Kwanza nitoe pole kwa Waislamu waliofunga mwezi mtukufu wa Ramadhani katika kipindi kigumu, ambako bei za vitu hasa futari ni kaa la moto na chanzo cha mahangaiko makubwa. Najua Ramadhani ni nguzo muhimu. Muumini hupaswa kujitenga na dunia akimsabihi Mola na kutafakari maisha yake ya kimwili na kiroho.
Japo wanaoshiba walitushauri tuwe tunapeana hongera kwa kazi, nawapeni pole. Ni kwa sababu kazi nyingi mnazofanya hamzifaidi kama kikundi cha watu wachache kinavyofaidi jasho na damu yenu. Nitawapa hongera kwa vipi iwapo mmekuwa mashahidi wa ufisadi unaonuka na kutisha? Sina mshipa wala kiburi cha kuwatukana tusi hili.
Leo nimelazimika kubadili mfumo wa kuwasiliana nanyi. Badala ya kuandika makala jumla, nimeamua kuandika barua lenga. Ni katika kujaribu kukumbushana wajibu wetu kwetu, taifa letu na vizazi vyetu.
Hakuna ubishi kuwa sasa hivi nchi yetu inajiendea. Huu si uzushi wala uchochezi. Ni baada ya serikali tunayoiita yetu ambayo kinadharia ni yetu na kivitendo siyo, kujitenga nasi kiasi cha kulinda maslahi ya kikundi cha watu, chama hata familia kwa kuhujumu maslahi yetu. Sitatafuna maneno. Kwa mapenzi makubwa kwa nchi yangu na watu wake naandika. Heri kuonya kuliko kushabikia uoza baadaye tukaishia kujuta.
Licha ya kuandika huwa nasoma makala nyingi ninazobahatika kuzipata. Siwezi kuwataja wachambuzi wote, huwa napata changamoto na mori wa kukumbushia haya.
Nchi yetu imo kwenye wakati mgumu.
Kwanza ukiondoa kutamalaki kwa ufisadi na matumizi ya hovyo, tuna ombwe la kukosekana kwa sera na falsafa inayotutawala. Usiniulize ni sera gani tunakwenda nayo. Nikisoma katiba naona kuwa tunajenga nchi ya kijamaa.
Nikitoka nje naona tunajenga nchi ya kichuuzi na kifisadi ambapo wachache tuliowaamini madaraka wanaonekana kushindwa kuongoza wakiwa ‘bize’ kwenye kujineemesha. Huu si uchochezi. Niorodheshee ahadi tulizopewa wakati wa uchaguzi zilizotekelezwa nitarudi chuoni kusoma.
Pili tuna ombwe la taasisi wakilishi za umma. Katiba inaseme Bunge litawakilisha wananchi walio wengi likiihoji serikali na kuikagua. Nikirejea ambayo nimekuwa nikishuhudia ambayo kadhalika nanyi mmeyashuhudia, sioni kitu kama hicho. Bunge letu limetekwa na CCM kiasi cha kugeuka kama NGO ya CCM. Halina tofauti na WAMA au EOTFL ya Salma Kikwete na Anna Mkapa.
Tatu tuna serikali kubwa kuliko uwezo wetu kiuchumi. Wachambuzi wengi wameonya kuwa serikali hii nyemelezi ni mzigo kwa wananchi. Bahati mbaya wahusika wamezidi kushindilia nta kwenye masikio huku macho yao yakipofuka yanapopambana na ukweli huu. Badala ya kuwa na serikali inayofanana nasi, tumekuwa na serikali inayofanana nao hao wanaoshiba kwa jasho letu.
Simchukii Rais Jakaya Kikwete. Nampenda. Ndiyo maana nimejitoa mhanga kumfikishia ujumbe huu. Umma unalalamikia mawaziri wake. Kujua hili anaweza kusoma makala mbalimbali ambazo zinaionyesha hata kuisema vibaya serikali kutokana nayo kuwa mbaya. Wiki zilizopita nilisoma timu ya JK ya Ansbert Ngurumo. Nimesoma karipio la Happiness Katabazi dhidi ya Marmo na Kingunge kutaja wachache.
Nimechukua wachache kati ya wengi ambao wamejitolea kusema ukweli hata kama unauma. Nilisoma makala ya Kibanda ya ‘Kikwete niliyemfahamu’.
Nimeshuhudia makala za waandishi mamluki wanaolipwa kwa kuupamba uoza. Nimesoma hasira za wachambuzi dhidi ya kashfa kama BoT, Richmond, Tangold, ANBEN, Fosnik, Daveconsult, TanPower na Buzwagi ya Karamagi.
Nimesoma mawazo na ushauri hata wa wafadhili kwa serikali wakiitaka ieleze ukweli. Hawa ni wanadiplomasia ambao mara nyingi huzunguka na kutumia falsafa. Ukiona wanasema jieleze, jua wanamaanisha jitoe umechemsha.
Sijasoma mawazo ya wananchi ambao mara nyingi hawana muda wa kuandika zaidi ya kujitokeza kwa umoja wao mitaani kueleza kesi yao. Japo vyombo vya habari vina nguvu ya ajabu, dhima ya kuiokoa nchi yetu isiachiwe vyombo hivi peke yake.
Wakati umefika kwa wananchi kuamua hatima ya nchi yao. Umefika wakati kwa wananchi kuifundisha serikali la kufanya. Wamekuwa wakiishauri la kufanya isifanye. Namna hii inataka nini kama si kwa wananchi kutumia mahakama yao kuu ambayo ni maandamano na migomo ya amani?
Rais ameshauriwa avunje Baraza la Mawaziri aunde lenye watu wenye udhu. Amekataa. Ameshauriwa awawajibishe wote wanaokabiliwa na tuhuma za ubadhirifu, amekataa. Ametakiwa atimize ahadi zake kama kupambana na ufisadi, dawa za kulevya, kurekebisha mikataba ya madini, kurejesha nyumba za umma, kuwajibika yeye binafsi na familia yake, kutaja mali za watawala na mengine mengi. Amekataa! Hii maana yake ni nini? Je, hii ni kuwadharau na kutowajali wananchi? Atajibu mwenyewe.
Umefika wakati wa umma kupata majibu sahihi ama kuyatafuta kwa njia ya pili (Plan B).
Kwanini wananchi ambao kisheria na kikatiba ni wenye nchi wababaishwe na mtu waliyemwajiri? Ni kichaa gani anayeajiri mtu ili amtawale na kuharibu mali zake badala ya kumuongezea tija?
Kuna ulazima wa pande zote kubadilika. Tusitegemee kuhoji na kulalamika peke yake vitaleta majibu. Hii nchi ni yetu. Je, tunadharauliwa hata kupuuziwa kwa sababu tunasema badala ya kutenda? Wahenga walisema, maneno matupu hayavunji mfupa na maji ya moto hayachomi nyumba. Pia matendo hukidhi haja maridhawa.
Wahenga hawakuishia hewani. Wametoa jibu. Wanasema kuwa simbiko halisimbuliki ila kwa mikukuliko na haki haiji kwenye sahani ya dhahabu.
Sasa tumeishajiridhisha kuwa nchi yetu haiko kama ambavyo tungetaka na watawala wameamua kwa sababu binafsi kutupuuzia. Nini kifuate? Tuingie mitaani? ‘Vox populi vox dei’ wakubwa watasikia na kutoka usingizini na ulevi wa madaraka.
Safu hii ni fupi. Je, tufanye nini? Tuanze kuandamana na kugoma tukitaka matatizo yote yanayotukabili yashughulikiwe na walioomba kuyashughulikia. Kama hawawezi wawapishe wenye kuweza.
Serikali ifanye yafuatayo:
Mosi, ipambane na ufisadi kwa kuwawajibisha watuhumiwa tulio nao sasa.
Pili, Baraza la Mawaziri lipunguzwe.
Mali zote za umma zilizomo mikononi mwa wezi zirejeshwe, wao wakifikishwa mahakamani.
Serikali itangaze sera na mipango yake.
Bunge lirejeshewe hadhi yake.
Miiko ya uongozi irejeshwe na katiba iandikwe upya kuendana na matakwa ya umma badala ya CCM.
Mawazo ya wananchi yaheshimiwe na kutumiwa. Ahadi za serikali zitimizwe kinyume chake, serikali iwajibike. Hakuna haja ya kuendelea kuteseka tukingojea 2010.
Wasalaam.
No comments:
Post a Comment