Leo ni miaka mitatu na siku chache tangu Dk Sengodo Mvungi afariki dunia. Kwanza, niwatahadharishe wasomaji wa safu hii. Makala hii nimeiandika nikiwa soba kabisa bila kupata kitu chochote. Hivyo, msishangae mkidhani nimedesa kwa mtu. Hii inaonyesha sura yangu ya pili ambayo wengi hawaijui. Hayo tuyaache.
Japo Mvungi alizikwa, kuombolezwa hata kupendwa na wengi, sijui kama bado wengi hao wanamkumbuka. Sijui kama wanakumbuka yale mema yote aliyosimamia na kutenda. Sijui kama wanamkumbuka kama moja wa watu waliosukuma taifa mbele taifa. Sijui kama kama ndani ya kipindi kifupi tu cha miaka mitatu aliyotoweka angesahaulika kirahisi hivi hasa kwa wale walioangusha kazi pevu aliyofanya. Kusema ukweli; kitendo kilichofanywa cha kuzika Katiba Mpya ni dharau ya aina yake kwa marehemu Dk Mvungi. Kwa utamaduni wa kiafrika, mja anapoaga dunia, waliosalia hupenda kuyaenzi yale aliyoyatenda hasa katika mwisho wa uhai wake. Hata hivyo, tokana na dhuluma na dharau hii, sijui kama hao watukufu bado wana hamu naye kwa namna wanadamu tulivyo wasahaulifu kana kwamba kuna watakaoishi milele. Dk Mvungi aliyefia nchini Afrika Kusini mnamo 21 Novemba, 2013 wakati akifanyiwa matibabu baada ya kushambuliwa na majambazi nyumbani kwake. Heri wangemwimbia wakamwachia uhai wake ili aendelee kulitumikia taifa lake na watu wake bila kinyongo wala kuchoka katika nafasi zote alizotumika nchini.
Kwa tunaomfahamu na kumkumbuka, Mvungi alikuwa msomi mbobezi wa sheria, mchangamfu, asiye na makuu ambaye angeweza kujichanganya na makapuku bila kujali hadhi yao kimaisha, mwanasiasa na mtetezi wa haki za binadamu wa kupigiwa mfano. Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) wanalifahamu hili na ni mashahidi tosha wa umahiri wa Mvungi katika kutetea haki za wanyongo. Mbali na hiyo, mchango wake katika kuandika Katiba Mpya iliyouawa na mafisadi haumithiliki ingawa umesahaulika kutokana na kuzikwa kwa katiba husika na majahiri wasiojua kuwa siku yao nao ipo. Wale waliofanya kazi naye kwenye tume hii wanajua umahiri na kujitoa mhanga kwake kwa niaba ya wenzake. Wale waliobahatika kukutana naye iwe ni kikazi au nje ya kazi, ni mashahidi tosha wanaoweza kumweleza marehemu Mvungi alivyokuwa mtu wa watu. Kwa maana hiyo, wengi walidhani; wenye mamlaka walilomteua kuwa mjumbe wa kamati ya kukusanya maoni ya wananchi ya Katiba Mpya wangeipitisha tena bila kuichafua na kuichakachua kama njia mojawapo ya kumuenzi mzalendo huyu mtoto wa taifa hili aliyelipenda bila shaka yoyote. Hata hivyo, hii haikuwa. Ni kiburi na kujilisha pepo kiasi gani? Kwani, wao wataishi au kudhulumu milele? Binadamu ni nini zaidi ya kuwa mavumbi yanayongoja kutawanyishwa na upepo na wadudu?
Dhumuni ya kuandika waraka huu–licha ya kumkumbuka Mvungi angalau iwe faraja kwake, familia yake, marafiki zake na wapendwa wake–nalenda kumrejesha kwenye hadhira lau kutafakari urathi alioacha kama mwadamu muadilifu na mpenda na mtetea haki. Najua hawezi kujibu waraka wangu; lakini anaona. Kwani walichoua ni mwili si roho ya marehemu. Katika kumbukumbu yangu ya Dk Mvungi, licha ya kuongea na wasomaji, naongea na wenye madaraka watende haki kama sehemu ya kumuenzi Dk Mvungi aliyekuwa mpigania haki mahiri na asiyechoka.
Pili, tupambane na ujambazi na kila aina ya jinai vilivyotamalaki nchini mwetu. Kwani, kilichomuua Mvungi si kingine bali ujambazi huu huu ambao utawala uliopita ulionekana kuridhika nao kiasi cha kuulea kutokana na serikali kuwa goigoi na iliyokuwa ikijiendesha bila uongozi imara na wenye visheni. Sasa mambo yamebadilika. Tuna serikali mpya yenye makali angalau. Tunawaomba wenye mamlaka waliopo kulifanyia kazi hili ili tusipoteze Dk Mvungi wengine ambao taifa linawahitaji. Hatutaongelea waliomuua Dk Mvungi kwa vile kesi iko mahakamani.
Tatu, tupambane na ufisadi na ulafi wa kimfumo unaohamasisha wahalifu kutafuta utajiri wa haraka hata kwa kuwaua wenzao. Ningependa siku moja kila mtanzania aeleze alivyochuma mali zake ili wanaopata utajiri kwa njia haramu wataifishwe na kuwajibishwa kisheria jambo ambalo bila shaka litaondoa motisha wa baadhi ya wenzetu kutenda maovu kama, kuwadhuru, kuwaua na kuwaibia wenzao.
Nne, katika kutenda haki kwa watanzania wote, tunapaswa kurejesha kanuni na maadili ya utumishi wa umma. Maana bila kanuni hizi tutapoteza muda kwa kutegemea ukereketwa wa viongozi wachache.
Mwisho, napenda kuiomba jamii ya watanzania popote ilipo, imuenzi marehemu Mvungi kwa kupigania na kutenda haki; vitu ambavyo vilimtambulisha ulimwenguni. Pia tunaipa mkono wa rambirambi familia ya marehemu katika kuadhimisha miaka mitatu ya kifo cha Mvungi. Najua wao huadhimisha maisha ya marehemu kila sekunde, kila dakika, kila siku, kila wiki, kila mwezi na kila mwaka. Nawaombea faraja katika safari hii ngumu yenye kila majaribu na kukatisha tamaa. Faraja kubwa ni moja kuwa yeye alitangulia, sie tuko nyuma yake. Kwa wale waliozoea ulevi naomba wanisamehe. Huu ni msiba. Auhitaji utani hasa ikizingatiwa kuwa kila nafsi itaonja mauti.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.
No comments:
Post a Comment