Hivi karibuni kaya yetu ilikumbwa na matukio ya kihayawani na ya kutisha ambayo sipendi kurudia kwa sababu za kitaalamu. Hata hivyo, leo nataka nije na mkakati wa kupambana na wahalifu waliotamalaki kayani hasa hawa wa kada ya chini. Nikiwa zangu Kinondoni si nikakutana na mkubwa wa wilaya bwana Ali Heppy akiwaomba wenye mbavu za mbwa kutopangisha mlevi yeyote bila kuwa na barua toka kwenye sirikali za mitaa na mataa. Bwana Heppy alisema “nitumie nafasi hii kuwaomba wenye nyumba usimpangishe mtu nyumba yako bila kwanza kuona barua kutokasirikali ya mtaa alikokuwa akiishi awali ili kubaini kama ni mzuri au mbaya, maana wengine ni majambazi na wakimbizi.”
Kwanza, pamoja na ulevi na madude yangu nilishangaa sana kusika mkubwa wa wilaya wa sirikali akiwabembeleza walevi badala ya kutoa amri na nini kitafuatia atakapoikhalifu mlevi. Pamoja na utekelezaji huu wa kisiasa, mlevi natoa maangalizo ili kuepusha kuendelea kucheza na ngoma ile ile wakati tukijua kuwa hakuna kitakachofanyika hasa ikizingatiwa kuwa walevi wetu siku hizi wamekuwa wabinafsi, wapenda vitu kiasi cha kuruhusu wahamiaji haramu na wahalifu kupanga na kujificha kwenye mbavu zao za dog.
Pili, kutegemea vijibarua vinavyoweza kughushiwa kuwa vitatatua tatizo ni kujidanganya. Kama wapo wanahizaya wanaoghushi shahada, vyeti na nyaraka mbalimbali ambavyo vinahitaji teknolojia ya juu kuvitengeneza, watashindwa vijibarua vya serikali ya mtaa?
Tatu, je huko sirikali ya mitaa na mitaani ni salama au zitawaacha wahusika kwenye mataa? Mbona huko ndiko kwenye chimbuko la rushwa ndogo ndogo? Toeni vitambulisho vya uraia na namba ya utambulisho.
Sitaki nionekane kuwa najidai, ngoja nitoa mfano mdogo toka hapa Ukandani namba hiyo huitwa Social Insurance Number. Huwezi kupata leseni ya udereva, kupanga nyumba, kutibiwa, kuajiriwa wala kufanya lolote bila kutaja au kuonyesha namba hii. Namba hii imewekwa kwenye kompyuta na kila unapokuwa katika Kanada unajulikana pindipo kompyuta ikisoma namba yako.
Nikirejea home ambako kila mlevi anatanguliza njaa yake, napinga wazo la vijibarua. Kwanza, kuna aina fulani ya ubaguzi na uroho. Nitoe mfano, wakija wachainizi na magabacholi hata al shabaab wanashobokewa na kufichiwa madhambi yao. Acheni ushamba na kubaguana wakati huku utashani wote tunaitwa chinga uwe gabacholi, chainizi, mmanga wala nini wao hawajali. Wanaweka kwenye kapu moja chingaz. Hata hivyo, nawapenda watasha kwa kitu kimoja. Si wabaguzi kama hawa wabaguzi uchwara wetu wanaokimbia shida kwao na kuja kwetu kudengua wakati ni maskini wa kutupwa. Hapa ukitaka toto la kitasha unaoa bila kipingamizi; na siyo sawa na wahaindi na waarabu wanaobagua waswahili.
Kitu kingine nilichojifunza kwa walevi wa huku ni kwamba hakuna kuaminiana. Hivyo, huwezi ukaingia kwenye kaya ya wenyewe kinyume cha sheria eti ukawahonga vijisenti wakajiweka hatarini. Huku wakikunasa utalia na kusaga meno. Wala hawababaikii wageni hata wawe wazungu wa bwimbwi wenye njuluku za kumwaga.
Nimalizie kwa kushauri yafuatayo kama mtaalamu wa makosa ya jinai:
Mosi, wabunge waende bungeni na kupeleka mswaada wa kuwashughulikia wenye mbavu za mbwa waroho wanaoshirikiana na wahalifu. Mfano, mnaweza kuamru kuwa atakayekamatwa amempangisha mhalifu awe wa ndani au nje nyumba yake inataifishwa na anafungwa mvua 25.
Pili, sheria imtake mhusika kumtunza mlevi au walevi aliokuwa amewapangisha kinyume cha sheria hata watakapokuwa wamehukumiwa kwenda lupango au kuamriwa kuondoka kayani basi mhusika awalipie nauli ya pipa kurejea kwao.
Tatu, jengeni utaratibu wa kuvizi na kuvamia mbavu za mbwa mnazoshuku huku mkiweka mashushu watakaojifanya ima wahalifu au wahamiaji haramu wanaotafuta mbavu za mbwa za kupangisha, mtawapata kirahisi.
Nne, imarisheni ulinzi wa mipaka yenu hasa kwa kufanya ukaguzi wa kielektroniki na si mikaratasi ya akina Adam na Eva. Hii ni karne ya sayansi na tokonolojia jamani.
Zikomo kwa mbiri!
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.
No comments:
Post a Comment