How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 3 December 2008

Kikwete jiepushe na Kagoda kama Richmond

KATIKA mambo ambayo aliwahi kufanya rais Jakaya Kikwete kiasi cha kuonyesha ushujaa tangu aingie madarakani, hakuna lililovutia kama kuacha tume teule ya Bunge kumkaanga rafiki yake na mshirika wake mkuu, Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani, baada ya kupatikana na kuguswa na kashfa ya kampuni ya Richmond.

Kwanza tungemshauri rais achukue msimamo kama aliochukua wakati wa kushughulikia kashfa iliyomtoa madarakani Lowassa pamoja na kuwa mshirika na rafiki yake wa siku nyingi. Arejee alivyoshindwa pale alipotaka kuitumia TAKUKURU kumsafisha Lowassa na wenzake bila mafanikio.

Pia asiogope kuwa nchi itayumba. Haiwezi kuyumbishwa na mafisadi kama serikali si fisadi. Ila kama atashikilia msimamo kuwa nchi itayumba kwa hofu ya mafisadi, itayumba kweli kutokana na nguvu ya umma.

Pia Kikwete asichelee kuvunja baraza la mawaziri. Kufanya hivyo kutamuongezea heshima iliyotoweka. Kwani kutathibitisha kuwa yeye si mmoja wao. Ila haya hayatakuwa na maana kama Kikwete mwenyewe hatakuwa msafi kuanzia nyumbani kwake.

Kwa mfano NGO ya mke wake ya WAMA inatia shaka hata kama ina nia nzuri. Arejee yanayomkuta rais mstaafu Benjamin Mkapa kutokana na matendo ya mkewe.

Ingawa yaliyomtokea Lowassa ni historia, yana somo tena kubwa tu. Hivi karibuni kuliripotiwa taarifa kuwa wamiliki wa kampuni jingine la kijambazi la Kagoda lililoiba zaidi ya asilimia 40 ya pesa ya mfuko wa madeni ya nje (EPA), linaonekana kutoshikika. Sababu, Msajili wa Makampuni, BRELA, hana taarifa zake! Uongo ulioje?

“Mafaili yote 22 yalichukuliwa na Timu ya EPA, sisi hapa hatuna rekodi yoyote inayoweza kutuonyesha ni nani wamiliki, lakini ukienda huko kwa kuwa wana mafaili yote watakueleza kila kitu.”

Hayo ni maneno ya ofisa mwandaminzi mmoja wa BRELA ambaye hakutaka kutajwa jina. Hapa kuna mashaka na maswali. Je kamati ya rais inakaa na mafaili haya ili iweje iwapo rais ameishautangazia umma kuwa ameiacha ofisi ya mwendesha mashitaka wa serikali (DPP) kushughulikia kashfa ya EPA baada ya kamati kumaliza kazi yake?

Rais ana maslahi gani katika kampuni hii? Rais anaingiaje hapa? Ni kupitia watu wake yaani wajumbe wa kamati aliyoiteua ambao wanawajibika kwake moja kwa moja. Je kuna kazi nyingine ya siri aliyowapa zaidi ya kuchunguza na kutoa taarifa ambazo kwa sasa ziko mikononi mwa DPP?

Ukiachia mbali hili la kukalia mafaili ya makampuni nyemelezi kubwa likiwa la Kagoda, kitendo hiki kinahitimisha shauku ya umma juu ya uadilifu wa wana kamati.

Edward Hosea Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, walilalamikiwa walivyokuwa na maslahi ya kifisadi kwenye kashfa ya Richmond kwa nyadhifa zao walijaribu bila mafaniko kumsafisha Waziri Mkuu aliyelazimika kujiuzulu, Lowassa.

Kuonyesha ithibati ya shaka hii, rais bado aliwateua kwenye kuchunguza ufisadi wakati nao wakikabiliwa na tuhuma zile zile! Je rais hakujua madhara ya kufanya hivi? Je kama hana maslahi, alilazimishwa na nini kuchagua watu wenye kutia shaka?

Kuonyesha kuna mchezo mchafu unaendelea, msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Omega Ngolle, alipoulizwa na vyombo vya habari kuhusiana na hili alisema kamwe ofisi hiyo haitaeleza undani wa kampuni hiyo na kwamba haioni sababu ya kufanya hivyo.

Kwanini kuunyima umma taarifa ambazo ni mali yake na si ya watendaji wa serikali binafsi? Wapi utawala bora na wa sheria hapa?

Je mparaganyiko huu na ukosekanaji wa taarifa za Kagoda ni hitimisho la madai kuwa serikali kupitia chama chake cha Mapinduzi (CCM) vilinufaika na wizi huu kiasi cha kuufumbia macho hadi upinzani uliposhupaa?

Kutokana na unyeti wa suala la EPA na madai yaliyokwishatolewa dhidi ya serikali na watendaji wake, ni dhahiri: kuaminiana kumetoweka na hakuhitajiki.

Nani wataiamini serikali au watendaji ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawawajibiki kwa misingi ya nafasi zao bali kulazimishwa na upinzani?

Hapa ndipo rais na kamati yake wanapaswa kujiweka mbali na uchunguzi na ushughulikiaji wa sakata hili kama kweli ni wasafi na hawana maslahi yoyote. Na kama watang’ang’ania basi umma uwatake waache kuingilia mambo.

Huwezi kuwa mtuhumiwa, hakimu, shahidi na mwendesha mashitaka. Rais mwenyewe aliwahi kuonya kuhusu hili. Ni vizuri yeye na watendaji wake wakalitekeleza.

Kitu kingine ambacho ni kama kimesahaulika ni ukweli kuwa wataalamu wengi wa benki kuu walitumika katika wizi huu. Mamlaka hazijaonyesha ni kwa vipi zimeziba mianya hii ambapo watu tena wataalamu wa ndani hushirikiana na matapeli na wezi kuiba mali waliyopewa kutunza.

Kwa mfano katika kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa EPA hatujasikia majina ya washirika wa marehemu Daudi Ballali hata warithi wa mali zake.

Maana kisheria linapokuja suala la mali, mhusika akifa, anayemrithi hurithi pesa na madai mengine yahusianayo na marehemu. Hivyo wanasheria wangetafuta jinsi ya kuhakikisha warithi wa Ballali wanafikishwa mahakamani ili pesa yetu isipotee.

Ingawa serikali imekuwa ikijifanya kutosikia hili, kuna haja ya bunge kuunda tume ya kuchunguza kifo cha Ballali na jinsi alivyohusika kama msimamizi wa benki kuu na mtuhumiwa katika wizi wa EPA ili kuepusha hili kufanyika tena.

Jumuia ya wahalifu ni kama ya mitindo. Wakiona aina fulani ya wizi imefanikiwa sehemu fulani basi jua watairudia tu.

Kitu kingine anachopaswa kufanya Kikwete licha ya kujisafisha ni kuhakikisha anakuwa mkali bila kuonea wala kumpendelea mtu. Kwa mfano amkamate Mkapa na familia yake waeleze walivyopata utajiri wakati wakiwa madarakani.

Hii itafanya wa chini ya Mkapa kuogopa na kuachana na ndoto za kukomoana wala kulalamika kuwa wameonewa.

Kila la heri rais Kikwete. Kaza uzi na wembe uwe ule ule.

Source: Tanzania Daima Desemba 3, 2008

No comments: