How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 1 November 2016

Onyo na Ushauri: Mlioghushi Msingonje Kifo Kiwafichue

            Kadhia ya kughushi vyeti na sifa za kitaaluma ni janga na tatizo kwa Tanzania kitaifa hata kimataifa kwa Afrika. Baada ya kuingia sera za uliberali mamboleo (neoliberalism) kama njia ya kuchuma bila kufuata kanuni, kulijitokeza jinai mbali mbali kama vile ufisadi, ubinafsi, wizi wa mali za umma na sasa kughushi.
            Hivi karibuni mbunge wa Vunjo mheshimiwa James Mbatia alitoa pendekezo safi kuwa katika mchakato unaoendelea wa kuhakiki sifa na vyeti vya kitaalumu Tanzania, na vyeti la rais John Pombe Magufuli na wasaidizi wake kama vile makamu wa rais na waziri mkuu vihakikiwe pia. Kwani nao ni watu tena watanzania wanaopaswa kuongoza kwa mstari wa mbele.
            Katika kutafakari ushuri huu adhimu na muhimu, niliwaza juu ya watu au al maarufu vilaza walioghushi tulio au tuliokuwa nao kwenye nafasi za juu. Wapo wachache wanaojulikana. Kadhalika wako wengi wasiojulikana japo wanajijua.  Leo naandika kutoa ushauri kwa wote walioghushi kuweka mambo yao vizuri. Hii ni kutokana na visa viwili vilivyojitokeza baada ya kufariki kwa watu mashuhuri wawili walioaminika kuwa walikuwa wamesoma hadi kufikia shahada ya uzamivu (PhD) wakati ukweli ni kwamba walighushi. Hivyo, hawakuwa na sifa walizokuwa wakidai walikuwa nazo.
            Nitawataja si kwa kuwachukia bali kutaka kuonyesha ni namna gani hakuna siri ya milele. Wa kwanza ni aliyekuwa rais wa Malawi marehemu Bingu wa Mutharika. Huyu bwana alipenda kuitwa daktari wa uchumi japo hakuwa na sifa hii. Baada ya kufariki, ukweli ulifumka kuwa kumbe PhD yake alikuwa ameipata toka chuo cha mitaani kiitwacho California Miramar University (CMU). Uki-google chuo hiki utapata ukweli kuhusiana nacho. Hata hivyo, Mutharika alitunza siri hii hadi mauti yalipomfika hapo tarehe 5 Aprili, 2012.
            Mwingine aliyejulikana kama daktari wakati hakuwa na hata shahada moja si mwingine bali Didas Masaburi, meya wa zamani wa Jiji la Dar Es Salaam aliyefarika tarehe 11 Oktoba, 2016. Wengi walimjua bwana huyu kama msomi bobezi ingawa hakuwa. Kwani katika kusoma wasfu wake uliosomwa na mdogo wake, hakuna hata sehemu moja kulipoonyeshwa kuwa Masaburi alisomea udaktari wa falsafa ukiachia mbali kutokuwa na shahada hata moja. Ukitaka kusoma wasfu wa Masaburi nendahttp://mtanzania.co.tz/?p=22490 au soma habari tangulizi kwenye gazeti la Mtanzania la tarehe 18 Oktoba, 2016.
            Ukweli ni kwamba mabwana tajwa hapo juu, pamoja na umaarufu wao, walikuwa waongo na walitenda jinai. Walichuma kwa kutumia elimu feki jambo ambalo linawaingiza kwenye watu walioibia mataifa yao.
            Wapo wengine walio hai ambao walitajwa na mwanaharakati Msemakweli Keinerugaba aliyefikia hata kuwatungia kitabu kiitwacho Orodha ya Mafisadi Tanzania /The list of Shoddy Degree and Diploma Holders. Katika kitabu hiki chenye kurasa 39 wametajwa vigogo wakiwamo Diodolus Kamala, Mary Nagu, Wiliam Lukuvi, Makongoro Mahanga, Antony Diallo, na  Emanuel Nchimbi. Baada ya Keinerugaba kuwataja wahusika, wapo waliotishia kwenda mahakamani kumshitaki kwa kuwazushia, kuwachafua na kuwavunjia heshima. Baada ya muda, waligwaya na kujikali kimya kama ishara ya kuogopa ukweli zaidi usifichuke.
Japo Keinerugaba alikosa serikali makini na adilifu kuunga mkono hoja yake, bado ana hoja tena yenye mashiko. Kwa mfano Kamala alipokea shahada yake ya uzamivu hapo tarehe 6 Desemba, 2012 toka chuo kikuu cha Mzumbe. Ajabu, kabla ya hapo alijulikana kama daktari bila stahiki. Pia na mwingine aliyezoeleka kama daktari bila stahiki ni Nchimbi aliyepokea pia shahada toka chuo hicho.
Ukiacha hao, pia wapo waliowahi kuwa mawaziri ambao binafsi niliwahi kuhoji elimu zao. Hawa ni Saada Mkuya na Adam Malima ambao CVs zao zinatia shaka.
Kwa wanaojua utaratibu wa kufikia kukubaliwa kusomea na kupewa shahada ya uzamili, wanaelewa kuwa ili kuchaguliwa lazima mwombaji awe na shahada ya kwanza (Bachelor) au ametoa kazi nyingi zenye manufaa za kisomi (scholarly works) kama vile articles, mihadhara na vitabu. Malima hana hata sifa moja kama hii. Je aliwezaje kufanya Masters bila kuwa na shahada ya kwanza wala kidato cha sita? Mkuya naye kadhalika. Ukienda kwenye tovuti ya bunge lililopita utapata sifa za wahusika. Amepata shahada ya uzamili bila kuwa na shahada hata moja! Je wahusika watajitokeza wapinge madai haya?
            Turejee tulikoanzia. Kama alivyoshauri Mbatia, tunashauri wote watakaogundulika kuwa walighushi, warejeshe mafao na mishahara yote waliyopokea wakati hawakuwa na sifa huku wakifikishwa mahakamani ili haki itendeke na liwe somo kwa wengine. Tusiishie hapa. Kwani tunao wengi tu maprofesa, walimu, majaji, mahakimu, wakunga na askari n.k. kwa ushauri mwepesi ni kwamba walioghushi, wasingoje wafariki ndiyo uoza wao ufichuke. Kwani hili licha ya kuaibisha wapendwa wao waliobakia, lina madhara makubwa kwa jamii nzima. Wakati wa kuondokana na watu kuishi bila kuhenyekea sifa wanazodai wanazo wakati hawana ni sasa.  Nashauri katika hili jamii na serikali isiwe na simile na yeyote. Tusiangalie cheo wala sura bali tuwasake na kuwapatiliza kwa makosa waliyotenda.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili juzi.



No comments: