Kwanza, nikiri. Juhudi zako za kuleta maendeleo ni za kupigiwa mfano. Tangu uchukue ukanda, hakuna kilichoharibika. Sana sana kilichokosekana ni kubadili mfumo wetu wa hovyo uitwao uwekezaji wakati kiuhalisia ni uchukuaji unaowawezesha wageni kutuibia kwa kisingizio cha uwekezaji. Je hapa alaumiwe nani iwapo tumejiwekea mifumo ya kujiiibia na kuibiwa?
Mheshimiwa Rais, niruhusu nitoe mfano toka hapa Kanada na baadhi ya nchi za Kiafrika nilizodurusu mifumo yao ya uwekezaji. Ukitaka kuwekeza hapa Kanada, unapaswa uwe na si chini ya Dola za kimarekani 200,000 au Dola 75,000 kama umewekeza kwenye kampuni ya Kikanada chini ya kinachoitwa designated Canadian angel investor group. Ukiwa na kiasi hiki, unapewa visa haraka haraka kuingia na kuanza kuishi na familia yako huku ukipewa ukazi wa kudumu au uraia––––kama utautaka––––baada ya kuishi hapa kwa miaka mitatu bila kutoka. Hapa wanao watasoma na kutibiwa bure sawa na wakanada. Hii ni kwa mujibu wa tovuti ya serikali ya cic.gc.ca.
Mheshimiwa Rais, ukitaka kuwekeza na kuingia Botswana, unatakiwa kuwa na ima Pula za Botswana milioni moja au Euro 82,000 au Dola za kimarekani 93,000. Kwa Tanzania, kama si mtanzania, unapaswa kuwa na Dola 500, 000 na mtanzania Dola 100,000! Kwa Namibia ni Dola za kimarekani 135,000 au NMD 2,000,000. Kwa nchi zote tatu, raia wao hawahitajiki kuwa na kiasi chochote. Je sisi tunafanya hivyo kumkomoa nani? Jibu ni kwamba ni kwa sababu tunawanyima watanzania wenye uraia pacha fursa ya kuwekeza kwao na kuendeleza nchi zao baada ya kusotea fedha ughaibuni. Matokeo yake, wanatafuta nchi nyingi kwenda kuwekeza wakati wanao uwezo wa kuwekeza kwao. Kwanini tusiwamotishe watu wetu wenye uraia wa nchi nyingine lau kwa kuwawekea sharti katika kupewa uraia pacha kulingana na uwezo wao wa kuwekeza nchini badala ya kupoteza muda tukibembeleza wageni wakati watu wetu wanazo fedha nje lakini wanahofia kurejea nyumbani na kuibiwa kwa vile hawaruhusiwi kufanya baadhi ya mambo?
Mheshimiwa Rais, niliwahi kuandika makala juu ya namna Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda anavyoweza kusaidia watu wetu wengi wasio na ajira au wastaafu kuishia maisha bora huku wakianzisha miradi inayoweza kuwasaidia wao na familia zao huku wakitoa ajira kwa wengine na kuwa vyanzo vizuri vya kodi na maisha bora. Baada ya makala hiyo kusomwa, nilipata maombi mengi toka ughaibuni yakitaka niwaunganishe na gwiji huyu wa kilimo na uwekezaji bila mafanikio tokana na kutokuwa na mawasiliano yake. Nilijaribu kutafuta baruapepe au simu yake toka kwa rafiki yangu Spika Mstaafu, Mzee Pius Msekwa, bahati mbaya hakuwa nayo. Nilikwamia hapo na kushindwa kuwasaidia wenzangu waliovutiwa na uwekezaji wa Mzee Pinda.
Mheshimiwa Rais, naomba ujiulize. Je mfumo wetu wa uwekezaji unatusaidiaje kama nchi wakati wezi wengi tena wa kigeni wanautumia kwa kusaidiana na wezi wasio na uraia pacha wala uzalendo kuingia na kupiga fedha na kuondoka? Rejea kilichotokea wakati kampuni ya kihindi Rites Consortium lilipojifanya kuwekeza kwenye Reli na kuishia kutupiga mabilioni na kuondoka. Je mfumo wetu wa uwekezaji unatusaidia kama taifa au kutuumiza? Kwa nchi za magharibi, ukiwekeza, watakutoza kodi, utaajiri watu wao na kuwalipa kiwango cha juu cha mshahara, kulipia bima na mambo mengine. Mfumo wao, kimsingi, ni wa kuwahudumia na si wa kuhudumia matapeli kama ilivyo yetu iliyochakaa na kujaa ujanjaujanja. Mifumo ya hapa haina huruma na mgeni. inamhudumia mwananchi kwa mgongo wa mgeni. Nitoe mfano wangu binafsi. Mie na mke wangu tuna nyumba hapa. Tumeinunua kwa kulipa aslimia 30 na zinazobaki tunalipa taratibu kwa kutozwa riba kubwa tu. Tunafanya kazi na kutozwa si chini ya aslimia 30 ya mishahara pia tunalipa kodi ya manunuzi.
Mheshimiwa Rais, hapa wanahimiza watu waongeze ujuzi. Ukianza, unapewa tuzo kwa sharti kuwa lazima uchukue mikopo ya masomo ambayo hutozwa riba pindi tu ukimaliza masomo. Mfano, katika shahada yangu ya uzamivu, nadaiwa karibu milioni 100 za kitanzania. Japo huu ni uwekezaji kwangu na familia, umeiingizia fedha nyingi Kanada kwa sababu tu imenipa fursa ya kuongeza maarifa.
Mheshimiwa Rais, sasa turejee kwa wanadiaspora waliowekeza ima kwenye ajira, biashara au elimu. Je tunawasaidiaje na kujisaidiaje kama nchi inayohitaji uwekezaji uwe mkubwa au mdogo? Tumeshindwa kuwa na mfumo hata wa kuhamisha fedha za watu wetu bila kukatwa na kuibiwa. Hivi, mfano, kama mtanzania anataka kurejesha nyumbani Dola za kimarekani kiasi chochote. Kwanini tusiwe na utaratibu wa kupeleka fedha hizo kwenye ubalozi wetu akapewa risiti ya malipo zikatumika kulipa wafanyakazi huko, akaenda kuzipokea nyumbani ambako atakuwa ameokoa aslimia kumi ya fedha husika? Mfano, nikiweka Dola 200,000 ubalozini zikalipa mishahara nikaja kulipwa na serikali sitakuwa nimeokoa Dola 20,000 kiasi ambacho, kwa mikoani kinaweza kujenga banda au kuanzisha kijibiashara ya ufugaji hata wa kuku, mbuzi au samaki.
Mheshimiwa Rais, hii ndiyo njia inayotumiwa na wageni wengi nchini kuhamisha fedha zao bila kupoteza hata senti. Hebu wachunguze wawekezaji au hata wafanyakazi wa kigeni walioko nchi kwa vibali vya kufanya kazi. Utakuta kila wakisafiri kwenda kwao hawahamishi fedha. Lakini ukiuliza fedha yao iko wapi huioni. Inapitia kwenye balozi zao ambapo huenda kulipiwa kwao.
Mhe. Rais nisikuchoshe, nashauri uanze kudurusu namna ya kuwavutia watanzania waioko nje. Kuna fedha inaweza kuingia na kunufaisha taifa. Chukulia mfano mtu ambaye anapata mshahara wa Dola 100, 000 kwa mwaka. Huku anakatwa kodi si chini ya 36,000. Je anaweka akiba kiasi gani? Je kama anaruhusiwa kuhamisha fedha yake baada ya kuamua kurejea nyumbani atakuwa na fedha kiasi gani na zinaweza kusaidia taifa kiasi gani? Naomba tutafakari pamoja.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment