The Chant of Savant

Tuesday 11 April 2017

Kashfa za Makonda zitalifikisha wapi taifa?

       Image may contain: 2 people     Japo mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda anaweza kujiridhisha kuwa ndiye alianzisha vita dhidi ya biashara na utumiaji wa mihadarati, ukweli unabaki pale pale kuwa vita hii ilianza zamani. Hata hivyo, si vibaya kupongeza uthubutu wa Makonda kukumbushia vita hii japo kwa namna ya hovyo na yenye kuleta utata na kudhalilisha ukiachia mbali uvunjaji wa sheria, kuna kila sababu ya kupambana na balaa hili. Je, kama taifa, tunapambana na kadhia hii kisayansi na ilivyo?
            Tangu Makonda ataje majina ya vidagaa, hatuoni cha mno kinachotokea kama tulivyotegemea. Badala yake, tunaona juhudi kubwa zikielekezwa kwenye mambo ya hovyo kama kumtetea Makonda dhidi ya kashfa ya kughushi vyeti. Badala ya kuelekeza nguvu zetu zote kwenye janga la mihadarati, nguvu kubwa, kwa sasa, imeelekezwa kwenye kulindana, kulidhishana na kutafuta kila visingizio kwa mhusika kuendelea kuwa madarakani japo umma umeishaonyesha wazi kutomkubali mhusika tokana na uchafu wake binafsi.
            Hakuna kinachoshangaza kama ukimya wa serikali hasa rais John Magufuli katika kukabili kadhia hii ya jinai ya wazi. Tokana na mkwamo na kizungumkuti vilivyopo, inafikia mahali wengine wanakata tamaa kuwa kilichoibuliwa kama vita dhidi ya mihadarati ima ni nguvu ya soda au kutafuta umaarufu wa shilingi mbili. Tutatoa sababu kwanini hii dhana inaweza kuwa na mashiko.
            Mosi, jemadari wa vita dhidi ya mihadarati amekuwa akitangaza vita kila aina ilmradi kuiweka hadhira kwenye hali anayotaka yeye kwa ajili ya kuepusha janga kuu linalomkabili binafsi. Tunasema hivi kutokana na ukweli kuwa hata yale matamko, ukiachia mbali mikakati ya rais kupambana na kughushi kama njia ya kurejesha heshima ya elimu na uwajibikaji havisikiki tena. Tulizoea kusikia watu wakitumbuliwa tokana na kughushi vyeti vya kitaaluma. Lakini baada ya kashfa ya Makonda kufumka, juhudi zote dhidi ya kughushi zimeyeyuka. Huwa najiuliza hali ingekuwaje kama mtuhumiwa angekuwa mpinzani au yule asiyemfurahisha rais kama ilivyotokea kwa waziri mmoja aliyetimuliwa hivi karibuni. Je katiba yetu inatushauri tufanye  hivi kweli? Sijui kama wahusika  wanajua madhara wanayolisababishia taifa mbele ya mataifa mengine. Ukiachia hilo, sijui wanatoa mfano gani kwa jamii iliyowaamini madaraka ikitegemea watu wote watendewe kwa usawa.
            Kama haitoshi, rais Magufuli aliahidi kupambana na mafisadi na wote waliojilimibikizia utajiri wa kutia shaka. Makonda ametuhumiwa na baadhi ya wabunge kuwa ana mali nyingi kinyume na stahiki yake. Hakuna kinachosikika kumchunguza hata kutoa maelezo ya nini kinafanyika kuonyesha ukweli ni upi. Vyombo vyote husika vinaonekana wazi kumgwaya mteule huyu asiyeguswa tokana na ukaribu wake kwa rais. Je namna hii kweli tutashinda. Kwanini shughuli za umma zinafanywa kana kwamba ni suala la mtu binafsi?
            Kuna ushahidi tosha kuwa Makonda anaogopewa na vyombo husika. Rejea mfano wa hivi karibuni ambapo Spika wa Bunge la Muungano Mheshimiwa Job Ndugai alitoa amri ya kumkamata  mbunge wa Kawe Halima Mdee kwa kumtukana spika. Unashangaa inakuwaje nguvu kubwa kama hii kutumika wakati  Makonda alipowatukana wabunge wote kwa ujumla wao kutotumika nguvu kama iliyoamrishwa itumike kumsaka Mdee. Je ni kwa sababu Mdee ni mbunge wa upinzani au ni kwa vile Makonda ni mkuu wa mkoa na mtu wa karibu na rais? Nani mara hii aliyesahau mbunge wa CCM, Peter Serukamba aliyewahi kutukana wazi wazi tusi zito kama eff you  h akutumiwa polisi wala hakuchuliwa hatua? Hii inatia doa na kujenga shaka kwa utawala wa Magufuli. Sijui kama yeye na washauri wake wanaliona hili kama lilivyo.
            Ukiachia mbali hili la kutukana wabunge, Makonda anatuhumiwa kuvamia kituo cha Clouds na kusababisha mtafaruko kwa maslahi binafsi. Tokana na kuogopewa na vyombo husika, hata Waziri mwenye dhamana alipounda tume ya kuchunguza tuhuma dhidi ya Makonda ili atumbuliwe, aliishia kutumbuliwa kama onyo kwa wengine wanaotaka kushughulikia kashfa zinazomkabili Makonda. Hivyo basi, tunaweza kusema; vyombo kama Baraza la Mitihani la Taifa, Tume ya Maadili ya Viongozi, Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) , Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama vyote vimeonyesha wazi kumgwaya mhusika kiasi cha kuanza kujengeka chuki dhidi ya serikali tokana na ulegelege wake na upendeleo wa wazi kwa Makonda.
            Tumalizie hapa kwa kuwataka wahusika wafanye kile kiitwacho soul searching kwa kiingereza yaani kujisuta na kuchukua uamuzi ugumu kwa pamoja au kila mmoja kivyake wakijua fika kuwa kuna kesho. Haiwezekani mambo mengine yakakwama tokana na matatizo ya mtu mmoja au watu wawili. Ofisi za umma si sehemu ya kuimarishia urafiki,ukaribu au jambo lolote zaidi ya shughuli za umma. Kwa taasisi zinazohusika na jinai husika, zinapaswa kuondoka kwenye woga zikizingatia kuwa hakuna mwenye kuweza kuzidi taifa hata awe anapendwa au ana mamlaka kiasi gani.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.

No comments: