Baada ya mwenyekiti mpya wa Chama Cha Makabaila (CCM) dokta Joni Kanywaji Makufuli kufichua kuwa kumbe CCM inamilki vitega uchumi zaidi ya 500 kayani, kijiwe kimeamua kumkabili kumwambia aitumbue CCM kwa kurejesha mali hizo ambazo nyingi ni viwanja sirikalini.
Msomi Mkatatamaa ndiye analianzisha, “Jamani mmesikia hii mpya kuwa Chama Cha Makabaila kinamilki viwanja na vitega uchumi kayani kote?”
Kabla ya kuendelea, Mpemba anachomekea, “Japo nilikuwa najua kuwa ufisadi huu wa kunyakua umekuwapo kwa muda nrefu chini ya chama kimoja, sikujua kuwa kumbe walokuwa wakifaidi ni mafisadi na si chama hata kama nacho kina hatia ya kukwapua ardhi.”
Msomi anaendelea, “Nakubaliana nawe. Hili si jipya. Jipya ni kwamba huu ni mtihani kwa dokta Kanywaji anayesema anataka kuwaondolea wachovu kero. Nadhani kero mojawapo ni kutwaliwa kwa viwanja na ardhi yao na kutumiwa na chama kimoja wakati ni mali ya wote bila kujali vyama vyao.”
Kapende anapoka mic, “Kisheria, alichosema mkiti ni ushahidi tosha kukishughulikia chama chake. Hapa nashauri tushupae kuhakikisha vile viwanja vinarejeshwa sirikalini kama alivyofanya kwenye kota za Migomigo baada ya mafisadi kutaka kuwadhulumu wachovu.”
Mipawa anakatua mic, “Nakubaliana na ushauri wako. Ila nitaongeza kidogo. Lazima tumbane jamaa si kurudisha tu viwanja vilivyokuwa vikifisadiwa na kumilkiwa kinyume cha sheria na CCM bali arejeshe na nyumba za wachovu alizouza Nkapa.”
Mijjinga naye anaamua kutia guu, “Ukisikia ujipu ni huu. Kwanza, ilikuwaje kaya ya kijamaa kuruhusu chama tena twawala kujiingiza kwenye uporaji viwanja na ukabaila? Je chama kinachotawala na kufanya biashara kitaacha kuichuuza kaya?”
Kabla ya kuendelea Mgosi Machungi anamchomekea, “Mgosi unataka kaya iuzwe maa ngapi wakati iishauzwa? Huoni jamaa anavyohangaika na ufisadi uioanzishwa na chama hiki hiki kinachotusanifu kuwa kipo kwa ajii ya wachomu? Hapa azima tiseme ukwei kuwa dokta wa majipu azima aitumbue CCM kwanza ndipo aendee na majipu mengine.”
Msomi anarejea, “Nadhani jamaa alipofichua siri hii hakujua madhara yake. Kwa vile tuna ushahidi wa kukiri kwake, kama atafanya vinginevyo, tunaweza kwenda hata kwenye mahakama za kimataifa kudai ardhi ya wachovu au siyo? Hakuna kilichoniacha hoi kama alivyoshangiliwa na wachovu huku vigogo wakishikwa na bumbuwazi kwa kumpitisha kwa kura zote wasijue atawatumbua.”
dada Sofia Lion Kanungaembe anakula mic, “Hakuna aliponikuna dokta Kanywaji kama kuzifichua asasi za wizi kama vile umoja wa vijana na akina mama na wazazi ambazo ni taasisi za kiulaji zisizo na faida kwa chama wala umma. Nangoja kuona atakavyotumbua wakubwa wa asasi hizi ambazo zimetumika kwa muda mrefu kama mirija. Halo halo!”
dada Sofia Lion Kanungaembe anakula mic, “Hakuna aliponikuna dokta Kanywaji kama kuzifichua asasi za wizi kama vile umoja wa vijana na akina mama na wazazi ambazo ni taasisi za kiulaji zisizo na faida kwa chama wala umma. Nangoja kuona atakavyotumbua wakubwa wa asasi hizi ambazo zimetumika kwa muda mrefu kama mirija. Halo halo!”
Kanji anakula mic, “Veve sangaa hii jumuiya! Iko witu wingi kama vile SUKITA nakula juluku ya chovu. Mimi ona ajabu sana kweli. Kama chama namilki mali nyingi hiwi, kwanini kila chaguzi nenda kwa gabacholi ombaomba kama sikini?”
Mheshimiwa Bwege anatia buti, “Nyie mnashangaa samaki kufa kiu wakati amezungukwa na maji! Kwa kaya yetu ilivyojaliwa–kama chama twawala kisingekuwa kinafanya kazi ya kuwala wachovu–kina uwezo wa kuifanya kaya hii kuwa Ulaya nayo ikatoa misaada kwa kaya chovu duniani. Hata hivyo, unategemea nini unapokuwa na hamnazo wakisimamia shamba la bibi wakati bibi mwenyewe ni kipofu? Hapa kweli mtakoswa kuliwa hata kama neno lenyewe najua linaudhi? Ukisikia ubwege ndiyo huu na siyo wa jina kama langu.”
Mgosi anarejea, “ tate nane tate nane.Waahi maneno yenu yanamiumiza kwei kwei. Yaani tinatenzwa kama hatina akii jamani? Sasa nasema wazi kuwa azima tiende kwa huyo dokta Kanywaji na timwambie atiudishie mai zetu haaka kabla hatijatia mtu zongo.”
Kabla ya Mgosi kumaliza, Kapende anamchomekea, “Kaka ngoja nikuchomekee hata kama sina tabia hii.”
Kabla ya kuendelea, Mgosi anajibu, “Kapende angai maneno yako. Tiheshimiane. Yaani wewe ni wa kunichomekea mimi?”
Kapende anajibu huku akicheka, “Sina maana mbaya Mgosi. Ninachotaka kusema ni kwamba habari kuwa chama tena kinachojidai kutetea wanyonge kinamilki viwanja zaidi ya 500 ni kufuru ya kupaswa kuwatia chuki wahanga wakafanya kitu cha maana. Hapa lazima ikiwezekana tuanzie hapa kwenda kumuona dokta Kanywaji kumtaka arejeshe mali zetu na kulipa fidia kwa miaka ambazo mali za umma zimetumiwa kinyume cha sheria.”
Kabla ya kuendelea Mipawa anakula mic, “Kwanini tusiondoke hapa tukaanzia pake SUKITA na kutaka kujua walioifilisi huku tukitaka watupe hati zake ili tumpe dokta Kanywaji kama kianzio?”
Kabla ya Mipawa kuendelea, Msomi anamchomekea, “Sidhani kama kuna haja ya kuamini kuwa dokta Kanywaji anaweza kutatua kila tatizo wakati sisi wahanga tukiangalia kama hayatuhusu. Kwanza, yeye ni mwana chama hicho hicho. Pili, hawezi kufanya kila kitu. Hivyo, nashauri tumsaidie kwa kwenda na kukamata mali zote za umma tunazojua bila kungoja CCM iorodheshe na kuficha baadhi. Ni rahisi kujua viwanja vya umma vinavyomilkiwa na CCM kinyume cha sheria. Si huwa wengi wanapaki mikangafu yao pale?”
Kijiwe kikiwa kinanoga si lakipita shangingi la kigogo wa CCM aliyeua SUKITA. Acha tumtoe mkuku!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
No comments:
Post a Comment