Epistle to Afrophobic South Africa

Epistle to Afrophobic South Africa

Wednesday, 5 November 2008

Niliwaambia nitaepa EPA na nimeiepa

WALEVI ni watu wa ajabu hasa wale wa kahawa. Hebu fikiria watu wanalewa kahawa ilhali haina kilevi, ukiachia mbali ‘caffeine’ kidogo tu ambayo inatosha kumlewesha mtoto lakini si mtu mzima. Ila kwa vile walevi si wazima kiakili, inawalewesha kiasi cha mimi kuwalewesha na sanaa na ngonjera hadi wanalala chari!

Najua mnakumbuka sakata la Elewa Paka Anadokoa au EPA. Hapa paka ni mimi na washirika wangu bila shaka. Wengi walidhani kama nisingewatimua na kuwasulubu washikaji zangu walevi wangenitoa shingo. Thubutu! Mie bingwa wa sanaa Bwana. Hata kama mshirika wangu Eddie Mpendamali walevi walimfurusha, bado nazimanya sanaa.

Baada ya walevi kulishikia bango kuwa lazima niwatose marafiki zangu, nami sikulaza damu. Niliwaahidi kuwa nitawaridhisha. Nilipowaambia nitawaridhisha nilimaanisha jambo moja.

Wao bila akili walizidi kujipa matumaini wakingojea raha! Ebo! Raha jipe mwenyewe usingoje kupewa. Nani awezaye kuwaridhisha wengine kabla ya kujiridhisha kuwa amejiokoa yeye na washirika zake?

Nimewaridhisha badala ya kutatua matatizo. Nimewapa maneno matamu na matupu na siku zinazidi kupuyanga. Ila mambo yakiendelea hivi, huko tuendako naanza kuona woga.

Ila kwa vile walevi ni waroho na walafi wa ulaji na manywaji si haba nitawapa takrima na mambo yataisha niendelee kupeta. Upo hapo? Shauri yako kama hutii akilini. Waliwa wadhani wala na waacha wadhani wangojewa. Senzi kabisa.

Tuendelee na dunia ya walevi. Kuwaweka sawa sikuacha sanaa. Niliunda tume ya uongo na ukweli iliyoundwa na washikaji zangu ambao tena ni vibaka kuliko hata mimi.

Alikuwapo Johnso Mwananyika, Eddie Washea na mgambo mkuu wa kijiwe, Saidia Mwemwa. Ukiondoa Mwemwa ambaye tumeoa nyumba moja, waliobaki ni mawakala wangu wa udokozi wa kahawa kwenye kashfa ya kahawa ya Monduli.

Nilikuwa natoa maelekezo ya nini kifanyike na nini kisifanyike. Kimsingi tume hii ilikuwa kanyabwoya ya kuwaibia zaidi walevi. Maana wajumbe wa tume walilipwa kashata na kahawa nyingi kuliko hata zilizoibiwa. Upo hapo? Wizi ndani ya wizi.

Kama walevi wangejua wasingeiita hii tume kanyabwoya tume ya nonihino, bali tume yangu ya kuzugia na kujiokoa.

Eti walevi walinishinikiza niwasulubu washikaji zangu wakiongozwa na yule rafiki yangu wa kimanga kwa jina la utani Roast Tamu L’ Aziz! Walitaka nimtose Jitu la miraba minne yule rafiki yangu gabacholi Patel! Jamani niseme mara ngapi? Hatoswi mtu hapa zaidi ya walevi wenyewe na kijiwe chao.

Walevi hawajui kitu. Hawajui: hawa wadau niliwatuma mimi ili nipate uchache wa kuwahonga walevi wanichague kuwa dingi wao wa Kijiwe!

Kwanza tusilaumiane. Walevi ndio mlikula takrima ya kashata na tangawizi huku mkibukanya kashata zangu msijue ni zenu. Hamkumbuki nilipowapa mishiko hadi wake zenu wakaonja hata nyama? Kumbe hamkujua kuwa nilikuwa namkaanga samaki kwa mafuta yake?

Kwa vile walevi wanazidi kushupaa, lazima niunde kamati nyingine ya kuchunguza kashata zilivyoliwa na kahawa ilivyonywewa. Kwa vile huu mkenge niliowatwisha kuwa jamaa zangu wamerejesha kahawa na kashata unaanza kufanya kazi, ili kusogeza muda, lazima nije na tume ya kuchunguza ulaji ili siku nyingine tuepuke janga hili.

Juzi nilipokea simu toka kwa mpinzani wangu Kapende akitaka nihakikishe vibaka wanafikishwa kwenye mahakama za kijiwe ili wasulubiwe. Huyu naye hajui kama walevi anawaongoza. Nani anaweza kujitoa kafara kwa ajili ya adui yake?

Kilichonichekesha hadi mbavu kuuma ni pale nilipowafunga kamba kuwa kashata na kahawa vimerudishwa. Wapuuzi hawa. Nani karejesha kilichomezwa kiwe na thamani na sura ya kile kile alichokula? Hata chatu akitema alichokuwa kameza kitakuwa si kile kile bali mzoga tena mchafu tu.

Sasa wanaotaka kashata na kahawa virejeshwe wakati tuliishavi---- na kuvikojoa, kama si mataahira ni nini? Kama mkitaka kashata na kahawa zenu basi tunyongeni sisi tuliokula na kunywa. Lakini nani atathubutu hili iwapo wanywaji na walaji ni walevi wenyewe waliofakamia takrima zama zile?

Mie nafanya mambo kama Tunituni aliyeunda tume ya kupambana na rushwa ikamfichua akaikalia hadi kesho. Tunituni wa Makapi alinizidi. Kwani yeye hakuwa tayari kutoa kilichokuwamo kwenye tume yake. Mimi ingawa sikutaja kilichomo, nilifanya kosa kuahidi kuwaridhisha walevi.

Sasa natoa onyo. Wale wanaotaka tusulubiane wakome na kukomaa. Nani anategemea nyani amhukumu ngedere wakati wote ni wezi wa mahindi?

Sasa tuangalie mambo kiutu uzima. Hivi hamkuonywa na yule mzee aliyekuwa akinywa kahawa bila kulewa kuwa msipwakie kila zagazaga inayotaka ukuu wa Kijiwe?

Hamkumbuki zama zile aliponishtukia mie na mshirika wangu Mbwa Mwitu baada ya kugundua kuwa sisi ni vibaka? Sasa mnalia nini iwapo walevi nyie mlinipa ukuu mkijua fika mie ni kikwapuzi?

Natoa taarifa kwa washirika zangu kama Yusuf Mihanji aliyekuwa amekimbia kijiwe akidhani nitamuumbua. Rudini tuleni na kunywa. Walevi hawana bao.

Jana nilifanya kikao na wakili wangu na kumpa maagizo atangaze kuwa atawafungulia kesi walioiba kahawa. Hii kumbuka. Ni gea bab kubwa.

Tutafungua kesi tena za madai ingawa wezi walivunja ghala la kijiwe. halafu kesi zitapigwa tarehe hadi siku ya kiama. Upo hapo? Hapa wanoko wote nitakuwa nimewaacha solemba.

Pia nitoe onyo. Walevi mnaoota tusulubiane acheni uvivu wa kufikiri. Hakuna nguruwe awezaye kumuua ngiri wakati wote ni dugu. Sasa ona iko wapi logic mi tumia komba jiwe yenu. Nyinyi levi kio jinga sana. Kama taka mi acha kula basi nenda juu kazibe hon!

Kwanza kabla ya kuendelea ngoja niwape vunja mbavu. Nina mpango wa kusilimu siku si nyingi ingawa walevi wanachelea hili kwa kuogopa wanaweza kuzuiwa kulewa.

Juzi nilikiambia kijiwe kuwa umaskini wake unasababishwa na kutopata misaada kutoka kwa watu wa God. Ajabu wakati nikiwaweka kamba hawakushtuka kuwa kijiwe hakiwezi kuendelea kwa kutegemea pesa ya sadaka!

Nataka kusilimu ili kuondoa ufisadi uliotamalaki kwenye kijiwe. Kuna watu wananiona kama sina dini na dini yangu ni ufisadi. Ili kuwapata watu wa God lazima nijifanye nimesilimu. Nitasilimisha hata kijiwe ingawa walevi hawataki. Nawatania. Hii ni ‘straight talk’. Msijali sana.

Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 5, 2008.

1 comment:

Anonymous said...

SIKUFAHAMU LAKINI NAPENDA KUWASILIANA NAWE MIMI NI MTANZANIA NA CONTACT YANGU NI HII HAPA CHINI:

edwardmkwelele@yahoo.co.uk

nipo uk london kwa sasa,
thank you