How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 31 December 2008

Tunapofunga mwaka kwa sanaa na longolongo

WAINGEREZA, mabingwa wa fitina, husema money talks, bullshit walks; kwa tafasiri yangu na Kiingereza changu cha kukopa, nisome hapa; mwenye pesa si mwenzio na upuuzi husambaa.

Juzi tulishangilia vigogo walipogonga lupango na kuchomoka kama hawana akili nzuri. Tulihoji. Hayo mahekalu waliyojidhaminia si matokeo ya utumiaji madaraka vibaya na ufisadi ukiachia mbali uhujumu? Leo Kijiwe kina kikao maalumu cha kutoa shinikizo na kubaini usanii na mazingaombwe.

Mgosi Machungi analianzisha. “Wagoshi mmesikia vigogo waivojizamini kwa mihekau ya wizi? Hatielewi mantiki ya kufungua kesi haafu mtu akajizamini kwa mai ya wizi jamani.”

Kapende anatia timu. “Hivi hamjui! Hii geresha kuepusha Kagodam kwa kisingizio cha matumizi mabaya ya madaraka. Kama ni matumizi mabaya, wangeanza na Tunituni na si washikaji zake.”

Kabla Kapende hajamaliza mzee Maneno anakwapua mic. “Hivi mwaishi nchi gani au mmeishiwa? Hapa yule mwarabu aliyetajwa na Bangusilo Ibra M7ha anafanya vitu vyake. Hamkusikia wakati wa Richmonduli Bangusilo alivyozoza hadi Eddie Ewassa akatimuliwa. Mi naona Richmonduli na EPA ni dugu moja.”

Anakohoa na kuendelea. “Kagodamn ni CCM na CCM ni Kagodamn. Hivi huyu mwarabu wa Ewasasa Rosti Tamu L’Aziz ni nani Kayani mwetu hadi awatie wakubwa msambweni?

Yawezekana halindwi. Wakubwa waliomtuma wanamlinda ili naye awalinde. Wakimtosa anawatosa na siri inafichuka. Na mtawakuta ambao hamkuwategemea.”

Mara Mbwa Mwitu anadakia. “Danganyika hii sina hamu. Mmesikia mkuu alivyopewa udaktari na Manyang’au baada ya kuwakataliwa kuja kuiba ardhi yetu. Ama kweli wajinga ndiyo waliowao.”

Kabla ya kuendelea, Makengeza anampoka mic na kuzoza. “We fisadi Mbwa Mwitu unayeshirikiana na Mpa. Sorry unayeiba kashata na kahawa usivuruge mada yetu kwa habari uchwara za Chekacheka na shahada za upogo na uongo.”

Alivyotaja Mpa akakatiza nilimkata jicho nusu limtoboe. Nilichukia kama Chekacheka anavyonichukia.

Mzee Mzima naingilia kwa kasi mpya na ari ya hasira. “We Makengeza, koma na ukomae. Usipende kuniingiza kwenye utani uso kichwa wala mguu. Nani anaiba kahawa na kashata zetu kama si upumbavu wenu? Kwani mlinichagua bure? Mbona mlizipwakia hata tangawizi? Mlidhani kuna cha bure duniani. Uliza takrima ilikuwa ya nini, alikula nani na anapata nini sasa? Vitu vingine haviliwi.”

Kabla sijaendelea, Mzee Kidevu alitoa tahadhali. “Mzee hotuba baba hotuba”-akimaanisha nachonga sana. Namjibu kwa hasira. “Acheni uvivu wa kufikiri. Mbona Kaya inapoliwa nanyi kufanyiwa ma-EPA na mahepe hamlalamiki mnalalamikia vikashata na kahawa tunavyokula na kunywa wote?

Mbona tumewaona wezi tena wakubwa wakijidhamini kwa mali za wizi na hamuandamani? Mbona mkuu ametajwa na genge lake kuwa nyuma ya wizi wote huu hamshinikizi akitoe badala yake mnamwamini naye anawachezea ma-EPA mchana?”

Nakohoa na kufuta kijasho chembamba na kuendelea. “Hivi mwataka kusema madafu bilioni 12 ni dili kuliko madafu bilioni zaidi ya 500? Mbona tunageuzwa majuha na tukisema mnakuja na taarifa hotuba hotuba baba.”

Kabla ya kuendelea kunema, Kapende anapiga pini nyingine. ‘Ingawa mzee siridhiki na yako, umenena. Kuna mafisadi wengi tena wakubwa tu hawajagushwa. Yuko wapi Mengjii, Anna Mgando, Rost Tamu l’Aziz, Endelea Chenga, Eddie Ewassa, Malengesi, na wengine wanaojulikana kutu-EPA na kutulichimonduli?

Mkiambiwa hii kaya ni pepo ya Mabwege mwasema mwatukanwa wakati ni kweli. Mbona hamuibani Nambari wahedi ielezee ilipopata takrima? Ajabu mlionywa na mzee Mchonga kuwa awanunuaye naye kanunuliwa hamkutia akilini. Alimzuia Chekacheka akisema hajakomaa kiakili mkamuona mzee wa watu mzushi wakati ni ukweli mtupu. Jamaa ni mweupe hafai hata kuwa katibu kata.”

Kicheko na mibeuo kwa sana.

Mara Mpemba anaingilia. “Yakhe mie nkubaliana nawe. Huyu bwaana hana maana. Enda fungua kesi ziso kichwa wala nkia akiacha zile muhimu! Mie naona akina Ngonjwa, Rambaramba na Jona waonewa tu. Hawa nao Bangusilo ili Kagodam ipite kama alivosema mzee mzima ambaye kama shahada wanizopewa zingekuwa na maana basi angepewa yeye. Hapa twaingizwa nkenge tuu. Tushaonya Kaya yaliwa na watu wake.”

Kabla ya kuendelea, Machungi anamkatiza. “Ami tiheshimiane. Haya mambo ya kuiwa yaishie kwenu siyo hapa.”

“Acha nseme mgosi twaliwa. Kama hatuliwi mbona hatufurukuti?” Anajitetea Mpemba.

“Loo! Matushi mengine. Tifuukute ii iweje? Kwanini tisiwapige mawe kama Mbea?” Anachomekea Mgosi.

Mara Kapende anaepusha zari. “Mkane mkubali kweli tunaliwa sana . Hivi tusingekuwa tunaliwa, Kaya yetu ingekuwa hovyo hivi? Angalia pale Chuo Kikuu cha Manzese vijana wanavyohujumiwa. Je haya siyo matumizi mabaya ya madaraka? Pale Pemba kuna nini na miafaka uchwara?”

“Yakhe wasema ukweli. Sie twaliwa tena kote kote si bara wala pwani. Karafuu Pemba yakwama ukitafuta soko waambiwa wahujumu uchumi! Dhahabu kule Musoma, Shinyanga na kwingineko yajaa watu wafa na umaskini. Kama si kuliwa huku nini shehe? Angalia hata hao viranja wenu. Nao waliwa kweli kweli. Wakesha kula kutwa ughaibuni kuomba ilhali mali wankalia!”

Mbwa mwitu anaingilia tena. “Acha Ami nikukosoe. Hatuliwi tu. Tumekeketwa akili wakubwa kwa wadogo. Hatujitambui japo twajiona wajanja wakati tu mafala. Bila kulianzisha hapa tukaachana na ufisadi mdogo mdogo kama ninaosingiziwa, tutaendelea kuliwa sisi wake zetu watoto wetu na hata ma.”

“Mbwa mwitu inatosha. Subutu hayo unayosema hatikubai. Titakufa na mtu. Mtu atile na watoto zetu hata wake zetu. Ohoo titapiga mtu zongo.”

Makengeza anaingilia naye. “Hapa hakuna cha zongo, dongo wala gongo. Ni kuingia mitaani na kuhakikisha kinaeleweka. Vinginevyo tukubali tuliwe si na watoto wala wake zetu hata mama zetu. Msiogope kusema. Tunaliwa, tutaliwa sisi na mama zetu.”

Kabla ya kumaliza Mgosi anajitetea. “Utaliwa wewe Kapende na Mpemba siyo mgosi.” Titamkabii Chekacheka na genge ake atiambie yeye yuko wapi, Kagodam ni nani na ana husiano gani naye na kwa nini amfiche na kutizuga na matumizi mabaya ya madaaka. Ajue. Kiichomkuta kibwendo na ungo kitampata.Tiamue. Kwani mbwai mbwai?”

Anakohoa na kutema bonge la mate na kuendelea. “Kwanini hationi oodha ya list of shame ambayo ndiyo mama wa kufichuka kwa ufisadi wote? Nani anandanganya nani hapa?”

“Hee! Utadhani pilato akiwasulubu akina Rambaramba na Mgonjwa!” Anadakia Mzee Ndomo. Tumeanza kwa kimombo. Tunamaliza kwacho. A camel is a horse designed by committee. Hii sitafsiri.

He kumbe kesho ni mwaka mpya? Kila la heri mlio safi na kila la shari mlio wevi na mafisadi.

Chanzo: Tanzania Daima Desemba 31, 2008.

No comments: