How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 24 January 2023

Waswahili Pangeni uzazi Ila Zaaneni


 Novemba 15, 2022 ni maalumu duniani (un.org, Nov. 15, 2022), siku ambapo binadamu walifikia idadi ya bilioni nane. Wapo walioshangangilia kuwa angalau tunaongezeka tokana na kuishi maisha marefu na hivyo, kuyashinda magonjwa. Wengi walisikitika wakisema tumekuwa wengi mno kiasi cha kutishia uhai wa dunia yaani wachoyo sisi na viumbe wengine wasio na mchango wowote katika kuharibu dunia yetu. Binafsi nina yafuatayo:

Kwanza, ni kuwaambia Waswahili wasidanganywe na ongezeko hili ambalo limechangiwa kikubwa na mataifa mawili yaani China na India. Hivyo, msishangae kuwaona hawa jamaa kila mahali hata kule Matarawe, Mfaranyaki, Matemamanga, Namasakata, Nakapanya, na Mbamba Bay wakiuza chupi na ukwaju na upuuzi mwingine kana kwamba sisi hatuwezi kufanya hivyo. Wamezaana na kuongezeka na kuamua kutafuta riziki kwa wale wanaoona kuwa kuzaa ni matatizo. Nadhani tatizo si kuzaa bali kuandaa mazingira mazuri ya kutumia akili na raslimali zilizopo vizuri badala ya kuruhusu wengine kuja kuzifaidi na kufaidisha kwao wakati sisi tukiendelea kuumia.

Pili, niwaonye. Waswahili mko wachache sana duniani japo mna ardhi kubwa kuliko wote. Hivyo, mnahitaji kuzaana na kuzalishana sana tu vinginevyo mtakuwa kila ambacho wamombo huita extinct creatures. Hapa Kanada, tokana na kupungua kwa idadi ya watu, serikali inatumia fedha nyingi kuingiza wageni ili wazae na kuendeleza nchi. Pia, wanapofika wanalazimika kufuata mila za hapa hata kama hawazitaki. Pia, wanaonekana si bora kama wenyeji wao tofauti na kwetu ambapo wageni huonekana wa maana kuliko sisi hata kutulazimisha kufuata mila zao bila kuwalazimisha Hapa wana fedha. Sisi tukifikia hapa tutatumia nini kuvutia wengine? Na tunavyobaguliwa, hata tukiwakaribisha, watatutawala kama inavyooanza kuonekana. Rejea mfano wa wenzetu toka India ambao wamekaa miaka kwetu lakini wamegoma kuchanganyikana nasi.

Tatu, japo Mwenyewe aliyewaumba ambaye hakuna amjuaye bali kumsingizia aliwapendelea ingawa mnabaguliwa na kuchukiwa karibu na kila rangi duniani kwenye mfumo huu wa kibaguzi na kitwahuti. Kwani aliwapa ardhi kubwa na raslimali nyingi ambavyo wengi wanaitamani hata kutamani mtoweke wachukue wao. Nyinyi ni sawa na wengine hata kama hamjiamini, kujithamini, na kuthaminiana.

Nne, mna upendo wa mshumaa wa kukaribisha wageni kwenu wakati mnakataliwa kwao. Rejea Waswahili wanavyobaguliwa hata kuuawa huko Asia na Mashariki ya Kati kwa sababu ya asili au rangi ya ngozi yao. Mfano, hawa wachina waliojaa Tanzania, waliwabagua Waafrika wakati wa Ukovi wakati gonjwa lilianzia kwao. Huko India, na Mashariki ya Kati hali inajulikana. Rejea hata mnavyobaguliwa nchini na barani mwenu. Imefikia mahali hata Waswahili wanajiita waarabu huko Sudan.

Tano, hebu tufanye hesabu kidogo japo wengi hawazipendi. Kwa sasa, bara la Asia lina watu wapatao 4,734,852,393 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni za Wordometer. Bara hili lina ukubwa wa kilometa za mraba 44,579,000.  Linganisha na Afrika yenye ukubwa wa kilometa za mraba 30,370,000 na idadi ya watu wapatao 1,416,625,724. Waswahili hawafikii hata nusu yao. China peke yake ina watu wapatao 1,452,462,600 ambao ni wengi kuliko Waswahili. Kwanini wasivamie Afrika kutafuta riziki na kufanikiwa tokana na ujinga wa Waswahili? Hivyo, wanaoshangaa utitiri wa wachina Afrika wajue ukweli huu. Watashindwaje kutuvamia wakati China yenyewe ina ukubwa wa kilometa za mraba 9,596,961. Hii maana yake ni nini? Waafrika wakizaa kama wachina, wanapaswa kuwa si chini ya watu bilioni nne na nusu angalau.

Sita, mfano mwingine wa karibu na nyumbani ni Nigeria ambayo ni ndogo kwa eneo kwa takriban kilometa za mraba 23,534 kuliko Tanzania lakini ina watu wapatao 206,139,589. Kenya ambayo haifikii hata nusu ya Tanzania ina watu wapatao 53,771,296. Uganda ina 45,741,007. Kenya na Uganda zikiwekwa pamoja–––jumlisha Burundi na Rwanda–––bado Tanzania inazizidi kwa eneo la ardhi hata raslimali. Linganisha na Tanzania ambayo ni kubwa kuliko hawa majirani zake yenye idadi ya watu wapatao 59,734,218. Je kama hao hapo juu wasio na ardhi wala raslimali wanazidi kuongezana, nyie mnaacha ili waje wachukue nchi yenu? Inakuwaje Nigeria yenye watu wengi kuliko nchi tatu hapo juu inaendelea kuzaa nanyi mbane ili iweje? Tanzania ikilinganishwa na Nigeria, inapaswa kuwa na watu wasiopungua 210,000,000. Ikilinganishwa na Kenya na Uganda, inapaswa kuwa na watu wasiopungua 150,000,000.

Saba, sasa nini kifanyike? Zaaneni na kupanga mipango ya kuwaendeleza watu wenu badala ya kuruhusu wageni waje kuwaibia, kuwabagua na hata kuwahujumu. Nchi ya India inaingiza fedha nyingi toka nje toka kwa raia wake walioko nje. Pia, inaingiza fedha nyingi tokana raia wengine wa kihindi waliopelekwa nje na ima wakoloni au dhiki ambao hutumia kila mbinu kutengeneza fedha na kutuma kwa ndugu zao hata wengine kuhamia kule ingawa wengi hurejea walikotoka baada ya kugundua ugumu wa maisha ulioko kule.

Mwisho, Watanzania na Waafrika hawana sababu yoyote ya msingi ya kujinyima kuzaa. Wakifanya hivyo, watakwisha kwa vile dunia nzima inawachukia, kuwabagua na kutamani raslimali zao. Cha mno, unganisheni nchi zenu muwe na taifa lenye nguvu badala ya kuogopana na kutegana kama ilivyo. Kwa ukubwa wa bara la Afrika, kama lingekuwa limeungana, hakuna nchi hata moja inayopaswa kuaminishwa kuwa kuzaa au kuongezeka kwa idadi ya watu ni tatizo.

Chanzo: Raia Mwema kesho.


No comments: