The Chant of Savant

Sunday 14 August 2016

Kufungiwa Mseto ni vitisho na uonevu


            Kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la Mseto tokana na kile kinachodaiwa kuandika habari za uchochezi, kuna kila sababu na ushahidi kuwa hatua hii–licha ya kulihujumu  gazeti na kutishia uhuru wa vyombo vya habari–imelenga kulikomoa na kulinyamazisha gazeti kama onyo kwa magazeti mengine yasiyolalia upande wa watawala.
Kwanza, inashangaza kuona Tanzania bado inatumia sheria ya kikale ya mwaka 1976 iliyotungwa wakati wa mfumo wa utawala wa chama kimoja
Pili, kuna mambo kadhaa yanayothibitisha kuwa uamuzi huu umefikiwa kwa hasira, visa au kutojua na kuheshimu haki za kikatiba. Kinachogomba sana ni suala lenyewe lililosababisha kufungiwa gazeti. Mbona magazeti mengine yameandika makubwa kuliko hili na hayakufungiwa bali kuamriwa yakanushe na kuomba msamaha? Rejea gazeti moja la kila wiki kuandika habari za ufisadi wa waziri mmoja mwanadamizi na kupotea kwa zana muhimu ya kivita kwenye taasisi moja nyeti bila kufungiwa? Je kuna sacred cows na black sheep hapa?
Tatu, tokana na ukandamizaji wa haki hizi za kikatiba za raia, kuna maswali kadhaa yanakosa majibu yaani:
Nne, kwanini kampuni moja kufungiwa magazeti mawili ndani ya kipindi kifupi kama hakuna namna? Kukosea kwenye taaluma yoyote ni jambo la kawaida. Linapotokea hili, mhusika hupewa fursa ya kujitetea au onyo; ndipo hatua zaidi hufuata. Kitendo cha kulifungia gazeti la Mseto tena bila kupewa haki ya kisheria ya kueleza upande wake ni dalili za watawala kutoa vitisho na kufanya udhalilishaji hasa kwa vyombo vya habari visivyolala kitanda kimoja nao.
Tano, kwanini waziri mhusika hakujua kuwa kufungia magazeti mawili tena ya kampuni moja ni kuwanyima fursa ya kufanya kazi waajiriwa wa magazeti husika, ukiachia mbali kuwanyima wananchi haki ya kupata na kutoa habari? wakati rais anahangaika kutengeneza ajira, waziri wake anaua hata zile ambazo zimeishatengenezwa na sekta binafsi! Rais wa kwanza wa Marekani George Washington aliwahi kusema, “Iwapo uhuru wa kujieleza utaondolewa, kwa ububu na kimya, tutapelekwa machinjioni kama kondoo.” Je nani takubali udhalilishaji huu?
Kimsingi, msingi mojawapo wa utawala bora na wa sheria, ni kuruhusu, kuvumilia na kuishi sambamba na uhuru wa kujieleza, kutoa na kupata habari. Sitaki niamini kuwa serikali yetu imefikia hapa. 
Sita, kwanini waziri hakuweka maanani kuwa mwandishi aliyeandika habari husika alipewa tip–hata kama baadaye ilibainika kuwa feki, kama inavyodaiwa–akiwa na lengo safi la kufichua uovu?       Saba, je hapa kosa ni nini iwapo mwandishi alitumia taarifa alizopata akiamini ni sahihi? Kisheria, huwa inaadhibiwa nia na si kitendo. Chini ya dhana ya mistake of fact, mtuhumiwa anapotenda kosa akiamini kuwa alichokuwa akifanya si kosa, hupunguziwa makali ya adhabu. Mfano, kama nikimpiga mtu risasi akiwa shambani mwangu nikiamini kuwa niliyempiga risasi ni nguruwe anayeshambulia mazao yangu, siwezi kushitakiwa na kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia. Sambamba na nayaraka husika, serikali inajua fika kuwa habari za uchunguzi hutegemea tips na nyaraka. Hivyo, basi, kama mwandishi alijiridhisha kuwa nyaraka husika zilikuwa sahihi, waziri hakupaswa kufungia gazeti kwa miaka mitatu.
Isitoshe, hata serikali yenyewe imekuwa na waajiliwa wengi wenye vyeti feki iliowaajili ikiamini ni sahihi; na serikali yenyewe haijatimliwa madarakani kwa kuanjiri watu ilioamini wana sifa hata kama ikibainika kuwa hawakuwa na sifa. Hapa tunaangalia nia (spirit) ya kutenda kosa husika na si kosa. Kwenye makosa ya jinai kuna vitu viwili muhimu viitwavyo mens rea (nia ovu) na actus reus (tendo lililokatwaza kisheria). Katika kushughulikia kesi vitu hivi huangaliwa sana ili kuamua kama mhusika alitenda kosa analokabiliwa nalo kwa makusudi au bahati mbaya.
Nane, kitu kingine, makosa ya kiuhabarishaji yanapotokea, mhusika–licha ya kupewa fursa ya kujitetea, mara nyingi, huambiwa akanushe habari husika na kumuomba msamaha mhanga.
Tisa, kwanini waziri alikurupuka na kuchukua uamuzi mzito hivi ndani ya muda mfupi? Haiwezekani kosa litendeke tarehe 4 Agosti na hukumu ifuatie tarehe 11 Agosti yaani siku tatu baada ya kosa kutendeka–kama kweli lilitendeka.  Waziri alikuwa na haraka ya nini au alifanya maamuzi yake ima kwa chuki au kushinikizwa? Maana haiingii akilini kwa waziri –ambaye tunaamini amesoma barabara–kuchukua uamuzi kwa pupa na haraka hivi na haki ikatendeka. Hapa–kwa ushahidi wa mazingira (circumstantial evidence) ni kwamba waziri alishaamua kuadhibu gazeti bila kutoa muda wa kutosha kusikiliza upande wa pili. Waziri hakuvaa viatu vya mwandishi ndipo akaamua–angekuwa yeye angefanya nini–katika mazingira kama haya ambapo kupambana na ufisadi ni sehemu mojawapo ya malengo mahsusi ya serikali ya rais John Magufuli.
Kumi, sijui kama waziri alijiuliza maswali yafuatayo na kutoa haki kwa watuhimiwa kabla ya kufikia uamuzi wake:
a)      Je aliuita utawala wa gazeti na kuupa fursa ya kutosha ya kujitetea?
b)      Je aliotoa onyo au karipio kabla ya kufikia uamuzi wake?
c)      Je aliwaamuru wahusika kukanusha taarifa husika na kumwomba mhusika msamaha wakakataa?
d)      Je muda uliotumika kufikia hukumu ulikuwa unawatosha?
e)      Je Kama waziri alitoa haki hizo husika; kama alifanya hivyo, wahusika walitoa utetezi gani  na nini misingi ya waziri kukataa utetezi wenu na kutoa adhabu kali kiasi hicho?
f)       Je amewapa fursa ya kupinga uamuzi wake?
            Kimsingi, kuna maswali mengi hasa ikizingatiwa kuwa kisheria, hakuna anayepaswa kuhukumiwa bila kusikilizwa.
            Baada ya kupata habari za kufungiwa gazeti, niliwasiliana na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Halihalisi inayomilki gazeti husika Saed Kubenea aliyesema, “Barua ya Maelezo - Idara ya serikali - ilifika ofisini kwetu Jumatatu saa 10 jioni. Kumbuka hii ni siku ya mapumziko hapa Tanzania - Nane Nane. Ikataka tueleze kwa nini tumeandika hiyo stori inayomtaja ‘rais aliyepo madarakani.’ Basi. Tukajibu. Tuliekelezwa majibu yafike ofisini Maelezo kabla ya saa 3 asubuhi ya kesho yake.”
            Kwa uchache, hivyo ndivyo ilivyokuwa hali. Ni vema msomaji ambaye ni mdau wa habari na haki za kiraia za kikatiba ukasoma na kuamua mwenyewe.
            Mwisho, kwa ukiukwaji huu wa katiba, nashauri gazeti liende mahakamani kuitaka ibatilishe uamuzi huu wa ajabu.
Chanzo: Mwanahalisi leo.

No comments: