Mwezi jana, safu hii iliwapayukia CCM na mbinu zao za porini kutaka kukigawanya na hatimaye kukizamisha Chama Cha Wananchi (CUF). Tuliongelea jinsi CCM imekuwa ikipiga dana dana mazungumzo ya kutafuta muafaka ili hatimaye wanachama wa CUF wauasi uongozi wao kutokana na kushindwa kuleta suluhu.
Leo tutaangalia upande wa pili wa shilingi. Waingereza husema, "It takes two to tango." Kwa wafuatiliaji wa mtafaruko wa Zanzibar, watakubaliana nasi kuwa kimsingi kinachoitwa mtafaruko ni kinaweza kutafsiriwa kama ubovu wa muungano, kutawaliwa na katiba mbovu na ya zamani ya chama kimoja, wizi wa kura na uongozi mbovu pande zote yaani CCM na CUF.Mtafaruko ulioigharimu nchi yetu ulianza mwaka 1995 baada ya rais wa Zanzibar wa wakati ule, Salmin Amour kuiba kura.
Ushahidi upo. Uchaguzi tajwa licha ya kushutumiwa na taasisi za kimataifa kuwa ulikuwa wizi mtupu, Tanzania bara ilipeleka majeshi visiwani. Jeshi lilipiga na kunyanyasa wapiga kura na wananchi wa kawaida ukiachia mbali kuua.Bahati mbaya wakati ule nchi ilikuwa ikitawaliwa na watu wawili vichwa maji, Salmin na Benjamin Mkapa.Historia ni ndefu.
Baada ya CUF kuibiwa kura mwaka 1995 wengi tulidhani wangetia akilini na kubadili mbinu ya kupambana na dhuluma. Lakini wapi!Mpaka tunavyoandika ni miaka takribani 13 tangu zahama hili liikumbe nchi na CUF wakiwa na uongozi ule ule wanacheza ngoma ile ile ya jogoo!Katika kukuna vichwa na kutafuta dira ya kuelekea kupatikana suluhu, safu hii imegundua kuwa bila kupangua safu ya juu ya uongozi wa CUF, hakuna la maana litakalofikiwa.Tutatoa sababu.
Kwanza siyo chuki wala chuku, uongozi wa sasa wa CUF wa Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif sharrif Hamad umechoka na kuparaganyikiwa. Umeshindwa ku-deliver.Umechusha na kuishiwa kiasi cha kuwekeza kwenye maapizo na maneno zaidi ya matendo. Uulize. Yako wapi matokeo ya mazungumzo ya muafaka? Utasukumia kila lawama kwa CCM.
Lakini tukiangalia mitafaruko tena mikubwa zaidi ya huu kwenye nchi nyingine kama Kenya na Zimbabwe tunapata somo moja kuwa uongozi wa sasa si makini na hauna hoja za msingi licha ya kukosa mikakati na mbinu muafaka.Kwanini Laila Odinga wa Kenya ameweza kwa muda mfupi huku Morgan Tsvangirai wa Zimbabwe akikaribia kufanikiwa?Jibu ni rahisi kuwa wawili hawa wana hoja na wanajua aina ya adui wanayepambana naye tofauti na CUF.Hivi karibuni tuliaminishwa na uongozi wa CUF kuwa sasa suluhu ya mtafarako itafikiwa muda si mrefu.
Tukiwa tunangojea hili, mara CCM wanakuja na usanii wa dana dana kiasi cha kushindwa kufikia suluhu.Mtafaruko ulianza wakati CCM ikiwa chini ya Mkapa na Philip Mangula. Leo CCM imebadili safu yake; kuna Jakaya Kikwete na Yusuf Makamba. CUF kwa upande mwingine, bado ina watu wale wale walioshindwa ku-deliver! Je ni kwanini? Sababu ni uongozi wa juu wa CUF kugeuza chama mali ya watu binafsi wawili yaani Seif na Lipumba.
Kwa mtu anayejua udhaifu wa Kikwete, Makamba na Amani Karume, kama CUF wangekuwa wamejipanga vizuri, wasingekuwa wanaanza arifu na ujiki kila uchao. Maskini wameshindwa kuutumia udhaifu huu!Upungufu mwingine ni pupa na papara kwa upande wa CUF. Wamekuwa wakiukwaa mkenge kutokana na Seif kuangalia kiti cha rais wa Zanzibar kiasi cha kudhoofisha chama bara bila kuangalia vikwazo vya kukifikia. Mbinu ambazo amekuwa akitumia ni zile zile. Hakuzibadili kulingana na wakati na mazingira.
Mchungaji Christopher Mtikila aliwahi kuwataka CUF na upinzani kwa ujumla kugomea chaguzi kutokana na kuandaliwa na CCM katika mazingira yale yale ya kizandiki. Hawakumsikiliza zaidi ya kuingia kwenye uchaguzi bila kuondoa vikwazo vilivyowaangusha siku zote!Kimsingi hoja ya Mtikila ilijikita kwenye ubovu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umekuwa nidyo chaka la kufanyia dhuluma zilizoshuhudiwa visiwani. Hakuna chaka kubwa kama katiba viraka tuliyo nayo. Huwezi ukawa na katiba iliyoandikwa na watu wachache kinyume cha sheria na taratibu ukafanikisha demokrasia.Katika ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilitungwa na tume iliyoteuliwa na rais wa mfumo wa chama kimoja ili kufanikisha kuunganisha vyama vya Afro Shiraz na TANU. Haikuwa na ajenda hata moja ya mfumo wa vyama vingi.
Kutokana na udhaifu huu, CCM wakijua wazi, wamekuwa wakiitumia katiba hii kuvuruga uchaguzi wa Zanzibar na hali yote ya kisiasa.Kimsingi CUF bila kuwa na uongozi mpya na wenye madai mapana, hakuna litakalofanyika. Hapa ndipo wasi wasi na ushauri wa Mtikila vinapokuwa dira kwenda kwenye suluhu.Je Lipumba na Seif watakubali kumeza kidonge hiki kichungu kinachowanyang’anya umaarufu na ulaji?
Hakuna ubishi kuwa ushawishi wa Seif visiwani umeporomoka kiasi hata cha yeye kuwa kimya au kusema mambo kupitisha muda. Rejea madai kuwa alirejeshewa maslahi yake kama waziri mkuu kiongozi wa zamani. Kama ni kweli kwanini umma haujui msingi ya kufanya hivyo kisirisiri na kwanini alikuwa amezuiliwa kupewa marupurupu yake? Je kurejeshewa maslahi nyuma ya pazia hakuwezi kuchukuliwa kama rushwa kisiasa?
Hili linathibitishwa na kukosekana uwazi wala msuluhishi huru katika mazungumzo kama ilivyokuwa kwa Kenya.Ukiondoa vyombo vya habari vyenye kuwekwa kinyumba na CCM, vyombo huru vimekuwa vikiliangalia suala la Zanzibar kwa huruma kiasi cha kuepuka kuuangalia ukweli kama ulivyo. Wachambuzi wenge wamekuwa wakiisakama CCM peke yake kana kwamba ndiyo kikwazo pekee cha kupatikana kwa muafaka wasijue na CUF ina mchango mkubwa wa mkwamo huu!Wachambuzi huru watailaumu CUF kwa kutumia mbinu zile zile za kizamani na uongozi uliochoka.
Umefika wakati kwa Seif kung’atuka ili damu mpya ishike hatamu za uongozi wa CUF. Hatakuwa wa kwanza. Al Gore alikuwa anapendwa nchini Marekani hata baada ya kuangusha kiutata na George W Bush. Hata kwenye uchaguzi unaotarajiwa Novemba hii, alishauriwa agombee. Lakini alikataa kutokana na kushindwa kuleta ushindi mwaka 2001.Mzee Edwin Mtei na Bob Makani baada ya kushindwa kuleta ushindi kwa CHADEMA, nao waliamua kung’atuka. Sasa umefika wakati muafaka kwa CUF kubadili uongozi wake ili kusonga mbele badala ya kucheza ngoma ile ile kwa zaidi ya miaka 15-mtafaruko.
Kwa upande wa CCM pamoja na kuwa na uongozi na serikali mpya, nao wafikie mahali wafanye vitu kiutu uzima. Mdharau mwiba mguu huota tende. Watanzania wangetaka suluhu ya mtafaruko wa Zanzibar ili wafanye mambo mengine ya ujenzi wa taifa badala ya kulalia na kukeshea upuuzi kila uchao.Maalim Seif na Lipumba wakubali wameshindwa. Hivyo waachie ngazi ili damu mpya yenye visheni na mikakati mipya itafute suluhu ya mtafaruko wa Zanzibar.Kila la heri.
Source:Dira ya Tanzania Juni 24, 2008.
No comments:
Post a Comment