How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 19 April 2024

Mafyatu tunakumiss Edward Sokoine


Mpendwa Fyatu Edward Moringe Sokoine ole Severe.
Najua umelala kwa miaka 40. Juzi nilisikia chawa mmoja akikuita mzee. Kwa uchache, nikupe bonge la kumbukizi. Uliondoka mbichi miaka 45 tena kwa utata. Hata hivyo, ilisemekana, ulifyatuliwa na mfumo uliouamini na kuutumikia kwa mapenzi na uaminifu mkubwa japo hakukuamini wala kukupenda. Nakumbuka wabaya wako walivyokufyatua uliowanyima amani na usingizi tokana na uchapakazi na uzalendo wako kwa mafyatu wanyonge. Hata ulipopata ‘ajali’ pale Dakawa, 12 Aprili, 1984 ukitokea Dodoma kwenda Dar, mengi yalisemwa. Wapo waliosema ulisokoiniwa au kufyatuliwa na waliotuaminisha tusiamini yalikuwa mapenzi ya Mungu.
            Niseme wazi. Kifo chako kilikuwa tata kikiacha utata hadi leo. Si wote wanaoamini uliitwa na Muumba zaidi ya kuwahishwa na wabaya wa kaya. Tunakumbuka. Tunajua. Kilitokana na juhudi zako za kutetea, kutenda, na kuleta haki kwa mafyatu. Ni kama jana. Nakumbuka kasheshe zako za kuwanasa wahujumu uchumi na walanguzi wa bidhaa. Nakumbuka ulivyopiga vitu uvivu, ufisadi, na wizi kwelikweli. Hata siku unasomewa wasifu wako, wengi wasiokuwa waaminifu na wazalendo walishangaa kujua ulikuwa na pea chache za viatu. Hukujilimbikizia mali. Hukupendelea, wake, watoto, marafiki wala ndugu zako kwenye ulaji. Hakika, hukula bali kuzalisha. Wengi walikuonea wivu huku wengine wengi, hasa mafyatu, wakikupenda.
            Ulifanya mengi moja ikiwa vita dhidi ya wahujumu uchumi na walanguzi  mbali na vita ya Kagera ulivisimamia kishujaa. Tunakumbuka dunia ilivyostuka na kuhuzunika. Tulihuzunika na kukutunza kama dafina mioyoni. Ulikuwa mchapakazi asiye mbabaishaji wala muongo. Japo ulipewa majukumu ya kisiasa, hukuwa mwanasiasa mtekelezaji mwaminifu mwema wa kupigiwa mfano.
            Uliipenda na kuithamini elimu. Ulipochaguliwa mbunge ukagundua kiwango chako cha elimu kilipwaya, uliacha uwaziri mkuu na kwenda Yugoslavia kujinoa ulikonyakua shahada katika Sayansi ya Siasa (Political Science). Kwa uamifu, udhu, na weledi wako, hukutafuta shahada ya heshima wala kuinunua kama ilivyo siku hizi. Uliamini katika ukweli tena kwa vitendo. Hukupenda sifa wala sanaa za kisiasa wala hukufanya maigizo ambayo siku hizi ndiyo namna ya kuwafyatua mafyatu watoe kura ya kula. Uliporejea ukiwa umeiva kwelikweli, Mzee Mchonga alikurejeshea uwaziri mkuu ili umsaidie kuongoza kaya wakati wa kipindi kigumu. Kipindi kile mafyatu waliteuliwa kwa sifa za kweli na siyo kujuana au kuwa na uhusiano na wateuzi. Mafyatu wote walikukubali na kukuunga mkono ingawa wabaya wachache kwenye system walikuchukia. Ulikuwa mwiba kwao. Hivyo, hata ilipotokea ‘ajali’ waliamini ilikuwa ya kutengenezwa. Hii ni kutokana na maelezo yasiyoingia akilini kuwa Dumisani Dube, MuAfrika Kusini aliyesemekana aligonga gari lako ndiye alikufyatua. Ajabu ya maajabu, huyo hakuonyeshwa. Na kama angeonyeshwa, asingekuwa na jeraha saa ingine asijue hata hiyo ajali.
            Kuepuka kuonekana ninazusha, hatukuonyeshwa picha ya majeruhi wengine. Tulichoambiwa ni kwamba gari lako ‘lilipogongwa’ wewe  ndiye pekee uliyeumizwa. Na kweli, walikuumiza hadi kukutoa duniani. Wengi tulishangaa, kwanza, ilikuwaje ufe wewe peke yako bila majeruhi hata mmoja. Pili, kwa waliojua afya bora, walishangaa ilikuwaje eti ufe hatujui kwa msutuko au majeraha. Hata mwili wako hatukuonyeshwa tujiridhishe. Kawaida, wakifyatuka wanene kama wewe, miili yao huwekwa wazi Bungeni, Karimjee, hata viwanjani ili mafyatu wawaone na kuwaaga. Kwako, yote haya hayakufanyika. Kwa vile mafyatu si mataahira, tulishuku. Kulikuwa na mkono wa mtu. Hata hivyo, tunamshukuru Mungu. Waliokufyatua nadhani wote walishafyatuka. Kibaya sana, waliondoka na siri ya kufa kwako. Naamini bado siri hii inawatesa kwa sababu hawakutenda jambo jema.
            Kwa tunaokumbuka zama zako, uliamini kuwa uongozi ni utumishi wa umma na si utumikishaji wake. Uliamini kuwa uongozi ilikuwa ni kuwatengenezea mafyatu mazingira na maisha bora. Hukuamini katika kuwala na kuwanyonya mafyatu hadi wengi wakifa njaa na umaskini wa kutengezwa. hukuujua uchawa wala upanyabuku bali uongozi na utumishi wa umma. Hapakuwa na wingi wa skandali za upigaji au upendeleaji.
            Nimalizie. Habari njema, ni kwamba hata wale wabaya wako waliokufyatua, wengi walishafyatuliwa. Waliacha kila kitu walichokilinda hata kwa kudhulumu hata roho za wenzao. Marafiki zako akina Rashid na wengine walishafyatuka. Aliyebaki ni mzee Cleo. Haraka, ngoja nikujuze yaliyotokea. Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea uliyofia haipo tena. Badala yake kuna Uhujumaa na Kujimegea. Wakubwa wanamega kama hawana akili nzuri au hawatafyatuliwa. Siku hizi, siyo siri tena. Wanene ni matajiri tena ghafla bin vuu. Hakuna anayeshangaa wala kuhoji! Si ajabu wala mwiko kuwa na chawa kwenye ofisi za mafyatu tena wanye madoadoa tokana na ufisadi na wizi wao. Zamani mlijenga kaya. Siku hizi, wachache wanaila hadi kuiuza kwa wachukuaji na kuibomoa. Habari ndiyo hiyo. Guess what. Tuna uchakachuaji mwakani. Mafyatu wanashangaa miaka yote huwa huadhimishwi wala kukumbukwa. What’s up? Lala salama Fyatu mwenzetu, Ed Morning Sokoi4 ole Severe.
Chanzo: Mwananchi Jtano.

No comments: