Wiki hii mlevi sikupata vile vitu vyangu. Nilikuwa kwenye msiba hata kama uliwahusu wachovu ambao sikuwahi kukutana nao. Baada ya kunyaka taarifa kuwa wanakaya kwenye kijiji cha Iringa Mvumi waliamua kuwanyotoa roho wataalamu wa kupima udongo ili kuwawezesha kuzalisha vyakula vya kuwatosha, nilijihisi kupasuka kwa hasira. Nilitamani nichukue cha moto na kwenda kutangaza mauaji ya halaiki. Hata hivyo, niligundua kuwa hili si jibu.
Kuna mambo muhimu ya kujifunza tokana na kadhia hii hata kama ni ya kilevi na kinyama.
Mosi, kuna haja ya kuhakikisha wote walioshiriki jinai hii wanakamatwa na kutupwa lupango wakingoja kuwa na date na pilato ili wapewe stahiki yao kisharia.
Pili, nashauri sirikali ianzishe tena elimu ya ngumbalu ili kuondoa huu ujinga uliokwamia kwenye akili za baadhi ya walevi hasa wa kule mashambani ambao wanaweza kupwakia kila upuuzi hata bila kutumia bongo zao. Unategemea nini unapokuwa na kaya inayotumia masaburi kufikiri badala ya bichwa?
Tatu, kaya ianze safari ya kupiga vita kila aina ya ushirikina uwe ni wa kidini, kisiasa, hata kijamii. Nadhani hapa tunaweza kuona matokeo ya kuruhusu matapeli fulani kuwajaza walevi woga na kuwaibia ima kwa kuwahubiria dini au kujifanya waganga njaa wa jadi. Ama kweli ujinga ni zigo kubwa tena la manonihino! Nani angeamini kuwa hata mchungaji ambaye amethibitisha kuwa wengi ni wachunaji angeshirika dhambi hii? Je tunao wachunaji wapumbavu na katili kama hawa kiasi gani kayani? Rejea kutamalaki kwa dini za kishirikina, kilaji, waganganjaa wa jadi na matapeli kila aina bila kusahau hata vyama vya siasa vinavyoendesha siasa za kitapeli kama vile vinavyomilkiwa na walevi binafsi wakivigeuza NGO zao za kutengenezea njuluku.
Nne, tuanze mchakato wa kuondoa kaya yetu kwenye unafiki wa kimfumo ambapo halaiki ya walevi hujisikia raha na kushabikia kuua vidokozi na vibaka huku wakinyenyekea na kushobokea mibaka kama ile ya Escrow, Epa, UdA, Kagoda, na mingine mingi iliyotamalaki na kutapakaa kayani. Angalia vibinti vyetu vinavyonyotolewa na ngoma kutokana na ujinga na umaskini na hakuna anayehoji wala kuwa mkali!
Tano, kaya inapaswa kuanza safari ya kuusaka ubinadamu na kuuzika unyama na uhayawani kama ulioonyeshwa na walevi wa kule Mvumi Iringa. Tumegeuka kaya ya samaki ambao hulani kulingana na saizi.
Sita, lazima tuanze kuwashughulikia walioteka uhuru wetu huku wakichezea kaya yetu kiasi cha kuacha walevi wawe wajinga, majuha na wakatili wa kutupa kiasi hiki. Kaya haiwezi kuwa salama wakati imejaa mijitu mipumbavu na mikatili inayoweza kufanya lolote ima tokana na woga au kutafuta rizi. Nani haoni wanavyonyotoa roho walevi wenye ulemavu wa ngozi? Unategemea nini unapokuwa na kaya walevi walio wengi wajinga wanaoweza kuamini kila kitu? Mijitu imekuwa mikatili hadi inauana. Hata hivyo, tuna bahati, zingekuwa zama za utumwa tungeuzana kwa sana kama walivyofanya baadhi ya mababu zetu wenye roho mbaya.
Saba, nashauri kitaalamu kuwa kila kijiji kiwe na kituo kidogo cha ndata ambao wanaweza kusaidia kuzuia unyama na upuuzi kama huu tunaoogelea.
Nane, wataalamu au walevi wetu wanaoingia kwenye maeneo mageni ima wapewe ulinzi wa askari au waruhusiwe kupeperusha bendera ya taifa kwenye magari yao. Kwani, walevi wetu wamezoeshwa kuogopa bendera kama alama ya sirikali. Pia nashauri sirikali izifidie vilivyo familia za wahanga wa ujinga wa taifa unaotishia kuliteketeza taifa letu.
Kabla ya kusahau, nadhani yote yaliyopendekezwa hapo juu hayawezi kufanyika wala kufanikiwa bila kuwa na ile kitu iliyouawa na mafwisadi wenye ulaji kuogopa kunyea debe yaani KATIBA MPYA. Chonde chonde wahusika. Turejesheeni katiba yetu mpya ya walevi ili tuitumie kurekebisha na kukomboa kaya yetu inayoendelea kutopea kwenye mikono michafu ya mafwisadi na sasa wauaji! Ni hatari; hasa tunapogeuka kaya ya wapumbavu na wanayama.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.
No comments:
Post a Comment