The Chant of Savant

Tuesday 25 November 2008

Je kukamatwa kwa Mramba na Yona mwanzo au mwisho wa picha?

Kwa mara ya pili tangu rais Jakaya Kikwete aingie madarakani ameupa raha umma wa watanzania.
Mara ya kwanza alifanya hivyo ingawa bila kujua wala kutarajiwa mwezi Februari aliporuhusu rafiki na mshirika wake mkuu, Edward Lowassa kukaangwa na kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Dr. Harison Mwakyembe.

Katika uchunguzi wake, kwa mara ya kwanza, waziri mkuu tena mwenye ushawishi alifukuzwa kazi kwa aibu tena bila kutarajiwa wala kutarajia.

Kitendo cha tarehe 25 Novemba 2008 cha kuwafikisha mahakamani vigogo wa serikali na chama Basil Pesambili Mramba mtu aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika utawala wa Benjamin Mkapa na Daniel Yona, kadhalika mwenye ushawishi na kiburi kwenye utawala wa awamu tatu ukiachia mbali kuwa mshirika na mwandani wa Mkapa, wapo wanaosema ni mwanzo tu wa kuwafikisha wote waliokuwa wakijiona wao ni wao na nchi ni mali yao.

Kutokana na kufunguka kwa pazia hili, wapo wanaosema watakaofuatia ni akina Rostam Aziz anyedaiwa kuwa nyuma ya kampuni tatanishi la Kagoda lililoiba mabilioni ya shilingi toka Benki kuu kwenye mfuko wa madeni ya nje (EPA).

Umma wa Watanzania umechoka sana na unachukia rushwa ya kimfumo ambayo imekuwa ikilisumbua taifa lao na kulifanya maskini wakati lina raslimali nyingi barani Afrika.

Ukiangalia uzito na ushirika (connectivity) wa wahusika, kama kweli serikali imeamua kujitofautisha na mafisadi wanaosadikiwa kuitia mfukoni, uwezekano wa Mkapa, Mkewe, watoto wao na washirika wao wengine kunusurika ni mdogo. Je Kikwete ameamua kujitofautisha na genge la ujambazi lililopoteza sifa yake ya kuwa kipenzi cha watu?

Je nini kinamsukuma Kikwete kuchukua hatua kali sawa na zile za marehemu Levy Mwanawasa wa Zambia au Dr. Bingu wa Mutharika wa Malawi? Je ni hofu ya kutotaka kufikishwa mahakamani baada ya kumaliza muda wake kutokana na kuzidi kudhoofu kwa Chama Cha Mapinduzi ambacho kisipobadilika kinaweza kutoa nafasi kwa upinzani kuchukua nchi?
Je ni kutaka kuchaguliwa tena awamu ya pili? Yote yanawezekana.

Je ni kutokana na shinikizo la upinzani ukiungwa mkono na umma au mbinyo wa wafadhili nyuma ya pazia?

Kama Kikwete amefanya hivyo kwa bahati mbaya au makusudi, ajue amefanya kile wazungu huita "To open Pandora's box" yaani kumuita bwana matatizo ambaye daima huitika.

Kwa hatua iliyokwishafikiwa, kama Kikwete atarejesha majeshi nyuma, kuna uwezekano akaishia kuwa muathirika. Na kama ataendeleza uzi ule ule, kuna uwezekano akaibuka kuwa shujaa asiyetarajiwa.

Ikumbukwe. Tangu Kikwete aingie madarakani, alikuwa hajawafanyia lolote watanzania. Si lile aliloahidi au walilotarajiwa. Muda ulikuwa ukimtupa mkono kiasi cha umma kuanza kulalamika moja kwa moja hata kuchukua hatua. Rejea kupigwa mawe msafara wake kule Mbeya hivi karibuni ukiachia mbali magazeti ya kweli kumkosoa moja kwa moja.

Je Kikwete amesikia kilio cha waliomchagua huku akipuuzia laghba za mafisadi waliomzunguka?

Ukiangalia kesi inayowakabilia Mramba na Yona ingawa haturuhusiwi kuijadili kishiria, inahusiana na uwekezaji hasa kwenye sekta ya madini ambao kimsingi umekuwa ndio mkuki unaowachoma watanzania. Wengi hujiuliza inakuwaje Tanzania izidiwe na nchi kama Kenya, Burundi,Rwanda hata DRC wakati ina madini kuliko nchi hizi?

Kikwete alirithi nchi iliyoparaganyikiwa kiuchumi kutokana na kukosekana kwa uadilifu na umakini kwa mtangulizi wake aliyetanguliza maslahi ya kifamilia na urafiki. Je umefika wakati wa Kikwete kutumbua jipu?

Tumkumbushe, waziri wa nishati na maendeleo ya madini, William Ngeleja aliamriwa na waziri mkuu Mizengo Pinda kuuambia umma nini kinaendelea nyuma ya pazia kuhusiana na umilikaji na utwaliwaji wa kinyume cha sheria wa mgodi wa makaa ya Mawe wa Kiwira unaosemekana kutwaliwa na rais mstaafu Mkapa akishirikiana na mkewe, mtoto wake na rafiki na mshirika wake Yona. Ilikuwa ni kwenye kikao cha bunge cha 12 ambacho Ngeleja aliahidi angewataja wamilki na hatima ya mgodi.

Hadi yote haya yanatokea Ngeleja hakuwa ameeleza chochote! Alilidanganya bunge na umma na hakujali. Je kwa wahusika kuanza kupanguliwa na kufikishwa mbele ya haki, Ngeleja atanusa upepo na kujivua uhusika?

Je kukamatwa na kushitakiwa kwa Yona hata kama ni kwa makosa tofauti na utwaliwaji na umilkaji wa mgodi wa Kiwira ambaye aliwahi kutishia kuwa mwenye ubavu aende mahakamani ni mwanzo wa kuelekea hili la Kiwira ambalo nyuma yake kuna Tembo au tuseme The elephant in the seating room?

Maswali ni mengi. CCM imekuwa ikitajwa mara kwa mara kuhusiana na karibu kashfa zote za mabilioni. Juu ya hili CCM imegawanyika kwenye mitandao hatari ya kimaslahi kiasi cha kutishia uhai wake. Je umefika wakati wa Kikwete kuibadili CCM kabla haijambadili?

Kwa vile Kikwete ameamua kufanya mapinduzi ya kifikra kwa vitendo na dhahiri, tumpe CHANGAMOTO.

Umma unataka hata wale walioko nyuma ya Richmond, kampuni kidhabu iliyokuwa ikijiingizia shilingi bilioni moja na ushei kwa siku bila kufanya lolote zaidi ya jinai na kushirikiana na magenge ya mafisadi waliokuwa madarakani, nao walipie dhambi zao.

Je umefika wakati muafaka wa kuondoa udhia kwenye safu za utawala wa Kikwete. Haya shime baba. Kama utabadilika tuko nyuma yako.

Muhimu katika yote, umma ungemtaka bwana Kagoda anayejulikana mbele ya haki sawa na wengine. Kwani nchi hii ni mali ya umma na siyo mafisadi uchwara waliokuwa wakijificha nyuma ya pazia la utukufu wakati ni watukutu.

Kikwete ana pa kuanzia. Aige kwa Bingu wa Mutharika jirani yetu Malawi. Mutharika alipoingizwa madarakani na Bakili Muluzi rais wa zamani aliyetaka na kulenga kumtumia kwa kutumia utukufu wa chama, alikiasi chama na umma wa wamalawi ulimuelewa na kumuunga mkono. Tangu afanye mapinduzi haya adhimu ya kifikira amezidi kuwa imara na salama tofauti na wanaotisha kuwa ukiachia chama kibovu nawe utazama nacho. Je ni kipi bora? Kung'ang'ania mtumbwi uliotoboka ufe nao au kujaribu kushikilia ubao ili ukoke? Akili timamu inasema. Bora ni kujaribu ubao badala ya mtumbwi uliokwishaonyesha wazi kutoboka.

Wakati umefika wa kuuonyesha na kuuhakikishia umma kuwa ndiyo wenye nchi na siyo genge dogo la mafisadi.

Tuhitimishe. Tunamshauri Kikwete ashikilie uzi ule ule. Mwanzo wa ngoma ni lele. Tumkumbushe. Kama alivyosema waziri mkuu Pinda kuwa hatima ya mkurugenzi wa Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Edward Hosea na mwanasheria mkuu, Johnson Mwanyika itajulikana karibuni, basi na ijulikane ili tusonge mbele.

Kikwete ana bahati na ana kila sababu ya kutojipiga mtama. Wanaomtisha kuwa nchi itayumba watayumba wao. Kwani unaweza kuiangusha serikali lakini siyo umma.Kikwete ana pa kuanzia na nchi haijayumba zaidi ya kuungana na kushikamana nyuma yake kupambana na ugaidi wa kiuchumi na kisiasa.

Yote yanawezekana. Muhimu, Kikwete ameanza kusafisha nyumba yake ambayo kusema ukweli ilikuwa chafu, basi aumbe umma uliomchagua kwa kishindo usimame naye kwa vile sasa unaelewa lugha anayoongea.
Naamini tutashinda na wakati wa kushinda ni huu.
Je huu ni mwanzo wa vita dhidi ya ufisadi mkongwe Tanzania au mwisho wa mwanzo wa business as usual? Haya shime Jakaya tuko nyuma yako usituangushe na hatutakuangusha. Asiyevuta nasi si mwenzetu. Na pema ujapo pema ukipa si pema tena. Mafisadi wako kufa na mtu kutetea ufisadi wao. Je umma uko kufa na mtu kutetea nini zaidi ya taifa lao? Kumeishaanza kujikotokeza mawazo kuwa hiki kilichotokea kinalenga kuepusha mshawasha wa Kagoda na EPA kwa ujumla. Ni vizuri serikali isitoe mashiko kwa dhana hii. Hii maana yake ni kuhakikisha wote waliotumia madaraka yao vibaya au kujihusisha na ufisadi wanafikishwa mbele ya mahakama na haki inaonekana ikitendeka.

Chanzo: Freethinking unabii.














Fisidunia alipokataa kurejeshapesa ya EPA.


BAADA ya kuwafunga kamba walevi kutaka wezi wa kahawa na kashata maarufu kama EPA, yaani ‘Elewa Paka Anadokoa’ kwa maana nyingine ‘Elewa Wakubwa ni Wezi’ au EWA, si jamaa na washirika zangu wanataka kunitaja ili mzee mzima niadhirike! Huwezi kuamini. Wanataka kufichua kilicho nyuma ya pazia baada ya kuona nimewageuzia kibao na kukoswa msimamo! Hawa watu hawajui ukubwa.

Niliwafunga kamba wana Kijiwe kwa kutoa msamaha ambao baadaye waliukataa. Nilitaka vibaka wa kashata na kahawa warudishe mambo yaishe nisijue ndiyo yalikuwa yakianza! Kama hii ingepita huenda ingeniokoa. Sasa naona kama mambo yanaelekea kubaya kiasi cha kutaka kuniadhiri mzee mzima.

Kwanza walevi waliuliza wapi nilikuwa nimepata mamlaka ya kusamehe dhambi tena ninayoshiriki vilivyo? Wapo waliosema wazi kuwa mimi ni mnafiki na fisadi kuliko mafisadi waliowahi kuwapo kwa sababu ni mnufaika mkuu! Kweli walevi wana mambo tena mambo mambo! Hivi bila kukiibia kijiwe kashata na kahawa, walevi ningewahonga nini ili wanichague? Walitaka niwahonge mke wangu?

Akina Mgosi Machungi, Kanji na Makengeza walijitahidi kurejesha. Niliwaita wanakijiwe na kuwatangazia ‘neema na mafanikio’ ya utawala wangu wasijue nilikuwa namkaanga samaki kwa mafuta yake mwenyewe!. Nilidhani huu ungekuwa mwisho wa onyesho hili la umahiri wa sanaa. Kumbe hola bwana! Ndiyo mambo yameanza!

Baada ya wana kijiwe kuhanikiza kuwa sina mamlaka ya kumsamehe mwizi, niliamua kujipiga mtama na kuruhusu akina Machungi na Kanji wafikishwe kwa pilato. Nilipata ithibati na kutaka wote waliokwapua wakamatwe nisijue nilikuwa najichongea! Kumbe wengine walikuwa wananilia ‘timing’ bwana.

Punde si punde nilipata ujumbe wa simu toka kwa Fisidunia Malengelesi. Inaonekana alikuwa amechukia sana. Maana simu ilivyokuwa ikitweta na kuwaka kwa hasira sina jinsi ya kueleza.

Jamaa halina akili nzuri. Maana lilisema halirudishi kashata wala kahawa na kama nitaendelea kuwasumbua wezi waheshimiwa wenzangu, atatoa ushahidi unaoonyesha kuwa nilinufaika na ujambazi huu wa mchana. Fisidunia huyu anasema anao ushahidi unaonihusisha mimi, familia yangu, wenzangu na chama changu cha Mafisidunia na masaniidunia (CCMM).

Njemba imenishika pabaya. Mbwa mwitu na wezi wenzangu wanasema wazi kuwa niliwatumia kuibia kijiwe ili kupata kashata na kahawa ya kuwahonga wana kijiwe wanichague kuwa mkuu wao. Na ni kweli.

Kwanza, ngoja nikusomee ujumbe wenyewe. “Mpayukaji usinitishe hata kidogo. Mimi siyo kama akina Kanji ambao unaweza kuwatia jamba jamba. Mimi ni mwizi na mjanja kama wewe tena aliyekubuhu. Usidanganywe na ukuu unaopewa na hao wasiokujua ulivyo. Wadanganye na kuwatisha hao hao wasiojua uoza wako.

Ukiendelea tutaumizana halafu mwisho wa yote utayejilaumu ni wewe na mkeo. Uliponijia na dili lako nilikuwa na langu. Tuliiba nikijua siku hizi zitakuja na nitajitetea kama ambavyo nimepanga kufanya.

Wewe ni mwanasiasa nami naijua sheria. Hapa ieleweke ni fisi wawili waliokuwa wakiwinda pamoja kila mmoja na lake. Ulitaka kunitumia kupata ukuu nami nilikutumia kupata ukwasi. Hivyo kaka kaa ukijua, ukiendelea kunifuata fuata nitakuchafua wewe na mkeo.”

Baada ya kupata ujumbe huu wa maudhi, nilinywea na kuhisi kijasho chembamba kikinitoka wallahi. Maudhi ya kiumbe huyu yalifanya niikumbuke busara ya wahenga isemayo ongea na watu uvae viatu na ongea na kuku utembee peku peku.

Tazama hawa wezi nilioshirikiana nao ni wachovu wasiojua wala kuweza kuniokoa bali kujiokoa wenyewe hata kwa kuniangamiza na maulaji yangu!

Hata pira la Manchester nililokuwa nikiangalia badala ya kuwa ‘spectacular’ liligeuka ‘spooktacular!’

Sikudhani kuwa hata washirika wangu wa zamani kama yule Razi kumwaga razi wakisema niwasulubu washirika zangu. Razi anasema eti nimeshughulikia walioloa kwa damu huku mchinjaji mkuu nikimwokoa! Jamaa yangu wa Kimbushi inabidi atie akili hapa.

Kama kuchinja ng’ombe alichinja Ballalii. Je akina Razi wanataka niwatose akina Mrambaramba, Kigodaabu, Mengjii, Ewassa bingwa wa Richmonduli, Ngasongua na vibaka wengine? Kumbuka haya siyo majina yao bali ya utani kijiweni kutokana na umahiri wao wa kuhomoa.

Baada ya sanaa zangu kuanza kushtukiwa, lazima nitafute nyingine. Nitawambia walevi kuwa haraka haraka haina baraka. Wanipe muda waone hata kama kuona kwenyewe ni kuona mazingaombwe, sanaa na kusikia ngonjera.

Kwanza kuna watu wanataka kunichanganya. Mmojawapo ni Eddie Washea ambaye huwa tunamtania Dokto. Jamaa linapayuka payuka hovyo kiasi cha kujichanganya. Juzi lilisema eti hatuwezi kuwasulubu wezi wote maana kijiwe kitayumba.

Jana linasema eti kila kigogo kitakatwa lisijue nalo ni gogo tena kubwa tu! Hili jamaa sijui lina nini kichwani mwake! Hata huu udokta tunaomtania itabidi tuufute badala yake tumuite Ze. Eddie Washea. Ze inasimama badala ya zezeta.

Kuna mijitu haina maana kabisa, haijui kuwa ushikwapo shikamana! Badala ya kurejesha uchache na kukubali iozee lupango eti inataka nami nimwage ulaji wangu. Mijitu hii ilikuwa inajiona ni miheshimiwa kwa vile ina ukubwa katika kijiwe. Lakini imesahau! Uhalifu haulipi na hauna ukuu hasa ukuu wenyewe unapotumika kukwapua badala ya kulinda mali za kijiwe. Ingawa mimi ni hovyo sasa nimeonekana hovyo kabisa kutokana na mijitu kuanza kunichenjia.

Kwanza ngoja niongee taratibu wanoko wasinisikie. Sijui kipindi kile cha kusaka njuluku tuliingiwa na nini! Maana tulighushi kama mataahira kiasi cha kufanya kazi ya kutufichua kuwa rahisi kama ilivyotokea.

Inaonekana rafiki yangu Tunituni aliyeasisi na kubariki mpango huu alipatwa na ugonjwa wa uvivu wa kufikiri. Naye ananipa kazi kweli kweli kumlinda, maana kama hii mijizi inayonitishia maisha itamwaga mtama kwenye kuku naye hatanusurika ingawa nimejitahidi kumkingia kifua yeye mkewe na marafiki zake.

Ama kweli hakuna kazi kama kumtafuta shetani mimbarini.

Namna hii kufikia 2010 kijiwe hakitakuwa na rushwa! Tia akilini usijenilaumu.

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 26, 2008.







No comments: