The Chant of Savant

Tuesday 17 January 2023

Kutaifisha Mifugo ni Ukoloni Serikali Itafute Suluhu

Taarifa kuwa ng’ombe 3,083 zilitaifishwa na serikali hivi karibuni baada ya kukutwa kwenye mbuga ya Wanyama ya Tarangire, siyo habari nzuri si kwa wafugaji, wahanga, wananchi, serikali wala taifa kwa ujumla. Kweli bado tunanyang’anya mifugo kwa kuingia eti kwenye mbuga au hifadhi kwenye karne ya 21! Tunamkomoa nani zaidi ya uchumi wetu hasa ikizingatiwa kuwa hawa Wanyama wanaopigwa mnada huuzwa kwa bei ya kutupwa na mara nyingi kununuliwa na makundi ya wafanyabiashara wanaoshirikiana na waendesha minada? Je hii ni haki kwa wafugaji wetu walioko karibu na mbuga na hifadhi ambazo zimetokea kuwa tishio kwao na mifugo yao?
            Je nini kifanyike? Ingawa wahusika walikaririwa wakisema kuwa kupiga watuhumiwa faini hakuzuii wao kuendelea kuingiza mifugo yao kwenye maeneo husika, kwanini wasiongeze viwango vya faini au kutafuta njia mbadala na mujarabu itakayohakikisha suluhu inapatikana badala kufilisiana na kuumizana?  
        Naishauri serikali kuwatafutia wafugaji wake maeneo ya malisho hasa ikizingatiwa kuwa kinachoitwa mbuga au hifadhi ni ardhi ambayo, kabla ya kuundwa Tanzania ilikuwa ikitumiwa na wafugaji bila kikwazo chochote. Kimsingi, ni ardhi yao waliyonyang’anywa. 
        Ajabu, aliyewanyang’anya ardhi ya malisho yao sasa anaanza kuwanyang’anya hata mifugo yao na kuongeza uhasama na umaskini.
        Hawa wahanga wana akili na maarifa ya namna ya kutunza hata kuharibu wanyama.                 Kwanini hatuwaangalii hivi? Mtu aliyekwishapoteza vyanzo vyake vya mapato na maisha ana hasara gani akihujumu hawa wanyama wasio tena na akili ya kuweza kutoa ushahidi dhidi yao? Kuendeleza mbinu hatarishi za kunyang’anyana mifugo kunaweza kujenga mazingira hatarishi ambapo watakaolipia ni wanyama hawa hawa mnaotaka kuwalinda. Lindeni wanyama na wafugaji kwa pamoja kwa kuweka utaratibu mzuri wa kugawana raslimali hii.
        Mbali na kuwadhulumu, unapotaifisha mifugo ya mtu na kuipiga mnada, unamtia umaskini yeye, familia yake, jamii yake hata eneo atokako. Kwani, unamnyima uwezo wa kujikimu na kuchangia kwenye uchumi wa taifa. Pia, ifahamike, kwa wafugaji, Wanyama si utajiri tu kwao bali ni alama yao ya heshima katika baadhi ya jamii. Hivyo, mfugaji anapofilisiwa Wanyama wake anaathirika kiuchumi na kijamii. Kutaifisha Wanyama wa mfugaji hakuna tofauti na kumuua yeye na jamii yake. Maana, ndiyo kazi anayojua. Ni sawa na kumtoa Samaki majini ukategemea aendelee kuishi.
        Kama serikali imeweza kuwatafutia Wanyama makazi, inashindwaje kuwatafutia wananchi wake maeneo ya kufugia na kulisha mifugo yao? Wanyama hawawezi kuwa bora zaidi ya watu na mifugo yao. Inakuwaje wenye ng’ombe wakamatwe na kuwekwa ndani? Je hilo ndilo jibu au kufanya watu waichukie serikali yao tokana na maamuzi na sheria za kikoloni na za kizamani?                 Kumbukeni, Ni hawa hawa waliowapigia au ambao watawapigia kura. Mbona Wanyama wanapoingia kwenye makazi ya watu kudhuriwa na waathirika wala serikali kutiwa ndani? Mbona madereva wanapovunja sheria za barabarani hupigwa faini bila kutaifisha magari yao au kwa vile wenye magari wengi ni matajiri na wakubwa kama wakoloni walivyotunga sheria hizi makusudi kujilinda?
        Ushahidi unaonyesha kuwa Wanyama wamekuwa wakiingia kwenye maeneo ya wananchi. Lenani Seyani, mmoja wa wafugaji anasema “sisi na hifadhi sio maadui, kipindi hiki wanyamapori wameanza kuja kwa wingi maeneo yetu ya makazi huku Terati na kwingineko na tumekuwa hatuwadhuru licha ya kuja na magonjwa” (Mwananchi, Desemba 27, 2022).
         Hawa ni watanzania walioamua kufanya kazi ya ufugaji. Kutaifisha ng’ombe zao, licha ya kuionyesha serikali kama mnyanyasaji, haiisaidii, serikali, wananchi wala Tanzania. Nini maana ya kupigania na kupata uhuru sasa? Nadhani serikali yetu ilirithi ima sheria au mawazo ya kikoloni.                 Kimsingi, kuwapatia wafugaji malisho ni jukumu la serikali hasa ikizingatiwa kuwa serikali iliwakuta hao wafugaji wakiishi vizuri tu na Wanyama kwa maelfu kama siyo mamilioni ya miaka. Hapa kinachopaswa kufanywa, ni kuelimishana na kutafatuta suluhu pamoja badala ya serikali kujifanya ina haki kuliko wafugaji wakati serikali na nchi ni mali ya watanzania popote walipo.
        Kama ambavyo serikali iliondoa ujinga wa kuzuia watu wa mipakani kuuza mazao nje ya nchi, iondoe haya makatazo ya kuingiza Wanyama kwenye mbuga. Kwa mfano Wamasai, huwa hawali nyamamwitu. Hivyo, wapewe mafunzo na vibali juu ya namna ya kuchangia mbuga na hifadhi bila kuleta madhara kama ilivyokuwa kwa miaka milioni nyingi iliyopita kabla ya kuja hizi serikali na mataifa yaliyotengenezwa na mkoloni mwaka 1884.                 Nashauri watenge maeneo ya hifadhi na mbuga lau nusu ambapo wananchi wataruhusiwa kuingiza mifugo yao na kulisha huku wakipewa jukumu la kuhakikisha Wanyama hawadhuriwi. Huu ni mfumo unaotumika kuondoa migogoro baina ya binadamu na Wanyama uliokwishafanyika sehemu nyingi duniani. 
        Mfano, jamii zinazosifika kwa kuwinda na kuua Wanyama zinapowezeshwa kiuchumi na kielimu juu ya faida za Wanyama na kuona matunda yake, hugeuka kuwa walinzi wazuri wa Wanyama kwa vile wana faida kwao na nchi zao. Na wafugaji kadhalika. Wakielimshwa na kupewa jukumu la kusimamia Wanyama, watawalinda kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya kuingia ukoloni.
Chanzo: Raia Mwema Kesho.

No comments: