Kwa kuzingatia ulazima na umuhimu wa ndoa,hatuna budi kukiri. Si kitu cha kuchukulia lelemama au kimzaamzaa au kukurupukia. Kama tutafutavyo, kuthamini mali au vitu tuvipendavyo na kuvilinda, inabidi tuilinde ndoa maana ikivunjika, madhara yake ni makubwa si kwa wanandoa tu bali kwa watoto, wazazi, ndugu, marafiki hata jamii kwa ujumla. Hivyo, kama tunavyotumia muda mwingi kutafuta vitu kama vile fedha, amani, furaha, tutafute namna ya kufanya ndoa iwe chanzo cha kila kitu hasa vile tusivyoweza kununua kama vile amani, furaha, na raha mbali ya watoto, ridhiko,mapenzi, upendo, hata maisha marefu yenye mafanikio kiakili hata kimwili.
Leo, kwa kutumia taaluma na uzoefu wetu, tutajikita katika kudurusu na kushauri mambo ya lazima na muhimu katika kudumisha na kushamirisha ndoa. Tumedumu katika taasisi kwa zaidi ya robo karne mbali na kujielimisha na kutafiti. Tuanze kwa kuifasiri ndoa. Kwa mujibu wa Kamuni ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), ndoa ni ‘ukamilifu wa makubaliano ya muungano wa mwanamke na mwanamme kuishi pamoja kuwa ni mume na mke kulingana na sheria, mila, au desturi za sehemu fulani” (uk. 211).
Tokana na kutoielewa vizuri au kushindwa katika ndoa, au wasioelewa wanaosema eti ndoa ni ndoana. Kamusi tajwa hapo juu inafasiri ndoana kama “kipande chembamba cha chuma au waya kilichopinda sehemu ya nchani ambacho hufungwa mwisho wa mshipi ili kuvulia samaki samaki” (uk. 211). Pia, neno ndoana linaweza kuitwa ndoano. Kama tutakuwa wakweli, ndoana, haina uhusiana na ndoa hata kwa chembe. Inaweza kuhusishwa kichovu, au tokana na kufeli katika taasisi hii au kishairi. Tunaamini katika ndoa, hakuna kutegana wala kuvuana kama wafanyavyo wavuvi kwa samaki au wawindaji kwa wanyama. Badala yake kuna kupendana, kukubaliana, na kuamua kuishi pamoja si kwa ajili yenu tu bali hata wengine, yaani watoto, wazazi, ndugu, jamaa na jamii zenu. Ndoa ni makubaliano na siyo kutegana au kuwindana au kuumizana.
Tafsiri ya sahihi ya ndoa ni muungano wa hiari baina ya mwanamke na mwanaume-wenye kufikia umri wa kujiamria mambo wanayoyaelewa na kuyakubali- wasio na uhusiano wa damu ufanyikao wa hiari na mujibu wa sheria kanuni, mila, utashi, mapenzi, kwa mujibu wa jamii na wanandoa. Kabla ya kuendelea, kuna aina kuu tatu za ndoa kwa waafrika walio wengi. Ndoa za kiasili ambapo mume mmoja huwa na idadi isiyojulikana ya wake kulingana na mila za wahusika. Ndoa za kikristo au muungano wa watu wawili yaani mke na mume wasio na uhusiano wa damu tu, na waislamu zihusishazo mume mmoja na mke au wake hadi wanne.
Kitu muhimu na nguzo ya taasisi hii adhimu, ni jinsia mbili tofauti. Japo siku hizi wanadamu wameoza kufikia kuongeza aina haramu ya ndoa baina ya watu wa jinsia moja, bado ukweli unabaki palepale kwa maana yake halisi kuwa ndoa ni baina ya mwanamke na mwanaume tena waliofikia umri wa kujiamria na wasio na uhusiano wa damu. Hata hivyo, kuna jamii kama vile waarabu ambao uruhusu ndoa za ndugu wa damu.
Kitu kingine muhimu kuhusiana na taasisi hii, ni ukweli kuwa huleta ulinganifu, uchangamfu, na usawa kama inazingatiwa na kufuatwa inavyopaswa japo wakati mwingine inaweza kuwa kinyume. Usishangae kukuta mzee wa miaka 50 na kijana wa miaka 30, wakiishi kwa usawa na kuaminiana tofauti hata baina ya wahusika na wazazi wao.
Dikteta Idi Amin alikuwa aliogopewa na kusifika kwa ukatili. Lakini siku zote, alikuwa akijitahidi kufanya aliloweza ili wake zake wampende na kumkubali kama binadamu aliyekamilika. Pamoja na kuogopewa, mamlaka makubwa, na ukatili wa Mafarao wa Misri, mara nyingi, walikuwa wakisikiliza ushauri wa wake zao Malkia hata kama hawakuwa wakiupenda au kuunga mkono. Hii ndiyo tabia ya asili ya mapenzi. Mwenye kupenda hana ubwana, ufalme, ukuu, utajiri, wala usomi. Ukiona hali hii haimkumbi basi jua mapenzi aliyomo ni ya kutaka kitu fulani siyo upendo hasa. Mapenzi hasa kwenye ndoa ni kubembelezana, kusikilizana, kuheshimiana, kujaliana, na kujitoa mhanga kwa ajili ya mwenzio. Ndiyo maana waswahili husema mwenye mapenzi haoni-ingawa ina tafsiri nyingi kutegemea na hali yaliyomo mapenzi.
Tumalizie kwa kionjo. Kwa mujibu wa utafiti wa Chuo cha Magonjwa ya Moyo cha Marekani (23.2.23) unaonyesha kuwa wanaume wasiowahi kuoa, wana uwezekano wa kufa mara mbili ya kufa ndani ya miaka mitano ikilinganishwa na wale ambao waliwahi kuoa au wanawake walio katika mahusiano. Tungependa kusikia mrejesho wa makala hii toka kwa wasomaji na kutoa majibu au ufafanuzi kuhusiana na ndoa.
Chanzo: Mwaanchi Jpili iliyopita.
No comments:
Post a Comment