Kwanza, nashauri tuhamie ughaibuni kwa sababu ya kodi na tozo zimezidi kiasi cha kufanya nitamani ningezaliwa wakati wa mkoloni. Leo nitafyatukia tozo zilizotamalaki zikitufanya tuwe makapuku nao wawe wakwasi hadi wanafuga chawa, funza, kunguni, na viroboto.
Zifuatazo ni tozo kwa mafyatu hasa wale wanaoliwa na wawalao. Kwanza, ni tozo ya mbavu za dogi kwa wasio na mbavu zao za mbwa au kodi ya njengo kwa wenye mbavu zao za mbwa. Hapa sijagusa tozo ya kiwanja hata kama siyo chako ilmradi unaonekana juu ya kiwanja hicho kisicho chako bali cha mwenyewe.
Hakuna anayeishi bila kununua kitu hata kama vingi ni kanyabwoya na visivyokidhi viwango tokana na kuwa na wanene wasiokidhi viwango pia. Hapa kuna tozo au kodi ya mauzo tena bila kuuza. Hii haikuepushi tozo ya manunuzi. Tokana na kutengeneza mazingira rafiki ya kifo ili mafyatu wafyatuke haraka, siku hizi, lazima mafyatu wawe na bima. Hivyo, lazima utozwe tozo ya bima ya afya isiyo afya bali upigaji mtupu tena mchafu uliokosa ubunifu. Afya gani unalipia kumuona daktari anayekupa kikaratasi ukanunue dawa dukani mwake?
Kama haitoshi, kuna tozo la mwenge usiotumlikia majumbani kwetu ukiachia kuneemesha chata twawala tu. Bado tozo za wanene kwenda kutanua na wapendwa wao ughaibuni kwa raha zao. Ongeza tozo ya oksijen japo ni chafu tokana na wingi wa ngwarangwara mbali na ya kaburi kama utafyatuka au kufyatukiwa na jamaa au ndugu maana jeneza halinunuliwi bila kodi na tuzo nyingine.
Ipo pia tozo ya kanywaji kwa wapataji kama mie mbali na ile ya lichigala kubwa.
Kuna tozo fichi ya muuza baa anayenifichia siri zangu ili bi mkubwa asinyake mambo yangu ya kando japo anao wengi anaowatoza tozo ili ajiishie siyo kuishi. Nikitoka baa, ipo tozo ya barabara japo mbanano na mashimo hasa kwetu wenye vikwata moto viitwavyo magari.
Kodi ya kushua hata kama sishibi hata kufanya hivyo. Usisahau tozo ya choo cha kulipia japo si huduma bali hujuma ukiachia mbali harufu mbaya, mainzi, na uchafu.
Tozo zinaendelea. Ipo ya kadi ya chama cha mafyatu hata kama hakina faida wala maana kwangu. Ongeza tozo ya bi mkubwa hata kama ana nongwa nirudipo kayani ukiachia mbali kufyatukafyatuka bure tokana na matatizo yaliyotengezwa na ngurumbili wenye roho mbaya. Kuna tozo ya kitegemezi skulini na michango lukuki japo elimu yenyewe ni makaratasi bila ajira ukiachia mbali michango lukuki ya kipigaji. Kisivyo na akili eti kilitaka nikipeleke English Medium au Intaneshno sijui iweje? Kwani madingi wangu walinipeleka huko?
Kabla sijatulia, kuna tozo ya wachunaji au ya dini aka sadaka au zaka nk. japo wanaoipokea hawatoi wala kueleza inavyotumika ila kuukata tukigeuzwa maskini wa kutengezwa na ujinga wetu na utapeli wa kimfumo. Hapa sijaongelea tozo ya ndata anaponikamata baada ya, ima kuupiga, kupiga ndumu, au kuonekana nimelewa wakati wa kazi wakati wao hawafanyi kazi zaidi ya kuzurura kusaka njuluku za kijinai.
Tozo zinaendelea. Ipo ya usalama wa kaya hata kama si salama bila kusahau ya amani hata kama kaya ni vurugu. Japo sina kipato, bado nalipa kodi ya mapato ili wanene wapate japo siku zote nakosa na kupatwa. Japo sijaendelea, nalipa kodi ya maendeleo japo kuna maanguko na kutokuendelea. Pia, kuna tozo ya kuua mbu na chawa japo wanafugwa na kunenepeshwa. Ipo tozo ya maji japo bomba siku zote kavu.
Bado nalipa tozo ya rununu na runinga japo napigwa kwa vibando na vifurushi.
Ongeza tozo ya kuzikana, vikoba, mikopo kausha damu, tozo ya babu na bibi kijijini. Kila nikiwaza ni tozo hadi napendekeza kaya yetu iitwe kodiland kama siyo tozoland ili tuache kutozana tozo usiku hadi tunatoana roho! Kweli, wamejua kututenda.