Baada ya rahis kutoa amri kuwa wachovu wafyatue vinyemelezi, Kijiwe kimeamua kutoa angalizo juu ya ushauri na ushawishi huu ambao unaweza kukwamisha maendeleo na harakati za kaya za kujikomboa na umaskini na uombaomba.
Leo anayelianzisha ni Mbwamwitu. Baada ya kuamkua anakula mic, “Wazee mmesikia amri ya rais dokta Joni Kanywaji Makufuli kuwa lazima wachovu wafyatue vitegemezi kama hawana akili nzuri? Je nyie mmepanga kulitekeleza vipi?” anamalizia maswali yake huku akimdeku da Sofia Lion aka Kaunungaembe.
Mgosi Machungi hajivungi; anakula mic, “Mwenzenu sihitaji hivyo vitegemezi kwani ninavyo vingi kwei kwei. Laiti munene angejua adha za kuwa na vitegemezi ukuki waa asingetoa tamko hii ambao wengi wataichukuia siiyasii kiasi cha kuzaisha tatizo jingine. Tisiunge mkono ushaui huu hasa usawa huu wa kaya maskini na ombaomba.”
Msomi Mkatatamaa anakula mic, “Nadhani daktari wa tujipu alikuwa anatania watani zake wazaramizi vinginevyo–kama alimaanisha–basi akubali kuwa anatengeneza majipu mengine. Sioni motisha ya watu wenye kuelewa mambo kuongeza vitegemezi hasa usawa huu wa kutumbuana na kubana matumizi. Kama ni elimu ya bure, hivyo vitegemezi si kabichi kuwa vitakuwa ndani ya miezi mitatu ndiyo vifaidi hiyo elimu ya bure. Vingi vya vitakavyofyatuliwa vitaingia kwenye shule za bure wakati jamaa akimalizia ngwe ya pili kama wachovu watampa. Hivyo, ushauri huu uchukuliwe kama utani na si ukweli.”
Mpemba anapoka mic na kudema, “yake mie siamini kama rahis alikuwa atania. Maana alirudia kauli yake ya kutaka watu wafyatue vitegemezi kwa kuwataka hata akina mama wasitumie madawa ya kuzuia kuzalisha vitegemezi. Nimjuavyo mimi dokta Kanywaji huwa si mtu wa utani. Nadhani alishauriwa vibaya au aliangalia vibaya mambo kiasi cha kutoa amri ya kuunda bomu ambalo wakati likifyatuka atakuwa mstaafu.”
Kapende anamuunga mkono Mgosi kwa kusema, “hata mimi nilishangaa kusikia kauli hii ambayo asipotafuta namna ya kuiweka sawa, inaweza kukamisha mipango yake mizuri. Nadhani hao vitegemezi anaotaka tufyatue hawahitaji elimu ya bure tu. Wanahitaji matunzo na mahitaji mengine muhimu kama vile ajira kwa wazazi wao, malazi na makandokando mengine.”
Mzee Maneno anaamua kumpinga Kapende, “kusema ukweli mimi namuunga mkono mtani wangu. Kama kaya inaweza kupokea wakimbizi na kuwapa uraia kila siku ukiachia mbali kujaa magabacholi na machina kibao, kwanini tusipunguze kutoa uraia wetu kama njugu na kujifyatulia wanakaya wenyewe? Nadhani hasara wanayosababisha wakimbizi wa kiuchumi toka Uhindi na Uchinani hata Unigeriani na Kenya ni makubwa kuliko vitegemezi tutakavyotengeneza wenyewe.”
Mijjinga anamuunga mkono Mzee Maneno, “nyie mnashangaa la kujaza wakimbizi wa kiuchumi! Hamuoni hili la kuunda umoja na vijikaya visivyo na ardhi huku vikitushupalia kuwa turuhu free movement vimuvu na kuchukua ardhi yetu? Hamjaona vijikaya uchwara vilivyotuzunguka vinavyotia kila mchakato wa kutaka kuja kufaidi ardhi yetu au hamuoni?”
Mpemba anakamua mic, “yakhe naamini kuwa hapa wasomi tuna tena wengi kweli kweli. Hata mie naona hili laingia akilini sana. Heri huyu bwana azuie uingiaji wa wakimbizi uchwara wa kiuchumi na miungano na vijikaya vingine wakati ule wa Zenj bado wantoa jasho. Heri angefyatua ajira na viwanda kwanza, haya ya vitegemezi yakaja baadaye baada ya kuona matunda ya majaribio yake wallahi.”
Kanji anakula mic, “veve Pemba sema kitu ya maana sasa. Kana Kufuli nafyatua jobs naveza leta endeleo kuba sana. Sana kama chovu nazaa kama kuku hapana ona kaya takosa riziki ya kulisha yeye? Kwanini hapana soma toka India. Kule hindi nazaa kama kuku na kila siku vatu naongezeka na nateseka sana.”
Da Sofia anampoka Kanji mic, “kwa vile mipango ya Kiswahili–mara nyingi ni ya muda mfupi–huenda mhishimiwa ametumia kigezo hicho bila kuangalia mambo mengine muhimu yanayoyitajika kama vile hospitali na zahanati za kutosha, huduma safi, madaktari na wakunga wa kutosha na mambo mengine nyeti.”
Mipawa ambaye muda wote alikuwa akiangalia huku akitabasamu, anawaacha wana kijiwe hoi. Anakula mic, “beng’we, sasa mie acha nitume fedha ya kununulia ng’ombe tayari kuongeza ngoma ya pili ili nitekeleze agizo la rahis bila kughairi wala kuuliza. Nyinyi mmeambiwaga mfyatuage vitegemezi mnaanza kuumiza vichwa wakati sirikali lipo litabeba mzigo wake. Nawashaurini tutekeleze wito wa rahis wa kufyatua vitegemezi huku tukimtaka naye afyatue huduma kama wajibu wake au vipi?”
Msomi aliyekuwa akinong’ona jambo na Mpemba anaamua kutia guu tena, “japo sina wasi wasi na uchapakazi na mipango ya bwana Kanywaji, hili sitaliunga mkono hasa kama mchumi. Huwezi kuongeza idadi ya wana kaya wakati iliyopo inakuelemea. Huwezi. Kufanya hivyo ni kujipiga mtama. Hivyo, nisiseme mengi, kuna haja ya kupanga kwenda kuonana na rahis kumshauri akanushe kauli hii kabla hajatengeneza balaa jingine. Nadhani kwa sasa kaya aihitaji vitegemezi badala kujitegemea.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si Mipawa akaaga anaelekea zake usukumani kutafuta ngoma ya pili ili afyatue vitegemezi! Wote tulibaki hoi tusijue la kumshauri. Ama kweli usilojua sawa na usiku wa kiza!
Chanzo: Tanzania Daima leo.
1 comment:
hana mpango huyu
kisha zoea
CHAGULAGA YA KISUKUMA
Post a Comment