Baada ya rais John Magufuli kuridhia kufunguliwa ubalozi wa tanzania nchini Israeli, wengi walishangaa hata wengine kumlaumu wakiona kama anakwenda tofauti na msimamo wa Tanzania bila kujua kuwa mambo yamebadilika tena sana. Kwani, alichofanya ni tofauti na msimamo wa Tanzania ulioasisiwa na baba wa taifa Mwl Julius Nyerere. Hivyo, wengi waliona kama anakiuka miiko ukiachia mbali kuonekana kama anaangalia ndani (inward looking) akipuuzia uhusiano wa kimataifa. Rais Magufuli alikaririwa hivi karibuni akisema “nimeamua kurudisha uhusiano na Israeli, kwa kumteua Balozi tu umekuja ujumbe wa watalii wapatao 600 kutoka nchi hiyo, fedha zimeingia.”
Katika kudurusu hili, nitatoa sababu zifuatazo:
Mosi, siasa za sasa na za wakati wa akina Mwl Nyerere ni tofauti sana. Wakati wa Mwalimu, dunia ilikuwa kwenye kile kinachoitwa vita baridi (Cold War) kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti wa Kirusi (USSR) kama mataifa mawili kandamizi na koloni bila kujali nani alikuwa upande gani. hata hivyo, baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin hapo 9 Novemba,1989 dunia ilibadilika kwa kiwango kikubwa baada ya upande wa Magharibi ukiongozwa na Marekani kufanikiwa kuuangusha upande wa Mashariki ukiongozwa na Urusi. Hivyo, siasa za wakati ule ni tofauti kabisa na za sasa. Wanaoona kama ni ajabu kuanzisha uhusiano na taifa la kizayuni lenye sifa ya kuwakandamiza Wapelestina, inabidi waelewe hili.
Pili, tujiulize. Hivi kama Palestina ingekuwa huru na sisi tukiwa tunatawaliwa ingekuwa tayari kutoa sadaka ya uchumi wake eti kwa sababu ya taifa la Kiafrika kama Tanzania? Hili sitalijibu. Jibu lake unaweza kulipata mwenyewe kwa kuangalia ima uhusiano baina ya masalia ya waarabu yaliyoko Tanzania au tabia za nchi za kiarabu dhidi ya waswahili. Hivi karibuni kumekuwa na taarifa nyingi za vifo vya waswahili huko Mashariki ya kati vya wafanyakazi wa ndani wa kiswahili tokana na ubaguzi na ubaguzi, ujinga na unyanyasaji wa waajiri wao ambao bado huamini kuwa mtu mweusi ni mtumwa au abid. Mbali na hilo, rejea namna hawa wapalestina tunaowakingia kifua walivyotuuzia ndege mbovu wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere pamoja na kuwaamini na kuwatetea.
Tatu, ili kujua kuwa kwa sasa kila nchi inaangalia maslahi yake, rejea kitendo cha nchi ya kiarabu kama Misri kusaini mkataba na Israeli maarufu kama Mkataba wa Camp David uliofanyika huko Camp David mnamo tarehe 17 Septemba, 1978 baina ya rais wa zamani wa Misri Anwar El Sadat na waziri mkuu wa zamani wa Israeli, Menachem Begin. Kumbuka. Wakati Misri ikiingia mkataba na Israeli, mataifa yote ya kiarabu yalikuwa yameapa kutohusiana na Israeli. Lakini baada ya Misri kuona hatua hii inaathiri uchumi wake, iliamua kuingia mkataba wa makubaliano na ushirikiano na Israeli. Kama waarabu ambao ndiyo ndugu wa wenzao wa Palestina waliona madhara ya uhafidhina wao, sisi ni nani? nadhani tulichelewa.
Nne, ukiachia mbali Misri, hebu angalia Palestina yenyewe inavyoshirikiana na Marekani ikitegemea itatue mgogoro taifa ambalo ndiyo mhimili mkuu wa uwepo na ustawi wa Israeli tokana na kuipa fedha nyingi za misaada kuliko nchi yoyote ulimwenguni. Hapa hujaongolea kuiwezesha Israeli kijeshi na kijamii. Tanzania ni nani kuendelea na misimamo ya kikale? Ni vizuri kufahamu kuwa mahusiano ya kimataifa ya sasa yamejikita sana kwenye uchumi kuliko siasa na mambo mengine kama ilivyokuwa hapo zamani. Siasa za kisasa zinataka hivyo.
Tano, kwa wanaokumbuka namna Tanzania na nchi nyingine zilizokuwa mstari wa mbele kupigania ukombozi wa Afrika Kusini zilivyoathiri uchumi na maisha ya watu wao kuhakikisha makaburu wanang’olewa, ni mashahidi kuwa namna ambavyo Afrika Kusini sasa inawatenza watu wao ni somo tosha juu ya kuhatarisha uchumi na maisha ya nchi kwa ajili ya siasa za nchi nyingine. Hakuna anayeunga mkono ukaburu unaofanywa na Israeli dhidi ya Palestina. Hata hivyo, pia hakuna ambaye yuko tayari kuhatarisha uchumi wa taifa lake kwa ajili ya taifa jingine. Hii maana yake ni kwamba, badala ya nchi moja moja kujitoa mhanga kuhakikisha Palestina inapata uhuru wake, nchi zote zinapaswa kuungana pamoja na kukabili mataifa ya magharibi ambayo kimsingi ndiyo mihimili mikuu ya ukaburu unaoendelea nchini Palestina. Kwa nchi maskini kama Tanzania, kuendelea kuitenga Israeli na kupoteza fursa za kiuchumi, ni kujitia kitanzi kwa ajili ya jambo ambalo halitafanikiwa kutokana na hatua kama hiyo. Siasa za mapenzi ya mshumaa zimepitwa na wakati kama tulivyoeleza tokana na kuanguka kwa ukuta wa Berlin.
Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli kuhakikisha anafanya biashara na Israeli lakini siyo kugeuzwa mmojawapo wa watu wa kutumika kuhalalisha ugaidi na unyama inaowafanyia wapalestina. Aeleze wazi wazi msimamo wake kuwa lengo lake ni mahusiano ya kibiashara lakini si kujiingiza kwenye siasa za ndani katika mgogoro huu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
4 comments:
Salaamu Mwalimu Mhango,
Maamuzi haya ya rais Magufuli kuurudisha uhusiano wa kibalozi na taifa la Israel kwa maoni yangu nadhani serikali yetu ilichelewa sana kufanya hivyo.Tukiachilia mbali tu kumalizika vita baridi(cold war) kati ya kambi ya Magharibi na Mashariki kambi ambazo kama ulivyozieleza zilikuwa ni za kikoloni kwa kutafuta makoloni kwa mtindo wa itikadi(ideology) za kisiasa.Na kwa wale viongozi ambao walikuwa wakipambambana na ukoloni huo walipambana kwa kuanzisha kambi yao ya "kutofungana na upande wowote"(Nonalignend Movment) kambi ambayo mmoja wa waasisi wake ni Mwalimu Nyerere na kwa vile Mwalimu Nyerere alikua ni kiongozi wa zama zake ambae ni mpenda haki,uadilifu,usawa na mpigania uhuru hakusita wala kufumbia macho kupambana na mataifa yoyote yale yenye siasa za kibaguzi na ukandamizaji wa mataifa mengine likiwemo taifa la Afrika Kusini na Israel na hata hakuwa tayari kuyakubali masharti kandamizi ya wakoloni hawa wa kambi za magharibi na mashariki.Na matokeo ya siasa ya Mwalimu Nyerere na msimamo wake huo ulimpa heshima na kulipa heshima taifa letu kutoka kwa marafiki na maadui kwa pamoja japo nchi yake na wananchi wake waliathirika.Kwa hiyo zinapoondoka sababu na visababisha kunakuwepo na muono mpya na maamuzi mpya na hivyo ndivyo alivyoamua rais Magufuli,kwani sababu za kimsingi za kuendelea kutokuwepo na uhusiano wa kiubalozi na taifa la Israel hazipo tena ikizingatiwa na viashiria au sababu zote ambazo ulizoziandika katika makala yako hii.
Inaendelea................
Kama utakumbuka Mwalimu Mhango,wakati Mwalimu Nyerere akijitolea muhanga yeye mwenyewe na Taifa lake kuyatetea mataifa manyonge,nchi kama Kenya,cote d'lvoire(Ivory Coast) Turkey zilikuwa na uhusiano kamili wa kidiplomasia na nchi za South Africa na Israel na nchi hizo hazikuona mateso wala ukandamizwaji wa wananchi wa South Afrika wala wanachi wa Palestine,na hii ndio sababu ilyomfanya Mandelea kukataa mwaliko wa kuitembelea Kenya na mwaliko wa kutunikiwa medali ya juu kabisa nchini Turkey.Naam Mwalimu Mhango,umeitolea mfano hai kabisa nchi ya Misri kuchukua maamuzi ya kufanya mahusiano ya kidiplomasia na nchi ya Israel kwa pande zake zote kwa masilahi ya Misri na wananchi wake,wache niongezee tu kwa kusema kwamba tatizo la Palestine lingemalizika siku nyingi sana endapo nchi za kiarabu wangetaka kulimaliza tatizo hilo,lakini kwa UNAFIKI wa nchi za kiarabu hawakuwa tayari na hawapo tayari kulimaliza tatizo la wananchi wa Palestina kwa vile tu kwamba wao wenyewe kwa wenyewe hawana umoja unostahiki kuitwa umoja na wapo chini ya matawa na mapendekezo ya Amerika na nchi za kimagharibi.Ni waaarabu hawa tunawaona wanauana wenyewe kwa wenyewe bila sababu za kimsingi na zinazokubalika na tunaishi kwa mafano hai kwa matatizo yote ya kukosekana amani,usalama na vita vya kisaikolojia na vya ardhini kuanzia Iraq,Syria,Libya na hatimae Yemeni.Leo hii kwa siri na dhahiri mataifa ya kiarabu yanashirikiana kikamilifu na taifa la Israel katika masilahi yao ya kisiasa na kiuchumi na wanaendelea kushirikiana kikamilifu na Israel dhidi ya taifa la Irani,Irani ambayo kwa hali na mali ndio taifa pekee ambalo limeshikilia bango la matatizo la Palestina na wananchi wake.Kama waarabu wangekuwa na muono wa mbali wangefanya majuhudi makubwa kwa kuwekeza katika Bara letu la Afrika,lakini kwa vile wana tabia ya kuwadharau waafrika wamejikuta wanatanguliwa na nchi kama ya Turkey ambayo inawekeza kwa kasi sana katika bara la Afrika wakishindana na nchi ya China.Tukumbuke tu hapa jinsi gani viongozi wa Saudi Arabia walivyomdhalilisha rais Obama katika ziara yake ya mwisho nchini humo kwa kupokelewa na Meya wa mji wa RIadhi na hata kumwita abdi nyuma ya pazia.Hawa ndio waarabu ambao wanachekwa na mataifa yote ambayo yenye muono wa mbali wa kuwa na umoja na nguvu za kisiasa kiuchumi na kijamii ukizingatia kwamba wana sababu zote za mafanikio kuanzia dini,rasilimali,mali ghafi,wasomi nguvu kazi na mweko wao wa kijiografia.
Inaendelea
Wache nami nimalizie kwa kuandika kwamba Tanzania ilichelewa kurudisha mahusiano yake ya kibalozi na taifa la Israel,kama ni maaumizi ya kurudisha mahusiano hayo basi isiwe tu upande wa kiuchumi bali uwe uhusiano wa pande zake zote kisiasa,kiuchumi,sayansi,kiteknolojia na hata kijeshi pia.Na hapa hatuongelei kwa wale wakereketwa wa kidini kwa kumsifu Magufuli kwamba amewarudishia nafasi ya kuhiji mji mtakatifu wa Jerusalem kwani ruhusa ya hija hiyo ilikuwepo kwa miaka mingi tu na nadhani hata Mwalimu Nyerere alikataa kwenda kuhiji nchini Israel kwa hoja hiyo hiyo ya kuisapoti Palestina.
Anon.,
Kama kawaida, nashukuru kwa mchango wako wa nyongeza kwa yale niliyotongoa. Nakubaliana nawe kwa mengi hasa ikizingatiwa ulivyojikita kwenye kueleza unafiki wa waarabu na dharau zao kwa waafrika ambao nao kama vipofu wanaendelea kujipendekeza kwao kwa kisingizo cha uislam.
Ni kweli Tanzania tulichelewa sana kustukia janja hii. Sijui kama sisi tungekuwa katika hali waliyomo wapalestina kama wangepoteza muda hata kulaani kitendo hiki ikizingatiwa karibu waarabu wote bado wanawaona waafrika kama watumwa.
Post a Comment