Hivi karibuni, mbunge wa Muleba Kusini profesa Anna Tibaijuka alipokea tuzo toka umoja wa mataifa ukitambua mchango wake katika kuhamasisha maendeleo. Hili si jambo jipya hasa kwa mtu aliyewahi kuajiriwa na umoja wa mataifa. Tunampongeza kwa kutambuliwa mchango wake. Hata hivyo, madai kuwa aliacha kuchukua fedha ilioandamana na zawadi aliyopewa tokana na sababu za kimaadili ni kituko cha kufungia mwaka huu. Tibaijuka alikiririwa akisema “na huambatana na zawadi ya Dola za Marekani 100,000 (Sh milioni 200). Sikuzichukua fedha hizi, kama mnavyojua maadili ya nchi yetu unaweza ukapokea yakaibuka mambo mengine.” Hii si kweli. Ukichukua zawadi iliyokatazwa kisheria na kuifanya mali binafsi ndipo yanapozuka hayo anayodai Tibaijukaa. Lakini ukiisalimisha kwa serikali, huo ndiyo uwazi, uwajibikaji na uzalendo na si mtima nyongo kama alioonyesha mhusika. Hivyo, madai ya Tibaijuka ni si ya kweli na ni ya ajabu sana hasa kwa mtu ambaye historia inamtambua kama mtu aliyewahi kuivunja hiyo sheria akapokea zawadi tena nono tu. Je Tibaijuka kaifahamu hii sheria jana tu au ni kutaka kuwageuza watu majuha? Kama alikuwa na nia nzuri, kwanini asiipokee hii fedha na akaikabidhi kwa serikali? Nadhani; Tibaijuka awe mkweli kuwa ana kinyongo; na kama siyo, basi hakuwa tayari kuona fedha hiyo inatumiwa na umma badala ya yeye binafsi. Hakuna sheria inayomzuia kupokea zawadi au tuzo akawaviwasilisha serikalini zaidi ya roho mbaya tu ya kawaida kwa wale wanaoacha vitu kama hivyo kwa vile hawataweza kuvifaidi. Hivyo, Tibaijuka alimua kucheza mchezo wa “kama mimi sipati heri wote tukose” ambayo mara nyingi ni dalili za mtima nyongo hasa kwa mtu aliyekaririwa akikiri kuwa fedha ile ingesaidia wahanga wa tetemeko mkoani mwake. Ana bahati hao wanaompa kura kama hawatamwadhibu kwa mtima nyongo huu vinginevyo alichofanya kingegeuka kuwa mwanzo wa mwisho wa ubunge wake.
Tibaijuka aliongeza “sikuichukua kwa sababu ya yaliyonikuta hapo mapema, kulikuwa na uwezekano wa kuichukua lakini nikasema kwa hali halisi ya nyumbani, hatuna sheria ya kupokea tuzo, michango na zawadi kwa hiyo mimi nikaicha mezani wao wafanye wanayotaka.” Hapa Tibaijuka naona kama anajichanganya; kama si kutaka kupotosha hata kudanganya. Kama nukuu yake anasema “hatuna sheria ya kupokea tuzo, michango na zawadi kwa hiyo mimi nikaicha mezani wao wafanye wanayotaka.” Kama ni kweli mbona sasa amechukua tuzo au ni yale ya kuacha nyama ukanywa supu ukasema sijala kitu kitu hii? Je amechukua tuzo hiyo kwa sheria ipi wakati anakiri mwenyewe kuwa hakuna sheria inayomruhusu kufanya hivyo? Sijui, kama Tibaijuka alitafakari maneno yake yaliyonukuriwa hapo juu toka kinywani mwake. Au anapanga kusema alikaririwa out of context? Tunamtaka Tibaijuka awe mkweli kwake binafsi na kwa wale anaolenga kuwaelezea haya mafanikio yake tata. Maswali ni mengi kuliko majibu. Je ina mana Tibaijuka hajui kuwa tuzo si mali sawa na fedha tena yenye thamani kuliko hiyo fedha aliyokataa? Kwa wanaojua maana na athari za tuzo kwa mhusika, tuzo ina athari chanya kubwa kwa mpokeaji kuliko fedha inayoandamana nayo. Na ndiyo maana watoa tuzo hutangaza kuwa wanatoa tuzo lakini si fedha. Fedha huandamana na tuzo kama msindikizaji; lakini tuzo ndiyo big deal. Hivyo–kama kweli Tibaijuka alidhamiria kufanya anachotaka kuhadaa umma kuwa alifanya–basi angekataa vyote hadi apate ushauri wa kisheria. Hata hivyo, kama profesa, Tibaijuka alipaswa kujua vitu rahisi na vya msingi kama hivi. Vinginevyo alichofanya ni kujichanganya na kuendelea kudanganya umma. Ni utata mtupu. Na wala haitamsaidia kukimbia kila alicholenga kukimbia. Akubali kuwa alikosea; atubu na kurejesha fedha haramu ya Escrow na kuanza upya vinginevyo zimwi hili litaendelea kumuandama tu.
Pia Tibaijuka alipaswa kufahamu kuwa hakuna sheria inayozuia kuchukua vitu hivyo anavyotaja. Vinginevyo, asingechukua mabilioni ya Escrow. Nadhani Tibaijuka aliona milioni 200 ni vijisenti hasa ikizingatiwa alishapokea mabilioni pamoja na kutokuwapo sheria ya kufanya hivyo anayoongelea kwa sasa na kujidai kuisheshimu. Sijui kwanini wakati akipokea mabilioni ya Escrow hakukumbuka maadili na sheria anayoongelea kutaka aonekane safi wakati alishajichafua siku nyingi?
Tibaijuka pia alikaririwa akisema “lakini kwa sababu jamii haina uwezo wa kuchimba chini, unabaki kuwa uongo na kushindwa kujua ukweli umesimama wapi, lakini wao (UN) wanajua hii ni propanda la sivyo nisingesimama hapa na tuzo.” Tibaijuka awe mkweli. Kwanza inashangaza mtu anayeitwa profesa anayepaswa kufahamu madhara ya mijumuisho katika kutoa madai anapoihukumu jamii nzima kwa uzembe na mapungufu yake. Kama suala la Escrow ni propaganda, alishindwa nini kusimama na kujitetea? Kama ni propaganda, alishindwa nini kwenda mahakamani kuwachukulia hatua anaodai wanamchafua wakati alijichafua mwenyewe? Pili, Tibaijuka anapaswa kueleza ni jamii ipi maana neno bila kutofautisha ni ipi ni tata. Je alimaanisha jamii ya dunia nzima, Tanzania au huko kwao?
Tumalizie kwa kumtaka Tibaijuka awe mkweli. Je Tibaijuka anataka kumdanganya nani wakati kila kitu kiko wazi kuwa alichukua mabilioni ya Escrow?
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili jana.
No comments:
Post a Comment