Kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza dokta Joni Kanywaji wa Makomeo kwa kutumiza mwaka mmoja kwenye ulaji. Pili nimpe salamu za walevi kuwa tumekubali baadhi ya vitu vyake hasa kuwapiga wapigaji waliozoea kutupiga tukapigika japo tumekataa vingine. Leo nataka nimpe ushauri wa nguvu biggie ili afanye maamuzi magumu. Hii ni kutokana na kauli aliyotoa hivi karibuni akiongea na waandishi wa umbea wakati wa kuadhimisha mwaka wake mmoja kwenye ulaji. Kwanza, tumpe shavu; tunamkubali ingawa hatukubali huu msimamo wake mpya wa kusema kuwa hawezi kufukua makaburi kwa sababu hataweza kuyafunika. Oh boy oh bo! We need to open all closets to see the skeletons in there. Lo! Hivi kazi hapa iko wapi hata nikifikiri kilevi kati ya kufukua na kufukia makaburi? Kama yamemshinda si aniite nimpe tafu kwa kuyafukua na kuyafunika tena bila kuhitaji tingatinga wala ndinga? Sisi kwa ngoa, usongo na uchizani wetu tutayafukua, kuyafukia hata kuyatia nari kama ikitakiwa kufanya hivyo.
Wakati aliposema anaogopa kufukua makaburi kwa vile hana uwezo wa kuyafukia, nilikuwa kwa mama Beti nikinyaka kanywaji na washirika na washikaji zangu. Kwanza, tulidhani jamaa alikuwa akitania. Lakini baada ya kurudia kuwa hatakuwa tayari kuyashughulikia makaburi yaliyozika uchumi wa kaya yetu, tulijua kweli jamaa hatanii; anaogopa majinamizi, mabufulu na ndogo za ajabu ajabu ambazo kwa walevi ni kitu cha kawaida hasa usawa huu ambapo maisha yamegeuka jinamizi la kutisha katika mpito wa kuweka kaya kwenye mstari. Pili, tuliona hapa kuna fursa kama atatushirikisha tukamsaidia kuyashughulikia hayo makaburi bila kujali ukubwa wake wala harufu yake. Tatu, tunadhani kuwa kufukua makaburi na kuyahakiki na kuyafukia ndiyo njia ya kuweka mambo hadharani ili kila mmoja ajulikana ana nini kwenye closet yake kama wasemavyo kwa kimombo. Nne, tunashauri kama anahofia ujasiri wetu si basi atumie ndata na ndutu wayafukulie na kuyaufikilia mbali haya makaburi yanayomhangaisha jamaa?
Baada ya kugundua kuwa Kanywaji hatanii, baadhi ya walevi walianza kuguna na kuhoji: ujasiri wa jamaa umeende wapi hadi anapambana na majipu, ugonjwa hatari, lakini anaogopa makaburi tena yaliyojaa mifupa na uchafu? Mbona alisema kuwa hataogopa yeyote linapokuja suala la kusafisha kaya hata kama ikihitaji kufukua makaburi? Je ni kwa sababu ya waliozikwa humo au ni sababu tu? Je anaogopa mabaki yaliyomo au ukubwa wa makaburi yenyewe? Kama ataogopa makaburi, atawaweza wauza bwimbwi na mafisadi na majambazi ambao wako hai? Je haya makaburi anayogopa ni ya watakatifu au wahalifu tunaowajua waligeuza kaya yetu shamba la chizi?
Mlevi mmoja alituacha hoi alipodai kuwa hata angekuwa yeye angeogopa kuyafukua makaburi hasa ikizingatiwa kuwa waliozikwa humo wengi wao ni hai. Baada ya kusema hivyo, wengi walimtaka athibitishe. Ndipo akatuacha hoi kwa kuulizwa swali. Je ni wangapi wanatembea lakini wamekufa siku nyingi na ni wangapi walikusa miaka mingi lakini bado wana nguvu kuliko waliohai hawa ambao wamo kwenye makaburi anayoogopa dokta Kanywaji pale ikulu?
Tokana na bangi, ujinga na ulevi, kila mlevi alianza kutafsiri tamko la kuogopa kufukia makaburi. Wapo waliopendekeza dokta Kanywaji akaribishe walevi wamsaidie kuyafukua na kuyafukia makaburi anayoyagwaya. Kwetu sisi tuliokwishapigika makaburi ni makaburi bila kujali ukubwa wa waliomo wala ukubwa wa makaburi yenyewe. Tukishafyatua ile kitu yetu hata hiyo harufu mbaya itokayo kwenye hayo makaburi wala haitusumbui.
Hivyo, tunamshauri jamaa aangalie kwenye makaburi husika aone kama kuna mifupa na midude kama EPA, Kiwila, Loliyondo, NssF, NbC na madude mengine yanayojulikana na wale waliozikwa nayo au walioyazika. Kama siyo kutafuta visingizio, hakuna sababu ya kuwashughulikia wagonjwa tena wa vichaa kama wale wa kwenye bandari na kuogopa makaburi vinginevyo hayo makaburi yawe yamejaa mabomu yanayoweza kumlipua yoyote aliyeshiriki kwenye zama zake au wale waliojaa kwenye makaburi yale. Hapa naona kama ile mikangafu ya walevi iliyotwaliwa ikichungulia toka kwenye hayo makaburi ogopwa. Naona mabulungutu ya noti na mihadarati kwenye makaburi. Naona majina makubwa ya zama zile yakichomoza toka kwenye makaburi ogopwa. Naona wasiotarajiwa wakichomoza mikono yao kuomba makaburi yao yasifukuliwe. Naona tuliodhani ni waja, kumbe vinyamkera, wakianza kupumua baada ya Dokta Kanywaji kusema hatafukua makaburi yao.
Tumalizie kwa kusema wazi: bila kufukua makaburi, hatuwezi kutatua matatizo yaliyosababishwa na makaburi haya ukiachia mbali kutotenda haki kwa waathirika, waadhirika na hata makaburi yenyewe.
Chanzo: Nipashe Jumamosi juzi.
No comments:
Post a Comment