The Chant of Savant

Thursday 7 May 2009

Mpayukaji kugombea ubunge 2010



KWANZA nitoe pole kwa waathirika wa mabomu ya Mbadala. Nyumba yangu ilikwenda na maji. Sijui nitalipwa au wajanja watanifanyia kama wazee wa Jumuia ya Afrika Mashariki!

Kwa vile msimu wa ulaji kwa njia ya kura umeanza, mzee mzima nina mpango kamambe kugombea uheshimiwa hata kama sina heshima. Kama wezi wengi wameweza kujipenyeza kwenye siasa ambayo ni ulaji wa urahisi, kwa nini mjanja nijivunge au kushindwa?

Nimeishaandaa zana zote. Nina digrii za kughushi saba toka vyuo vya Commonwealth, Havard, Edinburg aliposomea Mchonga, na Open University of the World (OUW) mjini New york na Bangarole India .

Nimeishaongea na madigara wa Kigabacholi na Waarabu kunidhamini ili nikiishaukwaa niwapigie debe wawekeze na kuchukua nchini. Hapa tutadhamini timu za mpira wa miguu na kutoa misaada mashuleni.

Yule Mwarabu wangu wa Dubai atashusha Dolari za kuhonga wajumbe wa mkutano wa uteuzi. Kila atakayehudhuria na kukubali kunipa kula lazima nimpe ulaji wa madafu 500,000.

Ingawa sijatajwa kwenye kashfa sugu za Richmond na EPA, Deep Green Finance, Meremeta, Kagoda na madudu mengine, nilipata mgao wa pesa kwa ajili ya kuwahonga walevi wanaopenda ulabu na wake zao wapenda vitambaa, khanga, T-shati, nyama choma na upuuzi mwingine. Mi si fisadi papa wala nyangumi.

Pia nimeishapata makanjanja wa kunifagilia kwa sana ili walevi wajue mie ndiye mkombozi yule waliyeahidiwa kuja kuwapeleka Kanani kwenye nchi ya nyama choma na divai.

Mie bonge la mjanja. Nimeishaingia ubia na makanisa na misikiti fulani kunipigia chapuo tayari kutawazwa kuwa mheshimiwa Mpayukaji Msemahovyo PhD Phil, MA in lies and hypothetical thinking, BSc. Umbea, Dip in Corruption and mafia. Cert. in Mass mobilization, MBA, Masters in Money making etc, mbunge wa jimbo la Tumboni kwenye Mkoa wa Ulaji.

Kwenye digrii zangu, hakuna digrii inahitaji kuwa na akili sana kama ile ya MA in lies and Hypocrtical thinking. Duniani wanazo watu wachache. Kwa Bongo ni mimi, Ben Makapu wa Mkapaa na Joe Makamba tu na katika Afrika ni mimi Robert Mugabe, Jack Zuma, Yoweri M7, Joe Makamba na Moi Kibaki.

Mipango yangu mikubwa kuliko tembo. Nitaingia na kauli mbiu mpya ya Usongo mpya, Mapenzi mapya na Mambo mapya na makubwa. Hapa sina shaka walevi wataniamini.

Nitaanza kula na kunywa nao. Nitawasalimia kwa kuwataja majina huku tukikumbatiana kama vile ni washikaji wa siku nyingi. Pia nitahakikisha shangingi langu linakuwa dala dala la kusafirishia walevi kila watakapotaka kwenda.

Mke wangu ataanzisha NGO ya kutetea maslahi ya wanawake. Atahakikisha anapigana hadi wanawake nao wanaoa na wanaume kudeki na kuosha watoto.

Ili kunogesha mambo, nitaanzisha foundation ya Mpayukaji Anthropological Society of Mawazo (MAS) kwa ajili ya kutetea haki za viumbe wote. Pia nitaanzisha mfuko wa kutetea watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe.

Ingawa nina miaka lukuki tangu niingie nyumba za ibada, nitaanza kusali kama mtu aliyempokea Yesu na mtume jana. Nitaanza kuandaa harambee kwa ajili ya kuchangisha pesa za kusomesha watoto wa maskini na kugharimia matibabu.

Hapa lazima ninunue vyandarua kama 500 na madawati 200 kwa ajili ya kusaidia hospitali na shule za Uswekeni.

Pia nitanunua mipira kibao kwa ajili ya kusaidia timu za Uswekeni jimboni kwangu. Nitaongeza na jezi ambapo nami nitavaa moja na kucheza na watoto wa mtaani ambao kabla ya kugombea nilikuwa nawaona wote vibaka.

Ila huu msaa wangu wa milioni tano nitauvua na kuvaa mweku mweku. Maana walevi hawaaminiki wanaweza kukuliza.

Pia wale wazee wa kikabila nimeishawaandalia dawa yao. Nitawahonga viongozi wao wanivishe nguo za kijadi na kunitawaza kuwa mzee wa kabila bila kusahau tukio hili kwenda sambamba na kutawazwa kuwa kamanda wa vijana wa Mkoa wa Ulaji.

Pia ile nyumba ndogo niliyozaa nayo nitaihonga ili isilete kidomo domo ikatibua. Mwanaharamu niliyemkana lazima awe mtoto kipenzi ila kwa siri.

Kumfunga kamba mama yake, nitamtafutia shule ya kimataifa ili ajue mwanae anaandaliwa kuwa msomi na kiongozi. Nitamuahidi kuwa akimaliza shule ya msingi, nitampeleka London kusoma sekondari.

Pia kuna hawa wafa na nguna au wakulima. Nitawaahidi kuboresha bei za mazao yao . Pia nitakopa mbinu toka kwa jamaa yangu Pita Pinda wa Kupinda.

Nitawaambia kuwa kuanzia sasa kila kijiji jimboni Ulaji kitakuwa na trekta na Hallow. Pia nitaahidi kusambaza maji kila kijiji. Hapa ndipo Mwarabu wangu wa Dubai atanipiga tafu. Nitaleta vijana toka chuo cha maji kufanya tathmini ya mradi mzima.

Kwa vile mimi ni bonge la msanii, nimeishaanza kumtetea mwenyekiti wa chama chetu cha Mapinduzi (attention! Siyo CCM) kwa kila upuuzi anaofanya.

Kumshawishi asinisahau kwenye baraza la mawaziri, nimeanza mtindo wa kutishia kuwafikisha mahakamani wale wote wanaompinga. Katika kufanya hivyo, napandisha mwenembago na mori kama morani wa Kimasai nakuapia mizimu na miungu yote ya kweli na uongo.

Juzi nilipata habari njema toka kwa mwenyekiti. Nilipojiunga na mtandao maslahi wa adui zake waliokuwa rafiki zake alichukia sana.

Nasikia. Tangu ajue nimerejea kwenye mtandao wake amefurahi na ametuma ujumbe: kama nitaendelea kuwa mtoto mzuri, nisiwe na wasi wasi baada ya uchaguzi.

Kama waliwa wa DECI, sasa nina kazi moja-kupanda ili hatimaye nivune ingawa kwenye siasa hakuna kuaminiana. Tofauti na DECI nina uhakika. Kwani mkurugenzi wa upatu huu wa kisiasa ana rugu la dola tofauti na wale wahuni na wachungaji wapuuzi wa DECI.

Ingawa wapuuzi wanaweza kuona mipango yangu kama ndoto za Alinacha, wajue mimi naipendwa sana. Kwanza mimi ni ‘beautiful’ kama Njaa Kaya Kikwekwe mwenyekiti wangu. Pia mimi ni kijana mwenye miaka 65.

Tatu uzoefu umeonyesha. Hakuna tapeli au msanii anaweza kuchukiwa kutokana na kuwa na lugha tamu iwatoayo walevi kwenye chuki.

Nne, mimi ni chaguo la Mungu kama bosi wangu. Tano, mimi ni mtu wa watu. Je, kuna mtu wa fisi? Hayo tuyaache!

Sita, nimeleta amani kwenye jimbo langu kutokana na biashara zangu. Saba, nina uzoefu wa kuwaweka watu sawa kwa kutoa ahadi nyingi kemkem na za kusadikika.

Du! Kumbe ukurasa umejaa. Tuonane kwenye uchaguzi. Ila chunga mipango si matumizi na si kila ving’aavyo ni dhahabu. Nyingine hugeuka adhabu na ghadhabu.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 6,2009.

No comments: