


Rais wa Misri Hosni Mubarak amepata pigo jingine baada ya jeshi kukataa kuwashambulia na kuwatawanya waandamanaji. Kama Mubarak atanusurika basi utakuwa muujiza wa karne hii.Waandamanaji wanasema kuwa hawatatoka mitaani wala hawako tayari kujadilina na yeyote bali kumuona Mubarak akiachia ngazi. Wamemchoka na hawamtaki. Marekani nayo imesema wazi kuwa inangojea serikali ya mpangilio ya mpito.
Baada ya polisi kujikomba na kuua watu, kwa kuogopa kile wachambuzi wanachosema Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Mubarak alilazimika kuwaondoa polisi mitaani.
Mkuu wa majeshi ya Misri Luteni Jenerali Sami Hafis Anan alilazimika kukatisha ziara yake ya kikazi nchini Marekani.
Jeshi limesema wazi kuwa madai ya waandamanaji ni ya halali na ya haki. Hivyo, halioni haja ya kuwashambulia wala kuwatisha. Hakika hili ndilo jeshi la wananchi kwa maana halisi siyo haya mashimboshimbo yetu yanayotumiwa na mafisadi kututisha. Ni jeshi linalotumia akili na si kutii amri hata kama ni za kipuuzi na kiuaji kama polisi wetu na majeshi mengine zandiki ya kiafrika.
Akina Shimbo wanapaswa kusoma hili kwa makini na kuacha kujikomba kwa watawala majambazi. Siku ikifika hata ulete vifaru mizinga na madege yanayokunya moto huwezi kushinda NGUVU YA UMMA. Je yanayoendelea huko Misri yanatoa somo gani kwetu ambao tuko kwenye hali mbaya kuliko hata hao wamisri?
Pamoja na juhudi za waandamaji kuungwa mkono na dunia nzima, kuna swali moja kuu. Je baada ya kumdondosha Mubarak, nani atachukua hatamu? Wachambuzi wengi wanahofia Misri kuwa kama Iran ambapo wahafidhina wa kiislamu (Muslim Brotherhood) wanaweza kujipenyeza na kutengeneza himaya nyingine ya kihafidhina kama ya Mahayatollah wa Iran. Hili likitokea litakuwa pigo kwa Marekani na Israel na ulimwengu wa magharibi.