Hivi karibuni jambo moja lenye kuzua utata lilitokea bungeni ambapo rais Mstaafu Kanali mstaafu Jakaya Kikwete alishangiliwa na wabunge kuliko ilivyowahi kutokea bungeni. Wapo wabunge waliosema wazi kuwa wanammiss. Je kwanini walifanya hivyo? Hii nadhani inatokana na kutopenda au kufurahia namna mambo yanavyokwenda ndani ya serikali, Chama tawa na nchi nzima. Kwa namna hiyo basi, namuonea huruma Magufuli kutokana na kuchukiwa kwa sababu ambazo nyingine ni za kujitakia na nyingine ni matokeo ya hao hao wanaokuwa missed. Je mapenzi haya mapya ni matokeo ya ukosefu wa kumbukumbu au usanii?
Wakati mwingine unaweza usimuonee huruma Magufuli hasa kutokana na kushindwa kufukua makaburi na kushindwa kuyafukia kiasi cha sasa kuanza kuandamwa na makaburi hayo hayo. Sijui kama na Kikwete alidhihakiwa na kujiridhisha kuwa shangwe hiyo ilitokana na mapenzi ya kweli au ngoa na visasi ukiachia mbali kujiridhisha angalau. Rafiki yangu mmoja alinipigia sifa kutaka mawazo yangu. Nilijibu kwa mkato kuwa njaa au tumbo vinapopindua kichwa, lolote laweza kutokea. Kwani, waliomshangilia Kikwete ni hao hao waliomrushia kila dongo baada ya kudhihirisha kuwa alikuwa rais wa hovyo aliyepoteza muda kuzunguka dunia na kuacha taifa lijiendeshe lenyewe huku kila mtu akijifanyia atakavyo. Hii ndiyo maana haya mapenzi mapya yanatia kila shaka.
Leo tutagusia baadhi ya sababu zinazofanya Magufuli achukiwe. Na ataendelea kuchikiwa sana tu kama ifuatavyo:
Mosi, ni kutokana na hatua ya Magufuli ya kubadili mfumo na utaratibu wa kiulaji kwenye chama chake kwa kupunguza nafasi za wajumbe wa baadhi ya vikao vya chama kiasi cha kuwanyima wengi ulaji wa dezo waliouzoea bila stahiki. Hii hatua ni nzuri kwa wanachama waliokuwa wakibebeshwa mzigo; au kushuhudia ruzuku ya chama chao kuishia kuliwa na kundi dogo la wachache. Hata hivyo, kwa walionyang’anywa ulaji, watamchukia sana hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi huwa hawapendi mageuzi au mabadiliko.
Pili, sababu nyingin ni kuzuia wabunge na maafisa wa serikali kuibia umma kwa njia ya vikao, makongamano na warsha na kusafiri hovyo hovyo ughaibuni kama ilivyokuwa huku wakijilipa au kulipwa marupurupu kibao kwa uzururaji huu ambao, kimsingi, haukuwa na tija kwa taifa. Hatua hii ni nzuri kwa wananchi wa kawaida waliotwishwa mzigo kiasi cha kodi yao kuishia kuliwa na genge chache la wamangimeza huku wao wakiteseka.
Tatu, kupiga vita ufisadi na mihadarati nalo ni jambo litakalofanya Magufuli achukiwe sana hasa ikizingatiwa kuwa utawala uliopita ulikuwa ni kama umehalalisha jinai hizi. Wauza unga hawataacha njia yao ya kutajirika haraka izibwe kirahisi, huku washirika zao ambao ni maafisa wa serikali waliowezesha biashara hii kwa kupewa chao nao wakimchukia Magufuli.
Nne, kitu kingine kitakachofanya Magufuli achukiwe sana ni ile hali ya kuonyesha upendeleo na kukumbatia hata kukingia kifua baadhi ya wasaidizi wake wanaoonekana kuwa kama hawaguswi. Mfano mdogo ni kitendo chake cha kupuuzia kubatilisha uteuzi wa mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda ambaye anakabidhiwa na tuhuma za kughushi, kuvamia kitu cha Clouds na mengine mengi kama vile ubabe hata ubabaishaji. Hili halina faida yoyote kwa Magufuli. Kwani, hata wananchi wa kawaida waliokuwa wakiunga mkono juhudi za Makonda, wameanza kuhoji kunani haguswi. Unaweza kuona utitiri wa miziki iliyotungwa kumshambulia yeye. Wananchi watazidi kumtupa mkono Magufuli katika hili kutokana na tabia yake kutumia muda na nguvu nyingi kumlinda mtu mmoja ambaye akiondoka hakuna kitakachoharibika.
Kinachogomba zaidi, hata Makonda mwenyewe amegundua udhaifu wa Magufuli kiasi cha kufanya kila liwezekanalo kumsifu, kufanya anachodhani kitamfurahisha rais ili aendelee kumuona mwenye manufaa kwake. Hata hivyo, mbinu hii inaanza kupata pigo hasa baada ya rais kuruhusu wimbo wa Wapo unaoongelea walioghushi vyeti ukitaja wazi wazi jina la Bashite au Daudi Bashite linadaiwa kuwa jina hali la Makonda. Pia kumteua profesa Kitila Mkumbo aliyewahi kusema kuwa Makonda hastahili kuendelea kuwa mkuu wa mkoa hata kwa wiki moja ni dalili kuwa Magufuli ameanza kuona ubaya wa kumtetea mtu mmoja dhidi ya umma wa watanzania. Kimsingi, kama Magufuli ataendelea na msimamo wake wa kumkingia kifua mtu aliyekwishachafuka, itamgharimu kisiasa bila sababu yoyote ya dhahiri wala ya msingi.
Tano, ni ile hali ya Magufuli kujenga chuki bila sababu na vikundi vingi kama vile wapinzani na vyombo vya habari kwa kuminya uhuru wao kiasi cha kumuona kama rais mbabe.
Sita, ni ile hali ya kujichanganya au kujipinga. Kwani alipokuwa Zanzibar kwenye kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi alikaririwa akimshangaa rais wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar (BMZ) Dk Ali Mohamed Shein kuwapa nafasi wapinzani kwenye serikali yake jambo aliloapa kuwa lisingetokea chini ya utawala wake. Je amefanya nini baada ya kumteua Profesa Kitila Mkumbo kwenye serikali yake hata kama ni jambo jema kwa nchi?
Tumalizie kwa kumtaka Magufuli aendelee na mageuzi huku akiachana mengine yasiyo na maana wala faida kwa taifa kama kumkingia kifua mtu binafsi mwenye matatizo yake binafsi.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
No comments:
Post a Comment