MIE ni mtu mkubwa tu. Nimewahi kutumikia kijiwe katika nyadhifa nyingi nono nono tu. Pamoja na ukubwa wangu, nina roho ndogo na nyepesi kama fisi hasa nionapo wale viumbe wanaovaa gagulo.
Na huu umegeuka mzigo unaoninyima raha kiasi cha kufanya maisha yangu yakose maana hasa baada ya kustaafu.
Nikiona mguu tu huwa nachanganyikiwa. Nikiona kiuno ndiyo usiseme. Huwa nakufa ghafla na kufufuka baadaye. Maisha ya namna hii yana gharama zake hasa aibu na majuto usiambiwe. Kwani kila mtu angetaka aheshimike na kuthaminiwa. Kwangu hili hakuna. Ni mateso. Mateso matupu usisikie.
Nilianza na house girl nikamdunga mimba akanizalia mwanaharamu. Sijui hapa mwanaharamu ni mimi mama mtu au mtu mwenyewe! Nimejaribu kumkana bila mafanikio.
Baada ya kunogewa nilimdunga aliyekuwa chini yangu na kumzaa huyu karukarange aliyevamia hekalu yangu na kuniacha nyang’anyang’a mbele ya mshirika wa bedroom.
Kwa vile ni mkubwa nilikimbilia vyombo vya dola nikawini kwa muda.
Ukweli huumiza lakini huweka huru na kuponya. Badala ya kuwakana wanaharamu wenu wakubaliane na muongee na washirika wenu wa bedroom kuliko kutenda ukatili huu kwa viumbe wasio na hatia.
Hawa ni matokeo ya upogo na ufisi wetu. Hivi unapovua zipu hovyo hovyo na kutumia ulichonacho kumulika kila gagulo unategemea nini?
Aliwahi kuniuliza mshirika wangu wa bedroom (mke wangu) iliyogeuka kuwa badroom nikabaki kutoa mimacho kama bundi. Maana alichukia kuliko mbogo! Pamoja na ujogoo wangu, siku ile nilinywea usiseme. Tuache utani usaliti ambea usikukute.
Je, huko nje mko mafisi kama mimi wangapi tena wenye nafasi usioweza kuwategemea?
Dada zetu nao wanatumia miili yao kama duka.... acheni tunaumizana baada ya kuliwazana.
Unajua ilikuwaje? Nilikutana na huyu dada wakati ule akiwa chuma nami nikiwa bosi. Ni kutoka kabila la akina anko ambao huishia kuwa sweetheat. Tuyaache mshanielewa. Yethu! Kama hujanipata basi kajinyonge baada ya kupata mbege na kitimoto siku ya Krismasi migombani.
Kule kama unazo utachukua kila gagulo bila kujali ukoo au nini. Unasani nadanganya?
Anakujia dada unamdeku na kumzimii huku ukimwaga ofa kwa sana kwa janaume moja analosema ni kaka mtu. kumbe loooh! Kajisemea Samba Mapangala mwalishwa sahani moja! Kwani haya hayapo na hatuyaoni hata kama twayalimbika?
Dada zenu nanyi punguza razi mtatumaliza ukiachia mbali kuziweka ndoa zetu matatani.
Nanyi midume wenye ndoa acheni uchu hata kama mna pesa na nafasi. Ukimwi haujui cheo chako ukiachia mbali kuzalisha watoto wasiotakiwa wanaoteseka hadi wawagongee milango.
Nanyi kwa roho mbaya eti mnawaitia polisi kwa vile mna madaraka. Acheni. Huu nao ni ukatili kwa watoto ukiachia mbali kuwa unyanyasaji usio kifani.
Ngoja nikumegee stori. Soma taratibu bi mkubwa asikusikie akaninyotoa roho bure. Nilikuwa zangu nimepowa homu bila hili na lile. Mara mlinzi wa mlangoni akaja ndani kuita.
Kwa vile bi mkubwa alikuwa zake saloon nilikwenda kudeku kunani. Hamad! Nakumbana na binti niliyemzaa kwa kuzini! Sura huulizi.
Kwa vile sikuwa nimewahi kumnyakisha bi mkubwa nyeti hii, kwanza nilimwamuru mlinzi arejee lindoni. Nilimkaribisha ndani binti yule na kumsihi aniambie yeye ni nani ingawa moyoni nilishajua yeye ni nani.
Bila ajizi si alibwatuka kuwa ni binti yangu niliyemzaa kule mushie! Bila kungoja aongeze nilimwambia. “Ndivyo ulivyotuma uje kunidhalilisha na kuvunja ndoa yangu na maadui zangu waliosikia kuwa nataka kugombea ubunge siyo?”
Binti hakuamini masikio yake. Aliuliza kupata uhakika. “Unasemaje baba?”
Nilimkatiza. “Nani baba yako mwanaharamu wewe?” Naye hakujivunga. Alinizodoa. “Leo baba unanikana kwa vile uliyofanya kunizaa uliyafanyia sirini usijue itafichuka!”
Nilimkazia macho na kumtishia nikisema: Unajua mimi ni nani?
Naye alijibu kwa kujiamini. “Wewe ni baba yangu mzinzi wa mama ambaye unanikana kwa vile una madaraka. Kumbe ukuu wote bure na hovyo!”
Kuona kibinti hichi cha kuzaa nje ya ndoa kinanipotezea muda na kuweza kusababisha bi mkubwa atukute, nilikiomba nikipe shilingi laki tano kiishie kikakataa. Kilidai hakikuja kula rushwa bali kuishi kwao yaani kwangu!
Kuona maji yamezidi unga niliwaita vijana wa polisi wakakichukua na kukificha lupango kabla ya kukifungulia mashitaka ya kuvunja na kuingia, kushambulia, kuvuruga amani, kutishia maisha na false presentation ukiachia mbali mistake of facts and abracadabra and bragadaccios.
Kufika mahakamani si watetezi wa haki za watoto walitaka kunivua nguo. Eti walinitaka kupima DNA! Kwa kujua ukweli ulioko nyuma ya longo longo zangu niligoma lau kuficha aibu. Maana ningekubali ningekuwa sawa nimejitundika kitanzini au kujipeleka majilini ilhali nikijua matokeo yake. Nani apime DNA? Thubutu yako. Hadithi ni ndefu.
Baada ya kunusurika zali la kibinti cha kuzaa nje ya ndoa, nimepiga marufuku getini kwangu kuonekana visichana au vivulana au wanawake wenye vitoto. Bila kufanya hivyo naweza kujikuta naumbuka bure huku mshirika wangu wa bedroom akinipiga talaka kipindi hiki ambacho sina ukuu tena ukiachia mbali uzee kuingia.
Zilzala hili limezusha bonge ya sheshe. Maana tangu habari hii ibumburuke mshirika wangu wa bedroom amenigomea. Huwezi kuamini tunalala mzungu wa nne huku akitishia kuomba talaka na kutoboa siri za mimali niliyoficha kama Freddie Chiluwa alivyobanikwa na bi mkubwa wake alipodai talaka.
Yaani huwezi kuamini. Kashafa na siri zangu za ulaji nilipokuwa na madaraka kijiweni zinaanza kufichuka. Mwenzenu roho inaniuma sina mfano.
Kwani nimemkana mwanangu mwenyewe ukiachia mbali ndoa yangu kuingia madoa kibao. Jina langu ndiyo usiseme. Kila mtu anajua mimi ni changupaka wa kutupa.
Hata maswahiba zangu hawaniruhusu kwenda majumbani mwao bila kuwepo kwa kuogopa nitawatongoza ama wake zao au vibinti vyao! Ama kweli hujafa hujaumbika walisema wahenga.
Nani alijua dume kama mimi ningetishiwa kuvikwa gagulo kutokana na tabia yangu ya chovya chovya na mulika mulika.
Je huko nje mko wangapi ambao arobaini yenu haijawadia kama yangu? Nanyi mkisoma mkasa wangu mnanicheka au mnanionea huruma? Natamani ningekua Jake Zumari aliyezaa na binti wa rafiki yake na wakakubali yaishe.
Hata hivyo ajue walikubali yaishe kutokana na kuwa na madaraka. Baada ya hapo linaweza kubumburuka tena akaumbuka.
Naona hiki kibinti kinakatiza na miguu mizuri kama ile. Sijui nikinyemelee? Loh! Kumbe sijamaliza balaa hili narukia jingine! Ngoja nijikate kabla mshirika wa bedroom hajanikuta akanivisha gagulo.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 4, 2010.
1 comment:
Hewalaa mkuu. Hii imewakilishwa barabaraa. Kwa staili hii mafisadi wenye uroho wa fisi maji watakwenda na maji. Na udumu nabii.
Post a Comment