The Chant of Savant

Wednesday 25 February 2009

Mpayukaji na bakora za Mnali



BAADA ya sakata la njemba moja fyatu kuwalamba mboko wafa na vumbi la chaki, mzee mzima niliamua kukusanya maoni ya walevi.

Nilitembelea baadhi ya sehemu za Bongo nikianzia kule Katerero kabla ya kuelekea Kanazi na Kasenene nikilala Kagondo.

Nilimuhoji mwalimu Nonihino ambaye makalio yake yalikuwa bado yamevimba kwa kulambwa njiti arobaini.

Alikuwa na haya ya kusema: “Mushaija mwandishi wa haabali uniache. Sina cha kusema. Huyu mshaija kanitia aibu kweri kweri. Siku hizi hata kwa baba mukwe siwezi kwenda, nitakwendaje na aibu bwana mwandishi? Kila ninapopita wanafunzi wananizomeya eti mimi ni Mnari!”

Naye Mwalimu Mtakakwa wa Chemujwahuzi alikuwa na haya ya kusema: “Muheshimiwa mwandishi wa habali, huyu bwana kwanza ni mwehu na siyo msomi. Mimi sikujuwa kuwa kuna mtu anaweza kuwapiga walimu kama mimi.

“Kwanza mimi nshomile nina setifikeiti ya education na kozi mbali mbali. Pia hajui kuwa wanafunzi ndiyo walioshindwa, hivyo kama ni kupiga, angewapiga wanafunzi hata kwa kuwaoneya, maana tukisema ukweli pia selikari ndiyo iliyoshindwa inayokopa tumishahara twetu huku ikirara kitanda kimoja na mafwisadi.” Anaangalia huku na kule kuona kama Mnari anaweza kuwa karibu na kuendelea:

“Kusema kweri mwenye kuferisha wanafunzi ni selikari. Walimu hatuna mishahara ya kutosha, hatuna madawati wala vitabu vya kufundishiya. Sasa wanategemea tufwanye miujiza gani wanafunzi washinde? Mbona selikari yenyewe imeferi kwenye kuwakamata akina Kagoda, EPA na Richmond? Au wanazani hatujui kwa vile tunaishi mashambani?”

Nilimuuliza nini mawazo yake kuhusiana na rais kuchukua hatua za haraka dhidi ya Mnari.

Alikuwa na haya ya kusema: “Hiyi bwana ni danganya toto, tungesikia yuko lumande tungefulahi. Nazani lais angetoa fidia na kutuomba msamaha kutokana na kuturetea kichaa kuwa mkuu wa wiraya yetu.”

Jamaa alisiliba sana na kumwaga sera kwa sana. Siwezi kuandika yote aliyoyasema pakakalika, maana kwake mkuu na Mnari haoni tofauti. Tuyaache.

Kutoka hapo nilielekea mkoani Lushoto ambako nilimuhoji rafiki yangu Mgosi Machungi aliyekuwa na haya ya kusema: “Kwanza huyu Mnai angepiga washambaa tungempiga zongo, ila hata hivyo kama tikishema ue ukweli, jamaa aipaswa kuwa mkuu maana wabongo timelala sana, tinahitaji mtu wa kutiamsha ili mambo yaende.

“Tazama tinavyochezewa na mafisadi na tisichukue hatua, unaona kina Liumba wanavyotizeshea kwa kuachiana bila aibu. “Heri atokee mtu atilambe bakoa tiweze kuamka na kulisogeza taifa mbee. Tinapaswa kuamka na kufa na mafisadi hasa wae wa madaakani tinaofanya makosa kuamini watatikomboa.”

Alipuliza moshi mzito wa sigara yake kali na kuendelea: “Kwanza alipaswa ateuiwe kuwa mkuugenzi wa Takukula ili awachape viboko mafisi na mafisadi. Au awe spika awachape viboko wabunge wanaozembea na kulala bungeni bia kusahau akina Chitahio na watoa ushwa waliojaa bungeni.”

Mzee mzima sina mbavu.

Mgosi aliendelea: “ Kama wameshindwa kumpa poomotion kusimamia maeneo hayo juu, basi wangempa ukuu wa tiafiki awanyoe wapiga mabao au awe waziri wa afya awakomeshe wezi wa madawa hospitai na wanaoomba rushwa wagonjwa.”

Hii babu kubwa. Eti Machungi anatamani Mnari angechaguliwa kuwa mkuu ili awachape bakora Kikwekwe, Kimdunge, Joe Makamba, Ewassa, Tunituni, Kagoda na bi mkubwa ajifichae kwenye Ngo!

Hii sikuweza kuikariri kama ilivyo kwa kuogopa tishio la kesi za kudai mabilioni mahakamani, hata hivyo wakati mwingine tunaogopa bure. Nakumbuka yule mbunge mwanasheria bilionea aliyetishia kushitaki magazeti kwa kufichua uchafu wake halafu akaishia kuufyata kama Grey Mgonjwa na mafisadi wengine waliotishia kushitaki. Mimi mtu akinishitaki namlamba bakora kama Mnari. Upo hapo?

Kwanza mimi siandiki kienyeji kama anavyotawala mkuu kwa ulevi wa tende akiwaachia washikaji zake kina Kagodamn na Liumba. Mie nakaanga, siandiki. Ukiwa fisadi nanyoa sipokei mshiko hata kama ni wa cheo cha uani kama Silva Rwamnyama. Mie natwanga kama sina akili nzuri.

Ila mimi si chizi wala mlevi wa madaraka wala kihiyo.

Lo! Badala ya kuhoji wananchi naanza kujihoji na kujikariri mwenyewe! Mwe! Huku kupayuka nako!

Kutoka Lushoto nilikwenda zangu Shinyanga. Nilimuhoji mzee Maduhu.

Alikuwa na haya ya kusema: “Mami mimi naona huyu Mnali angewapigaga wamafisadi kama yule wa pale Balyati, Endelea Chenga. Haka kajamaa mami kama kangekuwa na sirikali kangeweza kula sahani moja na wamafisadi hakya ya mama!”

Anakohoa na kuendelea: “Kwa kukatimua maulaji, mkuu amepata karata ya kuwaibia wapiga kura makura wakati wa uchaguzi ujao nakwambia mimi. Kama siyo kwanini asiwatimue akina Kandoo wanaowapigaga na kuwaibiaga wafanyabiashara ndoko ndoko? Kwanini asiwafunge akina Richmonduli na EPA ambao ni washirika na marafiki zake? Au ni kwa vile kacheo kake ni kaadogo?”

Kutoka pale nilirejea jijini Bongo ambapo mshirika wangu Mpemba alikuwa na haya ya kusema. “Yakhe mie huyu Nnali ankuna kweli kweli. Yeye apiga bakora wakati wao wapiga maisha. Lau yeye kawapiga mara moja ilhali wao wawapiga maisha yote, si usiku si nchana. Hivi huyu apigaye bakora na akopaye walimu nani awadhalilisha?” Ajabu anajijibu mwenyewe!

Anasema: “Mie naona wote sawa. Heri akupigaye mara moja akakoma na kukomeshwa kuliko akupigaye siku zote, wavunja haki za binadamu hawa ati. Maana walimu wetu sasa weshadhalilika kiasi cha kuishi kwa tuisheni ati, wamedhalilika kiasi cha wengine kuomba hata nauli kwa watoto kama ambavyo sirikali yaomba kwa wafadhili na wahindi inaowapa pesa yetu kila siku.”

Nilipokuwa nikiendelea kumhoji Mpemba mara nikasikia maajabu ya Kisutu ya mwizi kujidhamini kwa asilimia moja ya dhamana!

Baada ya kufika pale nilinyaka mazungumzo ya baadhi ya mgambo waliokuwa wakingoja mahabusu watoke mahakamani wawasindikize lupango.

Maongezi yao yalikuwa kama ifuatavyo: “Wajinga wanashangaa kwanini jamaa katoweka. Walitaka awataje wazito waliomtuma kuiba pesa ya uwezeshaji kwenye kusaka ulaji? Mbona kila kitu kiko wazi! Tunamshukuru Mungu kwa kipindi walichokuwa kwetu vigogo hawa si haba. Tumelamba lamba.”

Niliposogea karibu nizinyake zaidi, mara nikaamrishwa nitimke kabla sijawekwa chini ya usalama
Chanzo: Tanzania Daima Februari 25, 2009.

No comments: