Epistle to Afrophobic South Africa

Epistle to Afrophobic South Africa

Thursday, 13 November 2008

Ufunuo juu ya Tanzia


Nikiwa nimelala kwenye usingizi mnono mara nilioteshwa ndoto yenye wingi wa ufunuo.

Niliona wingu zito na tufani vya kutisha vikiigubika nchi ya Tanzia toka pande zote mashariki, magharibi, Kusi na Kaskazi. Nchi ilitetemeka huku miti mikubwa ikianguka.

Niliwaona wajoli walio uchi wakilalamika na kulaani sana . Walimlaani mfalme ambaye ufalme wake umejengwa kuu ya vichwa na nafsi zao akiwaibia na kuwakoga asijue nao wamekula yamini kujikomboa.

Jua lilipatwa na kiza kiasi cha kupoteza nuru yake. Ilikuwa ni gharika ya magharika. Kilichoshangaza ni kugundua kuwa wataalamu wa hali ya hewa waliliona hili kwenye vyombo vyao na kuonya. Bahati mbaya, wahusika waliwapuuza.

Wangezingatia na kutekeleza vipi wakati walikuwa kwenye usingizi mzito baada ya kulewa wakila na kunywa huku wajoli wakiangamia kwa njaa, magonjwa na unyafuzi? Ilifikia mahali wajoli wa Tanzia wakaanza kulia na kumkumbuka mzee Musa aliyekufa miaka mingi iliyopita!

Hali ilikuwa ngumu. Wanyama mwitu waliivamia Tanzia na kuiguguna. Wapo mafisi waliokuwa wamefugwa na watawala. Uchafu utokanao na maisha na mioyo ya binadamu tena wachache kati ya wengi vilitamalaki kiasi cha kuinajisi nchi nzima. Haya ni machukizo makuu kwa Mungu. Mapanya na wadudu wachafu waliinajisi nchi.

Kutokana na hali hii, Mungu aliweka nadhiri kuwateketeza wakuu wa Tanzia. Aliapa kuwatia adabu na aibu tena kwa kushutukiza. Mfalme wa Tanzia aliyejitapa kuwa kipenzi na mtetezi wa wajoli ghafla alijikuta akichukiwa kulika hata Firauni na Israili mtoa roho za watu.

Alijikuta akigeukwa na baadhi ya wapambe zake aliokuwa amewaacha wakaichafua nchi. Wajoli walikuwa wamewastukia wapambe na walamba viatu wa mfalme. Mfalme angejua vipi wakati alikuwa amelewa raha, sifa na kila aina ya ulafu?

Mfalme huyu aitwaye Jalala la Kaya Kichefuchefu alijikuta mtupu kama alivyozaliwa. Akiwa katika matembezi kwenye jimbo la Mbuya alijikuta akimwagiwa mvua ya mawe na wajoli walioikata na kuikataa mikatale.

Hakuamini macho yake kwa kile alichokiona! Akiwa ameghadhibika na kufura kwa hasira, aliwatuma watwana na mbwa wake kuwapatiliza wajoli waliomuonyesha hisia na mapenzi yao yaliyotibuka na kutumbukia nyongo baada ya kumpopoa na kumvulia nguo.

Bahari iitwayo Salama ilichafuka na kuonyesha hasira zake za ajabu. Ngurumo zilisikika kila upande wa nchi huku radi zikipiga kwa kasi ya ajabu.

Wajoli walimtaka mfalme awaonyeshe njia ya nusura asiweze. Walimzomea na kutishia kumtoa roho.

Mfalme akiwa hana hili wala lile, mara alisikia sauti za mabubu wakihanikiza wanataka haki. Visa vya kondoo kupigana na fisi viliripotiwa nchi nzima asijue vilikuwa somo la alama za nyakati kwake! Kama chumvi iliyovia, ufalme ulianza kumomonyoka kama siagi iliyowekwa juani.

Akiwa kwenye hakelu lake, Mfalme Kichefuchefu aliitwa na wasaidizi wake kushuhudia ajabu la mawe yaliyokuwa kwenye viwanja vya kasri yake kuanza kusema na kutishia kumshambulia!

Mara liliibuka Joka kubwa lenye pete na mapambo likihaha huku likizungukwa na moto mkali. Haraka haraka mfalme aliwaita wapiga ramli na watabiri wamwambie maana ya maajabu haya yote.

Mmojawapo aitwaye Kubunia alimwambia: yote haya yalimaanisha na kutabiri kuanguka kwa utawala wa Tanzia. Joka lilikuwa alama ya ufalme na moto uliwakilisha uasi ambao ungefuatia.

Mfalme alichukia sana na kumuona Kubunia mwasi na mwenye hila ya kutaka kumuangusha. Alimfunga kifungo cha maisha.

Baada ya hapo alimwita mpiga ramli mwingine aitwaye Tumbo Nile. Huyu kwa kujua mfalme asivyopenda kuambiwa ukweli, alimdanganya kuwa haya yalikuwa ni mapito! Na joka liliwakilisha wapinzani wa mfalme huku moto ukiwakilisha kushindwa kwa uasi.

Kutokana na ujuha wa mfalme na kuambiwa uongo akauamini, aliangusha sherehe kubwa kuadhimisha kunusurika kwake asijue mambo ndiyo yalikuwa yameanza!

Wapambe na wanywanywa waliowaugeuka umma waliitwa na kushereheka wasijue walikuwa wakishehekea mauti yao !

Akiwa kwenye karamu na wateule-najisi wake, mara mfalme alishuhudia mvua kubwa yenye radi ikianza kunyesha. Hapakuwa na dalili za mvua hata hivyo. Ndani ya mvua hiyo kulikuwa na wajoli waliobeba kila aina ya silaha tayari kuuangusha utawala wa mfalme aliozoea kuwahadaa kuwa ni wao.

Baada ya mfalme kuona wimbi la wajoli wenye hasira asijue nini kilikuwa kimewaingia hadi wakamuasi aliamrisha mkuu wa majeshi yake alete jeshi kuwadhibiti wajoli waasi. Maskini mfalme hakujua kuwa hata jeshi lake lilikuwa limemuasi baada ya kuchoshwa na maisha magumu na kudanganywa!

Majeshi yalikuwa yamepigika sawa na wajoli. Wakati mfalme na wapambe zake wakitumbua, hawakujua umuhimu wa jeshi. Wanajeshi walisahaulika kiasi cha kuanza kujiingiza kwenye ujambazi magendo na ufisadi. Walipogundulika walipatilizwa vikali.

Hivyo mgomo na kisasi vilikuwa vikiendelea chini kwa chini. Jeshi lilichoshwa na ufisadi na isirafu vya mfalme na wapambe zake ilhali wanajeshi wa chini wakikabiliwa na mazonge makubwa kuliko hata ya wajoli.

Mfalme aliyejulikana kwa kucheka cheka kwake alianza kuhofu. Maana wajoli aliowaona kuwa walevi walikuwa wamemstukia na kuamka tena kwa haraka kasi mpya nguvu mpya na ari mpya. Walijua kuwa kuwachekea chekea kwake hakukumaanisha mapenzi bali kuwaona mabwege.

Mfalme alitia nia kuwapatiliza wote wanaotishia ufalme wake asijue yeye na wapambe zake ndiyo walikuwa chanzo cha haya yote!

Kabla ya wingu hili la uasi kuikumba nchi ya Tanzia, mfalme alikuwa ameamrisha Fikra atiwe ndani. Kwani mawazo yake ya uamsho yalikuwa machukizo kwake. Alikuwa akingoja kumkamata Kuthubutu jamaa aliyemuogopa na kumchukia sana kutokana na ujasiri na tabia yake ya kuueleza umma wa wajoli kuwa walikuwa wakichezewa mahepe na mahoka mchana kweupe.

Kosa la Fikra lilikuwa kueleza ukweli kuwa mfalme alikuwa uchi, fisadi, mharibifu na mbabaishaji. Alichukia kuambiwa ukweli kuwa alikuwa akijilisha pepo. H akutaka kuzisoma alama za nyakati na ishara za matukio.

Tazama wakati mvua yenye radi ikiendelea kunyesha, mara angani kulitokea mpasuko uliosababishwa na radi. Mfalme alichanganyikiwa asijue maana yake nini!

Mara alipokuwa akiwaza na kuwazua zilikuja habari kuwa Fikri alikuwa ametabiri maafa iwapo mfalme asingesafisha hekalu lake lililokuwa limejaa mchwa, panya, nyoka, nge na kila aina ya uchafu.

Mfalme alichukizwa na ukweli kuwa undani wake ulikuwa umewekwa uchi kirahisi na haraka. Alizoea kujionyesha kama mpenda haki asijue wajoli walimjua. Alikuwa kizuizi na adui wa haki tena za umma. Alilewa sifa na nyimbo na ngonjera za wapambe wake hadi naye kugeuka mtumbuiza mwenye machukizo kwa wajoli.

Tazama nikiwa naendelea kuota naona vihongwe waliochukia wakibwaga mizigo na mikatale. Walionekana mamia kwa maelfu; wanawake, wanaume, watoto na hata ng’ombe. Walihanikiza wakisema ‘tunataka haki haki sasa’.

Wakiwa na nyuso zenye kunyanzi na miili iliyodhoofu, wajoli walivamia mitaa yote ielekeayo kwenye hekalu. Askari wa mfalme walisimama wakiwa wamepigwa butwaa wasijue la kufanya kuzuia wajoli waliokuwa wameamua kuikata mikatale.

Ingawa amri ilitolewa wampige mshale yeyote aliyethubutu kugoma au kuandama, askari walikharifu amri hii kwa kuona kuwa kweli wajoli walipaswa kupewa haki yao . Nao walishachoka na mzigo wa ufalme uliojaa wizi na matumizi mabaya ya pesa na raslimali za umma.

Kabla ya kujua majaliwa ya ufalme wa Tanzia, mara radi kubwa ilipiga nikatoka usingizini nikiwa kwenye kihoro kikuu.

Chanzo: Tanzania Daima Novemba 12, 2008.

No comments: