Hivi karibuni, nchi ya Korea ya Kusini iliingia kwenye historia ya dunia kwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopambana na ufisadi mkubwa bila huruma kuonea. Rais wa zamani wa nchi hiyo Park Guen-hye alijikuta akiondolewa madarakani na kusindikizwa gerezani anakongojea kusikilizwa shauri lake la kuruhusu rafiki yake Choi Soon-sil kutumia ofisi ya rais kujitajirisha kinyume cha sheria. Choi ambaye naye yumo gerezani akingojea kusikilizwa kesi yake, alitumia ukaribu wake na rais kuyasumbua makampuni mengi ya kibiashara kuchangia asasi yake isiyo ya kiserikali ambapo kipindi kimoja, alilazimisha kampuni ya Samsung kuchangia dola za kimarekani 69. Wakati akiingizwa gerezani hapo tarehe 31 Machi, 2017 bango moja lilimpokea likisema “hongera kwa kuingia gerezani. Toka ukiwa binadamu baada ya miaka 30.”
Park angekuwa rais wa kiafrika, nani angemgusa. Asingeondoshwa madarakani kwa aibu na kuishia korokoroni. Angetafutiwa mazingira ya kumlinda hata baada ya kuthibitika kuwa alitenda ufisadi. Lakini kwa wenzetu hilo hakuna. Hakuna aliyeko juu ya sheria; wala anayeruhusiwa kutumia ofisi yake kwa manufaa binafsi kama ilivyo kwa Afrika ambako marafiki, watoto, wake au waume na ndugu wa viongozi nao hujipachika uongozi kwa sababu wazazi au ndugu zao ni marais.
Hakuna ubishi. Kwa sasa, Tanzania inakumbwa na kashfa kubwa tu zinaohusisha hasara za mabilioni zilizosababishwa na baadhi ya watawala wetu na wasaidizi wao ima tokana na uroho, ujinga na ufisadi au roho mbaya kama siyo ulimbukeni. Kashfa hizi si mpya. Kinanchofanyika ni baada ya rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli kuingia madarakani na kufanya ambacho karibia watangulizi wake wote walishindwa kufanya–kuanza kufukua kila aina ya uoza–na kuchukua hatua hata kama si kwa wahusika wote. Zoezi la Magufuli la kupambana na ufisadi nchini limevutia wengi ingawa pia linakosolewa na wengi kutokana na kuhangaika na vidagaa huku mapapa wakisazwa. Wanaomuunga mkono Magufuli wanaona kuwa amethubutu. Wanaopinga harakati zake japo si wengi, wanaona kama hafanyi mambo kisayansi na hayawezi kuwa endelevu hasa kutokana na mfumo wa kikatiba wa kutekeleza haya ukiachia mbali mapungufu kama upendeleo wa baadhi ya watu wa karibu wake kama ilivyotokea kwa mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda anayetuhumiwa kughushi vyeti vya kitaaluma.
Mbali na Makonda, juzi baadhi ya wabunge wa upinzani waliposhinikiza kuwa marais wastaafu walioshiriki uoza na uovu huu washughulikiwe. Vyombo vya habari vilimkariri mbunge Kilombero (Chadema) Peter Lijualikali akisema “Haiwezekani mzee wangu (Andrew) Chenge na (Nazir) Karamagi walipitisha mikataba hiyo bila Rais aliyekuwapo kufahamu. Kinga ya Rais kushtakiwa iondolewe ili wahojiwe.” Baada ya Lijualikali kutoa pendekezo la kuondoa kinga kwa marais, spika wa Bunge Job Ndugai alisikika akiwaonya kwa kusema “Mabadiliko mnayoyataka yakipitishwa na viongozi mlionao wakikamatwa msije mkalalamika tena” akimaanisha mawaziri wakuu wastaafu Edward Lowassa na Fredrick Sumaye waliohamia kwenye kambi ya upinzani. Hapa unaweza kuona namna kulindana kulivyo tatizo la kimfumo zaidi. Badala ya spika kutumia mamlaka yake kuunga mkono haki ya kutenda haki, anaonekana kutoa vitisho kama ishara ya kuonyesha kuwa wapo wasioguswa. Hata hivyo, spika alisahau kitu kimoja kuwa hao mawaziri anaotishia nao watasombwa hawana kinga kama marais wastaafu ambao kimsingi ndicho chanzo cha ufisadi, uovu na uoza huu uliofanya taifa lenye kujaliwa raslimali lukuki kuwa maskini na ombaomba bila sababu zaidi ya ubinafsi, uchoyo, uroho na roho mbaya za baadhi ya watawala wetu waliogeuza ikulu kuwa chimbo la utajiri badala ya kuwa hekalu la haki la wananchi. Ingekuwa Korea ya Kusini, kauli ya spika ingemgharimu. Kwani, ameonyesha wazi kuunga mkono ufisadi.
Naye mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu wala hakuficha wala kuzungusha. Alitaka rais Jakaya Kikwete ashitakiwe kwa vile ndiye aliingia mkataba wa mgodi wa Bulyankhulu tarehe 5 Agosti, 1994. Na wakati ule hakuwa na kinga yoyote kisheria. Je rais atawashughulikia watagulizi wake na nani yuko tayari kumvisha paka kengele zaidi ya yeye aliyeanzisha na anayesimamia mchakato huu? Maana, ukiangalia ushahidi uliopo, mambo mengine hayahitaji hata uwe mtaalamu wa sheria wala msomi kujua kuwa kinachoenda kufanyika ni kinyume na common sense. Sijui tunatoa taswira gani kwa wananchi wetu na vizazi vijavyo kwa kupendeleana na kulindana hata katika maovu?
Kwa taifa linalotaka kujikomboa tokana na ufisadi lazima tujenge utamaduni wa kuhoji kila mtu bila kujali cheo chake. Wengi walidhani kama wahusika wanasingiziwa, wangejitetea na kuwataka wanaowatuhumu watoe ushahidi; wakishindwa wawajibishwe. Haiwezekani rais awe mlalamikaji, mwendesha mashitaka, shahidi, haki na polisi. Kufanya hivyo, licha ya kuwa kinyume cha sheria, kunakinzana na ahadi za rais za kuwatendea watanzania haki bila kujali ukubwa wa cheo cha mtu.
Tumalizie kwa kusema kuwa Tanzania inakabiliwa na matatizo yasiyo ya kawaida yanayohitaji majibu yasiyo ya kawaida yatokanayo na busara, ukweli, uwazi na ithibati vya aina yake. Siku zote huwa tunasikia watu wakiambiana wafanye maamuzi magumu. Korea Kusini walichukua maamuzi magumu. Nasi kama taifa, kama kweli hatuwadanganyi watu wetu na kuwageuza hamnazo, tunapaswa kufanya maamuzi magumu kwenye kupambana na ufisadi bila upendeleo wala kutishana. Natamani Tanzania ingekuwa Korea Kusini.
Chanzo; Tanzania Daima Jumatano leo.
No comments:
Post a Comment