taifa mabilioni ya shilingi.
Kila mtanzania amekata tamaa sasa. Kikwete aliyetoa matumaini wakati ule siyo wa sasa anayekatisha tamaa na kutia kila aina ya shaka.
Kikwete aliyepagawisha watu hadi kuitwa kipenzi cha watu na chaguo la Mungu siyo huyu wa leo ambaye serikali yake inaanza kubeba sifa ya kutenda madudu kuliko hata ile ya hovyo ya aliyemtangulia.
Kikwete mwenye ushawishi na urahimu taratibu anaanza kuwa mtu wa vitisho hata kuonekana wazi kukanganyikiwa na kujihami ukiachia mbali kujitetea hata kuzidi kudanganya na kutoa visingizio.
Wazungu wanasema unaweza kumwamini mtu yeyote duniani lakini si mwanasiasa. Kikwete anaanza kulithibitisha hili kwa kasi ya ajabu kuliko hata mtangulizi yake ambaye angalau awamu yake ya kwanza alifanya si haba akaja kutibua awamu ya mwisho ya utawala wake unaosifika kuiingiza Tanzania kwenye matatizo makubwa.
Kikwete amehangaika kuweza na kutaka kuwaridhisha wananchi. Lakini ameshindwa kutokana na kujikuta katikati. Huku ana wananchi. Kule ana kundi dogo la mafisadi wenye madaraka wanaowahujumu wananchi.
Ahadi zake zote zimegeuka kuwa ndoto za Alinacha kiasi cha kutotoa matumaini.
Hakika chanzo cha maanguko na kushindwa kwa Kikwete kinajulikana kwake na kwa watanzania. Kwanza ni historia: uongozi na ushindi wake vilipatikana kwa hila ya kuchafuana na kutumia hongo. Amejitahidi kukaa kimya kila zinaporushwa tuhuma kuwa CCM iliiba pesa na kura bila mafanikio. Ameshindwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na ushindi wake kuhusishwa na hongo iliyokusanywa kwa njia ya kuuibia umma. Kashfa mbili kuu kati ya nyingi zilizogeuka majinamizi kwa Kikwete zinajulikana kuwa ni EPA na Richmond .
Alitumia vyombo vya habari vilivyonunuliwa na mtandao wake kuwabomoa wenzake huku vikimjenga. Sasa hana mbinu. Kwani umma umeishastukia vibaya sana ingawa anajaribu kuitumia tena kwa kupenyeza watu wake kwenye baadhi ya vyombo hivyo.
Chanzo kingine cha kushindwa na maanguko ya Kikwete ni aina ya watu aliojizungushia. Licha ya kurithi makapi ya watu fisadi wa utawala wa Mkapa, Kikwete aliongeza watu wake chini ya dhana ya mtandao. Hawa ni wawezeshaji ima kwenye wizi wa kura au wa fedha. Na hii ndiyo imekuwa sababu kuu ya Kikwete kushindwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani waliowezesha wizi wa mabilioni ya pesa ya umma. Akifanya hivyo watafichua hata mwingine ambao umma hauujui kama ule wa bilioni 155 za Meremeta na nyingine nyingi ambazo hazijaanikwa.
Kukwepa hili Kikwete alifungua kesi zisizo na mashiko za matumizi mabaya ya madaraka zilizowahusisha wakubwa wachache. Wengi waliichukulia kesi hii kama danganya toto na njia ya kupoteza muda ili liende na umma usahau.
Ukiondoa hayo juu, serikali ya Kikwete licha ya kutotimiza ahadi, imebainikia kuwa na matumizi mabaya na makubwa ya pesa ya umma. Rejea kugundulika upotevu na utumiaji vibaya wa pesa za umma ifikiayo trilioni moja uliofanywa na wizara mbali mbali.
Kinacholipa nguvu hili ni ile hali ya Kikwete, serikali yake na chama chake kushindwa kutoa angalau maelezo zaidi ya vitisho na visingizio.
Kitu kingine kinachoonyesha kushindwa vibaya kwa Kikwete ni ile hali ya kutokuwa na falsafa wala sera za kutawalia. Ukimuuliza Kikwete hata watanzania wengine nchi yao inatawaliwa kwa sera zipi, hakika, hakuna atakayekupa jibu sahihi zaidi ya kupiga siasa.
Kikwete aliwapa ahadi watanzania kuwa angewaletea maisha bora kwa wote kwenye kile alichokibatiza kuwa safari ya Kanani ambayo imegeuka kuwa safari ya kwenda Misri au jehanamu. Kwani maisha ni magumu kuliko hata yalivyokuwa wakati akiilinganisha hali ya mambo ya Misri.
Mfumko wa bei umefura kiasi cha kutisha ukiachia mbali ufisadi na wizi mkubwa kuzidi kuongezeka huku serikali ikihusishwa na kujikuta haina cha kufanya.
Wakati haya yakiendelea, Kikwete anajikuta akikabiliana na matishio makubwa matatu.
Mosi kushindwa kutimiza ahadi zake.
Pili kutoonyesha ushawishi kwa kubadili maisha kiasi cha kuhofia kupoteza kwenye uchaguzi ulioko mlangoni sasa.
Na tatu ufisadi ukiachia mbali kukata tamaa kwa wananchi na migawanyiko kwenye chama tawala. Rejea migomo na migongano ya mara kwa mara baina ya serikali na wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyakazi wanaodai malimbikizo na kuongezwa maslahi mengine.
Hali hizi zimefanya watanzania kukosa imani na serikali ya Kikwete na Kikwete mwenyewe. Vitu hivi vinamchanganya Kikwete ambaye watani zake wamempa jina la Msanii huku kila asemacho wakikiita ngonjera. Na kweli ni hivyo. Kwa mfano alimwaga pesa isiyo na maelezo ya jinsi ilivyopatikana maarufu kama mabilioni ya Kikwete. Haikufua dafu. Hadi leo ukiuliza imeleta mabadiliko gani, hakuna jibu la maana utapewa.
Kipindi kuelekea kwenye uchaguzi baadhi ya wachumia tumbo walitunga vitabu kumwonyesha Kikwete kama tumaini lililokuwa limerejea. Waulize sasa wanasemaje. Ni aibu. Hawaongelei hili. Nadhani hata vitabu vilivyoandikwa vimeishatolewa kwenye shelves. Kwani licha ya kutokuwa na maana ni uongo na kujikomba vikilenga kumhadaa Kikwete na wananchi.
Kusuasua na kusogezwa sogezwa kwa kashfa za EPA (Kagoda) na Richmond ni ushahidi tosha wa kushindwa Kikwete kiasi cha kutofaa kurejeshwa kwenye uchaguzi ujao. Hili litategemea na umakini na uchungu wa wtanzania waathirika.Hakika Kikwete ni tumaini lililopotea.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 21, 2009.
No comments:
Post a Comment