MADAI yanayozushwa juu ya mawasiliano ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta na kinara wa Richmond, Mohamed Gire, ni upuuzi unaopaswa kutiliwa shaka na kupuuzwa.
Kwa nini sasa baada ya Bunge kuibua, kuchunguza na kuianika kashfa hii? Hata ukiyaangalia, hakuna mwenye akili awezaye kuyaamini.
Kusema Sitta alikuwa na mawasiliano na Gire, kitu ambacho Sitta hakanushi, hakumfanyi spika huyo kuwa fisadi wala mshirika kwenye ujambazi huu wa mchana.
Kwa cheo chake (wakati ule) cha Ukurungenzi wa Taasisi ya Uwekezaji (TIC), Sitta bila kupinga au kuvunja sheria, alikuwa na uwezo na uhuru wa kuwasiliana na yeyote aliyeonyesha nia ya kuwekeza nchini.
Na hii ndiyo kazi iliyokuwa inafanya alipwe mshahara na marupurupu yote yatokanayo.
Wale wanaojaribu kutushawishi na kutuaminisha kuwa Sitta ni fisadi, wangetueleza ni lini na pesa kiasi gani Sitta alipokea kutoka kwa Gire na akawezesha nini? Hata wangeonyesha sheria au taratibu alizovunja katika kuwasiliana na Gire.
Kama Sitta alidhamiria kupata pesa yoyote kutoka kwa Gire, basi onyesheni japo ushahidi badala ya uzushi. Ingawa Sitta si malaika, ukimlinganisha na wanaomshutumu japo yu mtakatifu.
Nadhani, watu wazima na wenye akili timamu wangejinasua kwenye uchafu huu kwa kueleza ukweli waujuao na si kulalama na kutafuta kuwachafua wenzao.
Hii haitaondoa nongwa yao. Na ukitaka kujua nani mwizi, tazama yule anayesema: “Na fulani alifanya hivi.” Jitetee mwenyewe.
Kwa nini mawasiliano ya Gire na Sitta yawe habari ilhali ile hali ya serikali kuruhusu Richmond ‘kuuza’ sijui kukabidhi au kushirikiana na Dowans mitambo inayojulikana kuingia nchini kinyume cha sheria?
Kama hawa wanaotaka kutuaminisha ni wasafi, ingawa ni wachafu, ili tuwaamini watwambie miujiza iliyotumika Richmond kuuza mitambo yake wakati iliishabainika ni utapeli mtupu na wizi wa pesa za umma.
Hivi kuna ufisadi wenye ukubwa na kuchukiza kama huu unaoihusisha serikali hii? Je, ‘uchafu’ huu wa kutengeneza wa Sitta unaletwa kwa makusudi ili kuepusha udadisi wa umma juu ya kashfa yenyewe? Ni upuuzi na harakati gani za kipuuzi hizi!
Hata kama kuna namna yoyote yenye kutia shaka Sitta alishiriki wahusika walichelewa. Kwa nini wamuone fisadi baada ya kuwafichua na wasimfichue kabla?
Au ni yale ya Waziri wa Nchi (Utawala Bora) Sophia Simba, kujua maovu ya wenzake akayaficha, asichukue hatua, aje kuyamwaga hadharani baada ya kushikwa pabaya?
Ikichukuliwa kuwa ‘majizi’ ya Richmond yapo kwenye saa yao ya mwisho kuumbuliwa, uongo mwingi dhidi ya Sitta na wanaopinga ufisadi utatungwa na kusambazwa kwenye vyombo vyao vya habari vya kifisadi.
Je, watu wetu watakuwa mataahira kiasi hiki kubugizwa uchafu na uongo huu unaoenezwa na wafa maji hawa?
Ni hivi, tulishuhudia kinara wa Richmond na EPA akipayuka kuwa angetaka achunguzwe kama kweli alishiriki uchafu wa Richmond! Haya hayamwingii hata kuku, achilia mbali wanadamu.
Kama huyu anashindwa kuwaamini wabunge wenzake ambao alishirikiana nao kuunda kamati teule ya Bunge, atawaaminije majaji?
Je, anataka achunguzwe kwa vile anajua atatumia ukaribu wake na mamlaka zinazowateua alioamini wanaweza kumchunguza na wamsafishe kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilivyofanya?
Huyu aliomba kuchunguzwa na majaji. Nani anataka kurudia upuuzi wa kuteua majaji hata mahakimu kama kwenye kesi ya shutuma za rushwa ya sh 500,000,000 alizotoa Augustine Mrema, dhidi ya mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wakati ule?
Ijulikane. Bunge lilipoamua kuunda kamati teule, jamaa huyu alikuwa bungeni na hakupinga wala kutoa wazo hili! Wabunge ni wawakilishi wa moja kwa moja wa umma kuliko hata majaji wa huyu jamaa.
Ambaye hawaamini wabunge tena naye akiwa mbunge, aache ubunge na akubali kufikishwa mbele ya mahakama ili akutane na majaji wake vizuri huko.
Kwa kutoliamini Bunge ni kashfa tosha, hasa ikizingatiwa mhusika ni mbunge na alikuwapo wakati haya yakiidhinishwa na ndani ya Bunge.
Je, mtapatapa huyu hakusema haya kwa vile aliamini angeihonga kamati teule na kujinasua ingawa hakufanikiwa? Acheni utoto na kutapatapa.
Nchi hii haiwezi kuenea mifukoni mwenu. Mnatakiwa kufahamu kwamba, pesa yenu itokanayo na ufisadi, haiwezi kumnunua kila mtu.
Turejee kwa Samuel Sitta. Yeye si mpumbavu kujipalia mkaa akijua utamchoma mwenyewe. Hapa ndipo unapata ushahidi tosha kuwa Sitta hakushiriki kwenye upuuzi huu.
Maana, angekuwa ameshiriki kama Spika, alikuwa na mamalaka ya kuweza kuizima kashfa ya Richmond bungeni. Na hii ndiyo dhambi aliyoitendea CCM kiasi cha mafisadi kukamia damu yake.
Tukirejea maneno ya mwenyekiti wa kamati teule, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwa kuna mambo yaliachwa ili kutowaaibisha wakubwa na wengine, kama ukweli ukirejewa, mafisadi hawana haja ya kumlaumu Sitta.
Tujalie, Mwakyembe na wenzake wakiamua kusema kila kitu, kweli kutakuwa na serikali au chama hapa? Je, ni vigogo wangapi walinusuriwa katika kile alichosema Mwakyembe, kuwa kuna mengine waliyaacha ingawa si vizuri kupindisha mambo?
Hapa ndipo serikali inapaswa kuchukua hatua kujinasua kwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa, vinginevyo inaweza kujikuta msambweni.
Hii njama ya kujaribu kuwapatiliza wabunge haisaidii bali kuchochea hasira na kujenga ithibati ya kuweza kuzobokwa yote bila kujali cheo cha mtu wala chama.
Kwanini hatupendi kuukubali ukweli hata kama ni mchungu kuwa kulikuwa na rushwa kwenye Richmond? Hapa lazima tukubali.
Bila kuwa na rushwa, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa asingekubali kirahisi kuachia ngazi. Alifanya hivyo kwa kujua dhahiri hatari iliyokuwa ikinyemelea serikali, chama na yeye binafsi bila kusahau bosi wake - Rais Jakaya Kikwete, ambaye ametajwa mara nyingi kuwamo kwenye mchakato wa kuileta Richmond, ukiachia mbali kufanya kazi kwa niaba ya bosi wake.
Hata hivyo, hawa wanaojilizaliza sasa wakumbuke: walipewa mwanya wa kujitetea. Lakini, hawakuwa tayari kufika mbele ya kamati kufanya hivyo!
Je, walijua kwenda kwao kungekuwa ni kujipaka mafuta na kuingia kwenye moto? Bila shaka. Wale wanaodhania kuwa maamuzi ya Bunge yanaweza kubatilishwa licha ya kuwa wajinga, wanapoteza muda na kuzidi kujiaibisha zaidi.
Muhimu, tukubaliane. Richmond ni balaa la taifa. Kama upuuzi huu unaoendelea utaachwa uendelee, matokeo yake yatakuwa mabaya kuliko ilivyotarajiwa. Ila ijulikane.
Hawa wanapoteza muda. Siku itafika watanyea debe tu, vinginevyo wajiue. Hivyo basi, kitu muhimu na cha maana kufanya ni kwa serikali kuwafikisha mbele ya mahakama.
Huko basi, kuna nafasi kubwa tu ya kujitetea kama wanadhani wamechafuliwa au kuonewa. Kwanini hawaipokei changamoto hii kama kweli hawana hatia? Hii ndiyo njia pekee ya kuwasaidia.
Mwisho, kuendelea kutumia njia za mwituni hakutaisaidia serikali wala watuhumiwa. Badala yake, kutaongeza hasira kiasi cha ufa kuzidi kutanuka na madhara kuwa makubwa.
Je, wanangoja nguvu ya umma kuingilia kama ilivyoanza kufanya kazi kwenye mamlaka ya Reli (TRL) ambako imeripotiwa hivi karibuni kuwa wafanyakazi wameamua kuchukua uendeshaji wa shirika baada ya wawekezaji kubainika ni wababaishaji na watafutaji ngawira wa kawaida?
Hakika hakuna upuuzi kama madai kuwa Spika wa Bunge, Sitta ni fisadi kirahisi hivyo tu, kwa sababu aliwasiliana na Gire.
Chanzo: Tanzania Daima Nov. 18, 2009.